|
Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa Wakala wa Mabasi yaendayo haraka (DART), Bi. Asteria Mlambo |
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Watoa huduma wa mradi wa mabasi yaendayo haraka jijini Dar es Salaam watapatikana kwa utaratibu wa kushindanishwa baada ya kutangaza zabuni kwa mujibu wa sheria za nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa Wakala wa Mabasi yaendayo haraka (DART), Bi. Asteria Mlambo alisema kuwa watoa huduma wote watapatikana kwa mujibu wa sheria za manunuzi na kanuni zinazokubalika.
“Mradi huu ni muhimu sana kwa nchi,” alisema, na kuongeza kuwa kama mradi huo ukifanikiwa, wananchi watapata faida nyingi na nzuri.
Bi. Mlambo alisema miji ya Africa inakuwa kwa haraka na kuwa kasi hiyo inahitaji kupanuliwa na kuimarishwa kwa miundombinu na huduma za usafiri.
Akifafanua zaidi, Mkurugenzi huyo alisema kuwa mradi utakapokuwa tayari kuanza, zabuni zitatangazwa ili kupatikana kwa watoa huduma bora.
Alisisitiza kuwa hadi sasa bado hakuna mtoa huduma aliyepatikana kwa kuwa taratibu za kuwapata bado hazijafanyika.
“Ninachoweza kuwataarifu watu ni kuwa tumeshaingia mkataba na kampuni ya REBEL Group itakayotoa huduma za ushauri wa jinsi ya kupata watoa huduma mbalimbali,” alisema.
Kwa upande wake, Mshauri Mkuu wa Ufundi wa Wakala huo, Bw. Dieter Schelling aliuelezea mradi huo kama wa kipekee katika eneo hili la Afrika.
“Kama mradi huu ukifanikiwa basi hata shughuli za biashara zitaimarika,” alisema.
Alisema kuwa shida inayowapata wakaazi wa Dar es Salaam kwa sasa ujenzi unapoendelea ni ya muda tu na kuwa suluhisho la kudumu liko karibu kupatikana.
Hivi karibuni DART iliingia mkataba na kampuni ya washauri itakayofanya kazi ya kupatikana watoa huduma muhimu kwa mradi huo unaotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwaka huu.
Hatua hiyo ilifikiwa baada ya kampuni hiyo ya REBEL Group ya Uholanzi kushinda zabuni na kushindanishwa na kampuni nyingine.
Mradi huu unalenga kupunguza kwa kiwango kikubwa foleni na msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam.
Barabara zinazohusika na awamu hii ni pamoja na kilomita 20.9 kutoka Kimara hadi Kivukoni; barabara ya Msimbazi kutoka Faya hadi Kariakoo-Gerezani na sehemu ya barabara ya Kawawa kuanzia Magomeni hadi Morocco.