Mhe. Jaji Engera Mmari Kileo, akizungumzia uzoefu wa Majaji Wanawake wa Tanzania katika kukabiliana na tatizo la matumizi mabaya ya mamlaka kudhalilisha kijinsia na kushawishi rushwa ya mapenzi ( sextortion) wakati Chama cha Majaji Wanawake- Tawi la Tanzania kilipoanda mkutano wa pembezoni ( side-event) sambamba na mkutano unaoendelea wa 57 wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu Hadhi ya Wanawake ( CSW). aliyekaa kati kati ya Jaji Kileo, na Naibu Mwakilishi wa Kudumu Balozi Ramadhan Mwinyi ni, Bw. John Hendra aliyewahi kuwa Mratibu wa UNDP nchini Tanzania, Bw. Hendra ndiye aliyekuwa mwendashaji wa mkutano huo, bado anakumbuka vizuri kiswahili, kwa sasa ni Katibu Mkuu Msaidizi na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Sera na Mipango katika Taasisi ya UN- Women
Bi. Anne T. Goldstein, Esg; Kutoka Chama cha Kimataifa cha Majaji Wanawake akizungumza wakati wa mkutano huo, Chama cha Kimataifa cha Majaji wanawake, kinafanya kazi kwa karibu na Chama cha Majaji Wanawake- Tawi la Tanzania, na ndiyo chimbuko la neno Sextortion. katika mchango wake licha ya kueleza kwa mapana udhalilishaji wa kijinsia na rushwa ya mapenzi, alihimiza sana umuhimu wa wazazi kuzungumza na watoto wao wote wa kike na wakiume kuhusu madhara ya ukatili huo na namna ya kukabiliana nao.
wajumbe wanaoshiriki mkutano wa 57 wa CSW wakijumuika na washiriki wengine kujifunza nini Chama cha Majaji kinafanya katika ajenda zima ya kupiga vita udhalilishaji wa wanawake na watoto wa kike
Mshiriki ambaye alijitambulisha kwamba ni askari Polisi kutoka nchini Zambia akiuliza swali
wajumbe kutoka Tanzania wanaoshiriki mkutano wa 57 wa CSW wakijumuika na washiriki wengine kujifunza nini Chama cha Majaji kinafanya katika ajenda zima ya kupiga vita udhalilishaji wa wanawake na watoto wa kike.
Na Mwandishi Maalum
Mwenyekiti wa Chama cha Majaji Wanawake Tawi la Tanzania, Mhe. Jaji Engera Mmari Kileo ameeleza kwamba jamii ikishirikiana inaweza kwa kauli moja kupiga vita udhalilishaji wa kijinsia na rushwa ya mapenzi.
Jaji Kileo ametoa kauli hiyo siku ya jumanne, wakati chama hicho cha majaji kilipoanda mkutano wa pembezoni ( Side event) sambamba na Mkutano wa 57 wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu hadhi ya mwanamke ( CSW) unaoendelea hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa,
Chama hicho cha Majaji, kiliandaa mkutano huo ikiwa ni mara ya kwanza kuendesha mkutano wa aina hiyo ndani ya viunga vya Umoja wa Mataifa, kwa lengo la kuelimisha, kufahamishana, kupashana na kubadilishana mawazo na wajumbe wengine, kuhusu matumizi mabaya ya mamlaka kwa lengo la kudhalilisha kijinsia na kushawishi rushwa ya mapenzi ( Sextortion).
Bw. John Hendra ambaye aliwahi kufanya kazi nchini Tanzania kama Mratibu wa UNDP ndiye aliyekuwa mwendeshaji wa mkutano huo uliovutia wajumbe wengi waliokuwa na hamu ya kujielimisha kuhusu sextortion. Hendra kwa sasa ni Katibu Mkuu Msaidizi na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Será na Mipango katika Taasisi ya UN-WOMEN
“ Unyanyasaji wa kijinsia na rushwa ya mapenzi ni mambo yanayotokea katika jamii yetu, yanatokea vyuoni, mashuleni, majumbani, maofisini na hata mitaani. vitendo hivi siyo tu kwamba ni kosa la jinai , bali pia ni ukiukwaji wa haki za binadamu” akasema Mhe. Jaji Engera Kileo ambaye alikuwa mmoja wa wasemaji wakuu katika mkutano huo.
Na kwa sababu hiyo na kwa kulitambua tatizo hilo, akasema,Tanzania kupitia Chama cha Majaji Wanawake, imekuwa ikitekeleza mikakati mbalimbali ikiwamo ya kuwaelimisha wanawake na watoto wa kike katika taasisi za elimu ya juu, mashuleni na katika maeneo mengine kuutambua na kutoufumbia macho ukatili huo.
Aidha amefafanua kwamba, udhalilishaji wa kijinsia na rushwa ya ngono, si tatizo linalowakumba wanawake na watoto wakike pekee , bali hata watoto wa kiume wamekuwa wahanga wa janga hilo.
Mhe. Jaji Kileo amesema hivi sasa kumekuwa na mwamko mkubwa wa kulitambua tatizo hilo, ingawa amekiri kwamba bado safari ni ndefu na changamoto nyingi.
Akazitaja baadhi changamoto hizo ni ufinyu wa raslimali ili kuwafikia walengwa wengi zaidi, kutokuwapo kwa utashi wa wahanga kujitokeza na kutafuta haki yao, uwezeshaji wa wakufunzi pamoja na uwezeshaji wa kiuchumi kwa wanawake na watoto wa kike.
Katika utoaji elimu hiyo wa suala zima la sextortion, Mzungumzaji mwingine alikuwa ni Bi. Anne Goldstein, Esq ambaye ni Mkurugenzi wa Elimu ya Haki za Binadamu, katika Chama cha Kimataifa cha Majaji wanawake.
Akitoa ufafanuzi kuhusu udhalilishaji wa kijinsia na rushwa ya mapenzi, Anne,alisema tatizo hilo haliko katika nchi zinazoendelea peke yake bali lipo duniani kote.
Akasema ni tatizo kubwa, sugu na lenye sura nyingi na kwamba kulikabili kunataka nguvu za pamoja na ushiriki wa wadau wengi.
Lakini akasema ni tatizo linaloweza kutafutiwa ufumbuzi ikiwa tu wadau wote wataonyesha utashi wa kufanya hivyo.
Akahimiza sana suala la wazazi kukaa na watoto wao wa kike na kiume na kuelezana kinabaubaga kuhusu madhara ya udhalilishaji wa kijinsia na rushwa ya ngono ikiwa ni pamoja na kuwajengea mazingira ya kuwa huru kueleza pale wanapohisi kutaka kufanyiwa ukatili huo.
Akasema chama cha Kimataifa cha Majaji Wanawake, kimekuwa kikifanya kazi kwa karibu sana na Chama cha Majaji Wanawake – Tawi la Tanzania, na kwamba wanajivunia uhusiano na ushirikiano huo na kitaendelea kufanya kazi kwa karibu na Majaji watanzania.
Naye Katibu Mkuu Msaidizi, Bw. John Hendra, yeyé pamoja na kuwapongeza Chama cha Majaji Wanawake kwa kazi nzuri, kwa ujumla aliipongeza Serikali na watanzania wote, kwa kukubali na kutambua kwamba kuna tatizo hilo la udhalilishaji wa kijinsia na rushwa ya ngono na hivyo kuamua kulikabili.
Akasema UN- Women itaendelea kufanya kazi kwa karibu na Tanzania katika maeneo mbalimbali.