Mhe. Tuvako Manongi, Balozi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, akizungumza wakati wa uwasilishwaji wa Taarifa ya Katibu Mkuu, kuhusu maendeleo ya maandalizi ya Ujenzi wa Majengo ya Kimataifa Tawi la Arusha yatakayotumika kushughulikia umalizaji wa mashauri ya Masalia ya iliyokuwa Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda ( ICTR) pamoja na utunzaji wa nyaraka na kumbukumbu za mahakama hiyo.
Majengo hayo yatajengwa katika eneo la Laki Laki Jijini Arusha, ujenzi wake unagharamiwa na Umoja wa Mataifa ambapo makadirio yanaonyesha yatagharimu dola za Kimarekani 8.79 milioni. Tayari dola za kimarekani 3 milioni za kuanzia zimekwisha kutengwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Akiwasilisha taarifa hiyo mbele ya wajumbe wa Kamati ya Tano, Mkurugenzi wa Idara ya Mipango na Bajeti ya UN, Bw. Johannes Huisman ameishuruku Tanzania kwa kutoa eneo hilo la Laki Laki.Akizungumza baada ya kuwasilisha wa taarifa hiyo, Balozi Manongi alisisitiza kwamba Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejizatiti katika kutoa ushirikiano na kuunga mkono kazi ya utekelezaji wa mradi huo muhimu ili uweze kukamilika kwa wakati. Na kusisitiza kwamba jambo la muhimu ni kwa pande hizo mbili yaani Tanzania na Umoja wa Mataifa kuhakikisha kwamba zinashirikiana na kuwasiliana kwa karibu katika kila hatua ya utekelezaji wa mradi huo