Na: Moshy Kiyungi, Tabora.
Septemba, 2019. Baadhi ya maneno yanayotumika Kimataifa yametokana na lugha zetu za Kiafrika, mfano wa karibu neno IKULU.
Neno hilo limetokana na hadhi ya nyumba ya makazi ya mtawala wa Watemi wa kabila la Wanyamwezi toka mkoa wa Tabora. Ikulu linaonekana kurasimishwa kutumika sehemu zote zilizopo ofisi za makao makuu ya Viongozi wakuu wa nchi.
Nyumba ya rais wa Marekani ‘White House’ inaitwa IKULU ya Marekani nk.
Maneno mengine yalitoholewa toka lugha za Wakoloni, mfano neno ‘Muziki’ ambalo lililetwa hapa nchini na Wajerumani.
Hii ilitokana na bendi zilizokuwa za askari na kuingizwa katika shule ya kwanza ya Serikali ya Tanga, ikiitwa ‘Tanga School’ wakati huo.
Madhehebu mbalimbali ya dini nayo yalichangiza kuingiza muziki na vyombo vya muziki vipya vilivyotoa mchango katika huu muziki.
Neno Kwaya lilitokana na neno la Kiingereza yaani ‘Choir’, nazo zikaanza kushika kasi.
Tofauti na hivi sasa ambapo baadhi ya makabila yanabeza nyimbo na ngoma za utamaduni wao wakidai ati zimepitwa na wakati!
Utakuta siku za sherehe za harusi wakipiga miziki ya taarab, hip hop, taradansi, na sasa hivi wamebuni ‘Singeli’
Mfano wa karibu ni watu wa kabila la Wanyamwezi toka Tabora, miaka hii hawahitaji kuzisikia kitu kinaitwa ngoma za asili za kabila lao Manyanga, Maswezi, Radu ama Ngelo ambazo zamani ndizo zilikuwa zikitoa burudani maridhawa katika sherehe mbalimbali.
Mbaya zaidi hata kuongea lugha yao ya Kinyamwezi wanajisikia ‘Kichefuchefu’, aibu ama eti ni ushamba kuzungumza lugha yao!
Lakini historia inaeleza kuwa Wajerumani hawakuzuia muziki au ngoma za kiasili, muziki mpya na wa kiasili vyote vilienda sambamba.
Ulipoingia utawala wa Mwingereza, ulileta mabadiliko mengi katika muziki kutokana na vita vya dunia. Askari waliotoka vitani (King Africans Riffles) maarufu kama KAR au KEA, walirudi wakiwa na hadithi kuhusu muziki,.
Vyombo vya muziki na hata mtindo wa muziki walioukuta katika safari zao za kivita, vyombo kama vile Akodian na Magitaa makavu (yasiyotumia umeme) yaliingia nchini.
Magitaa ya umeme katika bendi za muziki wa dansi yalianza kutumika kati ya mwaka 1957 na 1959.
Bendi ya Dar es Salaam Jazz hutajwa kama ilikuwa ya kwanza ya muziki wa dansi kuanza kutumia gitaa hilo, ikifuatiwa na bendi ya Western Jazz na zinginezo zikafuatia.
Wakati huohuo zaidi ya makabila mbalimbali kuchanganyikana na miji kuanzishwa, ndipo mwanzo wa kuzaliwa kwa Utamaduni mpya.
Muziki uliokubalika kwa makabila yote ni bendi mbalimbali zilizoanzishwa katika ukanda mzima wa Afrika ya Mashariki.
Wasomi wa Kiafrika wakawaiga Wazungu kwa kutengeneza klabu zao ambazo zilikuwa maarufu kama ‘Dancing Clubs’.
Huko zilipigwa nyimbo mbalimbali kwa kutumia santuri na kucheza mitindo mbalimbali kama vile Chacha, Tango, Foxtrot, Swing, Waltz na kadhalika.
