Na Moshy Kiyungi,Tabora.
Muziki wa rhumba umejizolea sifa na kupendwa na wapenzi wengi wa muziki humu nchini na Afrika kwa ujumla.
Sifa hizo zimetokana na baadhi ya wanamuziki waliokuwa hodari katika utunzi na upigaji wamuziki huo.
Makala hii inakujuza baadhi ya wanamuziki waliokuwa wakongwe, wanaokamilisha uhalisia wa simulizi hii.
Jina la Joseph Kabasele Tshama ‘Grand Kale’ ni miongoni mwa baadhi ya nguli aliyekuwa na Weledi mkubwa katika tasnia ya muziki hapa Afrika.
Hata hivyo baadhi wa watu kwa kutokuelewa kwao, wamekuwa wakichanganya majina ya Joseph Kabasele ‘Grand Kale’ na Kabasele Yampaya ‘Pepe Kalle’, wakidhani ni mtu mmoja ama ni ndugu.
Hao wote walikuwa ni wanamuziki mahiri wenye kupishana kwa mbali sana kwa umri.Joseph Kabasele ‘Grand Kale’ alizaliwa Desemba 16, 1930, mjini Matadi huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, wakati Kabasele Yampanya ‘Pepe Kalle’ alizaliwa Novemba 28, 1951 jijini Kinshasa.
Wataalamu wa muziki wanaeleza kuwa historia ya muziki wa dansi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), haimuweki pembeni nguli Joseph Kabasele ‘Grand Kalle’.Mkongwe huyo alisaidia kwa kiasi kikubwa katika mwelekeo wa muziki wa kisasa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Grand Kale atakumbukwa kwa kuwa yeye alikuwa mwasisi na kiongozi wa bendi ya African Jazz,iliyokuwa kubwa nchini DRC wakati huo.
Bendi hiyo iliwajumuisha magwiji wengine akiwemo aliyekuwa mpiga gitaa mahiri, Dokta Nico Kasanda, aliyekuwa mtunzi na mwimbaji wa Kimataifa Tabu Ley Rochereau na mpiga saxophone maarufu Manu Dibango.
Kabasele alikuwa kinara wa muziki wa Kiafrika na miongoni mwa watunzi na mwimbaji mkubwa katika bara hili la Afrika ya watu weusi wanaozungumza Kifaransa.
Nguli huyo alizaliwa huko Matadi nchini DRC, katika familiya maarufu iliyomjumuisha Joseph Malula ambaye alitokea kuwa Askofu wa Kanisa Katoliki.Grand Kalle alikuwa miongoni mwa watu wa zama hizo waliopata elimu.
Alimaliza elimu ya sekondari na kuajiriwa kazi ya kuwa mpiga mashine (typist) kwenye Kampuni za biashara katika Jiji la Kinshasa.Muziki ulikuwa kama wito wake na akagundua mwanya wa kuufuatilia na kwenye mwaka 1950, akawepo katika studio mpya iliyojulikana kwa jina la OPIKA.
Akiwa katika studio ya OPIKA, Grand Kalle aliungana na wanamuziki wa muda, ambao walikuwa Jimmy ‘Zacharie Elenga’ ambaye alikuwa ndiye nyota wa wakati huo.Pia walikuwepo wapiga magitaa mashuhuri Georges Doula na Albert Yamba Yamba na baadhi ya wapigaji muziki waliokuwa wakichipukia.
Kama alivyokuwa yeye, Chipukizi hao waliona muziki ndio ufunguo wa mafanikio, baadaye wakiwa nje ya mihangaiko ya kazi na pia baada ya maonevu ya Ukoloni.Mojawapo ya bendi za mwanzoni ambayo iliibuka kutoka mseto huo wa Kabasele ni wanamuiziki Georges Doula na Yamba Yamba, waliunda bendi ikijulikana kwa jina OTC.
