Na Moshy Kiyungi
Licha ya kuwa ni mwanamuziki, Akon ni mwekezaji maarufu aliyeamua kutumia tasnia yake ya muziki kukabiliana na maendeleo endelevu ya watu wa barani Afrika. Nyota huyo wa R & B alizindua mpango maalum wa kutoa mafunzo unaoitwa ‘Akon Angaza Afrika’ ambao una lengo la kutumia nguvu ya Jua kuzalisha umeme.
Katika uzinduzi huo uliofanyika katika mjini mkuu wa Bamako nchini Mali, Akon anayomatumaini ya kuwafikia watu milioni 600 barani wa Afrika. Mafunzo hayo yatafundisha wadau wa mradi huo jinsi ya kutunza mifumo ya nishati hiyo inayoendeshwa kwa nguvu ya jua. Samba Bathily ambaye ni mwanzilishi msaidizi wa mradi huo, alisema jua na teknolojia hiyo ya ubunifu itasaidia kuleta umeme katika nyumba na kwenye jamii kwa ujumla.
Akon alielezea sababu ya kuwekeza zaidi kwenye nishati ya umeme, alisema kwamba ni moja ya njia ya kutoa fursa za kiuchumi na huduma za kijamii kwa Bara la Afrika, ambalo sehemu kubwa ni giza kutokana na ukosefu wa nishati ya umeme. Rapa wa huyo wa R & B Akon, alifanya ziara katika nchi ya Liberia kwa ajili ya kuweka umeme wa jua katika shule mbili za msingi katika taifa hilo lililo Magharibi ya Afrika.
Akon ambaye ni mwenye asili ya nchi ya Senegal, anashirikiana na kampuni ya Bridge International Academies pamoja na ushirikiano na mashirika mengine ya Kimatifa kusimamia shule 50 nchini Liberia. Wakati msafara wake wa magari ulipokuwa ukipita katika mji mkuu wa Monrovia, chini ya ulinzi wa maafisa wa polisi, Akon alisema kuwa inasikitisha kuona kwamba hakuna umeme katika barabara ya kilomita 50 kutoka uwanja wa ndege.
Mradi huo wa Akon utasaidia watu wa bara la Afrika kuweza kuwa na umeme tofauti na sasa ambapo changamoto za ukosefu umeme umekuwa mkubwa sana. Majina kamili ya mwekezaji huyu anaitwa Aliaumie Damala Badara Akon Thiam, Mmarekani mwenye asili ya Senegal. Ni mtunzi, mwimbaji wa nyimbo za R & B, mtayarishaji wa rekodi, mfanyabiashara mkubwa pia ni mhisani.
Baadhi ya vyombo vya habari viliripoti kwamba Akon alizaliwa mwaka 1981, Taasisi zingine ikiwemo AP ilidai kuwa alizaliwa Aprili 30, 1973 mtaa wa St. Luis nchini Marekani. Ili kukwepa shughuli za kutafuta kibali cha uhamiaji, aliishi mjini Dakar, Senegal hadi alipofikisha umri wa miaka 7, kisha akabadilishana kati ya kuishi nchini Senegal na Marekani hadi alipofikisha umri wa miaka 15, alipohamia kabisa mjini Jersey, New Jersey huko Marekani.
Akon alikulia katika mandhari ya muziki na alifundishwa kucheza ala kadhaa ikiwemo djembe, kinanda, gitaa, ngoma na vingine vingi zaidi ya vyombo tano vya muziki. Alianza kutambua kipawa chake cha muziki, akaanza kujivunia historia ya muziki iliyokuwa kwenye familia yake kwakuwa alizaliwana wazazi Baba na mama yake wote walikuwa wanamuziki.
Mwaka 2003 alifungwa jela miaka mitatu kutokana na swala ya kuhusishwa ya wizi. Lakini makala ya jarida la Smoking Gun, ilieleza kuwa Akon hakushtakiwa na hatia yoyote ya uhalifu na hakutumikia kifungo chochote gerezani kati ya 1999 na 2002 kama alivyodai hapo awali. Yeye alisema kwamba jaribio la jarida la The Smoking Gun la kumharibia jina halikuwa na maana yoyote kwani hilo lilikuwa ni jambo alilojaribu kulisahau.
Akon alisema kuwa yeye hajawahi kukaa kwenye jela kipindi cha miaka 3 mfululizo, lakini amewahi kukaa kwa vipindi vifupi vifupi ambavyo vimefikia miaka mitatu. Baada ya kutoka jela alikutana na jamaa anayeitwa Stephen, ambaye ndiye aliyegundua kipaji chake kisha wakawa marafiki wakubwa. Kwa upendo alikuwanao Stephen, aliamua kumfundisha Akon maswala ya muziki akiwa huko Atlanta, Georgia nchini Marekani.