Inaamainika klabu ya kwanza Tanganyika ilikuwa mjini Tanga iliyokuwa ikiitwa ‘Young Novelty Dancing Club’. Baadaye ikaanzishwa Dar es Salaam ‘Young Generation Dancing Club’.
Klabu hizo ndizo chanzo cha bendi ya kwanza ya
Dar es Salaam Social Orchestra, ambayo baadaye ikawa bendi maarufu yaani Dar es Salaam Jazz Band.
Bendi hiyo ilikuja kujizolea umaarufu mkubwa wakitumia mtindo wa ‘Mundo’ huku wakijita ‘Majini wa Bahari’.
Nyingine ilikuwa YMCA Social Orchestra, kati ya miaka ya 1920 na 1935.
Baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia kumalizika mwaka 1945, Wamarekani waliweka radio yenye nguvu katika mji unaoitwa Kinshasa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Radio hiyo iliweza kusikika sehemu nyingi Afrika Mashariki, Kati na Magharibi, ikawa mwanzo wa Lebo maarufu ya Longisa nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Mwaka 1947 Lepodiville ambao sasa unaitwa Kinshasa, ukajulikana kama mji wa starehe.
Ikawa ndiyo sababu ya kuingwa muziki wa Kikongo, wakati huohuo Marekani ikijizatiti kueneza utamaduni wake sanjari na Ufaransa ikieneza muziki wa Jazz kwenye makoloni yake.
Lebo ya Galotone ya Afrika Kusini pia ilisambaza santuri ambazo ziliingiza mtindo wa Jive nchini.
Miaka mingi ya nyuma ilishuhudiwa vijana walikuwa na vikundi wakicheza mtindo huo wa Jive. Aidha bendi kadhaa ziliiga upigaji wa filimbi kumuiga mwanamuziki Spokes Mashiyane.
Mwaka wa 1954, Kenya ikaanza kuwa kituo cha kikubwa cha kurekodi muziki. Miaka mingi baadaye bendi za Afrika Mashariki zililazimika kwenda ili kufyatua santuri maeneo ya Kericho nchini Kenya.
Kuna baadhi ya wanamuziki hadi leo hufikiriwa kuwa ni Wakenya au walitoka Kenya. Mfano ni Frank Humplink na dada zake ambao walitoa vibao ambavyo bado vinasikika katika anga za muziki, kama ‘Embe dodo’, ‘Tufurahi Harusi’ na nyingine nyingi.
Mara baada ya nchi yetu kujipatia Uhuru mwaka 1961, pamoja na mapungufu yanayotajwa ya utawala wa Chama kimoja, kulikuwapo na mazuri mengi kutokana na chama hicho kuwa na dira inayoeleweka.
Kilielekeza kila kitu kadri ya matakwa yake jambo hilo lilikuza muziki humu nchini.
Sanaa ya Tanzania haikukwepa mwongozo wa chama tawala wakti huo cha TANU. Sehemu za kazi, vijiji, miji viliagizwa kuwa na vikundi vya utamaduni ambavyo vilikuwa ndivyo vikundi vya burudani baada ya kazi na pia kuelezea mipango na malengo ya chama na serikali.
Itakumbukwa kuwa miaka ya 1960, alikuwepo mhamasishaji maarufu mzee Makongoro, ambaye alikuwa akiimba nyimbo zenye mafunzo makubwa kwa jamii. Mmoja ya tungo yake ni ile “Dereva kalewa pombe”
Wakati huo ziliundwa bendi za majeshi kama vile Polisi Jazz
, Mwenge Jazz aliyo chini ya JWTZ, Magereza Jazz, JKT Kimbunga na Kimulimuli pamonja na Uhamiaji.
