- Pamoja na Changamoto ipo 'hangover' ya 'mission-towns' inasumbua bado!
Na David KAFULILA Juni23/19
Nimewiwa kuweka neno katika katika kipindi hiki cha mjadala huu wa Bajeti kutokana na ukweli kwamba hii ni Bajeti ya nne kati ya tano zinazohitimisha ngwe ya kwanza ya Rais Dr John Pombe Magufuli akiwatumikia watanzania katika nafasi ya Mkuu wa nchi, Mkuu wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu. Kifupi ni muda unaoweza kutoa picha ya kutosha kuhusu Taifa gani linasukwa chini ya awamu ya tano!
Kwakuwa mjadala wa Bajeti unagusa wadau wengi na hivyo niwajibu kila mdau kutoa maoni, basi ieleweke vema kwamba kutofautiana maoni miongoni mwa wadau wa nchi ndio afya ya mjadala wenyewe.
Binafsi nimependa kutamka kwa kifupi mafungu kumi (10) ya ukweli ambao ningependa yaeleweke kuwa ni kuweka kumbukumbu sawa kwasababu katika mijadala hii wadau tunaweza kuzidiana na kutofautiana kiwango cha taarifa.
# Fungu la kwanza ninapenda kutofautiana na maoni ya chama fulani kuwa takwimu za ukuaji uchumi ( Pato la Taifa) zina walakini kwa hoja kwamba huwa haiwezekani ukuaji wa pato la mtu mmoja mmoja kukua kwa kasi ndogo kuliko kasi ya ukuaji wa pato la Taifa. Kwamba haiwezekani Serikali iseme ukuaji uchumi ni asilimia7% kama ukuaji wa pato la mtu mmoja mmoja (per capita income) ni asilimia4.4%.
# Naomba ieleweke kwamba kwa mujibu wa takwimu za Bank ya dunia, nchi kadhaa katika miaka kadhaa zimepata kuwa na asilimia kubwa ya ukuaji pato la Taifa kuliko pato la mtu mmoja mmoja. Mfano; Kenya mwaka 2011 pato la Taifa lilikua kwa asilimia 6.1% lakini Pato la mtu mmoja mmoja ( per capita income ) ilikua asilimia 3.3%. Mwaka 2015 nchi hiyohiyo pato la Taifa lilikua kwa asilimia 5.7% wakati pato la mtu mmoja mmoja lilikua kwa asilimia 3% . Sio Kenya tu, Botswana mwaka 2017 pato lake lilikua kwa asilimia 2.4% lakini pato la mtu mmoja mmoja lilikua kwa asilimia 0.5% au Ghana ambayo mwaka 2017 pato lake ilikua kwa asilimia 8.1% wakati pato la mtu mmoja mmoja lilikua kwa asilimia 5.8%.Nikatika msingi huo hoja kwamba Pato la Taifa Tanzania haliwezi kukua kwa asilimia 7% kwakuwa pato la mtu mmoja mmoja ( per capita income ) ni asilimia4% inakosa uzito.
# Fungu la Pili; napongeza uamuzi wa Serikali kuongeza kodi ya uagizaji nje wa nywele bandia za kina mama . Nimeshangaa kuona hata hilo likipingwa kwasababu ni moja ya mambo yasio na tija kwa Taifa. Nimepata kusoma ripoti ya mtafiti Sam Piranty ilochapwa BBC Desemba2015 kuonesha namna Afrika inavopoteza fedha za kigeni kuagiza vitu visio lazma sana kutoka China.
# Katika ripoti hiyo ilionesha kwamba nchi ya Benin mwaka huo iliongoza kwa kuagiiza nywele na ndevu bandia za thaman ya dola 411( zaidi ya bilioni900) kutoka China. Nigeria iliongoza kwa kuagiza miswaki milioni 159 kutoka China. Afrika kusini iliongoza kwa kuagiza chupi za kiume milioni16 na Kenya iliongoza kwa kuagiza vyoo vya kukaa kwa zaidi ya dola milioni8 au bilioni20.
