Bi. Emiliana Aligaesha, Mama Shujaa wa Chakula aliyepata nafasi ya pili kitaifa mwaka jana 2012 chini ya mashindano ya MAISHA PLUS, MAMA SHUJAA WA CHAKULA 2012, amenyakua tunzo ya Mafanikio ya Mwanamke 2013 katika kundi la kilimo.
Mama huyu ambaye ni mkulima kutoka Mkoani Kagera, Wilaya ya Karagwe, Kata ya Kituntu, Kijiji Katembe, Kitongoji cha Nyakabanga ametwaa tunzo hii kutokana na jitihada zake katika kukuza kilimo katika kijiji chake kwa kuwa na mashamba yanayotunzwa kwa kanuni bora za kilimo.
Bi. Aligaesha anasema shamba lake ameweza kulitunza kwa ustadi mkubwa pamoja na umri wa miaka karibu 70 aliyokuwa nayo. Mama huyu ambaye ni mjane kwa sasa, anasema amejitahidi kulima mazao ya migomba na kahawa kwa kufuata ushauri wa kitaalam na kanuni mbalimbali za kilimo.
Tunzo hii imeandaliwa na Tanzania Women Achievement Award (TWAA) ambayo Rais wake ni Bi. Irene Kiwia. TWAA hutoa tunzo hii kila baada ya miaka miwili ili kutambua mchango wa akina mama waliotoa michango yao katika jamii kupitia sekta mbalimbali za kijamii.
Fuatilia habari katika picha katika hafla iliyofanyika leo Serena Hotel, Jijini Dar Es Salaam.
Bi. Emiliana ALigaesha akipokea tunzo yake kutoka kwa waandaji
Mama akitoa shukrani kwa waandaji
Kutoka kulia ni; Bi. Irene John ambaye ni mka mwana wa Bi. Emiliana Aligaesha akifuatiwa na Bi. Irene Kiwia ambaye ni Rais wa TWAA.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt. Marina Njelekela ambaye alipata tunzo ya TWAA mwaka 2011 akimpongeza Bi. Emiliana Aligaesha.
Kutoka kushoto: Dkt. Linda Ezekiel ambaye amepata Tunzo ya Mafanikio 2013 (Sekta ya Afya) aliyetoa mchango mkubwa katika kuanzishwa Kitengo cha Tiba ya Figo na Uchujaji Damu, akifuatiwa na mdau ambaye naye alikuwa miongoni mwa wageni waalikwa.
Mwanamitindo na mmiliki wa blog matata hapa mjini Bi. Shamimu Mwasha akiwa amepozi katika picha na Bi. Emiliana Aligaesha.
Bw. & Bi. Aminiel Aligaesha katika picha ya pamoja na mama yao mpendwa.
WASHINDI WA TUNZO KATIKA PICHA YA PAMOJA