MAMLAKA ya mapato Tanzania (TRA), imelitaka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kulipa deni lake la Shilingi 573 milioni kuanzia Jumatatu ijayo au wakate rufaa.
Habari zilizoifikia Globu ya Jamii zinasema kuwa TRA iliwasilisha barua ya kuitaka TFF kulipa fedha hizo juzi na kwamba iwapo TFF itashindwa kufanya hivyo basi wataitumia kampuni ya Majembe kupiga mnada mali za shirikisho hilo.
Chanzo hicho kimesema kuwa TRA ilifanya tathmini Machi 14 mwaka huu kutokana na ukaguzi wa hesabu za TFF na kukuta wana deni linalotokana na kodi (PAYE) na ongezeko la thamani (VAT) la jumla ya shilingi573 milioni.
"Hizo fedha zinatokana na deni la miaka mitatu ambazo ni kodi na pia mapato yatokanayo na makato ya mechi mbali mbali za Ligi Kuu ambazo zinafikia jumla ya kiasi hicho cha fedha."kilisema chanzo hicho
Alipoulizwa Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah kuhusiana na suala hilo alisema kwa kifupi "Sijaona barua yoyote kutoka TRA" Mwishoni mwa mwaka jana TRA pia ilishikilia akaunti za TFF na moja kati ya akaunti hizo ilikuwa na shilingi milioni 300 za udhamini wa Vodacom ambapo TFF ilikuwa ikidaiwa shilingi157 milioni kama kodi za makocha wa timu ya Taifa 'Taifa Stars' tangu kipindi cha enzi ya Mbrazil Marcio Maximo.
Kwa hali hiyo, TFF iliomba msaada wa serikali ambao ndio walipaji wa mishahara ya makocha wa Taifa Stars, na suala hilo tayari Naibu Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo Amos Makala alishaweka wazi kuwa suala hilo lipo kwenye hatua nzuri kwani linashugulikiwa Hazina na siku yoyote fedha hizo za makocha zitalipwa.