Kwa sababu ambazo hazikuwekwa wazi, Akon alishindwa kusaini katika record label ya rafiki yake Stephen, hivyo akabaki mtaani tu. Alianza kuandika na kurekodi nyimbo katika studio yake ya nyumbani. Tepu zake zilifika kwenye kampuni ya SRC/Universal, ambayo ilitoa albumu (LP) yake ya kwanza ya Trouble Juni 2004. Albamu hiyo ina nyimbo kama "Locked Up" na "Lonely", "Belly Dancer (Bananza)", "Pot of Gold", na "Ghetto."
Ilikuwa albamu ya kwanza kutolewa na kampuni yake mpya ya kurekodi ya Konvict Music. Wimbo wa "Locked Up" uliorodheshwa kwa nyimbo 10 bora nchini Marekani na tano bora nchini Uingereza Albamu hiyo ni mseto wa mtindo mwororo wa Akon wa Afrika Magharibi, ukichanganywa na MIDU kutoka Pwani ya Mashariki na Kusini. Nyimbo nyingi za Akon huanza kwa sauti ya kufunguka kwa mlango wa jela naye akitamka neno "Konvict".
Mwaka wa 2005 alitoa wimbo "Lonely" (ambao ni sampuli ya wimbo wa Bobby Vinton wa "Mr Lonely"). Wimbo huo uliorodheshwa miongoni mwa nyimbo tano bora kwenye orodha ya bango la nyimbo 100 mashuhuri, na ukaongoza kwenye chati katika nchi ya Australia, Uingereza na Ujerumani. Akon kisha alitoa wimbo mwingine ulioitwa 'Moonshine', akishirikiana na msanii kutoka New Zealand aliyeitwa Savage.
Wimbo huo ulivuma huko New Zealand na Australia, ukawa namba moja katika chati ya New Zealand. Akon hivi sasa ameanzisha kampuni mbili za kurekodi ambazo ni, Konvict Muzik na Kon Live Distribution. Anajulikana kama mmojawapo kati ya waimbaji waliofanikiwa kwa uhodari zaidi wa mtindo wa R & B karne ya 21. Msanii huyo Akon huingiza kibindoni zaidi ya dola milioni 30 kwa mwaka . Haya ni kulingana na jarida la Forbes.
Mwaka wa 2004 alipata umashuhuri kufuatia kutolewa kwa wimbo wa "Locked Up", uliokuwa wa kwanza kutoka kwa albamu yake ya kwanza iliyoitwa, Trouble. Albamu yake ya pili, Konvicted, ilimwezesha kuteuliwa kushindania Tuzo la Grammy kutokana na wimbo wa "Smack That". Albamu ya pili ya Akon, Konvicted ilitolewa tarehe 14 Novemba 2006, Ilikuwa na nyimbo alizoshirikisha waimbaji kama Eminem, Snoop Dogg na Styles P.
Albamu hiyo ya Konvicted ilipata kushika nafasi pili kwenye orodha ya Bango ' la nyimbo 200 mashuhuri, na kuuza nakala 286,000 katika wiki yake ya kwanza. Mwaka huohuo Akon alivunja rekodi ya orodha ya nyimbo 100 mashuhuri.
Wimbo wake wa "Smack That" ulipata mafanikio ya juu zaidi kwa kuruka kutoka namba 95 hadi namba 7. Ulipendekezwa kushindana katika kategoria ya Best Rap / Sung Collaboration katika mashindano ya 49 ya Grammy Awards, lakini ulishindwa na ule wa Justin Timberlake na wa T.I. wa "My Love". Msanii Akon mwaka wa 2006, alifungua kampuni yake mpya ya Kon Live Distribution chini ya Interscope Records. Msanii wake wa kwanza kusaini mkataba naye alikuwa ni Ray Lavender
Alishirikiana na msanii Chamillionaire kwenye tepu yake ya, Mixtape Messiah 2, akishiriki kwenye kibao "Ridin 'Overseas", ambacho alikuwa amekitayarisha. Julai 07, 2007 Akon alitumbuiza katika hafla ya American leg of Live Earth. Novemba 2007, Akon alirekodi toleo jipya la wimbo "Wanna Be Startin 'Somethin'" akiwa na Michael Jackson.
Ilipotimu Februari 2008, toleo jipya jingine la wimbo huo lilitolewa wakati wa maadhimisho ya 25 ya kutolewa upya kwa video ya Michael Jackson ya Thriller. Wimbo unaoitwa "Hold My Hand" wa R & B, Julai 2008, ulisambaa kwenye mtandao, ulioimbwa kwa ushirikiano kati ya Michael Jackson na Akon, na uliotungwa na Claude Kelly.
