Wakurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI’s) kutoka Umoja wa Wakuu wa Polisi Kusini mwa Afrika (SARPCCO) wanatarajia kuanza mkutano wa siku mbili jijini Dar Es Salaam kuanzia tarehe 18-19 mwezi machi mwaka huu chini ya uenyekiti wa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Tanzania.
Mkutano huo wa siku mbili utafunguliwa tarehe 18/03/2013 na Mwenyekiti wa sasa wa SARPCCO ambaye ni Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania IGP Said Mwema na kufungwa tarehe 19/03/2013 na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Tanzania.
Katika mkutano huo mambo mbalimbali yatajadiliwa ikiwemo jinsi ya kukabiliana na uhalifu unaovuka mipaka kwa kufanya operesheni za pamoja na ushirikiano baina ya SARPCCO na umoja wa Wakuu wa Polisi wa nchi za Afrika Mashariki (EAPCCO).
Vilevile, mkutano huo utajadili utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa na wakuu wa Polisi wa SARPCCO katika mkutano uliofanyika Zanzibar mwezi Septemba mwaka 2012.
Mkutano huo pia utaambatana na vikao vya Kamati Tendaji za SARPCCO ambazo zinajumuisha wajumbe kutoka nchi wanachama katika nyanja za Sheria, Mafunzo na kamati tendaji inayoshugulikia mambo ya wanawake na jinsia ambazo zitajadiliana ili kutoka na maazimio ambayo yatapelekwa katika mkutano wa Wakuu wa Polisi wa SARPCCO mwezi Mei mwaka huu.
Aidha, suala la michezo baina ya majeshi ya Polisi kwa umoja wa SARPCCO nalo litajadiliwa katika mkutano huo.
Imetolewa na.
Advera Senso-ASP
Msemaji wa Jeshi la Polisi (TZ).