Baada ya kufanya ‘Promosheni’ ya filamu kwa ajili ya radio stesheni ya mjini hapo, ilikuwa ikitumia herufi hizo OTC.Kabasele ‘Grand Kalle’ umaarufu wake ukawa hauna mfano, aliweza kubuni mtindo wake baada ya kuhamasika na kumuona muimbaji machachari ‘Tino Rosi’.
Sauti ya Rosi wakati akighani, ilikuwa ni yenye mvuto kwenye nyimbo zake, ikawa kivutio kikubwa kwa wakazi wa mji wa Kinshasa.Nyimbo zake za mwanzoni zilizo ‘hit’ zilitokana na mjumuiko wa wanamuziki vijana wa OPIKA, hususan mpiga gitaa Nicolas Kasanda baadaye akajulikana kama Dokta Nico, akipiga gitaa la kati la rhythm.
Wimbo Parafifi uliofyatuliwa mwaka 1952, ambao maudhui yake uliimba kumsifia mtangazaji wa radio aliyekuwa nchini Jamhuri ya Kongo Brazzaville.Parafifi ulikuwa ni utunzi wa Joseph Kabasele ulioweza kutia fora pamoja na ule ‘Kale Kato’ uliokuwa ukihadithia juu ya penzi la Kabasele kwa kimwana mmoja aliyejulikana kwa jina la ‘Katherine’.
Katika kipindi cha kati ya mwaka 1953 hadi 1955, bendi mpya iliyomjumuisha Kabasele, Nico na Dechaud, iliibuka kutoka kwa wanamuziki wa muda wa studio ya OPIKA wakajiita African Jazz.
Wakiazima jina hilo ambalo halikushabihiyana na mtindo wa muziki wa Kimarekani wa ‘Jazz’ kama jina lilivyo.African Jazz ilicheza muziki wa nyimbo za Latini, ambapo bendi hiyo ilichangia kiasi kikubwa kukua kwa rumba la Kikongo.
Waimbaji wengine kadhaa walianza kuiga mtindo wake kiasi kwamba watu wakaanza kuzungumzia kuanzishwe kwa shule ‘mchapuo’ wa Kabasele au wa African Jazz.Aidha baadhi ya nyota wengine aliokuwa nao katika African Jazz zaidi ya Dokta Nico Kasanda, Tabu Ley, Dechaud na Manu Dibango. Wengine ni pamoja na waimbaji Joseph Mulamba Mujos, Bombenga na mpiga gitaa Tino Baroza.
African Jazz iliweza kuweka fursa nzuri kuwa ni uwanja wa mafunzo kwa wanamuziki vijana wa kizazi kilichofuatia huko DRC.
Hadi kufikia mwaka 1960, African Jazz ilikuwa bendi ya juu nchini mwao na kuweza kufyatua maelfu ya santuri zilizotolewa katika nembo ya ‘DECCA’ na kuweza kuwapata mashabiki wengi katika kumbi mbali mbali.
Joseph Kabasele alikuwa karibu sana na kundi la Rocka Mambo, hadi kuleta muungano mzuri na kundi lake la African Jazz. Alishirikiana nao na kuweza kutoa vibao vyenye viwango vizuri hasa alipokuwa ameshirikiana na Jean Serge Essous, Nino Malapet, Rossignol na kina Pandi.
January, 1960 Kabasele na kundi lake la African Jazz pamoja na wajumbe wawakilishi wa iliyokuwa ‘Belgian Congo’, walifanya kitu cha kihistoria ambacho ni kongomano la utambulisho la kisisasa huko Brussels.
Miongoni mwa tungo zake alizozifanya katika kongomano hilo la kisiasa la mwaka 1960, ni utunzi wa wimbo uliojulikana kama ‘Independence Cha Cha’ na ule wa ‘Le Table Ronde’.
Independence Cha Cha, ulitambulika kama wimbo wa Kitaifa kufikia uhuru.
Utunzi mwingine wa Kabasele ‘Bilombe Ba Gagne’ ukiwa na maana ya wenye kujiamini wameshinda, ulielezea maisha ya madhira chini ya utawala wa Wabelgiji.Kipindi ambapo uhuru ulibadilika na kuelekea kwenye vurugu.
