Tanzania ipo katika kipindi cha mpito cha mabadiliko ya katiba mpya ya Tanzania baada ya serikali kuitika mwito wa vyama mbalimbali vya upinzani na wananchi kwa ujumla. Naishukuru serikali kwa jitihada zake za kuanzisha mchakato huu wa kidemokrasia wa mabadiliko ya katiba mpya chini ya uongozi wa rais wetu Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete.
Tukiwa wote ni mashahidi, bila ya shaka serikali imejitahidi kwa kuchukua hatua zote za kutekeleza suala hili kuanzia ngazi za mitaa, kata, wilaya, vijijini na mikoa yote kwa malengo ya kuhusisha wananchi na asasi na vyama mbalimbali hapa nchini kwa njia ya moja kwa moja au kwa njia ya kuwakilishwa kimantiki. Naam, na tumeona changamoto mbalimbali katika mchakato huu na kama tunavyojua au na kama tunayoomba mwisho wa yote haya yachukuliwe yale mapendekezo ya wananchi na mapendekezo ya asasi mbalimbali na vyama mbalimbali yatakayojenga taifa letu kuwa imara, kuwa na amani na kutuwezesha kuwa wamoja bila ya kuangalia itikadi yoyote yenye kuvunja amani na umoja wa taifa letu.
Kutokana na mipango ya tume ya mabadiliko ya katiba ilivyojipanga, rasimu ya katiba ipo njiani kutokana na muda wa sheria uliotolewa na bila ya shaka itafika wakati wake muwafaka katiba kuwekwa hadharani. Pamoja na yote haya yanayofanywa na serikali kuridhisha wananchi na vyama na asasi mbalimbali kwa kulitakia kheri taifa lake, suala la kujiuliza ni, Serikali imejipanga vipi au imeweka mikakati gani ya kuchukua hatua mara mchakato wa katiba utakapokwisha na katiba kuwekwa hadharani ili kuzuia watu wachache wasije wakaunda majeshi bila ya silaha ili kutuvunjia utulivu na amani nchini kwetu kwa kutaka kuitikisa serikali?
Ushauri Wangu:
Kama serikali ilivyoanza kupokea na kuridhia mabadiliko ya katiba mpya kwa kuhusisha vyama na asasi mbalimbali nchini na mpaka kuunda tume ya mabadiliko ya katiba mpya inayoongozwa na Mheshimiwa jaji Joseph Warioba (ambaye ni mmoja wa hazina ya taifa letu) na kushirikiana na watu wenye weledi na uadilifu mkubwa katika tume hiyo, ushauri wangu ni kuwa, chombo au idara au tume nyingine mpya ya kudumu iundwe 'maalum na hususan' ya kulinda amani wakati na baada ya katiba mpya kutolewa hadharani ambayo tume hiyo ihusishe au/na iwakilishwe na vyama na asasi mbalimbali na iwe na wanachama huru wasiofungamana na upande wowote wa asasi au vyama vya kisiasa, ambao wanachama hao wawe na nguvu ya kuchukulia hatua za kisheria asasi au chama chochote chenye uchochezi wa kuvunja amani nchini. Tume hii ishirikiane pamoja na serikali katika kulinda amani mara baada ya kipindi cha rasimu ya katiba itakapowekwa hadharani na baada ya kipindi cha katiba kukamilika na kupitishwa, na kwa yeyote iwe ni asasi au chama kisichotaka kujihusisha na kushirikiana na mchango wa tume hii ya kuweka amani baada ya katiba itakapotolewa iwe kipindi cha rasimu au kipindi cha mwisho wa kutolewa katiba, hapa ndipo tutamjua mzuri nani na mbaya nani katika taifa letu lenye usalama na amani ambalo watu wake hawakuangalia, hawaangalii na nataraji hawatoangalia itikadi za kidini, kisiasa au za kikabila kama tulivyorithishwa na wazee wetu na tuendelee hivyo hivyo ili kuendeleza usalama na amani kwa vizazi vijavyo vya Tanzania. Usalama na Amani siyo jukumu la serikali peke yake, ni jukumu la kila Mtanzania, na tukumbuke kuwa mbegu tunayoipanda sasa hivi ndio tutaivuna baadae.
Ushauri wangu tume hii yenye nguvu ya kulinda amani nchini ipatiwe kipengele au vipengele katika katiba yetu mpya ili kusiwe na walakini huko tunapokwenda, au inawezwa ikaundwa huru kama asasi au idara mojawapo ya serikali ya kulinda amani kwa yoyote mwenye kuleta utata juu ya katiba ili tuilinde katiba yetu adhimu.
