JAFO AZIAGIZA HALMASHAURI NCHINI KUHARAKISHA VIBALI VYA AZAKI, "HAWA NI WADAU WA MAENDELEO"
Charles James, Michuzi TV
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe Selemani Jafo amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kuhakikisha anasimamia zoezi la utoaji wa vibali vya usajili wa Asasi za Kiraia (Azaki) bila kuchelewesha.
Mhe Jafo amesema agizo hilo linakwenda pia kwa Mikoa na Halmashauri zote nchini kuharakisha kutoa vibali kwa Azaki zinazotuma maombi ya usajili ili kwa kuwa Azaki hizo zimekua mstari wa mbele katika kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali kuwaletea wananchi maendeleo.
Agizo hilo limetolewa leo jijini Dodoma wakati Mhe Jafo alipokua akifunga maadhimisho ya wiki ya Azaki yaliyodumu jijini hapa kwa juma zima na kuhudhuriwa na Azaki 500 na Taasisi 100.
Waziri Jafo amezitaka Asasi za kiraia nchini kuwa mabalozi wazuri katika kusemea mambo mema yanayofanywa na Serikali chini ya Rais Dk John Magufuli na kuzitama kusimamia malengo waliyojiwekea.
Mhe Jafo amesema kumekuepo na malalamiko kwenye Ofisi yake kuhusiana na kucheleweshwa kwa usajili wa Asasi hizo pindi wanavyoomba maombi ya usajili na kuwaahidi kuwa hata ikiwabidi kuomba kwenye Ofisi yake yupo tayari kusaini yeye mwenyewe.
Amesema maendeleo mengi yanayofanywa na Serikali hivi sasa kwenye sekta mbalimbali za Afya, Elimu, Miundombinu na Utawala bora yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na ukosoaji uliokua ukitolewa na Azaki hivyo ni vema wakapewa ushirikiano kwani wamekua ni wadau wa maendeleo nchini.
"Nakuagiza Katibu Mkuu wa Ofisi yangu hakikisha vibali vinatolewa bila vikwazo kwa Asasi hizi, ili mradi ina manufaa kwa Taifa na jamii kwa ujumla,na pia iwe na Sera zinazoeleweka katika kuchagiza maendeleo," amesema Jafo.
Amesema maendeleo mengi yanayofanywa na Serikali ya awamu ya tano,yametokana na mchango wa AZAKI wa kuibua changamoto zilizopo katika sekta mbalimbali hapa nchini,hivyo AZAKI zinastahili kupongezwa na kuskilizwa.
"Naomba niwapongeze sana AZAKI mmekuwa mkiibua matatizo yaliyopo sehemu tofauti, kwa mfano Hakielimu na tangazo lao la shule mbovu, yamesaidia serikali imeona na kuwekeza fedha nyingi katika sekta ya elimu kwa ajili ya kuziboresha na kufanya ujenzi.
"Katika sekta ya afya pia,barabara note mmekuwa mkipasemea na hivi sasa serikali inayafanyia kazi yote,na matokeo yanaonekana katika sekta hizo zilivyoimarika," Amesema Waziri Jafo.
Pamoja na hayo pia ameziagiza Asasi hizo za kiraia kuhakikisha wanasaidiana katika kuwezeshana na kurekebishana na sio kusemeana vibaya ili asasi nyingine zife jambo ambalo halikubaliki.
Amezitaka AZAKI hizo kuendelea kusaidia kulinda amani iliyopo kwa kutangaza mambo mema yenye ukweli ndani yake badala ya kutangaza mabaya wanayoyasikia bila kujua ukweli uliopo.
" Ndugu zangu kuna mambo mengi ambayo Rais Magufuli ameyafanya ndani ya kipindi kifupi cha uongozi wake, zaidi ya vituo vya Afya 360 vimejengwa, Hospitali 62 Nchi nzima na mpaka kufikia mwakani tutakua tumekamilisha nyingine 20 tena za kisasa kwa ajili ya kuhudumia wananchi wetu wanyonge.
Kama hiyo haitoshi Rais Magufuli ameamua kusimamia sera ya elimu bure kwa vitendo, Shule karibia zote kongwe zimefanyiwa ukarabati mkubwa na zaidi amekua akitoa elimu bila malipo kuanzia Elimu ya Msingi hadi Kidato cha Nne, kwenye miundombinu ndio usiseme hivi mnataka watanzania tupewe nini zaidi? Niwaombe tuendele kushirikiana, " Amesema Mhe Jafo.
Aidha amezitaka Azaki hizo kutumia Taasisi zao kutoa kuhamasisha wananchi kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 24 mwaka huu ili waweze kuwapata viongozi walio bora wenye kusimamia maslahi ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Katibu Mwenezi wa Chama cha Mapinduzi Humphrey PolePole amesema
AZAKI na Serikali ni kitu kimoja hivyo haina haja ya kuogopana kama kuna suala lolote ambalo linapawa changamoto wasisite kushirikiana katika kukabiliana nalo na kulipatia ufumbuzi.
Nae Mkurugenzi wa Azaki nchini Francis Kiwanga amesema Azaki zipo kwa ajili ya kujenga na sio kubomoa kama baadhi ya watu wanavyofikiria na kuahidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuleta maendeleo.
" Sisi tunaishukuru sana Serikali kwa kuendelea kutusapoti, mmekua na sisi kwa wiki nzima hapa Dodoma, viongozi wa kiserikali, Wabunge na wadau mbalimbali wameungana nasi katika kujadili maslahi mapana ya Taifa letu hasa katika ubia wa maendeleo, tuwaahidi kwamba Azaki itazidisha mapambano ya kuwakomboa watanzania kifikra ili kuweza kufikia lengo Kuu ifikapo 2020," Amesema Kiwanga.