HALMASHAURI ya Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam imepata hati safi kwa mwaka unaoishia Juni 30,2018 na kufanya halmashauri hiyo kuendelea kupata hati hiyo kwa mwaka wa tatu mfululizo.
Hayo yamesemwa leo Juni 28,2019 na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam Jumanne Shauri wakati anawasilisha taarifa ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG) katika kikao maalumu cha Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo.
Shauri wakat anawalisha taarifa hiyo ya CAG kwa Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo, amesema kuwa kwa mujibu wa Katiba ya mwaka 1977 (Rev 2005) ibara ya 143 na sheria ya ukaguzi wa umma namba 11 ya 2918 kifungu cha 10(1) ni jukumu la la Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali kufanya ukaguzi wa taarifa za mapato na matumizi ya fedha za umma Serikali Kuu,Serikali za Mitaa,Idara na mashirika ya umma.
Amefafanua baada ya ukaguzi huo anatakiwa kutoa matokeo ya ukaguzi na mapendekezo kutokana na ukaguzi huo na hatua zinazotakiwa kuchukuliwa na menejimenti zilizopo kwa mujibu wa sheria.
"Hati ya ukaguzi kwa mwaka wa 2017/2018 mwaka uliokaguliwa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala imepata hati safi na kufanya halmashauri yetu kuendelea kupata hati safi kwa miaka mitatu mfululizo.Tulipata hati safi mwaka 2017/2018, mwaka 2016/2017 na mwaka 2015/2016.Kwa mwaka wa 2014/2015 tulipata hati yenye mashaka,"amesema Shauri mbele ya wajumbe wa kikao hicho.
Kuhusu mapendekezo ya CAG ambayo yapo kwenye ripoti yake, Shauri amesema kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala imeweka mikakati mbalimbali kuhakikisha wanaishughulikia kikamilifu na kufafanua baada ya kupokea ripoti ya CAG ,Ofisi ya Rais-Tamisemi kupitia ofisi ya mikoa ilitoa ratiba ya kujadili taarifa hiyo kupitia vikao mbalimbali vya halmashauri.
Hivyo amesema Mei 20 mwaka huu kamati ya watalaam walifanya kikao, pia Kamati ya Ukaguzi nayo ikafanya kikao Juni 21 na Kamati ya Fedha na Utawala walifanya kikao Juni 26 mwaka huu.
"Hivyo leo hii baraza la madiwani kupitia kikao maalumu kimefanya kikoa ili kupata taarifa hiyo.Aidha halmashauri imejipanga kuzuia hoja zote kwa kuunda timu ya wataalam kushughulika na kushauri kuhusu kuzuia hoja zilizojitokeza zisijirudie tena na jinsi ya kutekeleza mapendekezo na ushauri wa Mkaguzi,"amesema Shauri.
Wakati huo huo akizungmza baada ya kufanyika kwa kikao hicho Shauri ametumia nafasi hiyo kueleza kuwa wakati wa kipindi hiki cha kuelekea mwisho wa mwaka wa fedha unaoishia Juni 30 , idadi kubwa ya walipa kodi wamejitokeza kulipa na kwao ni jambo la faraja kwani kuna muamko mkubwa wa wananchi wa kada mbalimbali kulipa kodi.
"Kasi ya ulipaji kodi kwa wananchi waliopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilala ni mkubwa, wengi wameendelea kulipa kodi ambazo wanatakiwa kulipa lakini tunaendelea kuhamasisha wananchi kuendelea kulipa kodi kwa maendeleo ya halmashauri yetu na Taifa kwa ujumla,"amesema.