Mkurugenzi wa kampuni ya Compass Communications, Maria Sarungi Tsehai (kushoto) akisisitiza jambo wakati wa kuwakilisha tathmini ya mashindano Miss Universe Tanzania mbele ya maofisa wa sanaa wa Baraza la Sanaa Tanzania (Basata) ambao hawapo pichani makao makuu ya baraza hilo Ilala jijini. Kulia ni Miss Universe 2011, Nelly Kamwelu
Mkurugenzi wa kampuni ya Compass Communications, Maria Sarungi Tsehai (wanne kutoka kushoto) akisisitiza jambo wakati wa kuwakilisha tathmini ya mashindano Miss Universe Tanzania mbele ya maofisa wa sanaa wa Baraza la Sanaa Tanzania (Basata) makao makuu ya baraza hilo Ilala jijini.
Baraza la Sanaa nchini (BASATA) limeipongeza kampuni ya Compass Communications kwa mafanikio makubwa waliyopata pamoja na kuandaa mashindano ya urembo nchini kwa muda mfupi.
Akizungumza katika kikao cha tathimini ya mashindano ya Miss Universe yaliyofanyika juzi makao makuu ya Basata, Afisa Sanaa baraza hilo Malimi Mashili alisema kuwa pamoja na kampuni ya Compass kuanza kushiriki katika mashindano ya Miss Universe mwaka 2007, waliweza kufanya vyema na kuitangaza Tanzania nje ya mipaka yake.
Alisema kuwa mrembo wake, Flaviana Matata ambaye alimaliza katika hatua ya sita bora, mpaka sasa anafanya vyema nje ya nchi katika sekta ya maonyesho ya mavazi au wanaminitindo.
Mbali na mafanikio hayo, Mashili alisema kuwa usimamizi bora wa kampuni hiyo imewafanya warembo kuwa na tabia njema na kuepukana na skendo mbali mbali ambazo zinawatokea warembo waliopitia mashindano tofauti na mashindano mengine ya urembo nchini.
“Ni mashindano bora ambayo kwa kweli yametuvutia sana, tunaomba muongeze bidii ili kuyaboresha zaidi kwani mashindano haya kwa sasa ni makubwa na warembo wengi wanayaulizia jinsi ya kujiunga nayo,” alisema Mashili. Pia aliwataka waandaaji wa mashindano hayo kutafuta udhamini wa televisheni ambayo itaonyesha moja kwa moja ‘live’ mashindano hayo ili kupanua wigo wa wafuatiiaji wake kama ilivyo kwa mashindano mengine ya urembo.
Mkurugenzi wa Compass Communications ambaye pia ndiye mwandaaji mkuu wa mashindano haya Maria Sarungi Tsehai aliishukuru Basata kwa usimamiaji bora wa mashindano katika sekta ya sanaa nchini na kusema kuwa watajiathidi kuongeza wigo wa washiriki kaika mashindano ya mwaka huu.
Maria alisema kuwa pamoja na changamoto zote wanazokabiliana nazo alisema kuwa wameongeza mikoa saba zaidi na kufanya jumla ya mikoa 14 ambayo warembo wake watawania mataji mbali mbali mwaka huu.
Mikoa hiyo ni Katavi, Rukwa, Mbeya, Iringa, Njombe, Ruvuma, Dodoma, Arusha, Mtwara, Dar es salaam, Mwanza, Kilimanjaro, Kagera na Manyara. Kwa mujibu wa Maria, Miss Universe Tanzania imeweka mikakati ya kuwaendeleza warembo ambao hawakufanikiwa kushinda katika mashindano hayo. Alisema kuwa mpango wao mkuu ni kuwapa msaada wa kielimu kwa kushirikiana na asasi mbalimbali za hapa nchini hususani zinazoshughulika na masuala haya ya elimu.