Meya wa Manispaa ya Ilala Mhe. Jerry Silaa akizungumza wakati wa ufunguzi wa kituo cha huduma kwa wateja eneo la Kariakoo mtaa wa msimbazi na Makamba,jijini Dar es salaam leo.
Kampuni ya simu Tanzania (TTCL) imezindua kituo cha huduma kwa wateja eneo la Kariakoo mtaa wa msimbazi na Makamba.
Akiongea wakati wa Uzinduzi huo, Mgeni rasmi ambaye pia ni Meya wa Manispaa ya Ilala Mheshimiwa Jerry Silaa amesema ni faraja kuona TTCL mkifanya huduma hizi za maendeleo hapa Dar es Salaam na kwingineko, kwani hii inazidi kuweka hai matumaini ya Watanzania kwamba kampuni yao hii bado ni imara na ipo mstari wa mbele kuchochea maendeleo ya sekta ya mawasiliano, na sekta nyingine za jamii na uchumi kwa ujumla.
Amesisitiza kuwa jambo la msingi zaidi kwa makampuni ya simu, ni kuongeza kasi ya kusambaza huduma hizi hadi vijijini ambako ndiko wanakoishi wananchi walio wengi.
‘Changamoto inayowakabili TTCL kama mhimili wa sekta hii hapa nchini kuongoza njia na wengine wafuate. Ongezeni juhudi, tuna imani kubwa na TTCL kwamba mnaweza, na tayari tunaona mwelekeo wa mafanikio mazuri kwa siku zijazo, ukizingatia kuwa mwezi huu pia TTCL imesaini mkataba na mfuko wa Mawasiliano (UCSAF) wa kufikisha huduma kwa mteja katika vijiji 103 katika maeneo mbalimbali nchini.’
Naye Afisa Mkuu wa Mauzo na Masoko wa TTCL Bw. Peter Ngota amesema Lengo la kuhamia Mtaa wa Makamba na Msimbazi ni kuwa karibu na wateja wetu, kama wote mnavyojua kauli mbiu yetu ni TTCL HULETA WATU KARIBU, vitendea kazi vimeboreshwa na tunatarajia wateja watapata huduma kwa haraka zaidi.
Aidha amesema, Kutokana na uwezo wa wafanyakazi, wigo wa mtandao na uzoefu wa kutumia mikongo na mikonga ya simu TTCL imekabidhiwa na Serikali ya Tanzania dhamana ya kuendesha, kusimamia na kuendeleza shughuli za Mkongo wa Taifa. Uwepo wa Mkongo wa Taifa uliojengwa na kuunganisha mikoa yote ya Tanzania, umesaidia kuwa na huduma bora zaidi ambapo kwa sasa wananchi tunaweza kupata huduma mbalimbali zikiwemo matibabu kwa njia ya mtandao, elimu kwa njia ya mtandao, biashara kwa njia ya mtandao na Serikali mtandao, Benki – Mtandao, Pesa - mtandao.