Waziri wa Wizara ya Viwanda na Biashara,Dr. Abdallah Kigoda (pichani) amesema kuwa mipaka ya nchi imekuwa chanzo cha uingizwaji wa bidhaa ambazo ziko chini ya viwango (feki) hali inayochangia kuleta athari kubwa kiuchumi na afya za watu wanaotumia bidhaa hizo.
Aidha waziri huyo ameeleza kuwa uingizaji wa bidhaa bandia nchini unatokana na taasisi zinazoshughulikia masuala ya viwango vya ubora kutoimarika kiutendaji.
Akizungumza katika ufunguzi wa Warsha iliyoandaliwa na shirika la dunia linalohusika na mambo ya kuandaa viwango (ISO) wakishirikiana na shirika linaloshughulikia viwango na ubora wa bidhaa nchini (TBS),warsha iliyokuwa ikijadili juu ya mfumo wa uzalishaji kuanzia malighafi, bidhaa, mtumiaji na taka inayotokana na bidhaa hiyo ilivyo na athari katika mazingira yaani (Life Cycle).
“Mkutano huu ni muhimu kwa nchi zinazoendelea kushiriki katika kuweka vigezo vya viwango vya ubora na kujiaandaa kuvitimiza ili kuweza kuuza bidhaa katika soko la dunia ili kuondokana na vikwazo katika uingizaji wa bidhaa zao kwenye soko hilo kutokana na bidhaa kutokizi ubora wa kimataifa na teknolojia dhaifu inayotumika kuanzia malighafi,bidhaa hadi usafirishaji” Waziri Kagoda.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa TBS Bwana Leandri Kinabo amesema kuwa mkutano huo ni muhimu kwani unalenga kuweka mikakati ya viwango,na uzalishaji bora unaozingatia ubora ili kushiriki kikamilifu katika soko la dunia (WTO) ukizingatia kuwa Tanzania ni nchi mwanachama wa soko hilo.
Hivyo amewataka wazalishaji kuzingatia utunzaji wa mazingira katika mfumo mzima wa uzalishaji kuanzia malighafi, bidhaa, usafirishaji na utupaji wa taka inayotokana na bidhaa hiyo (Disposal).
Baadhi ya washiriki wa mkutano huo ni kutoka nchi za Afrika Mashariki,Ukanda wa Kusini mwa Afrika (SADC) na pia unatarajia kuhudhuriwa na nchi za Malaysia, India, China na Uingereza.