Afisa Ubalozi wa Ubalozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Bw. Justin Kisoka ambaye pia alikuwa Mratibu wa Kamati ya Tano inayohusika na masuala ya Utawala na Bajeti akiwasilisha siku ya Ijumaa, taarifa ya Kamati hiyo mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Taarifa hiyo ilihusisha maazimio Nane ambayo Baraza Kuu liliyapisha kwa kauli moja, likiwamo lile linaloidhinisha ujenzi wa Majengo ya Taasisi ya Kimataifa ya Kumalizia Mashauri ya Masalia ya iliyokuwa Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ( ICTR) Tawi la Arusha. Majengo hayo ya kisasa yatajengwa katika eneo la Lakilaki Jijini Arusha.
Na Mwandishi Maalum
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepitisha kwa kauli moja Azimio linalopendekeza kuidhinishwa kwa hatua zote za Ujenzi wa Mradi wa Taasisi mpya ya Kimataifa itakayochukua majukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda ( ICTR).
Mradi huo wa majengo ya kisasa, utajengwa katika eneo la LakiLaki Jijini Arusha-Tanzania na utahusisha Ofisi, vyumba vya mahakama, na sehemu ya kutunzia nyaraka na kumbukumbu zote za ICTR. Eneo hilo la Laki Laki limetolewa na Serikali ya Tanzania kwa Umoja wa Mataifa.
Baraza Kuu limepitisha Azimio hilo katika mkutano wake uliofanyika siku ya Ijumaa ( April 12),mkutano ambao pia, Baraza lilipokea na kupitisha maazimio mengine Nane yaliyowasilishwa na Kamati ya Tano inayohusika na masuala ya Utawala na Bajeti katika Umoja wa Mataifa.
Taasisi hiyo mpya ijukulikanayo kama Mfumo wa Kimataifa wa Kumalizia Mashauri Masalia ya iliyokuwa Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari au kwa kimombo ( International Residual Mechanism forCriminal Tribunal )- Tawi la Arusha pamoja na kuhifadhi nyaraka itasimamia kesi za Masalia ambazo zitakuwa bado hazijakamilia baada ya ICTR kumaliza muda wake mwakani.
Azimio hilo pamoja na mambo mengine, linamtaka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, kuweka bayana uwajibikaji na uangalizi wa kina katika ujenzi wa mradi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba, sheria, taratibu, kanuni na miongozo yote ya Umoja wa Mataifa inayohusu manunuzi/ugavi inafuatwa ipasavyo katika utekelezaji wa mradi huu.
Gharama za mradi zinatarajiwa kuwa kiasi cha dola za kimarekani 8.78 Milioni ( takribani Sh.14 Bilioni). Fedha hizi zinalipwa na Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa. Mradi unatarajiwa kukamilika kabla ya mwishoni mwa mwaka 2015.
Aidha kupitia Azimio hilo, Baraza Kuu pia limeishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea na jukumu la kufuatilia kwa karibu mchakato wote unaohusiana na utekelezaji wa mradi na vilevile katika kuhakikisha kwamba inashirikiana na Umoja wa Mataifa kufanikisha Mradi huu.
Halikadharika kupitia Azimio hilo, Baraza Kuu limeelezea kufurahishwa na maendeleo ya utekelezaji wa mradi hasa kwa kutumia ujuzi wa ndani, (Local knowledge) katika ubunifu wa majengo (design), upatikanaji wa meneja wa mradi na maandalizi ya kina ya gharama za ujenzi.
Pamoja na pendekezo la kuidhinishwa kwa hatua za ujenzi wa mradi , Baraza pia kupitia Azimio hilo , linamtaka KatibuMkuu kufanya juhudi zote zitakazo pelekea kupunguza muda wa ujenzi wa mradi .
Katika hatua nyingine, Baraza Kuu pia linamtaka Katibu Mkuu kuanza mazungumzo na Asasi nyingine za Kimataifa ikiwamo ile ya Mahakama Afrika itakayoshughulikia Haki za Binadamu, juu ya namna bora ya kushirikiana katika matumizi ya miundo mbinu hiyo katika siku za usoni.
Mwaka 2010 Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa, lilipitisha Azimio nambari 1966 la kuanzisha Mfumo wa Kimataifa utakaomalizia Mashauri ya Masalia kwa zilizokuwa Mahakama za Kimataifa za Mauaji ya Kimbari yaliyotokea nchini Rwanda ( ICTR) na Mauaji ya halaiki yaliyotokea katika iliyokuwa Yugoslavia ya Zamani ( ICTY).
Katika azimio hilo Baraza Kuu la Usalama lilibainisha wazi kwamba Arusha ndiyo itakuwa makao ya Tawi la mfuno huo mpya na The Hague ikiwa ni makao ya Tawi jingine.