Aidha Kabasele alitoa kibao kingine cha ‘Toyokana Tolimbisana na Kongo’ ukiwa na maana ya tuelewane na tusamehe yaliyopita, ukihimiza kuungana wakongomani.Mwaka 1961 kundi la African Jazz likiongozwa na Joseph Kabasele, lilifanya ziara ndefu katika nchi za Afrika Magharibi na kusambaza mitindo yao iliyochanganya mahadhi ya Kiafrika.
Kwa wasikilizaji wa nchi za Ghana, Nigeria, Ivory Coast, Sierra Leone na Guinea,ulileta athari kubwa kwa wanamuziki wa huko.
Mfano wa karibu ni kwa bendi ya Bembeya Jazz ya nchini Guinea, iliweza kufaidika kwa ziara hiyo ya Joseph Kabasele ya mwaka 1961. Katika kipindi hicho kuliweza kuzaliwa muziki mchanganyiko wa Afrika Magharibi na Latin Amerika kwa kupatikana mitindo ya High-Life, Juju na Afro-Beat.
Mwaka 1960 Grand Kale alirekodi kibao kilichojulikana ‘Okuka Lokole’ ambacho ni kwa heshima ya mwanamuziki ‘Louis Armstrong’ ambaye alitembelea nchi ya Kongo kwa ziara iliyodhaminiwa na Serikali ya Marekani.
Nguli huyo baadaye alibadilika akawa kiongozi mkali, tabia ambayo ilipelekea wanamuziki wote kuihama bendi ya African Jazz mwaka 1963.
Kabasele aliunganisha nguvu akishirikiana na mwimbaji Jean Bombenga, mwanafunzi wake aliekuwa na bendi ya Vox Africa, ambayo baadaye ilitambulika kama African Jazz.
Hata hivyo halikufanikiwa kufikia kiwango cha iliyokuwa African Jazz original.Baada ya kundi hilo kupiga muziki na kurekodi kwa uchache nyimbo pia kufanya maonesho kadhaa, lilisambaratika mwaka 1969.
Kabasele baadaye akaenda kurekodi huko Ulaya akiwa na kundi la wanamuziki walikuwepo studio na kulipa jina ‘African Team’.Kundi hilo lilikuwa na wanamuziki, Mkameruni, Manu Dibango na Jean Serge Essous wa Kongo Brazzaville waliokuwa wapulizaji wa saxophone.
Alikuwepo mpiga fluti toka nchini Cuba aliyekuwa akiitwa Don Gonzalo. Kwa pamoja walicheza muziki kwa miondoko ya Afro-Latin Jazz.Kwenye miaka ya mwanzo ya 1970, Kabasele akawa Rais wa chama cha haki miliki cha Kongo Kinshasa SONEKA.
Aidha alionekana jukwaani mara chache sana kutokana na maradhi ya ‘hypertension’ sugu ambayo yalimuandama sana.Aliwahi kwenda Paris mara mbili kwa matibabu lakini alipata nafuu ya muda.
Mwaka 1980 Kabasele alitunikiwa Nishani ya ‘Mwalimu Mkuu’ wa muziki wa Zaire na Umoja wa Wanamuziki UMUZA.Grand Kalle alikuwa na sauti pamoja na staili kigezo, ambayo waimbaji wote wa Kongo wangeweza kupimwa kwa hiyo.
Bendi yake ya African Jazz ilikuwa ni mfano kwa kila kundi la bendi za Wakongo waliofuatia.Mchango wake katika mwendelezo wa rumba la Kongo, uliwafanya Wakongo wote wamwite ‘Baba wa muziki wa Kongo’
Joseph Kabasele ‘Grand Kale’ anakuwa miongoni mwa wanamuziki wakubwa wa karne ya ishirini, alifariki February 11, 1983 akiwa katika mji wa Kinshasa, huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Mungu aipumzishe roho yake pahala pema peponi, Amina.
Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa namba: 0713331200, 0736331200, 0784331200 na 0767331200.