Na Mwandishi Maalum, New York
Katika hali ambayo haijawahi kutokea katika Operesheni za Ulinzi wa Amani za Umoja wa Mataifa. Baraza Kuu la Usalama , jana (Ijumaa), kwa kauli moja, limepitisha azimio linaloidhinisha kupelekwa kwa Brigedi mpya ( Intervention Brigade) itakayokuwa na uwezo wa kutumia nguvu pale inapobidi kuyakabili, kuyadhibiti na kupokonya silaha makundi ya wanamgambo yenye silaha katika Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo,
Hii ni mara ya kwanza kwa Baraza Kuu kupitisha Azimo la namna hiyo na kutoa idhini ya utumiaji wa nguvu za ziada katika shughuli za operesheni za ulinzi wa amani ambazo kwa muundo na malengo yake ya asili ni kulinda amani na si kupigana au kutumia nguvu za ziada.
Brigedi hiyo mpya inayokadiriwa kuwa na wanajeshi 3,069 inaundwa na wanajeshi kutoka Tanzania, Afrika ya Kusini na Malawi na inatarajiwa wakati wowote mara baada ya kupitishwa kwa Azimio hili lililopewa namba 2098 (2013) kwenda DRC ambako itaungana na walinzi wengine wa amani waliopo huko chini ya Misheni Maalum ya Kutuliza Amani maarufu kama MONUSCO.
Uwepo wa Brigedi hiyo mpya itaiongezea uwezo MONUSCO kwa kuongeza idadi ya walinzi kufikia 19,815
Makundi ya wanamgambo yanayotarajiwa kudhibitiwa na Brigedi hii maalum na ambayo yamenyoshwa kidole na Azimio hilo, ni pamoja na kundi la M23, Jeshi la Kidemokrasia la Ukombozi wa Rwanda ( FDLR) na makundi mengineyo ambayo yamekuwa yakihatarisha amani na usalama katika eneo la Mashariki ya Kongo.
Kwa lugha nyepesi Baraza Kuu linatoa ruska kupitia Azimio hilo, kwa Brigedi hii maalum, yenyewe kama ilivyo au kwa kushirikiana na Jeshi la Kitaifa la DRC kutumia nguvu kubwa na kwa uhodari wa hali ya juu kuyakabili makundi ya waasi.
Upitishwaji wa Azimio hili na ambalo pia limeungwa mkono na Katibu Mkuu Ban Ki Moon, linafungua ukurasa mpya katika kushughulikia hali tete ya Mashariki wa DRC.Ulishuhudiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Mhe, Rymond Tshibanda N’tugamulongo ambaye pamoja na mambo mengine alilishukuru Baraza kwa kupitish azimio hilo muhimu kwa usalama na amani ya nchi yake na watu wake.
Azimio hilo pamoja na mambo mengine linaainisha wazi kabisa vigezo na mipaka ya uendeshaji na dhamana ya Brigedi hiyo itakayokuwa na batalioni tatu ya askari wa miguu, kikosi cha mizinga na kikosi maalum cha upelelezi itakayokuwa na makao yake makuu katika mji wa Goma. Na kwa ujumla imerejea na wajibu na dhamana wa MONUSCO kwa ujumla.
Kwa mujibu wa Azimio ingawa Brigedi hii inadhama pana na uwajibikaji mkubwa itakuwa ikiwajibika kwa Kamanda Mkuu wa Misheni (Force Commander) ya MONUSCO
Ingawa Azimio hilo ambalo kimsingi liliasisiwa na Ufaransa, limeungwa mkono na wanachama wote 15 wanaounda Baraza wakiwamo P5, hata hivyo kuna baadhi ya nchi ambazo licha ya kuunga mkono zilielezea waziwazi hofu yao juu hasa dhanana kubwa ya matumizi ya nguvu iliyopewa Brigedi.
Hofu ya nchi hizo ni pamoja na kwamba uwepo wa Azimio hilo siyo tu kulikuwa kunatishia madhumuni asilia ya operesheni za ulinzi wa amani lakini pia kuna hatari kubwa kwa walinzi wa amani kutoka nchi zao walioko DRC kujikuta wakilazimika kutumia nguvu na hivyo kuhatarisha maisha yao, jambo ambalo ni kinyume na dhamana ya awali iliyowapeleka huko.
Nchi hizo Guatamala, Pakistani, Argentina na Morocco zilisema kwamba Azimio hilo lilihitaji muda zaidi wa kujadiliwa ili hoja za pande zote ziweze kusikilizwa na kuzingatiwa. Zikatahadharish kwamba uamuzi huu wa kupeleka Brigedi itakayokuwa na uwezo wa kutumia nguvu, usijechukuliwa kama mfano wa kuingwa katika maeneo mengine bali uamzi huu umetokana na mazingira tofauti ya eneo husika.