CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kinatarajia kushiriki kwenye Mkutano Mkuu wa 76 wa Chama cha Kimataifa cha Waandishi wa Habari za Michezo (AIPS) unaotarajiwa kuanza kesho (Jumatatu) Sochi, Russia.
Mkutano huo wa kawaida wa mwaka ambao utashirikisha viongozi wa zaidi ya vyama vya waandishi wa habari za michezo 100 duniani, mwaka huu utaambatana na uchaguzi mkuu wa AIPS.
TASWA katika mkutano huo itawakilishwa na Mwenyekiti wa chama, Juma Pinto na Katibu Mkuu, Amir Mhando ambao wanatarajiwa kuondoka leo alasiri kwa ndege ya Emirates.
TASWA ni mwanachama hai wa muda mrefu wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Duniani (AIPS) chenye makao yake makuu Lausanne, Uswisi, ndiyo sababu kila mwaka tumekuwa tukishiriki mikutano hiyo kwa awamu mbalimbali za uongozi ukiwemo wa kwetu uliochaguliwa mwaka 2010.
Mwaka 2011 tulishiriki Mkutano Mkuu wa AIPS uliofanyika Seoul Korea, Korea Kusini na tuliwakilishwa na Makamu Mwenyekiti, Maulid Kitenge na mimi nikiwa Katibu Msaidizi.
TASWA pia ilishiriki Mkutano Mkuu wa AIPS uliofanyika Innsbruck, Austria Januari mwaka jana, ambapo Katibu Mkuu, Amir Mhando alihudhuria. Tunaamini hii ni njia mojawapo ya kukutana na wadau mbalimbali kwani AIPS imekuwa ikitoa nafasi za mafunzo kwa wanachama wake na semina za michezo mbalimbali.
Ujumbe wetu katika mkutano wa mwaka huu ambao utamalizika Ijumaa wiki ijayo ni mkubwa, hivyo tunaamini utakuwa na manufaa kwa chama na waandishi wa habari za michezo kwa ujumla.
Ahsanteni.
George John
Kaimu Katibu Mkuu, TASWA