Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania Katika Umoja wa Mataifa, Mhe Tuvako Manongi, Akizungumza wakati Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipojadili Utatuaji wa Migororo katika Afrika kwa njia ya Amani, majadiliano hayo yalifanyika hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa ikiwa ni sehemu pia ya Kuadhimisha miaka 50 tangu kuasisiwa kwa Muungano wa Afrika. Majadiliano hayo yalihitimishwa kwa kupitishwa bila kupingwa Tamko la Kisiasa kuhusu utatuaji wa Migogoro Afrika kwa njia wa amani. Tamko hilo liliandaliwa na Kundi la Nchi za Afrika katika Umoja wa Mataifa. Akichangia majadiliano hayo, Mwakilishi wa Kudumu Umoja wa mataifa Mhe Tuvako Manongi pamoja na kuzungumzia sababu na vyanzo vya migogoro isiyo kwisha Barani Afrika, pia alitoa wito kwa Afrika kukataa kugawanywa, kudharauliwa na kunyonywa. Pembeni ya Balozi ni Afisa wa Ubalozi , Bw. Noel Kaganda
Na Mwandishi Maalumu
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepitisha kwa kauli moja Tamko la Kisiasa kuhusu Utatuzi wa Migogoro Barani Afrika kwa njia ya Amani.
Tamko hilo ambalo ndani yake linaainsha na kutambua mchango mkubwa wa Muungano wa Nchi Huru za Afrika (OAU) na sasa Muungano wa Afrika ( AU) katika kuchagiza na kusimamia pamoja na mambo mengine, maendeleo ya nchi za Afrika na watu wake, kupiga vita umaskini, ujenzi wa utawala bora, demokrasia , haki za binadamu na utatuzi wa migororo kwa njia za amani.
Kabla ya kupitishwa kwa Tamko hilo, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, kwa siku nzima ya Alhamisi na ijumaa asubuhi lilijikita katika majadiliano ya mada iliyohusu ‘utatuzi wa migogoro kwa njia ya amani barani afrika’, ikiwa pia ni sehemu na Baraza hilo kuadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwa OAU na baadaye AU.
Miongozi wa viongozi wakuu walioshirikia majadilaino hayo, na ambayo yaliandaliwa na Bw. Vuk Jeremic, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ni Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, Rais wa Equatoria Guinea Theodore Obiang Nguema Mbasogo, Rais Mstaafu wa Burundi Jean Pierre Buyoya ambaye pia Mwakilishi maalum wa Muungano wa Afrika huko Mali na Sahel, wakiwamo pia mawaziri kadhaa wa Mambo ya Nchi za Nje.
Akiungana na wazungumzaji wengine katika mkutano huo, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Tuvako Manongi, pamoja na kuainisha sababu na vyanzo vya migogoro Barani Afrika, alisema, Afrika lazima ifikie mahali ikatae kugawanywa.
“Bara la Afrika lina fursa nyingi, Afrika inapanda chati. Afrika lazima ikatae kugawanywa, ikatae kudharauliwa na ikatae kunyonywa” akasema Mwakilishi wa Kudumu, Tuvako Manongi.
Na kubainisha kwamba, Afrika lazima pia ikatae kutambuliwa kama bara ambalo limejaa migogoro . “ Huu ni wakati wa kufufua upya pan africanism, hiki ni kipindi cha mwamko mpya wa Afrika. Lazima tufanye kazi kwa pamoja ili kuwapa matumaini watu wetu” akasisitiza Manongi.
Akasema wakati tukisherehekea maadhimisho ya miaka 50 wa OAU, ni vema kila mmoja wetu akaahidi upya kuimarisha ushirikiano kati ya Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika kama ilivyoainishwa katika Sura ya Saba ya Katima ya Umoja wa Mataifa.
Akatoa mfano kwa kusema uhusiano huo unapashwa kuendelezwa katika nyanja zote za usalama na maendeleo. Kama ambavyo imeshashuhudiwa katika uundwaji wa Jeshi la Mseto kati ya Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika katika Jimbo la Darfur ( UNAMID), Misheni ya Muungano wa Afrika huko Somalia, (AMISOM0 na tukio la hivi karibuni la kurejewa na kuongozewa uwezo mpya Misheni ya Kutuliza Amani katika DRC ( MONUSCO) kulikoendana na kuridhiwa upelekaji wa Brigedi Maalum inayoundwa na wanajeshi kutoka Tanzania, Afrika ya Kusini na Malawi.
Aidha akasema majadiliano hayo ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, yamefanyika ikiwa ni siku chache tu, tangu kufanyika kwa Mkutano wa Baraza la Usalama la Afrika katika ngazi ya Mawaziri nchini Tanzania, mkutano ambao pia ulijadili kwa kina pamoja na mambo mengine hali ya usalama barani afrika , vyanzo vya migogoro na ufumbuzi wake.
Karibu wazungumzaji wote wakiwamo wawakilishi wa Marekani na Jumuiya ya Ulaya waliochangia majadialiano hayo ya utanzuaji wa migogoro kwa njia ya amani, licha ya kutambua, kusifu na kupongeza kazi kubwa ambayo imefanywa na inaendelea kufanywa na Muungano wa Afrika na Taasisi za Kikanda katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, walisisitiza haja na umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kuendeleza ushirikiano wake na Muungano wa Afrika.
Aidha wazungumzaji huo walitambua na kukiri kwamba Bara la Afrika licha ya changamoto mbalimbali zikiwamo za migogoro inayoibuka hapa na pale, imepiga hatua kuubwa za kimaendeleo, kiuchumi na kijamii na kwamba Bara hilo linastahili kupongezwa na kuendelea kusaidiwa.