Na Mwandishi Maalum , New York
Maspika wa Mabunge kutoka mataifa mbalimbali duniani, wamemaliza mkutano wao wa Nne kwa kupitisha tamko ambalo pamoja na mambo mengine, linayataka Mabunge kuhakikisha yanasimamia na kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa Malengo na Ajenda Mpya za Maendeleo Endelevu ( Ajenda 2030).
Akihitimisha mkutano huo wa Maspika ambao hufanyika kila baada ya Miaka mitano, Rais wa Chama cha Kimataifa cha Mabunge ( IPU) Saber Chowdhur amesema, Maspika na wabunge wanawajibu wa kuhakikisha Serikali zao zinatenga bajeti za kutosha ambazo kwayo zitahakikisha utekelezaji wa malengo na ajenda mpya ya maendeleo endelevu.
Ajenda 2030 inayochukua nafasi ya Malengo ya Maendeleo ya Millenia ( MDGs) itapitishwa rasmi na Viongozi Wakuu wa Nchi na Serikali katika mkutano wao wa kihistoria na wa Kilele utakaofanyika kuanzia tarehe 25 hadi 26 mwezi huu wa Septemba.
Miongoni mwa mambo ambayo mabunge yanatakiwa kusimamia ili kuhakikisha kwamba malengo na ajenda hizo mpya yanatekelezwa kikamilifu pasipo kumwacha yeyote nyuma ni pamoja na kuhakikisha uboreshwaji wa vyanzo vya mapato ya ndani pamoja na kuziba mianya ya ukwepaji wa kodi. Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Ann Makinda ndiye aliyeongeza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huu muhimu na wa aina yake na ambao umefanyika ikiwa ni wiki chake kabla ya Wakuu wa Nchi na Serikali kukutana kwa mikutano muhimu na inayotarajiwa kuzungumzia mstakabali wa maendelele na ustawi wa watu na utunzaji wa mazingira.
“ Maspika wa Mabunge ambao tumekutana hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, tumepokea kwa kauli moja, Malengo na Ajenda mpya za Maendeleo Endelevu ambayo wakuu wa nchi na serikali watapisha wiki chache zijazo.
"Kama wawakilishi wa wananchi na wasimamizi wa Mabunge tunawajibu wa kuhakikisha kwamba, tunakuwa mstari wa mbele katika siyo tu, kuhakikisha tunapitisha mipango na sera za utekelezaji wa malengo na ajenda hii mpya, bali pia kusimamia ukusanyaji wa mapato ya ndani na kuziba mianya ya ukwepaji kodi” amesema Rais wa IPU Bwa. Chowdhury.
Maspika wa Mabunge kutoka mataifa mbalimbali duniani wakiwa katika picha ya pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Maspika hao wamepitisha tamko ambalo linatambua na kupokea malengo na ajenda mpya za maendeleo endelevu, na kuyataka mabunge kuhakikisha utekelezaji malengo hayo yanayochukua nafasi ya MDGs. Mhe Ann Makinda ni wa tatu kutoka kushoto mstari wa mbele.
Mhe. Spika akiwa na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania Katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi, wakati alipofika katika Ofisi za Uwakilishi na kisha kuzungumza na Maafisa. Mhe. Spika ameeleza kuwa moja ya mambo atakayoshauri ni pamoja na kutaka Maafisa wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwa na fursa ya kuja katika Umoja wa Mataifa kujifunza na kujijengea uwezo kuhusu mijadala ya kimataifa inavyofanyika na kufikiwa uamuzi katika Umoja wa Mataifa. Akasema anaamini kabisa kwamba kuna mambo ambayo wanaweza kujifunza.