WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema Serikali itaitisha kikao cha wadau mbalimbali kutoka taasisi za dini, mashirika yasiyo ya Kiserikali pamoja na vyama vya siasa ili kujadili mustakabali wa Taifa la Tanzania na hasa suala la amani na utulivu.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo jana mchana (Jumatano, Machi 20, 2013) wakati wa mahojiano maalum na kituo cha Redio Vatican kilichopo Vatican City, mjini Roma, Italia.
“Serikali inatarajia kuitisha kikao cha wadau wote kutoka vyama vya siasa, mashirika ya dini, NGOs, ili kutafakari nini kifanyike ambacho kitasaidia kuendeleza amani na utulivu... tutaitisha kikao hiki tarehe 4 Aprili,” alisema Waziri Mkuu wakati akihojiwa na Padri Richard Mjigwa, Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.