Na Woinde Shizza Michuzi Tv,Arusha
MAMLAKA ya usafiri wa anga Tanzania (TCAA) imesema kuwa Tanzania ina
upungufu wa marubani na wataalamu wa mitambo ya ndege, hivyo ni fursa
kwa watanzania walio wengi kujitokeza kusomea fani hyo ili kuweza
kuziba pengo hilo.
Afisa Habari wa TCAA,Bestina Magutu aliyasema hayo juzi,alipokuwa
akizungumza na wanahabari katika banda la mamlaka hiyo,lililopo katika
maonyesho ya kilimo na sherehe za nanenane,katika viwanja vya nanenane
vilivyopo Themi jijini hapa.
Alisema kuwa wakati umefika kwa watanzania wengi kujitokeza kusomea
fani hiyo,ambapo ametoa wito kwa wazazi na walezi kuwapeleka watoto
wao katika banda la mamlaka hiyo ili waweze kujifunza mambo mbalimbali
yanayohusiana na usafiri wa ndege.
“Unakuta mtoto anapokuwa mdogo ukimuuliza ukiwa mkubwa unataka kuja
kuwa nani anakwambia nataka kuwa rubani lakini ndoto zake zinatoweka
kutokana na kushindwa kujengewa msingi mzuri angali akiwa
mdogo”alisema Magutu.
Alisema kuwa mamlaka hiyo inamiliki na kuendesha chuocha usafiri wa
anga(CATC) kinachotoa mafunzo ya urubani,uongozaji ndege,taarifa za
usafiri wa anga,uhandisi na usimamizi wa shughuli katika viwanja vya
ndege hivyo watanzania wanapaswa kuchangamkia fursa hiyo.
“Mamlaka ya usafiri wa anga hapa nchini ina majukumu makuu mawili
ambayo ni udhibiti wa masuala ya kiusalama na kiuchumi pamoja na
utoaji wa huduma za uongozaji ndege kwa watoa huduma wote wa usafiri
wa anga katika viwanja vyote vya ndege”alisisitiza Afisa habari huyo
wa TCAA.
Aliongeza kuwa Mamlaka hiyo imekuwa makini sana katika kusimamia
masuala ya kiusalama kwa kuhakikisha kuwa ndege inaponunuliwa
ikaguliwa kwanza katika nchi ilipotengenezwa kabla ya kuingia nchini
ili kuhakikisha kuwa ina ubora unaotakiwa na kukagua huduma kwenye
viwanja vya ndege.
Alisema kuwa pia wanaangalia huduma zote zinazotolewa kwa
abiria,matumizi ya miundombinu ya kuruka na kutua ndege mafuta ya
ndege,huduma za uongozaji ndegeikiwa ni pamoja na utoaji wa
mawasilianoya taarifa za anga na mitambo ya kuongozea ndege na ile ya
kufanya uchunguzi katika anga.
Magutu alisema kuwa pia mamlaka hiyo imekuwa ikiangalia na kukagua
mara kwa mara kuona kama makampuni ya ndege yana uwezo wa kufanya
biashara hiyo,kukagua huduma kwenye viwanja vya ndege pamoja na vyuo
mbalimbali vinavyotoa mafunzo yanayohusianana usafiri wa anga