Na Moshy Kiyungi
Pasipo kuyataja majina ya gwiji wa muziki wa rhumba Joseph Kabasele ‘Grand Kalle, utakuwa hujakamilisha upaswavyo kusimulia historia ya muziki huo toka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Nguli huyo licha ya kwamba hatunaye duniani, jina na sifa zake zitabaki kuwa historia ya muziki nchini humo. Kabasele alikuwa ni baba na nyota kuu ilioleta maendeleo na mabadiriko makubwa kwenye muziki wa rumba DRC.
Kwa mujibu wa Wasifu wake unaeleza kuwa alizaliwa Desemba 16,1930 mjini Matadi huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Baba yake alikuwa akiitwa mzee Andre Tshimala na mama yake aliitwa Hortense Malula. Joseph Kabasele ndiye aliyekuwa kitinda mimba kwenye familia ya watoto sita.
Yaelezwa kuwa ndiye aliyekuwa mwanamuziki wa kwanza kuvitumia vyombo kadhaa vya muziki na kusababisha yatokee mabadiriko makubwa kwenye sekta hiyo ya muziki. Vyombo hivyo ni pamoja ja tarumbeta, Clarinet, Saxophoni na ngoma.
Mwanamuziki huyo alifahamika pia kwa majina ya ‘Grand Kalle’ , mwanamuziki wa kwanza huko Jamhuri ya Kidemorasia ya Kongo kutumia gitaa la umeme. Joseph Kabasele alikuwa Mkongomani wa kwanza kumiliki bendi yake binafsi ya African Jazz iliyoundwa mwaka 1953, pamoja na studio yake ya Surboum kwa ajili ya kurekodia muziki.
Sifa nyingine za mhenga huyo ni kwamba ndiye aliyemlea kimziki mwanamuziki Rochereau Tabu Ley pamoja kamkuza kimziki aliyekuwa mpiga gitaa mahiri nchini Kongo Dokta Nico Kasanda. Grand Kalle na bendi yake ya African Jazz, walikuwa wakwanza kusafiri kwenda nje ya nchi yao ya DRC.
Walifika katika nchi za za Ulaya, Ubelgiji,Ujerumani, Italia, Ufaransa na zingine nyingi kwa ajili ya kufanya maonesho. Kwenye miaka 1960, Kabasele alitungua kibao kilicho kubalika popote pale Barani Afrika cha Independance Cha Cha. Kibao hicho kilikuwa kikiisifia nchi yake ya Kongo kupewa Uhuru kutoka mikononi mwa Wakoloni.
Kupitia studio yake aliweza kufika Ulaya tena akiambatana na mwanamuziki Franco Luambo Makiadi na kundi lake lote la T.P. OK. Jazz pia akawanunulia seti ya vyombo vipya vya muziki. Grand Kalle alisoma shule ya msingi ya Institute Saint Joseph, iliokuwa ikimilikiwa na ma Padre, Jijini Kinshasa.
Akiwa shuleni humo, alijiunga na kwaya la Kanisa Katoliki akiwa na umri mdogo wa miaka 8. Kabasele alitokea kuwa mwimbaji mzuri huku akitumia kwa umaridadi sauti yake ya Tenor, huku akiendelea na masomo ya Sekondari kwenye Shule ya (Ecomoraph). Umaarufu wake ulipelekea kuwa kivutio na kipenzi cha wengi wakiwemo wanafunzi pia wanafunzi wenzake shuleni humo.
Licha ya uimbaji wa nyimbo, Kabasele pia alikuwa akipenda michezo na kupelekea kupendwa sana na watu hususan wanawake. Wahenga walinena kuwa “kila kizuri kina ubaya wake” Pamoja na sifa zote hizo, Kabasele alikuwa na tabia mbaya ya utovu wa nidhamu. Mapadre waladiriki kuchukua hatua ya kumfukuza Shule.
Katika kipindi cha Ukoloni, shule takriban zote zilikuwa zikimilikiwa na Mapadre, kwahiyo ikamjia vigumu kwa Grand Kalle kupata shule nyingine itakayo mkubali. Kwakuwa hapakuwa na shule inayo mkubali, ilimbidi atafute kazi. Nguli huyo akabahatika kupata ajiria kama Katibu kwenye makampuni tofauti Jijini Kinshasa.
