Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na wadau na viongozi wa mifuko ya hifadhi ya jamii wakati wa kilele cha maadhimisho ya wiki ya Mifuko hifadhi ya ya jamii iliyofanyika mjini Dodoma leo(picha na Freddy Maro)
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewahakikishia Watanzania kuwa mifuko yote ya hifadhi ya jamii nchini ni salama, iko katika hali nzuri kifedha, hakuna hatari ya mfuko wowote kufilisika, tofauti na uvumi ambao umekuwa unaenezwa na watu wachache katika siku za karibuni.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa mifuko yote ya jamii nchini inawekeza katika maeneo salama na kuwa uwekezaji huo ni endelevu na ni kwa manufaa ya wanachama wa mifuko husika.
Rais Kikwete ameyasema hayo leo, Ijumaa, Mei 17, 2013 wakati alipofunga Wiki ya Mifuko ya Hifadhi Tanzania baada ya kukagua maonyesho ya mifuko hiyo kwenye Uwanja wa Nyerere Square mjini Dodoma.
Katika hotuba yake iliyozungumzia masuala mbali mbali yanayohusu maendeleo ya mifuko ya hifadhi nchini na mafanikio ambayo yamepatikana katika eneo la kuboresha maisha ya Watanzania kupitia mifuko yahifadhi, Rais amesema tathamini ya kifedha ya mifuko yote ya hifadhi nchini imekamilika na kubaini kuwa mifuko yote iko katika hali nzuri na ni endelevu.
Amesema Rais Kikwete: “Raslimali ya mifuko ya hifadhi ya jamii imeongezeka kutoka sh trilioni 3.7 mwaka 2010 na kufikia trilioni 5.3 mwezi Desemba, 2012. Tathmini hii imefuta dhana ya watu wachache waliokuwa wanaeneza uvumi kuwa baadhi ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ipo katika hali mbaya kifedha.”
Uvumi huo ulitokana na Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali iliyotolewa mwaka huu ambako umeonyeshwa kuwa Mfuko wa Pensheni ya Watumishi wa Umma (PSPF) unaidai Serikali mabilioni ya fedha, jambo ambalo Rais Kikwete amesema ni kweli na kufafanua historia ya deni hilo akisema kuwa lilizaliwa Julai, mwaka 1999 wakati watumishi wote wa Serikali walipoingizwa katika mfuko wa hifadhi ambako watumishi hao walitakiwa kulipiwa mchango kiasi fulani na Serikali.
“Awali deni hili halikujulikana. Lakini maadamu limejulikana litalipwa na kwa kuanzia mwakani Serikali italipa kiasi cha sh bilioni 50 ikiwa ni sehemu ya kulipa deni hilo. Na wala hakuna mtumishi yoyote wa umma ambaye atakosa kulipwa malipo yake halali kwa sababu ya hali hiyo. Lengo letu ni kuona kuwa hakuna mfanyakazi atakayekosa mafao yake kwa sababu ya Serikali, yaani mwajiri wake. Hatuwezi kufanya kamari na mafao ya wafanyakazi.”
Kuhusu usalama wa uwekezaji wa mifuko hiyo, Rais Kikwete amesema: “Jambo jingine linalonipa faraja ni ule uhakika kuwa sasa uwekezaji unaofanywa na mifuko ya hifadhi ya jamii ni salama na wenye manufaa kwa wanachama wake. Kwa maneno mengine hakuna mwanya wa kuichezea kamari michango ya wanachama inawekezwa kwenye miradi inayomnufaisha mwanachama moja kwa moja na taifa kwa jumla.”
Rais amefafanua kuwa hali hiyo imetokana na kukamilika kwa Kanuni za Uwekezaji zilizoandaliwa na Mamlaka ya Mifuko ya Hifadhi (SSRA) kwa kushirikiana na Benki Kuu. “Tangu kuanza kutumika kwa kanuni hizo Mei, 2012, uwekezaji wa mifuko ya jamii umeongezeka kutoka sh trilioni 3.38 hadi kufikia sh trilioni 4.24.”