ZIKIWA zimebaki siku mbili baada ya Serikali kulitaka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), hadi Jumatatu Machi 11 kutangaza kutekeleza maelekezo waliyowapa, Rais wa Shirikisho hilo Leodegar Tenga ameomba kuonana tena na Waziri mwenye dhamana ya Michezo Dk. Fenela Mukagara ili kuzungumzia upya suala hilo na sasa watakutana March 19.
March 2 Rais Tenga alitangaza kukutana na Waziri Mukangara jana Alhamasi March 7 kwa lengo la kuzungumza naye kuwa maagizo ya kuikataa katiba yao na kutaka kufanya uchaguzi kwa kutumia katiba ya mwaka 2006 hayatekelezeki na kwamba wanaomshauri Waziri huyo mwenye dhamana ya michezo wanamshauri vibaya na hawaijui katiba ya TFF.
"Kamati ya utendaji haitaki hata kidogo kubishana na Waziri, tunaamini wakati anatoa maagizo yake hakujua ugumu na madhara yake na waliomshauri hawakumshauri vizuri.....:"Tunaomba kukutana naye tumueleze ajue kabisa agizo alilolitoa alitekelezeki na tutamshauri madhara yake kwa serikali kuingilia TFF madhara yake ni kufungiwa." alikaririwa akisema Tenga mapema wiki iliyopita.
Hata hivyo Waziri Mukangara aliwaita viongozi wa TFF wakiongozwa na Katibu mkuu Angetile Osiah Jumanne wiki hii na maagizo waliyopewa viongozi hao wa TFF ni kuhakikisha hadi kesho kutwa Jumatatu TFF itangaze kutekeleza maagizo waliyopewa na serikali ikiwemo kuitisha mkutano wa marekebisho ya katiba ndani ya siku 40 kuanzia Juzi na wahakikishe wamefanya marekebisho hayo hadi ifikapo Aprili 15.
Pia serikali iliwataka TFF kuhakikisha inaanza upya mchakato wa uchaguzi na hadi Mei 25 uchaguzi huo uwe umefanyika kwa kutumia katiba ya mwaka 2006 ikiwemo na marekebisho yote hadi ya mwaka 2010.
Hata hivyo, Katibu mkuu wa TFF Angetile Osiah leo aliwambia waandishi wa habari kuwa, Tenga ambaye alikuwa nje ya nchi amerejea juzi na kwamba tayari amewasiliana na Waziri Mukangara na kumuomba asitishe maamuzi yote ambayo ameshayatoa na anayotarajia kuyafanya.
"Katika barua pepe ambayo amemuandikia Waziri ambaye kwa sasa yuko nje ya nchi, Rais Tenga ameeleza kuwa alikwenda ofisini kwake tarehe 7 March kujaribu kumuona lakini akaambiwa amesafiri, hivyo kuomba kukutana na Katibu Mkuu wa Wizara, ambaye pia hakuwepo ofisini na hatimaye akakutana na Naibu Katibu Mkuu.
" Katika barua hiyo pepe, Rais Tenga amemshukuru Waziri kwa kuonana na ujumbe wa TFF juzi March 6 na kukubali kukutana naye tena March 19 kwa ajili ya mazungumzo juu ya maagizo yake pia kumuarifu amepokea maagizo yake aliyoyatoa kupitia kwa mjumbe wetu wa kamati ya utendaji kwa njia ya barua.
"Kwa heshima na taadhima, kukuomba usitishe hatua yoyote ile unayodhamiria kuchukua hadi hapo tutakapokutana na kupata maelezo yetu, TFF, juu ya maamuzi na maagizo uliyoyatoa.” alisema Angetile akinukuu waraka wa Tenga.
Tenga, ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu la Afrika (CAF) aliondoka jana (Machi 7 mwaka huu) kwenda Marrakech, Morocco kuhudhuria kikao cha kamati hiyo na pia Mkutano Mkuu wa CAF ambao umepangwa kufanyika Machi 10 mwaka huu ukihusisha pia ajenda ya uchaguzi wa rais.