# Ripoti hiyo ilikuwa mjadala mkubwa kwa misingi kwamba afrika lazima ipunguze matumizi ya fedha za kigeni kuagiza vitu visio lazma sana kiuchumi. .Hivyo uamuzi wa kuongeza kodi katika uagizaji nywele bandia ni jambo la maana saana kwa lengo la kuhakikisha kama Taifa hatuingii kundi la vinara wa matumizi makubwa ya fedha za kigeni kuagiza vitu visio muhimu sana kiuchumi .Nasisitiza bidhaa hii haina umuhimu sana kuagizwa nje na ingebidi kodi zaidi ya hiyo ingekuwa afya ili kama nilazma basi sizalishwe ndani
# Fungu la tatu nigusie kidogo kuhusu uimara wa uchumi ! ningependa kuanza kwa kupongeza uamuzi wa Serikali ya awamu ya tano mwaka jana2018 kukubali kufanyiwa kitu inaitwa CREDIT RATING...ambapo Serikali inapimwa katika mizania ya kimataifa kuona uwezo wake kumudu deni na kukopesheka ambapo kwa hakika kinachopimwa ni msuli wa uchumi wa nchi husika. Katika matokeo yake yalotolewa Machi4,2018, matokeo yanayopatokana katika tovuti ya Taasisi hiyo ambapo inaonesha kwamba Tanzania ilifanya vizuri kuliko nchi zote afrika mashariki kwa uwezo wake kiuchumi kumudu deni na kukopa zaidi..Ilikuwa habari nzito iliyozua mjadala Kenya ambapo Gazeti la Daily Business lilitoka na kichwa cha habari...." Tanzania Rated Higher than Kenya " kama inavyosomeka kwenye mtandao wa Gazeti hilo hapa-
https://www.businessdailyafrica.com/markets/marketnews/US-agency-assigns-Tanzania-higher-credit-rating-than-Kenya/3815534-4329666-jpuyco/index.html
Kwamba wakati kwenye viwango Tanzania ilionekana kuwa na B1, nchi za Kenya na Uganda zilikuwa na B2.
# Kwa Tanzania hii ilikuwa mara ya kwanza tangu tupate Uhuru ambapo kwa bahati nzuri tulifanyiwa tathimini huo na taasisi ya Moody's ambayo inaongoza duniani katika kazi hizo ambapo asilimia 45% ya kazi hizi duniani inafanya yenyewe. Vema ieleweke tu kwamba ripoti za taasisi hizi za credit rating ndio kwa kiasi kikubwa hutumiwa na mataifa mbalimbali duniani yanayomgozwa kisasa( modern gorvenance).
#Fungu la nne; Nilipenda nigusie kwann kelele kuhusu utitiri wa leseni na vibali zimekuwa kubwa sasa kuliko zamani. Je nikweli kwamba leseni na vibali husika vimeanza leo au awamu hii ya5? Kwanza ieleweke kwamba nakubaliana na ukweli kuwa utitiri wa vibali na leseni ni changamoto ktk urahisi wa kufanya Biashara. Lakini ieleweke pia kwamba utitiri huu haujaletwa na awamu ya 5 bali usimamizi madhubuti wa taratibu katika awamu ya 5 na kuzibwa kwa mianya ndio sababu ya utitiri huu wa vibali kuonekana machungu yake. Kabla ya awamu ya 5 nchi ilikuwa inakwenda kwa "mission-town" hivyo wingi huo wa vibali na leseni usingeweza kuleta maumivu.
# Fungu la tano linatoka Fungu la nne ambapo linahusu BLUEPRINT na mazingira ya Biashara. Kwamba uamuzi wa Serikali kukubali kuanza kutekeleza makubaliano yake na sekta binafsi yaliyomo ndani ya kutabu maarufu kama BluePrint ni uamuzi wa kimapinduzi kwani mapungufu ya kitaasisi, kimfumo, kisheria na kisera yaliyokuwepo tangu awamu ya tatu mpaka sasa yataanza na yameanza kufanyiwa kazi kurekebisha mwendendo wa biashara. Uamuzi wa kufuta takribani aina 54 za ushuru na tozo ambazo zilikuwa kero ni sehemu ya dhamira ya utekelezaji huo.
