Mheshimiwa Mathias Chikawe (Mb), Waziri wa Katiba na Sheria leo amefungua Mkutano wa Jukwaa la Tume za Uchaguzi za Nchi za SADC unaokutana Dar salaam kwa siku Mbili.
Jukwaa hilo linajumuisha Tume za Uchaguzi kutoka nchi za Tanzania, Zambia, Botswana, Swaziland, Madagascar, Angola, DRC, Lesotho, Malawi, Mauritius, Mozambique, Seychelles, Zanzibar na Zimbabwe. Jukwaa hilo lilianzishwa mwaka 1998 kwa lengo ya kuleta chachu ya mabadiliko katika nchi za SADC kwenye masuala ya uchaguzi. Jukwaa linahimiza uanzishwaji wa Tume huru za Uchaguzi, umuhimu wa kuweka mazingira stahiki ya kisheria na kitaasisi ili kuziwezesha Tume za Uchaguzi kufanya kazi za kusimamia uchaguzi kwa ufanisi.
Mhe Chikawe pamoja na mambo mengine amezitaka Tume za Uchaguzi zilizo katika Jukwaa hilo kuimarisha ushirikiano wao kwa lengo la kuboresha chaguzi Barani Africa ili chaguzi hizo ziwe kichocheo cha maendeleo na sio chanzo cha vurugu na vita. Mhe. Chikawe amesema kwa kupitia Jukwaa hilo, Tume za Uchaguzi zitaweza kutatua changamoto mbalimbali zilizopo za kisheria, kimuundo, kitaalamu na kifedha zinazozikabili Tume nyingi barani Africa ili kuhakikisha nchi za SADC zinakuwa na chaguzi huru na za haki
Wajumbe wa Jukwaa la Tume za Uchaguzi za Nchi zaq SADC wakimsikiliza Mhe Chikawe wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo.
Wajumbe wa Jukwaa la Tume za Uchaguzi za Nchi za SADC wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya ufunguzi wa Mkutano huo.
Mhe Chikawe (katikati) akibadilishana mawazo na Mhe. Jaji (Mst) Damian Lubuva, (kushoto) ambaye ni Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Mwenyekiti wa Kamati Tendaji ya Jukwaa hilo na Bw. Julius Malaba (Kulia) Mkurugenzi wa Uchaguzi Nchini.