Baada ya kifo cha ghafla cha mfalme wa Pop Michael Jackson, ambaye Akon alikuwa akifanya kazi naye katika miaka ya mwisho, Akon alitoa wimbo wa kuonyesha heshima unaoitwa "Cry Out Of Joy". Akon na Michael Jackson walikuwa marafiki wa karibu katika wakati huo wa mwisho wa maisha ya Michael Jackon
Aidha aliwahi kufanyakazi na Whitney Houston katika kutayarisha albamu yake mpya ya mwaka wa 2009 iitwayo I Look To You. Yeye alishiriki katika wimbo wa "Like I Never Left". Inadaiwa kuwa Akon aliwahi kushiriki katika ulanguzi wa madawa ya kulevya, lakini yeye alikanusha akisema hajawahi kutumia madawa hayo, ingawa maneno ya baadhi ya nyimbo zake yanakinzana na makanusho yake.
Mwaka 2014 alifanya kampeni yake ya Akon Lighting Africa ambayo alifunga umeme katika nchi 15 za Afrika. Akon ana mipango ya kurekodi filamu nzima yenye jina Illegal Alien. Filamu hii imejikita katika baadhi ya matukio ya maisha yake na mwigizaji Mekhi Phifer atamwigiza yeye.
Mnamo 27 Aprili 2008, Akon alionekana na Colby O'Donis katika Dance on Sunset. Serikali ya Sri Lanka imemuwekea ‘ngumu’ msanii Akon kwa kile kinachodaiwa kuwa aliingilia imani ya dini ya Budha kwenye Video ya wimbo wake inayokwenda kwa jina la Sexy Bith, ambayo inaonyesha mdada mrembo akicheza mbele ya sanamu hiyo.
Mamia ya waandamanaji walijitokeza na kuandamana hadi kwenye jengo la Kampuni ambayo inaandaa ziara ya mwanamuziki huyo mapema mwezi wa nane. Alipoulizwa Akon alikaririwa na jarida moja akisema kuwa hana taarifa hizo na wala hakuwaza kufanya hilo kwa dhamira.
Hii ni mara ya pili wanamuziki wa Afrika kuleta ‘Kasheshe’ huko Asia, kuna wakati mamia ya watu waliandamana huko Darusalaam – Brunei, kwa madai wimbo wa JB Mpiana wa Sultan De Brunei Kastiko. Walidema kuwa wimbo huo umemkashifu Sultani wao kwa vile umemtaja na wanadada wanacheza nusu uchi.
Aidha Akon analo Shirika lake la kutoa msaada kwa watoto wasiojiweza barani Afrika liitwalo Konfidence Foundation pia anamiliki mgodi wa Almasi nchini Afrika ya Kusini. Aliwahi kushiriki katika mikutano kadhaa na viongozi waandamizi ili kujadili utekelezaji wa miradi ya kuzalisha umeme mjini Kigali, Rwanda
Mikutano hiyo ilifautia baada ya Akon kuanzisha mradi wake wa “Akon Lighting Africa”. Serikali ya Rwanda inakabiliwa na matatizo ya vyanzo vyakuzalisha nguvu ya umeme ambapo imepelekea kutumia njia mbadala ya nishati ya jua ambayo itafikisha angalau asilimia 60 ya matumizi ya nishati ifikapo mwaka 2020.
Vyanzo vya habari vilifahamisha kuwa lengo la nyota huyo wa muziki mwenye asili ya Senegal ni kuchunguza maeneo mapya ya uwekezaji katika miradi ya Nishati mbadala katika nchi 14 za Afrika zilizochaguliwa. Akon hivi karibuni alifungua 'Solar Academy' nchini Mali kwa lengo la kufanya uvumbuzi wa maendeleo katika teknolojia ya Nishati ya jua kwa kuwaelimisha wahandisi ambao hushughulikia kazi ya kufikisha umeme katika maeneo ya vijijini barani Afrika.
Rapa wa miondoko ya R&B anayeongoza katika chati za juu za muziki huo duniani, alifanya ziara nchini Liberia kuweka umeme wa jua katika shule mbili za msingi katika taifa hilo la Afrika Magharibi. Nchini humo anashirikiana na Kampuni ya Bridge International Academies pamoja na ushirikiano na mashirika mengine ya Kimatifa kusimamia shule 50 nchini Liberia.
Mradi huo wa Akon utasaidia watu wengi wa bara la Afrika kuweza kuwa na umeme tofauti na sasa ambapo changamoto za ukosefu umeme umekuwa mkubwa sana.
Kila la heri Akon kukumbuka asili yako Afrika.
Mwandishi wa makala hii anapatika kwa namba 0784331200, 0713331200, 0736331200, 0784331200 na 0767331200.