Katibu Mkuu wa Yanga wa zamani, George Johnson Mpondela ‘Castor’ (kulia) enzi za uhai wake akiwa katika moja ya mikutano ya klabu hiyo. Kushoto ni mmoja wa wazee maarufu wa klabu hiyo Mzee Yusuf Mzimba. |
Na Mahmoud Zubeiry
Katibu Mkuu wa Yanga SC wa zamani, George Johnson Mpondela ‘Castor’ amefariki dunia jana saa nne usiku katika hospitali ya Muhimbili, Dar es Salaam alikokuwa amelazwa kwa matibabu ya moyo.
Mtoto wa marehemu, Hilton Mpondela amemwambia mwandishi wa habari hii leo kwamba, baba yake aliyekuwa pia mwanasiasa na mwanachama wa Chama cha Demokrasia ya Maendeleo (CHADEMA) alikuwa amelazwa hospitalini hapo kwa wiki tatu katika wadi ya wagonjwa wa moyo.
Hilton amesema kwamba baba yake aliyekuwa akiishi eneo la Machava, Kigamboni, Dar es Salaam amekuwa akisumbuliwa na maradhi ya moyo kwa miaka minne sasa. Amesema msiba upo nyumbani kwao, eneo la Karakata, Uwanja wa Ndege karibu na Kanisa Katoliki na kituo kidogo cha Polisi, maarufu Polisi Posti.
Marehemu ameacha mke na watoto tisa, ambao ni Pius, Robert, Hilton, Kennedy, Joseph, Collin, na wa kike Linda, Jaqcueline na Jennifer.
Hilton amesema mwili wa marehemu utasafirishwa Jumanne kwenda Tabora baada ya kuagwa kuanzia Saa 2:00 asubuhi hospitali ya Muhimbili tayari kwa mazishi yake Jumatano kijiji cha Misha wilaya ya Tabora vijijini.
Marehemu Mpondela alizaliwa kijiji cha Misha, Tabora, Septemba 28 mwaka 1942 na kipindi kirefu cha maisha yake alikuwa mtumishi wa Mamlaka ya Pamba Tanzania.
Alianza kujulikana zaidi Yanga SC miaka ya 1980 alipokuwa Meneja Utawala wa Mamlaka Pamba, makao makuu, Dar es Salaam alipoisiaida klabu hiyo kupata wachezaji nyota wa Pamba SC ya Mwanza kiulaini enzi hizo inatisha katika soka ya Tanzania na kutoa vipaji vingi.
Aliwakuna mno wana Yanga kuwa kuwasaidia kuwapata nyota kama Athumani Juma Chama ‘Jogoo’, Yussuf Ismail Bana, Juma Mhina, David Mwakalebela, Nico Bambaga, Fumo Felician na wengineo.
Haikuwa ajabu mwaka 1993 Mpondela alipochaguliwa kwa kishindo kuwa Katibu Mkuu wa Yanga SC chini ya Mwenyekiti, Dk Jabir Idrisa Katundu.
Hata hivyo, pamoja na mafanikio katika uongozi wake ikiwemo kuiwezesha klabu hiyo kutwaa Kombe la Afrika Mashariki na kati, sasa Kagame mjini Kampala Uganda na ubingwa wa Bara na iliyokuwa Ligi ya Muungano mfululizo, lakini sera zake za kutaka kuifanya klabu hiyo kuwa kampuni zilimuingiza matatizoni.
Mpondela alianza kupingwa na wanachama waliokuwa wakiwaunga mkono wafadhili wa timu hiyo wenye asili ya kiasia enzi hizo, chini ya marehemu Abbas Gulamali na hatImaye akachemsha na kubwaga manyanga Yanga SC.
Alipewa jina Castor alipokuwa Yanga SC kwa kufananishwa na rais wa zamani wa Cuba, Fidel Castor kwa misimamo yake.
Mwaka 1995 Mpondela alistaafu kazi Mamlaka ya Pamba na kwenda kugombea Ubunge wa jimbo la Kindondoni kwa tiketi ya CHADEMA, ambako hata hivyo aliangushwa na mgombea wa CCM, Peter Kabisa jimbo la kinondoni.
Mwaka 2007, Mpondela alirejeshwa Yanga SC na Mwenyekiti wa sasa na mfadhili wa klabu hiyo, Yussuf Manji kuwa Mjumbe wa Baraza la Wazee.
Mungu ampumzishe kwa amani marehemu George Johnson Mpondela - Amin.