Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Hussein Mwinyi akionesha ripoti na machapicho aliyozindua, wengine wanaoshuhudia ni Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Regina Kikuli na Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Donan Mmbando
Waziri wa Afya Dkt. Hussein Mwinyi akihutubia wakati wa uzinduzi huo
Mkurugenzi Mkuu TFDA, Hiiti Sillo, akiwasilisha maelezo ya utangulizi katika uzinduzi wa taarifa ya ufuatiliaji wa dawa za ALu na machapisho mbalimbali
Mwakilishi wa WHO, Dkt. Rufaro Chatora akiwasilisha salamu za WHO katika uzinduzi huo
========= ========= ========== TFDA YAZINDUA RIPOTI YA UFUATILIAJI WA KARIBU WA DAWA YA MALARIA AINA YA ALu KATIKA KUFUATILIA MADHARA YA DAWA Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt Hussein A. Mwinyi amezindua ripoti ya ufuatiliaji wa usalama wa dawa mseto ya Malaria aina ya Artemether + Lumefantrine (ALu) na kusema kwamba imethibitika kisayansi ni salama na haina madhara makubwa (adverse reactions) na badala yake ina madhara madogo yanayovumilika (side effects). Ripoti hiyo iliyoandaliwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kupitia mpango wa Ufuatiliaji wa karibu wa madhara ya dawa ya ALu, imezinduliwa mwishoni mwa wiki mkoani Dodoma na kuhudhuriwa na Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya nchini. Akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri Hussein Mwinyi amewataka wananchi waliokuwa na wasiwasi juu ya dawa hii kuendelea kuitumia dawa mseto ya Malaria aina ya ALu kwa kuwa ni salama. Sambamba na uzinduzi huo, Waziri pia amezindua machapisho yanayotumika katika ukusanyaji wa taarifa mbalimbali za wagonjwa kwa lengo la kufuatilia usalama wa dawa nchini. Machapisho hayo ni vitendea kazi katika mfumo wa ufuatiliaji wa karibu wa madhara ya dawa ambao unawezesha kukusanya taarifa nyingi zaidi na kuweza kufanya tathmini ya kisayansi ya uhusiano wa dawa na madhara yake. Kufuatia uzinduzi huo, Waziri amewaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya kutumia machapisho husika kama ilivyokusudiwa kwa lengo la ufuatiliaji wa madhara ya dawa kwa kuhakikisha fomu husika zinajazwa na kuwasilishwa TFDA kwa wakati. Naye Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dkt. Rufaro Chatora, ameahidi kuendelea kuisaidia TFDA katika kuhakikisha kuwa usalama wa dawa unaendelea kudumishwa nchini. Wakati huohuo, Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, Hiiti Sillo, amesema kuwa TFDA ipo katika hatua ya kukamilisha maandalizi ya ufuatiliaji wa karibu wa usalama wa dawa za kupunguza makali ya Ugonjwa wa UKIMWI (ARVs) katika mwaka wa fedha 2013/2014. Mfumo wa ufuatiliaji wa madhara ya dawa ya Malaria unaojulikana kitaalamu kama Cohort Event Monitoring (CEM) ulianza kutekelezwa nchini mwaka 2009 kufuatia mafunzo yaliyotolewa na WHO nchini Ghana ambapo TFDA ilishiriki. |