Huu ni mchango na ushauri wangu tu katika katiba mpya na nataraji suala hili litaangaliwa.
Nini Kinachofuata Baada Ya Katiba Mpya?
Serikali kama ilivyojipanga kwenye mabadiliko ya katiba mpya, vilevile ijipange kwa mabadiliko ya 'Kiuchumi' ya kunufaisha wananchi wa Tanzania kwa ujumla, kwani ikiwa tutasahau tunapotoka na kilichotufikisha hapa kazi yetu itakuwa haijakwisha na matokeo ya baadaye yatakuwa si mazuri.
Wakati huu huu wa kipindi cha mabadiliko ya katiba, serikali iandae njia ya kuonesha wananchi wa Tanzania 'A clear roadmap' ya kuwa mabadiliko ya katiba yanaenda sambamba na mabadiliko ya kiuchumi ya taifa letu na mabadiliko ya kiuchumi ya kuwawezesha Watanzania. Hapana! naona bado hujanifahamu. Mabadiliko haya ya uchumi ninayosema mimi siyo mabadiliko ya kujenga barabara za lami tu na magorofa makubwa mjini, mabadiliko ya kila Mtanzania kuwezeshwa kihali ili kupiga vita ufukara kwa kuwekewa ngazi na fursa mbalimbali za kihalali, za kimaadili na za kiutamaduni wa Kitanzania ili kuupiga vita ufukara. Wananchi wawekewe wazi ni muda gani na tutafika wapi, kwa mfano malengo ya miaka 10 (kumi) ya kuwawezesha wananchi, ingawa wote tunakubali kuwa siyo rahisi kuondoa ufukara wa watu zaidi ya milioni arubaini ndani ya miaka kumi, lakini angalau kuwe na malengo ya kufikia ngazi fulani, na malengo hayo yawekwe wazi kwa wananchi ili wajue serikali ina malengo gani kwao. Kufanya hivi ndiyo demokrasia inavyotutaka tufanye na ni njia mojawapo ya kuepusha vurugu na ni njia ya kuleta amani na usalama si Tanzania tu bali popote pale katika dunia hii ya leo. Njia hii (roadmap) ya kuwawezesha wananchi iwekwe wazi kwa wananchi katika njia zote za habari na hata kwa vipeperushi kikampeni lakini si kwa kampeni za kisiasa bali kwa malengo ya kutimiza majukumu hayo ya msingi. Baada ya haya, iwapo kutakuwa na vurugu zisizo na msingi kutoka kwa watu wachache wanaotaka kutugawa na kuvunja amani nchini kwetu, itabidi sheria ichukue mkondo wake kwa watu hawa.
Ningependa kutoa ushauri au mchango wangu mdogo kutokana na ninavyoona dunia hivi sasa inapoelekea. Kutokana na mtazamo wangu, demokrasia ya karne ya 21 (ishirini na moja) iwe ni demokrasia ya Kiuchumi ya kuwasaidia wananchi kutokana na 'Utandawazi' ambao tulioukubali kuupokea katika kipindi hiki cha karne mpya ya kizazi kipya. Demokrasia ya Kiuchumi ni mbali na demokrasia ya Kisiasa ambayo kama ilivyokuwa ikitumika katika zama za miaka na karne zilizopita, ingawa demokrasia ya Kisiasa itabaki kuwepo na inaweza kutumika kama ni chombo cha kupelekea mafanikio ya uchumi kwa Watanzania (lakini kama tukiwa makini) na kwa maridhiano na wadau. Mengi yanayotokea tunayoyaona sasa ni kuwa tumejisahau kuwa dunia inabadilika lakini sisi wenyewe hatujibadilishi na hiyo ndiyo hatari kubwa ya tunapoelekea.
Serikali ya awamu ya nne imefanya mengi mazuri ambayo tunayaona wazi ya kimaendeleo, lakini kutokana na mabadiliko haya ya utandawazi ambao unaelekea kutanda kwenye kila ngazi ya jamii lazima serikali ijipange tena kwa kuonesha njia ya kuwawezesha wananchi kikampeni ambayo isiyo ya kisiasa na ioneshe mifano ya kutekeleza malengo hayo katika kuwezesha watu wake Kiuchumi ili kuondoa au kupunguza umaskini wa wananchi. Rais wa zamani wa Marekani, Thomas Jefferson, amesema, "That government is best which governs the least, because its people discipline themselves."
Baada ya yote haya ningependa kumaliza kwa kusema ukilinda Utamaduni wa taifa umelinda amani ya taifa.
Huu ni mchango wangu wa katiba na samahani kama nimekosea.
Ndugu yenu,
Saleh Jaber.