Na Said Mwishehe, Globu ya Jamii
MWENYEKITI wa Mtandao wa Sauti ya Sober House Tanzania Al-Karim Banji ameiomba Serikali kusaidia upatikanaji wa maeneo ya ardhi kwa ajili ya shughuli za uchumi ikiwa pamoja na kuhakisha vijana ambao wanachana na matumizi ya dawa za kulevya wanajikita kufanya kazi kwa bidii.
Amefafanua kazi ya Soba House pamoja na mambo mengine ni kuhakikisha aliyeathirika na matumizi ya dawa za kulevya anaachana na dawa hizo na wanafanikisha hilo lakini changamoto kubwa baada ya hapo walioamua kuacha dawa wanakosa kazi ya kufanya na matokeo yake akirudi mtaani anaanza kutumia tena.
Banji ametoa ombi hilo wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Dawa za Kulevya Duniani ambayo hufanyika kila Juni 26 ya kila mwaka ambapo kitaifa yamefanyika katika Jiji la Tanga na mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Rais Samia Suluh Hassan aliyewakilishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora George Mkuchika.
"Changamoto iliyopo wale ambao wanapata huduma baada ya kurudi mtaani wanarudia tena kutokana na kukosa kasi .Hivyo inakuwa rahisi kushawishika na kurudi kwenye utumiaji dawa za kulevya.Ombi letu kubwa ni kupata maeneo ya shughuli za kiuchumi kama kufanya kilimo, ufugaji , ufyatuaji tofauli na aina nyingine ya kazi ambazo waliochana na dawa za kulevya watafanya wakiwa maeneo ya Soba,"amesema Banji.
Ametumia nafasi hiyo kuelezea viongozi wa ngazi mbalimbali wa Serikali waliotembelea banda la mtandao huo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Dawa za Kulevya Duniani ambayo kitaifa yamefanyika Tanga,Banji amesema iwapo Serikali itawasaidia kupata maeneo hata katika suala la kujiendesha itakuwa na unafuu kwani kupitia kazi ambazo zitafanyika kwenye Soba zitawaingiza kipato na hivyo waliopo kujikumu.
Amesema huduma ambazo wanazitoa kwa walioathirika na dawa za kulevya kwenye Soba zinagharama yake ikiwemo ya mhusika kukaa katika soba wakati anapata huduma , hivyo pamoja na kwamba kuna gharama inayotolewa na mhusika kwa kila mwezi lakini kuna mahitaji mengine muhimu ambayo yanahitajika.
Banji ambaye yeye anamiliki Life and Hope Sober House Bagamoyo ametoa mfano kwake anao vijana walioathirika na dawa za kulevya na sasa wanapata huduma wapo 48 ambapo naamini wangekuwa na eneo la kutosha wangeshiriki kikamilifu kufanya kazi za kujipatia kipato na kuendelea na shughuli nyingine za kijamii.
Kuhusu mtandao wa Sauti ya sober House Tanzania, Banji amesema mtandao huo upo kwenye mikoa 11 nchini na wanaohudumiwa katika Sober hizo ni watu 15000 na malengo yao ni kuongeza idadi ya mikoa ili kuwafikia wengi zaidi.
Hata hivyo amesema wale ambao wameamua kuachana na matumizi ya dawa za kulevya wanayo nafasi ya kuamua anataka kwenda kupata huduma wapi, hivyo wapo wanaokwenda kwenye Sober , wengine hospitalini na maeneo mengine yanayotambulika kisheria.
Kutokana na ombi hilo la Banji kwa niaba ya mtandao huo wa sober, Serikali imewahakikisha kuyafanyia kazi maombi hayo na kukiri iko haja ya kuangalia na namna ambavyo inaweza kusaidia katika hilo huku Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akieleza wazi kuwa atasimamia hilo kwani lina tija kubwa.
"Ni kweli kuna sababu ya kuangalia namna ya kuwasaidia wenye Sober house, kwa hapa Mkoa wa Tanga kuna maeneo mengi ya ardhi ambayo hayatumiki, hivyo ni wakati sahihi kuhakikisha wale ambao wameamua kuacha kutumia dawa za kulevya na wapo kenye hizi Sober wanapata maeneo ya kufanya shughuli za uchumi.Kuwasaidia maeneo kwa ajili ya
kuwa na ofisi peke yake haitoshi, wapewe maeneo wafanye kazi,"amesema Waziri Mwalim.
Kwa upande wake Waziri Mkuchika akizungumza akiwa katika banda la mtandao huo la Sauti za Sober Tanzania amekiri kuna wajibu kwa Serikali kuangalia na namna ya kuendeleakusaidiana na wadau kuhakikisha walioamua kuacha kutumia dawa za kulevya wanarudi kufanya kazi badala ya kukaa vijiweni.
Mwenyekiti wa Mtandao wa Sauti ya Sober House Tanzania Al-Karim Banji (aliyevaa suti nyeusi) akizungumza mbele ya Mgeni rasmi Waziri wa Nchi ,Ofisi ya Rais,Menejiment ya Utumishi wa Umma Umma Mkuchika ambaye amemuwakilisha Makamu wa Rais mama Samia Suluh Hassan wakati wa maadhimisho ya Siku ya Dawa za Kulevya Duniani ambayo kitaifa imefanyika Jiji la Tanga.
Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais ,Menejimenti ya Utumishi wa Umma George Mkuchika aliyekuwa muwakilisha mgeni rasmi Mama Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye banda la Mtandao wa Saut za Sober Tanzania wakati wa maadhimisho ya siku ya Dawa za Kulevya Duniani
Mwenyekiti wa Mtandao wa Sauti ya Sober House Tanzania Al-Karim Banji akiwa na wajumbe wengine wa mtandao huo wakimsubiri Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais Menijementi ya Utumishi wa Umma George Mkuchika aliyemuwakilisha Makamu wa Rais Samia Suluh Hassan aliyekuwa mgeni rasmi.