Leo, mwanahabari na mwanaharakati maarufu Amy Goodman amehutubia chuoni Carleton hapa Northfield. Mada yake ilihusu "threats to freedom of the press and the importance of independent media," yaani mambo yanayotishia uhuru wa vyombo vya habari na umuhimu wa media zisizo chini ya mamlaka yoyote. Ninaamini tafsiri yangu inaweza kuboreshwa. Amy Goodman ni maarufu kama mwendesha kipindi kiitwacho Democracy Now!, ambacho kinachambua masuala kwa mtazamo tofauti na ule wa watawala wakandamizi na propaganda zao za kurubuni watu na kuhalalisha hali iliyopo. Mtazamo wa Amy Goodman ni wa kichochezi kwa maslahi ya walalahoi, wavuja jasho, na wale wanaoonewa na kudhulumiwa. Ni mwana harakati ambaye hasiti kujitosa sehemu ambapo watu wanadhulumiwa ili kuwaunga mkono na kuwezesha sauti zao kusikika ulimwenguni. ![]() Baada ya hotuba yake, Amy alisaini nakala za kitabu chake, Democracy Now: Twenty Years of Covering the Movements Changing America. Wakati ananisainia, aliniuliza ninatoka wapi. Nilipomtajia Tanzania, alitabasamu, akasema "Julius Nyerere." Niliguswa, ingawa sikushangaa, kuwa Amy ni mmoja wa watu wa ughaibuni wanaomwenzi Mwalimu Nyerere. |
↧
Mwanahabari Amy Goodman Amehutubia Hapa Kwetu - Profesa Mbele
↧