Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar akihutubia kwenye Maulid Mjini Kiuyu
Makamu wa Kwanza akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Wete, Omar Khamis Othman Mjini Kiuyu
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema kuwa watu wenye nia mbaya wameamua kuyatumia matukio ya kuuawa na kujeruhiwa kwa viongozi wa kidini ili kuvunja umoja wa Wazanzibari.
Alisema hivi sasa Wazanzibari ni wamoja na watu hao wenye nia mbaya wanayachukulia matukio hayo kwa kutaka kuwagawa na kuwaletea mtafaruku kwa kuonyesha kuwa kuna tofauti za kidini Zanzibar wakati sio kweli.
Maalim Seif alisema hayo juzi usiku alipokuwa akihutubia katika hafla ya Maulid ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W), Mjini Kiuyu, Wilaya ya Wete, Kaskazini Pemba.
Alisema inasikitisha kuona wapo baadhi ya viongozi wenye nia chafu dhidi ya Zanzibar wenye tabia ya kutoa kauli za kujenga chuki na fitna miongoni mwa Wazanzibari chini ya kivuli cha matukio hayo.
“Ni jambo la kusikitisha kuna watu wenye nia chafu dhidi ya Zanzibar, ambao wameamua kuyatumia matukio haya kujenga chuki miongoni mwa Wazanzibari wenyewe kwa wenyewe,” alionya Maalim Seif.
Makamu wa Kwanza wa Rais alisema kinachoonekana kuna ajenda imetayarishwa ya kutaka kulazimisha chuki za kidini Zanzibar, licha ya kuwa Zanzibar ina historia ya miaka mingi ya watu kuvumiliana na kuishi kwa pamoja, pamoja na kuwepo watu wa imani tafauti.
Aliwataka wananchi wote wa Zanzibar hivi sasa wawe macho na ajenda zinazolengwa kuwavuruga na waendelee kuishi kwa mshikamano na umoja kama ambavyo wamekuwa wakiishi.
Maalim Seif alisema vitendo vya kuuawa na kujeruhiwa viongozi wa kidini Zanzibar ni mambo mageni na kwa miaka mingi Zanzibar imekuwa ni mfano bora wa uvumilivu wa kiitikadi za kidini, licha ya kuwa asilimia 98 ya wananchi wake ni Waislamu.
Alieleza kwamba wingi wa Waislamu Zanzibar haukuifanya ifunge milango kwa watu wa imani zingine na kwa wakati wote wamekuwa wakiabudu kwa mujibu wa imani zao bila ya bugudha yoyote.
Makamu wa Kwanza wa Rais alisema Katiba ya Zanzibar imeweka wazi haki ya mtu kuabudu kwa mujibu wa imani yake na uhuru wa mtu kuabudu umelindwa.
“Ni Sultani wa Zanzibar ambaye alikuwa Muislamu ndiye aliyetoa ardhi kwa Wakiristo kujenga Kanisa. Juzi nilipokwenda kutoa salamu za rambi rambi kwa Baba Askofu Shayo, baada ya kifo cha Padri Mushi, aliweka bayana kuwa lililotokea lisihusihwe na tafauti za kidini,” alisema Maalim Seif
Hata hivyo, Maalim Seif alisema inasikitisha kuona wakati Rais Jakaya Kikwete katoa maelekezo uchunguzi wa kina ufanyike na Kamishna wa Polisi Zanzibar ameshaweka wazi kuwa uchunguzi unaendelea, baadhi ya viongozi na magazeti ya Tanzania Bara yanachochea chuki za kidini na kusema kuwa Zanzibar kuna ugaidi.
Alisema hali hiyo inaonesha kuwa kuna ajenda imetayarishwa kutaka kulazimisha chuki za kidini Zanzibar, kwa sababu huko Tanzania Bara kumetokea matukio mabaya zaidi, lakini hayajahusishwa na ugaidi.
Alitoa mfano matukio ya kuuawa kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza na kuchinjwa kwa Padri huko Geita, kuwa ni mabaya kabisa, lakini hakuna hata chombo cha habari kimoja kilichohusisha matukio hayo na ugaidi.
“Nasema Zanzibar hakuna ugaidi, hakuna ugomvi wa kidini. Yanayotokea yametusikitisha sana, ni matokeo ya uhalifu wa kupindukia, linaloweza kufanywa lifanywe kuwanasa wahalifu hawa na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sharia,” alisema Makamu wa Kwanza wa Rais.
Aliwataka wananchi wote wa Zanzibar kwa wakati huu kuwa watulivu na wasitawaliwe na jazba na wala wasichokozane, pia wasikubali kuchokozeka.
Akizungumzia matokeo ya mtihani wa kidato cha nne yaliyotolewa hivi karibuni, Makamu wa wa Kwanza wa Rais alisema ni matokeo mabaya na ya kuliza, kwa sababu hayaoneshi mustakabali mwema kwa watoto wetu na nchi yetu hapo baadaye.
Alisema ni wakati muafaka Serikali, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, walimu na jamii nzima kujiuliza nini sababu ya matokeo hayo mabaya, na kujiuliza pia nchi inaelekea wapi?
Maalim Seif alisema sasa si wakati tena wa kutupiana lawama, lazima pande zote zikae zijadili wapi pamekosewa, ili ufumbuzi uweze kupatikana na hali kama hiyo isitokee tena siku zijazo.
Katika salamu za wananchi wa Kiuyu kwenye Maulid hayo yaliyojumuisha waumini kutoka maeneo mbali mbali ya Pemba, Unguja na Dar es Salaam walisema miongoni mwa malengo yao ni kuona umoja wa wananchi wote unaimarika.