Quantcast
Channel: MICHUZI BLOG
Viewing all articles
Browse latest Browse all 115264

Sherehe za mwaka mmoja tokea kuanzishwa kwa kikundi cha Island Exercise Group

$
0
0
 Baadhi ya wana michezo wa vikundi vya mazoezi wakiwa katika maandamano ya kusherehekea mwaka mmoja tokea kuanzishwa kwa kikundi cha Island Exercise Group zilizofanyika hapo katika uwanja wa makao makuu ya Brigedia nyuki Migombani.
 Vijana wa kitambi noma wakiwa makini katika mazoezi yao ya viungo wakionyesha umahiri wao kwa vile wao ni chem Chem ya kuenea kwa vikundi vyengine vya mazoezi hapa Zanzibar.
 Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi akiwa mwenye furaha akiambatana na Mumewe Balozi Seif wakiingia kwenye uwanja wa michezo wa Brigedia nyuki Migombani mara baada ya kuyapokea maandamano ya wana vikundi vya mazoezi. Nyuma ya Mama Asha ni Waziri wa Habari, Said Ali Mbarouk , Spika wa Baraza la Wawakilishi Pandu Ameri Kificho na aliyevaa track Suit ya Kijani ni mwakilishi wa jimbo la Rahaleo Nassor  Al-Jazira.
  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akisalimiana na Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Pandu Ameir Kificho ambae  naye alialikwa katika hafla hiyo na kushiriki pia kwenye maandamano hayo. Katikati yao ni Mwenyekiti wa Kikundi cha Island Exercise Group Brigedia General Sharif Sheikh Othman.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza katika maadhimisho ya mwaka mmoja tokea kuanzishwa kwa kikundi cha mazoezi cha Island Exercise Group hapo Migombani. Kulia ya Balozi Ni Waziri wa Habari Utamaduni, Utalii na Michazo Said Ali Mbarouk na Kushoto yake ni Mwenyekiti wa Kikundi hicho Brigedia General Sharif Sheikh Othman. Picha na Hassan Issa wa OMPR – ZNZ.
Na Othman Khamis Ame
Jamii Nchini inawajibu wa kuzingatia zaidi matumizi bora ya vyakula vinavyopunguza mafuta  kwa nia ya kujijengea afya bora sambamba na maisha marefu yenye kuambatana na akili iliyotulivu.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo mara baada ya kuyapokea maandamano ya wanamichezo wa mazoezi wa vikundi mbali mbali vilivyoshiriki katika uzinduzi rasmi wa Kikundi cha mazoezi cha Island Exercise Group  ambacho tayari kimeshatimiza mwaka mmoja hapo katika uwanja wa michezo wa Makao makuu ya Brigedia Nyuki Migombani nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Balozi Seif alisema upo muamko wa kutosha wa watu wengi kujiunga katika vikundi vya mazoezi jambo ambalo huleta faraja kwa afya zao lakini wakati huo huo baadhi yao wanashindwa kuzingatia mfumo mzuri wa matumizi ya vyakula wanavyotumia.
Alieleza kwamba si vyema kwa mtu kusubiri ushauri wa Daktari  wakati anapobainika kusumbuliwa na maradhi mbali mbali mengi kati ya maradhi hayo husababishwa na  ukosefu wa mazoezi.
“ Pamoja na mazoezi  yanayoendelea kuchukuliwa na wana michezo walio wengi  lakini bado wanapaswa kuepuka vyakula  vyenye kuleta athari kwenye miili yao”. Alisisitiza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Balozi Seif alifahamisha kwamba inavutia na kutia moyo kuona mazoezi yanayofanywa na wanamichezo katika sehemu tofauti yamekuwa yakishirikisha watu wa rika tofauti wakiwemo pia watoto wadogo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaasa wana michezo hao kuhakikisha wanadumisha suala la amani na Utulivu wa Nchi uliopo ambao kutokuwepo kwake maana yake hata muda wa kufanya mazoezi ambayo ni muhimu kwa afya za wanaadamu utatoweka kabisa.
Balozi Seif alisema zipo baadhi ya Nchi Duniani zikiwemo pia jirani na Tanzania  huadhimisha siku maalum ya kumbu kumbu ya mauaji yaliyotokea kwenye nchi zao kwa sababu  ya kuichezea amani.
Aliupongeza Uongozi wa taasisi inayosimamia vikundi vya mazoezi Zanzibar         { ZABESA } kwa juhudi zake mbali mbali zinazoendelea kuhamasisha kundi kubwa la watu hasa Vijana kujiunga na vikundi vya mazoezi.
Alisema mikusanyiko inayojumuisha wanamichezo hao mara nyingi huleta Umoja na upendo miongoni mwao na hatimae kuchangia kuondoa kwa makundi katika maisha yao ya kawaida.
Mapema katika Risala yao iliyosomwa na Mohd Ahmad wenyeji wa hafla hiyo Kikundi cha Island Exercise Group walisema kikundi chao kimelenga kuwakusanya wanamichezo tofauti hasa vijana katika harakati hizo.
Walisema vijana wengi ambao ndio wanaounda kundi kubwa katika jamii hujiingiza katika vitendo viovu vinavyosababisha kupata maradhi na hatimae kupoteza nguvu kazi  inayotegemewa na taifa.
Wana kikundi hao wa Island Exercise Group pia walieleza changamoto wanazopambana nazo ikiwa ni pamoja na ukosefu wa maeneo maalum ya kufanyia shughuili zao pamoja na sehemu za mazoezi.
Akimkaribisha mgeni rasmi katika hafla hiyo Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Said Ali Mbarouk alisema Wizara hiyo tayari imeshaliagiza shirika la Utangazi Zanzibar { ZBC } kuanzisha vipindi maalum vya mazoezi kutokana na umuhimu wake.
Waziri Mbarouk alisema hatua hizo itasaidia kuipa fursa Jamii majumbani kufuatilia vipindi hivyo kwa vile utafiti unaonyesha kwamba wengi wa wananchi hao wanakosa  muda wa kufanya mazoezi ya viungo.
Hafla hiyo ya kutimia mwaka mmoja tokea kuanzishwa kwa kikundi cha mazoezi cha Island Exercise Group iliyoongozwa na Brass Bendi ya Chuo cha Mafunzo Zanzibar na kupambwa na ngoma maarufu ya kibati ilijumuisha pia mchango wa papo kwa papo uliolenga kutunisha mfuko wa Kikundi hicho.
Zaidi ya shilingi milioni 2.8 zimeahidiwa kutolewa  kutoka kwa viongozi, maafisa pamoja na wana vikundi mbali mbali katika kusaidia kikundi hicho cha Island Exercise Group kinachoongozwa na Mwenyekiti wake Brigedia General Sharif Sheikh Othman. Balozi Seif naye aliahidi kuchangia shilingi Milioni 1,000,000/-.
Vikundi vipatavyo 39 kati ya 40 vya Mkoa Mjini Magharibi vilialikwa katika hafla hiyo vikiwemo vya Kizimkazi Wilaya ya Kusini,Mpapa na Pagali Wilaya ya Kati pamoja na kikundi maarufu cha Barafu kutoka Mkoani  Dar es salaam.



Viewing all articles
Browse latest Browse all 115264

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>