Mkuu wa mkoa wa Tanga Mhe. Chiku Gallawa akiwasisitiza viongozi wa dini kuwakumbusha waumini wao kudumisha amani na ushirikiano wa kindugu kwa wote bila kujali itikadi za kidini .
Baadhi ya viongozi wa dini waliofika wakisikiliza kwa makini hoja za mkutano.
Mhe. Gallawa akijibu hoja za wajumbe
Mmoja wa viongozi wa Dini akitoa maoni yake juu ya nini kifanyike ili kudumisha amani mkoani Tanga na taifa kwa ujumla.
Mmoja wa viongozi wa dini akitoa mapendekezo yake juu ya nini kifanyike ili kudumisha amani.
Mkuu wa mkoa Tanga Mh. Chiku Gallawa amekutana na viongozi wa dini mbalimbali leo tarehe 21/02/2013 mjini Tanga kwa lengo la kusisitizia umuhimu wa kuwakumbusha waumini na wafuasi wa dini zao kudumisha amani na kuachana na dhana ya ubaguzi wa kidini. Mazungumzo hayo yamefanyika ikiwa ni pamoja na kutaka kufahamu ni nini hasa wananchi wanahitaji serikali ikifanyike ili amani izidi kujengeka .
Akisisitiza hoja yake, Mhe. Gallawa amesema kuwa si muda muafaka kwa wananchi kuendelea kuilaumu serikali juu ya yale ambayo yanatokea bali wote kwa pamoja lengo liwe ni kuwajibika kwani serikali ni watu na watu wenyewe ni wananchi wote.
” Umefika wakati wa sisi wananchi kuelewa kuwa kila mwananchi katika mkoa wake ana wajibu wa kufanya katika kudumisha amani, si jambo la busara kukaa pembeni na kuisonda serikali kidole bali kushirikiana kwa pamoja kwa umoja wa kindugu kwa faida ya mkoa na taifa letu kwa ujumla. Wote tujifunze tuvumiliana na kuchukuliana kila mmoja na mapungufu yake”
Aidha wakitoa maoni yao juu ya nini serikali ifanye katika suala zima la amani, viongozi wa dini wamesema kuwa serikali haina budi kuchukua jukumu la kuielimisha jamii maana halisi ya amani na umuhimu wake kwa taifa. Pia wamewaasa wananchi kuwa na nia ya kweli na kurudi kwenye maadili mema.
Kwa upande mwingine serikali imeshauriwa kufanya uchunguzi wa kina kubaini kikundi chochote ambacho kinaonekekana kuwa chanzo cha uchochezi wa vurugu na kukichukulia hatua kali. Hali hii itaondoa wasiwasi na woga mkubwa ambao umetanda miongoni mwa wananchi na viongozi wa dini kwa ujumla.
Vilevile viongozi wa dini wamevikumbusha vyombo vya habari kutokuwa chanzo cha kuchochea vurugu kwa kutoa taarifa zinazoamsha hisia za chuki miongoni mwa waumini wenye imani tofauti badala yake kuwa ni vyanzo vizuri ya kudumisha amani.