MKURUGENZI wa Mashitaka Nchini (DPP), amewasilisha maombi Mahakama Kuu ya Tanzania ya kutaka kutaifisha nyumba saba za mke wa aliyekuwa mmoja wa Wakurugenzi wa Kampuni Superior Financing Solutions Aloycious Gonzaga, Magreth Gonzaga.
Katika maombi hayo namba moja ya mwaka 2019 yanayotarajia kuanza kusikilizwa mbele Jaji Sirilius Matupa, Novemba 26, mwaka 2019 saa tatu asubuhi, DPP, anaomba kutaifisha Plot no.199, Block D, no.121302 iliyopo Tegeta jijini Dar es Salaam, Plot no.200 Block D no.39021 ya Tegeta, Plot No.1378, Block E Tegeta ikiwa namba za hati 41275 na Plot No.176 Block B iliyopo Aman Gomvu ikiwa na hati namba 138598. Nyumba nyingine ni ya Plot No.191, Block B iliyopo Aman Gomvu ikiwa na hati namba No.132797 na No.174 Block B iliyopo Aman Gomvu ikiwa na hati namba 138597.
Awali kabla kuwasilishwa kwa maombi hayo, TAKUKURU ilitangaza kumsaka mwanamke huyo anayedaiwa kumiliki nyumba tatu za kifahari jijini, huku akituhumiwa kutakatisha fedha haramu kinyume cha Kifungu Na. 12(d) na 13(a) cha Sheria ya Utakatishaji Fedha Haramu Na. 12 ya Mwaka 2006.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Diwani Athumani, amesema wanamsaka Magreth kupitia tangazo lililotolewa kwa amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu inayosikiliza shauri la jinai namba 28 la mwaka 2019.
Alidai Magreth ambaye kwa sasa anadaiwa kukimbilia nje ya nchi, anatafutwa na TAKUKURU kwa tuhuma za kutakatisha fedha na kujipatia mali kupitia Kampuni ya Superior Financing Solution Limited (SFS) inayodaiwa kufanya biashara bila kulipa kodi ya serikali. "Wakati uchunguzi unaendelea, mtuhumiwa alitoroka nchini," Athumani alisema.
“Kisheria mtuhumiwa huyo anahesabiwa kama ni mtuhumiwa aliyetoroka. Kutokana na sababu hiyo, Takukuru inapaswa kutangaza kutafutwa kwake kabla ya kutaifisha mali alizojipatia kwa njia ya rushwa," aliongeza.
Aloycious Gonzaga na mwenzake Isaack Kasanga wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 5/2019 katika Mahakama Kuu Kitengo cha Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi 'Mahakama ya Mafisadi'.
Washitakiwa wanakabiliwa na mashitaka 45 ambayo ni kula njama kutenda kosa kosa moja, kughushi 12, kuwasilisha nyaraka za uongo tisa, kushindwa kulipa kodi na utakatishaji fedha mashitaka 30. Inadaiwa kati ya Machi 2, mwaka 2010 na Aprili 26, mwaka 2016 katika maeneo tofauti ndani ya Jiji la Dar es salaam washitakiwa hao walikula njama kwa kugushi,kukwepa kulipa kodi na kutakatisha.