Mashirika ya Umma nayo hayakuachwa kupewa maelekezo ya kuanzisha bendi. Shirika la Bima la Taifa (NIC), ilianzisha bendi ya Bima Lee, Shirika la Maenedeleo Dar es Salaam nalo likaanzisha bendi ya DDC Mlimani Parck Orchestra. Shirika la Usafiri Dar es Salaam nalo likawa na bendi ya UDA Jazz ikitumia mtindo wa ‘Bayankata’. Bodi ya Biashara ya Nje (BET) ilinzisha bendi ya Biashara Jazz, Kiwanda cha kukata Alimasi cha Iringa, nacho kilikuwa na bendi ya Tancut Alimasi Orchestra na nyingine nyingi.
Baadhi ya miji nayo yakaanzisha bendi zao kama ilikuwa bendi ya Kurugenzi ya Arusha na Kurugenzi ya Dodoma.
Bendi zilitunga na kuimba nyimbo zambazo zilipitiwa kabla ya kurekodiwa na kurushwa hewani tofauti na nyakati zilizofuatia.
Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD), ndiyo ilikuwa pekee ikitangaza na kupiga kila aina ya muziki wa nchi hii, tofauti na sasa ambapo kuna vituo vingi vya radio, lakini vimeshindwa kufanya kazi hiyo iliyoweza kufanywa na kituo kimoja cha Taifa.
Mwanzoni mwa miaka ya 1960, baadhi ya bendi ziliingia kwenye utamaduni wa kunakili nyimbo za kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Bendi hizo ziliiga mirindimo ya vyombo vya nyimbo walizonakiri kilichobadilika ni kuimba kwa lugha ya Kiswahili.
Mathalani nyimbo za “Lau Nafasi”, “Mtoto wacha kupiga Mayowe”, “Nachekacheka Kilwa”, “Rosa” na nyingine nyingi.
Pamoja na hayo kulikuwako na wanamuziki waliokuwa wakifuata nyayo za nchi za Magharibi na baadaye wakachangaya vyombo na milio ya kiasili, ukazaliwa muziki wa Afro Rock, sambamba na nchi nyingine katika Afrika.
Kipindi hicho mwanasiasa mmoja aliamua kupiga marufuku muziki wa Bugi, ambao ulikuwa ni maonesho ya muziki ya mchana yaliyokuwa yakimalizima majira ya saa kumi nambili jioni. Kupiga marufuku muziki huo ilikuwa ni sawa na leo upige marufuku wanamuziki wa kizazi kipya, pengo hilo halijazibika hasi leo.
Miaka ya 1980 na 1990 kulikuwa na mfumo wa utawala wa shughuli za utamaduni, ambao pamoja na kuweko maofisa Utamaduni wa Wilaya, Mkoa, pia kulikuweko na Baraza la Muziki la Taifa (BAMUTA).
Pia kulizaliwa vyama ambavyo vilifanya kazi kubwa ya kuunganisha wanamuziki kama vile Chama cha Muziki Tanzania (CHAMUDATA) na Tanzania Taarab Association.
CHAMUDATA ailiandaa maonesho makubwa yaliyounganisha wanamuziki nchi nzima, yaani “Top Ten Show” Kama ilivyo nchini Marekani.
Maonesho hayo yaliwezekana kwa ushirikiano mkubwa na Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA), Umoja wa Vijana na Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD). Halijawahi kutokea tena maonesho hayo yenye ukubwa wa aina hiyo hadi leo.
Kuvurugika kwa mfumo wa uongozi wa utamaduni umeacha shughuli za utamaduni mkononi mwa wafanyabiashara pekee, ambao lengo ni kupata faida za kiuchumi, matatizo na matokeo ya kufa kwa utamaduni si lolote kwao.
Serikali inatakiwa ichukue mzigo huu wa kufadhili au kusimamia ukuaji na uendelezaji wa utamaduni. Kuacha shughuli za biashara ya kazi za sanaa kwa wafanyabishara peke yake, hivi sasa mtoto wa Kitanzania anauelewa zaidi muziki na Utamaduni wa nje hasa wa Kimagharibi kuliko wake.
Nyakati hizo ndizo zilizozaa muziki wa kizazi kipya, maarufu kama Bongo Fleva, ambapo kuna mapinduzi makubwa sana katika muziki wa nchini Tanzania.
