Niwazapo nchi yangu, roho yangu husinyaa
Tokea enzi za tangu, mali za kugaa gaa
Lakini kuna ukungu, mnene ulozagaa
Masikini nchi yangu, wapi tunaelekea?
Tumejaliwa na Mungu, kila chenye manufaa
Watu, ardhi na mbingu, kote vimetapakaa
Bado tuko kwenye pingu, pakutokea hadaa
Masikini nchi yangu, wapi tunaelekea?
Tulianza wanguwangu, uhuru kupigania
Tukawan’goa wazungu, ili tubaki huria
Tukayapita machungu, nchi tukashikilia
Masikini nchi yangu, wapi tunaelekea?
Tukalikamata rungu, dola kuishikilia
Wakatupisha vipungu, nchi wakatuachia
Na ndipo kizunguzungu, kikaanza kutitia
Masikini nchi yangu, wapi tunaelekea?
Sera za kinyungunyungu zikaanza kutokea
Tukataifisha vyungu, kupika hatujajua
Uchumi ukawa gungu, ngoma ya kizazaa
Masikini nchi yangu, wapi tunaelekea?
Tukaanzisha ukungu, elimu kuihadaa
Tukakiacha kizungu, kama lugha fundishia
Kiswahili kawa dungu, bila ya kukiandaa
Masikini nchi yangu, wapi tunaelekea?
Elimu kawa Kurungu, aliyepotea njia
Tukaunda Kiswazungu, lugha ya kupotezea
Elimu mwogo mchungu, usomapo Tanzania
Masikini nchi yangu, wapi tunaelekea?
Na Shafi Kaluta Abedi