Fungu la sita nimependa kugusia dhana ya Uchumi wa Vitu dhidi ya Uchumi wa watu. Labda nianze kwa kurejea hoja ya Mchumi Dambisa Moyo kwenye kitabu cha Edge Of Chaos alichokizindua Aprili2018 na kusababisha mjadala mkali duniani ambapo pamoja na mambo mengine amerejea hoja muhimu kwamba Afrika imendelea kuwa tegemezi kwasababu viongozi wake hawana uwezo kufanya maamuzi makubwa kwa faida ya vizazi vijavyo kwa hofu za uchaguzi.
#Viongozi hao wanajikuta wanatafuta majibu ya muda mfupi badala ufumbuzi wa kudumu. Vema ieleweke kwanza kwamba takwimu za kiasi kinachotolewa na serikali kwenye sekta za maji, elimu na afya tangu awamu ha tano kuingia madarakani nikikubwa kuliko tulikotoka.Pia vema ieleweke pia kwamba kwenye nchi lazma ujenge kwanza msingi wa uzalishaji kabla ya huduma. Kuita ujenzi wa reli ya kisasa au Mradi mkubwa wa umeme wa zaidi ya 2100MW wa Stirgglers kuwa ni maendeleo ya vitu ni kutokuelewa dhana nyepesi kiuchumi kwamba ni uchumi unaozalisha unaoweza kuhudumia watu na sio kinyume chake.miradi hiyo mikubwa inaweka misingi ya kutanua uzalishaji na hatimaye kuongeza uwezo wa uchumi kutoa huduma zaidi.
# Lakini zaidi ya ukweli huo, tukitaka kujua lini uchumi wetu ulihudumia watu na lini ulihudumia vitu ni kuangalia upatikanaji huduma hizo. Miradi ya maji, umeme, elimu na afya ni mikubwa Karibu kila Wilaya. Wakati awamu ya 5 inaingia madarakani kiasi ambacho kilitolewa na serikali MSD kwajili ya kununua dawa na vifaa tiba hakikuzidi shilingi 31bn mwaka 2015 wakati leo kiasi kinachotolewa na serikali kwajili ya kununua dawa na vifaa tiba ni zaidi ya 270bn sawa na ongezeko la dawa kwa zaidi ya asilimia900%. Hizi dawa ni kwajili ya afya za watu sio vitu.
#Fungu la saba ningependa kugusia uwezo wa Serikali kukusanya kodi. Kwanza ieleweke kuwa duniani kote huchukua miongo kadhaa kwa mfanyabiashara kutamani kulipa kodi kwa mapenzi yake. Ni ushindan siku zote. Mapinduzi katika makusanyo ya kodi kutoka shilingi 850bn kwa mwezi mpaka wastan wa shilingi 1300bn sawa na ongezeko la asilimia zaidi ya 52% yanaweza yasitoshe lakini ni makubwa kupata kutokea tena ndani ya muda mfupi .
#Tumetoka kwenye kipindi ambacho serikali ilibidi kukopa ili kulipa mshahara ya watumishi wake. Madhara yake ilikuwa ni pamoja na Serikali kukopa mno kwenye hatifungani hata kufikia serikali kukopa kwa riba zaidi ya asilimia 17% kwa hatifungani za siku 365 . Madhara ya hali hiyo kwa sekta binafsi ilikuwa kusababisha riba kwenye bank za biashara kupaa kwani Bank za biashara hutumia kigezo cha riba kwenye hatifungani kuamua riba kwenye bank zao kwa sekta binafsi.