Bendi nyingi za muziki wa dansi zimeanzishwa, hasa kwa wale wakongwe na kuunda bendi zao binafsi.
Mfano ni Mafumu Bilal, Hussein Jumbe, Rashid Pembe, Banana Zorro, LadyJay Dee, Deo Mwanambilimbi na wengine wengi.
Kila kizuri kina athari zake.
Kukua kwa teknolojia na kuanza matumizi ya kompyuta katika utayarishaji wa muziki, kumeua vipaji na muziki kwakuwa yeyote anaweza kurekodi pasipo kubughudhiwa.
Vijana wameshika hatamu na muziki huu wa kizazi kipya, bila utaalamu wa kutaka kupiga ala za muziki kwa kuwa kila kitu kinafanywa na mashine za kisasa.
Miaka ya nyuma tulishuhudia bendi kubwa ya OTTU Jazz wakati huo, ilitumia mtindo wa ‘Discipline’, walitingisha mno baadhi ya wapenzi wa muziki wa dansi miaka hiyo.
Mabadiliko makubwa yakaaza kuonekana baada kuundwa kwa taasisi au kampuni kubwa za uburudishaji wa muziki kama vile Radio One, Clouds FM, Radio Uhuru, Times FM, Radio Free Africa (RFA) na nyingine nyingi.
Kati ya miaka ya 1970 na 1980, bendi za Maqius du Zaire, Makassy Orchestra, Orchestra Safari Sound, MK Group, Zaita Muzica, The Bantu Group, La Capitale, bado ipo ikiongozwa na King Kiki, Bana Maquis nayo ipo ikiongozwa na Tshimanga Assosa, Maquis Original, Orchestra Kamanyola ipo jijini Mwanza, zote zilikuwa na wanamuziki wengi toka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Baadhi ya wanamuziki hao ni Kitzengu Makassy ‘Mzee Makassy”, Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’, Baziano Bweti, Fred Ndala Kasheba, Ramadhan Mtoro Ongolla ‘Dk. Remy’, Kabeya Badu, Mukumbule Lolembo ‘Parash’, Mutombo Lufungula ‘Audax’, Mbuya Makonga ‘Adios’Mukuna Roy, Mbombo wa Mbomboka, Kaumba Kalemba, Ilunga Lubaba. Ilunga Banza ‘Banza Mchafu’, Radi Massiya ‘Dikubakuba’, Maliki Star, Pulukulu Wabandoki ‘Motto’ Kalala Mbwebwe, na Chimbwiza Mbangu ‘Nguza Vicking’.
Wengine ni pamoja na Chinyama Chiyaza, Massiya Radi ‘Dibakubakuba’, Dekula Kahanga ‘Vumbi’, Moses ‘Fan Fan’, Tchimanga Assosa, mapacha waliokuwa na mvuto wa kipekee Kasalo Kyanga na Kyanga Songa na wengine wengi.
Idadi kubwa ya vijana waliozaliwa miaka ya 1980 na 1990 mwanzoni, walianza hamasa ya kuwa wanamuziki na kujishughulisha na kazi hiyo kwa kasi.
Kipindi hicho ndicho kulitokea makundi mbalimbali ya muziki wa Hip hop, hii ikiwa ni pamoja na Gangwe Mobb, Dewplomatz, S.O.S Kwanza Unity, Underground Soulz, Hard Blasters na nyingine kibao.
Ilipotimu miaka ya 2000 na 2010, muziki uliokuwa juu sana ni wa ‘Bongo Fleva’ na muziki wa dansi ambao hasa vijana wapya au kitambo wakarudi kwa kasi kipindi hicho.
Baadhi ya bendi zilizojaribu kuja kivingine katika kipindi cha miaka ya 1990 katikati na mwishoni, zilirudi ama kuvuma kupita kiasi.
