Na Karama Kenyunko, globu ya jamii.
JAJI Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma amesema Jaji Mkuu Mstaafu, Othman Chande amechangia mabadiliko makubwa katika nyanja zote za mahakama ikiwemo kuhakikisha uhuru wa mahakama, kupambana na rushwa na kuondoa mrundikano wa mashauri.
Akizungumza wakati wa hafla ya kuagwa kitaaluma kwa Jaji Chande leo jijini Dar es Salaam, Jaji Juma amesema, yeye ni miongoni mwa watu walioshuhudia mabadiliko makubwa ya mahakama yaliyosababishwa na Jaji mstaafu Chande tangu alipoteuliwa mwaka 2004 kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani na baadaye Rais Jakaya Kikwete alipomteua kuwa jaji mkuu mwaka 2010 hadi 2017alipostaafu.
Amesema katika kipindi hicho Jaji Chende alianzisha mpango mkakati wa kuhakikisha mahakama inajitawala na haki inatolewa kwa usawa na kuongeza kuwa, Jaji Chande alikuwa miongoni mwa walioandaa Mpango Mkakati wa miaka 10 wa mahakama kuanzia 2015 hadi 2020 wakiwa na lengo la kuhakikisha wanaondoa mrundikano wa kesi za zamani kwa kila jaji kusikiliza mashauri 250 kwa mwaka.
Ameongeza, mapaka sasa mahakama inaendelea kufuata muongozo huo kwa kuhakikisha kuwa Mahakama za Mwanzo zinasikiliza kesi kwa miezi sita hadi kwisha kwake na Mahakama za Wilaya na Mkoa husikiliza kwa mwaka mmoja na sasa kila Jaji anatakiwa kusikiliza mashauri 100 kwa mwaka.
Aidha amewaomba wananchi waendelee kuwaamini, kuwapima kwa hukumu zinazotolewa na mahakama na kama hawajaridhika wakate rufaa, kwani mahakama ni muhimili unaofanya kazi kwa uwazi zaidi. Aidha amesisitiza kuwa, mahakama imejipanga kuona kila mtumishi ana kitambulisho kinachoonesha majina yake hivyo, akiomba rushwa ni yeye binafsi na si watu wote hivyo anapaswa kujiwajibishwa kabla ya kupelekwa kwenye Tume ya maadili.
‘’Ukiombwa rushwa useme na uwe tayari kutoa ushahidi, nenda mpaka Takukuru, mtaje mla rushwa. Ninaahidi tutaendelea kuwasaidia wananchi wasiingie kwenye mitego ya rushwa na tunawaelimisha waelewe taratibu za mahakamani,’’ alisema.
Kwa upande wake, Jaji mstaafu Chande, amesema mahakama ni taasisi ambayo inatakiwa kulindwa na kujilinda kwa kuwa huru ili kuhakikisha inafanya kazi kwa mujibu wa katiba na sheria na kutoa haki kwa usawa na uhuru hivyo ni lazima kulinda na kutetea uhuru wa mahakama kwani zipo taasisi nyingi zinazopima uhuru na zimeonesha kuwa unalindwa na kuheshimika hapa nchini.
Aidha ameongeza kua, mageuzi makubwa yameishafanyika na yanaendelea kufanyika ikiwemo kutenganisha majukumu ya wasajili na watendaji wake. Kwani kwa sasa mfumo mpya wa usikilizwaji wa malalamiko unasaidia ambapo asilimia 98 ya malalamiko yanasikilizwa kwa mwaka.
Naye, Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda amesema Jaji Chande ni chachu ya mabadiliko ya kimfumo katika mahakama kwani katika kipindi chake chote cha uongozi alihakikisha anasimamia masuala ya rushwa na mrundikano wa kesi na mahakama inakuwa na utawala binafsi katika utoaji wa haki kwa watu wote kwa usawa.
Akielezea safari yake ya uongozi, Jaji profesa Juma amesema, Jaji Chande alipata shahada ya Sheria kutoka Kitivo Cha Sheria, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1974, baadaye alisoma Shahada ya Uzamili katika Chuo Kikuu cha Webster huko Geneva mwaka 1982 na Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa alimteua kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Agosti 16, 2004 na Februari 6, 2008 aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani.
Desemba 2, 2010 Rais mstaafu Jakaya Kikwete, alimteua kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania, nafasi aliyoishika hadi alipofikia umri wa kustaafu kwa mujibu wa Katiba Januari 17, 2017.
Waliohitimu shahada ya Sheria pamoja na Jaji Mkuu Mstaafu Chande ni Pinda, Jaji mstaafu Dk Steven Bwana na wengine na baada ya kumaliza masomo yake alijiunga na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kama Mwanasheria wa Serikali alipokuwa Mwanasheria wa Serikali katika Benki Kuu ya Tanzania.
Pia Chande kwa kushirikiana na Reuben Mwaikinda, Maurice Pius Ndomba na Simon Ivasa-Merinyo Matafu walikuwa waendesha mashitaka wa makosa yanayohusu matumizi ya fedha za kigeni.
Pia alifanya kazi Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekudu huko Geneva Uswisi kama Mshauri Mwandamizi wa Mwendesha Mashitaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai kuhusu Rwanda.
Aliteuliwa kuwa Mwendesha Mashitaka Mkuu katika Mahakama ya Rwanda kuanzia Juni Mosi, 1999 hadi Julai 31, 2000.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba, Katibu Mkuu Kiongozi, John Kijazi, Jaji mstaafu, Augustino Ramadhan, Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG), Mussa Assad, mawaziri, wastaafu serikalini na mahakamani na wanasheria.
JAJI Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma (kulia) akifurahi jambo na Jaji Mkuu Mstaafu, Othman Chande