#Ndio sababu ya riba kwenye bank kufika asilimia 23% mwaka 2015 ni kwasababu serikali ilikopa kwa asilimia17%.lakini kwasasa pamoja na deni kuongezeka bado serikali haina kiu na udharula wa kukopa kulinganisha na tulikotoka. Ndio sababu inakopa kwa riba ya asilimia 5% mwaka 208 kutoka asilimia17% mwaka 2015 na hiyo ndio sababu ya kwann sasa bank zinakopesha kwa asilimia 13%mpaka 17% kutoka asilimia 23% kabla ya JPM.
# Fungu la nane nimependa kurejea kilichosemwa na Mkurugenzi wa IMF, Bi Christine Legarde alitembelea Tume ya Uchumi wa Afrika yenye makao yake makuu jijini Addis Ababa Ethiopia ,Disemba 2017 ambapo alipoulizwa ni mataifa gani Afrika ambayo mwelekeo wake kiuchumi unachukua njia ya vietnam kiviwanda alitaja Tanzania, Nigeria, Ethiopia na Kenya. ( Rejea Jarida la Quartz , Disemba2017). Huu ndio mwelekeo. Unachangamoto nyingi lakini JPM yupo kwenye njia sahihi.
Fungu la tisa niwakumbushe tu utafiti uliochapishwa kwenye Jarida la Havard Business Review ukioonesha kwamba China inatarajiwa kupoteza ajira kati ya milioni 85 mpaka milioni100 kutokana na gharama ya ujira kupanda. Ukweli huu ulisisitizwa pia na Prof nguli wa uchumi duniani, Joseph Stirglitz kwa msisitizo alipohutubia wanazuoni wa Tanzania ukumbi wa Nkurumah Chuokikuu cha Sar es Salaam mwaka jana kwamba mitaji hiyo inaweza kuelekea zaidi Afrika lakin nchi hizo ziwe na miundombinu ya viwanda ambayo pamoja na rasilimali watu ni pamoja ubora wa miundombinu kwa urahisi wa biashara
# Fungu la kumi nifunge kwa kusema hakuna njia ya kujenga uchumi isiyo na mbadala isipokuwa kinachozingatiwa ni gharama ya hiari( opportunity cost) isizidi gharama halisi. Ndio maana mijadala ya kiuchumi ni yakudumu. Walewale walioweza kuhoji kwann Serikali inakusanya kiduchu ndio wanalalamika kwann Serikali ikusanye sana, inaumiza wafanyabishara! Wale wale waliohoji iweje nchi ya nusu karne toka ipate Uhuru lakn imebaki haina reli wala ndege ndio haohao wanaohoji kwann ijengwe reli na kununuliwa ndege sio vitu vingine? Wale wale waliosema tunaporwa kwenye madini miaka yote ndio haohao wanaopinga kwann wawekezaji kwenye madini wafanyiwe unyama na kwamba ni kufifisha sekta ya madini. Na vipindi vyote wanaweza kuonekana kuwa na hoja hasa katika nchi ambayo bado tabaka la kati kiuchumi ni dogo hivyo kunakuwa na changamoto ya wasikilizaji wengi kutambua nilichokiita gharama ya hiari ( opportunity cost).
# Imekuwa bahati kwamba kwenye sekta kama ya madini iliyofanyiwa mabadiliko na kupitia msukosuko mkubwa kuliko sekta yoyote tangu awamu ya 5 kuingia madarani, ndio sekta ambayo mauzo ya nje yamezidi kuongezeka kinyume na ilivyokadiriwa na wakosoaji wa JPM. Sekta ya madini leo inachangia pakubwa kwenye pato la Taifa kuliko kabla na kwenye mauzo ya nje mchango wake umezidi kuongezeka kutoka mauzo ya takribani dola 1.2bn mwaka 2015 mpaka zaidi ya dola bilioni 1.6 mwaka 2018. Naam takwimu hazidanganyi lakini ni wazi kwamba ipo homa ya mpito kutoka'uchumi wa 'mission-town kwenda uchumi halisi '