Mathalani, African Revolution iliyotumia mtindo wa ‘Chumvi Chumvi Tutalamba’ ilirudi na mtindo wa ‘Tam-Tam’ chini ya uongozi wake Muumini Mwijuma ‘Kocha wa Dunia’, Mchinga Sound, Diamond Sound, Akudo Impact, Double Extra iliyokuwa ikiongiozwa na Ali Choki, Bwagamoyo Sound, Tanzania One Theatre (TOT Plus Band), Tabora Jazz ‘WanaSegere Matata’, Kiko Kidds, Nyanyembe Jazz, Dodoma International. Tatu Nane, Butiama Jazz, The African Stars, African Survivors Band ikiwa na wimbo wao wa “Maproso”, Malaika Band, The Kilimanjaro band ‘Wana Njenje’, Inafrica Band na nyingine nyingi zilitingisha zama hizo.
Bendi ya Chuchu Sound ni miongoni mwa bendi zilizotamba sana mwanzoni mwa miaka ya 2000 ikiongozwa na Omar Mkali ‘Babu Chuchu’.
Waliimba na kucheza katika mtindo wao wa ‘Chakacha’ au ‘Mduara’ kwa lugha maarufu. Bendi hiyo ilikuwa tishio ‘ikikabana shingo na bendi ya The Kilimanjaro Band ‘Wana Njenje’ pamoja na bendi ya Kilimanjaro Connection.
Ushindani ulikuwa mkubwa mno wakati huo ambapo tulishuhudia wanamuziki au waimbaji wakihama kutoka bendi moja kwenda nyingine kufuatia utitiri wa bendi za muziki zilizokuwepo nchini.
Kipindi hicho ndicho alichokuja mkali wa sauti ‘King of Melody’ Christian Bella, akitokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Ushindani katika muziki ulipamba moto, ikazaliwa bendi ya Stono Musica ‘Wanajelajela Original’ baadaye FM Academia chini ya uongozi wa Nyoshi El Sadat.
Kabla ya kuundwa kwa bendi hii, ilikuwa moja na Stono Musica kabla kutengena na Nyoshi akabaki na jina halisi lakini akaongezea neon la “The Dream Team”.
Marekani ikashika hatamu kueneza utamaduni wake duniani kwenye miaka ya 2000. Tanzania ikaupokea pakazaliwa neno muziki wa kizazi kipya, ukiacha wale walioanza kabla ya mwaka 2000, wakapatikana akina Dully Sykes, Manzese Crew, Wandava Kumi Ngangari (W TEN N), Jay More, Ngwair, Daz Nundaz, Madee, Mandojo na Domo Kaya.
Wengine nia Mr. Blue, Complex, Dudu Baya, Mr. Nice, Juma Nature, FSG, AY, GK, Q Chilla, Mwanafalsafa, aliyejaribu kutunga mashairi ya asili, Malaika Band, Lady JDee, Rehema Chalamila ‘Ray C’ na wengine wengi.
LadyJDee na AY ni wasanii wa mwanzo wa kizazi kipya kuthubutu kutoka nje ya mipaka ya Tanzania, ilhali wakijivika wajihi wa Kimagharibi.
Kukosekana udhamini au kujitangaza vya kutosha, kundi kama Boyz from the Army, Born Crew, Hot Girls, Big Dog Pose(BDP), Hot Port Family, Wateule, Mambo Poa, Uswahili Matola na wengine walithubutu bila mafanikio, wakapotea.
Wachuja Nafaka lilikuwa kundi mradi tu (Super Group) lilodumu kwa kipindi kifupi. Wasanii wengine walitamba katika miaka ya 2001 hadi 2004 ni pamoja na Zahrani a.k.a Big Punisher, Spula, Bushoke, Mr. Nice ambaye kwa kweli alitamba kupita maelezo nyimbo za kuchukua ala za kitoto na kuzirudia katika mtindo wa Bongo Fleva, alitamba nao kwa jina la “TAKEU”.
