Ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ukiwa katika picha ya Pamoja, muda mfupi kabla ya Iran, Syria na Korea ya Kaskazini kukaza buti na kukataa kata kata kuunga mkono kupitishwa kwa Taarifa ya Mwisho ya Mkutano wa mwisho wa Mkataba wa Biashara ya Silaha ya Biashara (ATT( , taarifa iliyokuwa na kiambatisho cha Mkataba. Ujumbe huu wa Tanzania ulioongozwa na Naibu Mwakilishi wa Kudumu, Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi na ulishiriki kikamilifu katika mijidala yote iliyofanyika mchana na usiku kuhakikisha kwamba maslahi ya Tanzania yalikuwa yanazingatiwa katika Mkataba huu. Moja ya Hoja kuu ya msingi iliyosimamiwa kidete na ujumbe wa Tanzania katika majadiliano hayo ilikuwa ni kuhakikisha kwamba silaha ndogo na risasi zilikuwa zinaingizwa na kwenye mkataba huo. Juhudi hizo zilifanikisha kuingizwa kwa silaha ndogo na rasasi ingawa Mkataba huo haukupitishwa kama ilivyotarajiwa.
Hizi ni baadhi ya silaha ambazo zinapashwa kudhibitiwa kupitia Mkataba wa Kimataifa wa Kudhibiti Biashara ya Silaha, Mkataba ambao licha ya kusubiriwa kwa hamu kubwa ulishindwa kupatikana mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya Iran, Syria na Korea ya Kaskazini, kutia ngumu na kudai kwamba Mkataba huo ambao Rais wa Mkutano wa mwisho wa Mkataba wa Kudhibiti Biashara ya Silaha ( ATT) Balozi Peter Woolcott kutaka upitishwe kwa kauli moja, haukuwa umezingatia hoja za nchi zao pamona na nchi nyingine na kwamba ulikuwa umekumbatia maslahi ya 'wakubwa' na kwa sababu hiyo walikuwa hawauungi mkono.