Bomba linalotoa maji katika kisima cha kaloleni na hatimaye kuunganishwa katika mtandao wa maji kwa ajili ya wakazi wa Mabogini,Pasua na Bomambuzi.
Kaimu mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Dk Ibrahim Msengi akiotesha mti katika chanzo cha maji cha kaloleni wakati wa kilele cha maadhimisho ya wiki ya maji iliyofanyika katika kata hiyo.
Mkurugenzi wa manispaa ya Moshi Bernrdette Kianabo akiotesha mti katika chanzo cha maji cha Kaloleni wakati wa kilele cha maadhimisho ya wiki ya maji iliyofanyika katika kata ya Kaloleni.
Mwenyekiti wa bodi ya mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingiara mjini Moshi ,Sharry Raymond akiotesha mti katika chanzo cha maji cha Kaloleni.
Na Dixon Busagaga wa globu ya jamii ,Moshi
HALMASHAURI ya Manispaa ya Moshi imewatoa hofu wakazi wa kata za Kaloleni, Pasua na Mabogini wanaotumia maji kutoka kisima cha Kaloleni kwamba ni salama kwa matumizi ya nyumbani licha ya taarifa kuwa yanaathiriwa na dampo lililopo jirani.
Wakizungumza katika kilele cha wiki ya maji,mkurugenzi wa manispaa,Bernadette Kinabo na kaimu mkurugenzi wa mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira Moshi (MUWSA),Isa Osena wamesema kisima hicho ni kirefu na hupimwa kitaalamu kila mwezi.
Kauli hiyo ilifuatia kitendo cha wananchi wa kata hiyo,kumpokea kwa mabango yenye ujumbe mbalimbali,kaimu mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro,Dk Ibrahim Msengi wakilalamikia usalama wa maji hayo lakini pia kutopata maji licha ya kisima kuwapo kwao.
Mwenyekiti wa mtaa wa Kaloleni,Ndama Bin Ndama,alisema wananchi hawana imani na maji hayo kutokana na majitaka yanayochurizika kutoka katika dampo kuu,lakini pia hawana maji licha ya kuwepo kisima eneo lao huku wakilalamikia maji kupelekwa kata za jirani.
Katika majibu yao,Kinabo na Osena walisema kisima kina urefu wa mita 100 na hupimwa kila mara na dampo likiwa umbali wa zaidi ya mita 60 na limetengenezwa kitaalamu kwa kuwekewa msingi wa saruji inazozuia maji kuelekea katika kisima.
Aidha Kinabo alisema MUWSA imetenga zaidi ya Sh Mil 236 kwa mwaka wa fedha 2013/204 kwa ajili ya kuongeza vyanzo vipya huku manispaa ikitarajia kuzindua mpango wa uoteshaji miti Mil 2 katika vyanzo na makazi kuanzia April 10 hadi 16 mwaka huu.
Awali kaimu mkuu wa mkoa,Dk Msengi akizindua kisima cha Kaloleni kilichoongeza uzalishaji wake kutoka lita za ujazo 71 kwa saa hadi lita 1200 kwa siku na kukarabatiwa kwa Mil 41.2, alitaka wananchi kukilinda na kuotesha miti kwa wingi.
Dk Msengi alisema hakuna sababu ya wananchi kuilaumu MUWSA au manispaa kuhusu upungufu wa maji wakati wao hawajaotesha miti ambapo alielezea mpango wa wilaya kutenga kila jumamosi ya mwezi kwa ajili ya usafi wa mazingira na upandaji miti.