Mr. Nice akauvusha muziki huo mbali sana, hususan katika nchi za Burundi, Kongo (DRC), Rwanda na nchi nyingine za Afrika, japokuwa hakudumu sana katika ‘game’ la muziki.
Profesa Jay, ambaye hivi sasa ni Mbunge, kwa upande wa msanii wa kiume, alionekana kuunyanyasa muziki wa kizazi kipya katika miaka ya 2001 hadi 2005. Zama hizo Profesa Jay alionekana kutokuwa na mpinzani, yasemekana yeye ndiye aliyesababisha watu wazima wausikilize muziki wa kizazi kipya.
Hauwezi kuutaja muziki wa kizazi kipya pasi bila Profesa Jay, Mb Doggy, ndiye mwanzilisha wa muziki wa mapenzi mazito, hata kama waliimba lakini si kwa kiwango cha Mb Doggy.
Kati ya mwaka 2005 na 2006 Mb Doggy kutoka Tip Top Connection, ilikuwa kipindi chake cha kunyanyasa katika muziki wa kizazi kipya., alionesha uwezo wake mkubwa katika tasnia hiyo.
Miaka ya 2005 na 2006 Ferouz naye alikuja juu sana, lakini hakwenda mbali. Wakati huohuo waliibuka akina Matonya, Abby Skills, Enika, Ali Kiba, Queen Darleen (japokuwa alikuwapo katika game tangu enzi za Historia ya Kweli ya Dully Sykes), lakini hakuwa msanii wa uhakika kipindi hicho.
Bila kuusahau muziki wa Taarab uliopamba moto, kipindi hicho ambao wataalamu wa muziki wanautaja kuwa unafaa kuwa muziki wa asilia wa Kitanzania ingawa una mahadhi ya Kiarabu na Kihindi kwa mbali.
Mwaka 2006 kundi la Jahazi Morden Taarab lilianzishwa chini ya uongozi wa Mzee Yussuf, akuvusha muziki huo ukiwa na vionjo vya kisasa.
Alisababisha takriban kila mtu asikilize Taarab hasa kwa tungo zake lakini hakuzingatia uhalisia wa taarab mwanana ya akina Shakira na Visiwa vya Zanzibar. Baadaye zikazuka bendi nyingine nyingi za akina Nasma Hamis Kidogo, Khadija Omar Kopa, Isha Mashauzi ambao yaelezwa kuwa waliua kabisa muziki wa taarabu, wao wakaita ni Tara dansi!
Mzee Yussuf ameachana na masuala ya muziki, ni Alhaj baada ya kwenda kuhiji Mecca.
Miaka ya 2010 muziki wa kizazi kipya na muziki wa dansi ulibadilika sana. Vijana wengi waligeukia katika muziki wa dansi. Lakini muziki wa Bongo Fleva umepiga hatua maradufu. Msanii Naseeb Abdul ‘ Diamond Platinumz, ameupeleka mbali sana muziki wa Tanzania nje ya nchi kwa kiasi kikubwa kupita msanii mwingine yeyote yule tangu muziki huu ulipoanza. Sambamba na Ali Kiba ‘King Kiba’ ingawa kwa muda aliamua kumuachia uwanja Diamond , na kuamua kurudi tena kwa kishindo.
Wasanii hao wameshindwa kuvaa viatu vya kina Salifu Keita, Mory Kante na wengine wengi wanaotumia Kora katika muziki wao.
Huenda Darasa ni msanii pekee wa hip-hop aliyeweza kufikisha watazamaji wengi kwa muda mfupi katika Youtube, kuliko msanii yeyote Yule wa hip– hop ya Kitanzania, hasa kwa kufuatia kibao chake cha “Too Much”.
Muziki wa Singeli umebadilisha mawazo ya baadhi ya vijana ambapo wanawatelekezea kina Man Fongo, Msaga Sumu, Sholo Mwamba, Dula Makabila wakiwa na matumaini ya kuirudisha Tanzania katika asili ya muziki wake.
Mwisho.
Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa namba 0784331200, 0767331200 na 0713331200.