Wito umetolewa kwa serikali za Afrika kutoa msaada kwa wakulima wanawake kama bara hilo linataka kufikia maendeleo endelevu kijamii na kiuchumi.
Akihutubia kongamano kubwa la kikanda la kilimo la muungano wa umoja wa vyama vya kilimo kusini mwa Afrika (SACAU) jana jijini Dar es Salaam, waziri wa Kilimo na Maendeleo Vijijini wa Nigeria, Dkt. Akinwumi Adesina alisema ni muhimu serikali na wadau wengine wanaosaidia maendeleo ya kilimo wakajua kuwa wakulima wengi katika bara hilo ni wanawake.
“Bila wakulima wanawake, bara la Afrika haliwezi kufikia malengo yake katika sekta hii ya kilimo,” alisema. Kongamano hilo litakaloangalia kwa undani swala la jinsi ya kuhudumia kifedha kilimo cha Afrika linatayarishwa na Baraza la Kilimo na Mifugo Tanzania (ACT) kwa kushirikiana na SACAU.
“Wakulima wanawake wanahitaji kupata mikopo nafuu, uhakika wa ardhi, na teknolojia,” alisema, na kuongeza kuwa mustakabali wa sekta ya kilimo katika bara la Afrika sio wa uhakika kama wanawake wakulima watawekwa pembezoni na mipango ya maendeleo yanayohusu sekta hiyo.
Kongamano hilo linaloangalia kwa undani swala la jinsi ya kuhudumia kifedha kilimo cha Afrika linatayarishwa na Baraza la Kilimo na Mifugo Tanzania (ACT) kwa kushirikiana na SACAU.
Waziri huyo alisema kuwa hakuna sababu ya bara la Afrika kuagiza chakula toka nje wakati zaidi ya asilimia 60 ya ardhi inayofaa kwa kilimo na ambayo bado haijatumika iko katika bara hilo.
“Kwa raslimali ya maji, ardhi na nguvu kazi ya kutosha tuliyonayo, tunatakiwa kulisha dunia,” alisema. Kwa upande wake, afisa mtendaji mkuu wa SACAU, Bw. Ishmael Sunga alisema kuwa wakulima wa Afrika hawawezi kuendelea kwa haraka na kuwa wakubwa kama hawataweza kupata huduma za uhakika za kifedha.
“Tusiishie kuona chakula kinapatikana katika ngazi ya familia tu, bali tuendeleze sekta hii, wakulima na kuongeza uzalishaji,” alisema. Mkurugenzi wa maendeleo ya mazao toka wizara ya Kilimo, Usalama wa Chakula na Ushirika, Dkt. Mshindo Msolla alisema ni muhimu kwa serikali za Afrika zikajitahidi kuwa na usalama wa chakula katika kila nchi kabla ya kufanya lolote.
“Ni muhimu tukazalisha kwanza chakula cha kutosha katika maeneo yetu Afrika kabla ya kufikiria kitu kingine kwanza,” alisisitiza. Akizungumza kwa niaba ya waziri wa wizara hiyo, Dkt. Msolla alisema kuwa serikali ya Tanzania inafanya juhudi kubwa sana kufikia mapinduzi ya kilimo kupitia mipango mbalimbali kama vili Kilimo Kwanza na mpango maalum wa kuendeleza kilimo katika ukanda wa kusini mwa Tanzania (SAGCOT).
Washiriki zaidi ya 200 kutoka nchi 14 za kusini mwa Afrika pamoja na wawakilishi wa vyama vya wakulima kutoka maeneo mengine ya Afrika wanashiriki kongamano hilo la siku tatu. Pamoja na mambo mengine, mkutano huo utaangalia ushirikiano kati ya SADC/COMESA/EAC katika maswala ya kilimo. Pia mkutano huo utaangalia makisio ya mahitaji ya bidhaa za kilimo duniani na kuona fursa na tishio lake kwa wakulima.
Pia washiriki hao wataangalia kama mfumo wa kifedha uliopo sasa unaweza au hauwezi kuendeleza sekta ya kilimo katika siku zijazo. Inatarajiwa kwamba Rais Jakaya Kikwete atahutubia mkutano huo leo (Jumanne).