Na Mwandishi Wetu
HATIMAYE bendi ya nguli wa muziki wa reggae nchini, Ras Inno Nganyagwa imekamilika na anatarajia kuizindua rasmi mwezi ujao jijini Dar es Salaam.
Ras Inno ambaye ni mshindi wa tuzo nne za mwanamuziki bora wa reggae Tanzania, amesema bendi yake hiyo ina wanamuziki 11 na itazinduliwa katika hafla maalumu katika ukumbi utakaotangazwa hapo baadaye.
Amasema nia ya kuanzisha bendi hiyo ni kuwa na ufanisi bora zaidi wa kufanya kazi zake za muziki, kwani bendi ya kudumu na wanamuziki wa kudumu hujenga ‘patern’ ambayo ni sawa na wachezaji waliozoeana uwanjani.
“Hiyo hulinda ladha ya nyimbo husika kutobadilika kila show, pia uhakika wa kufanya kazi njema nje ya nchi. Lakini pia kuwa na bendi huhakikisha upatikanaji wa tija ya kudumu, tofauti na ukiwa ‘solo’ tu bila jina la bendi kazi huja kwa misimu kutokana na mazoea ya hapa kwetu Bongo,” amesema.
Amesema bandi hiyo ni mojawapo ya miradi iliyo chini ya usimamizi wa taasisi yake mahsusi ya kuupromoti muziki wa reggae, kwa ushirikiano na wadau wengine miongoni wa mitindo mingine kwa kuzingatia weledi.
“Taasisi inaitwa Reggae Production House ambayo itahakikisha uzalishwaji wa vipaji vipya vya vijana wanaotaka kuingia kwenye reggae, kwa kufuata njia sahihi itakayowajenga kuwa wanamuziki bora wa reggae nchini watakaoweza kufanya kazi kimataifa.
“Dhima nzima ni kuufufua muziki wa reggae hapa nchini si kwa kuwa umekufa, la hasha, ila kuna mazingira yanayoufanya muziki huu uonekane kama haupo, lakini mahitaji yapo na mashabiki wana hamu kubwa nao.”
Aidha ameongeza kusema kwamba, ukimya wake wa muda mrefu una sababu kadhaa zikiwemo za kibinafsi kimaisha, lakini muda aliokuwa nje ya ulingo, ameyasoma vyema mazingira yanayoukabili mtindo wa reggae hivyo naamini ana dozi ya kuutibu.
“Ninayodhamiria kuyafanya kupitia taasisi yangu na vitengo vyake ikiwemo bendi, havijapata kuonekana kabla kwenye tasnia ya reggae hapa nchini. Hivyo basi naamini mwanzo huu wa mapinduzi, utaungwa mkono na wadau wote wenye mapenzi mema.”