Mwaka 1947, kutokana na ushawishi wa rafiki yake Georges Dula aka ‘Geoder’, alipelekea kwenda kujiunga na kundi la muziki la OTC. Bila kusita alikubaliana na pendekezo hilo, kwa kuwa aliona kwamba njia yake ya kuwa ‘Nyota’ inaanza kufunguka. Kuna kipindi Grand Kalle alifanikiwa kutoa wimbo Palmolive, ambapo aliwasifia wasichana kwamba ni warembo na wananukia manukato mazuri kama ya Sabuni Palmolive.
Mwaka 1950, wazo likamjia aende kujaribia kipaji chake kwa Mr.Moussa Benatard, ambaye alikuwa mfanyabiashara Myahudi tena mmiliki wa Studio ya OPIKA. Baada ya Myahudi huyo kumfanya majaribio, akaona kwamba Kabasele anacho kipaji, ila anastahiki asaidiwe, aongozwe, afundishwe namna ya kuimba kwenye Studio.
Ndipo alipowekwa chini ya usimamizi wa mpiga gitaa mashuhuri Zacharie Elenga ‘Jimmy’. Wakafanikiwa kutoa vibao vingi vya Ondruwe , Maboko Likolo, Baninga Baninga, Makombo ya Jimmy na Putulu Emata. Baada ya kuona amepata mafanikio ya nyimbo hizo kuwa mazuri, Grand Kalle akazidi kujipa moyo kwa kuchapa kazi vilivyo, akiwa na nia ya kutaka kujitegemea.
Mwaka 1951, Wazo likamjia la kuunda bendi yake binafsi na ilipotimu mwaka 1953, chini ya usimamizi wake wakaunda bendi ya African Jazz. Bendi hiyo ilikuwa na wanachama kama Roger Izedi, aliyekuwa mwimbaji na upiganji wa Marakasi, Etienne Diluvila aliyekuwa mwimbaji na Bettry, Nicolas Kasanda aliyekuwa akilicharaza gitaa la Solo, Charles Mwamba, Albert Dinga na Albert Taumani walikuwa pia ni wapiga magitaa.
Wengine ni pamoja na Isaac Musekiwa na Dominique Kuntina waliokuwa wakipuliza saxophone, Willy kwa upande wa tarumbeta , Antoine Kaya na Depuissant walikuwa wakizidunda tumba. Mwaka 1954, Grand Kalle bendi yake ya African Jazz walipata tenda ya kwanza na kwenda kutumbuiza katika jiji la Bangui nchini Afrika ya Kati kwenye uzinduzi wa ukumbi wa Dancing Bar Le Rex.
Ziara yao hiyo ilimletea furaha kubwa Grand Kalle sio kimapato, bali kuona yeye na kundi lake African Jazz wanakubalika hadi Kimataifa. Kabasele na kundi lake wakapata sifa nyingi kutokana na nyimbo nzuri kama Parafifi iliyorekodiwa na African Jazz mwaka 1957, Nzela Mosika, Ce n’est pas la peine de divorcer maintenant na nyingine nyingi.
Mwaka 1959, Orchestra African Jazz ikawa kwenye kipindi kigumu kutokana na utumiaji mbaya wa Pesa. Yasemekana Joseph Kabasele alitokea kuwa mbinafsi aliyeshindwa kuwajali wanamuziki wenziwe. Ujio wa Kijana Tabu Ley Rochereau kwenye bendi hiyo, ukaleta nguvu mpya.
Ley akaja na wimbo wake wa Kellya, uliopendwa sana na mashabiki wa muziki wa rhumba. Kundi hilo likaja kupumua kipesa wakati waliposafiri kwenda Ulaya mwaka 1960, kutoa motisha ya kuwasapoti Wanasiasa wa Kongo wakati wa mazungumzo ya Uhuru wa nchi yao yaliyofanyika Jijini Brussels, nchini Ubelgiji.
Safari yao hiyo ya Ulaya iliwaletea sifa nyingi na mafanikio makubwa. Africana Jazz wakatoa vibao vilivyo weka simulizi kwenye historia ya rhumba nchini Jamhumri ya Kidemokrasia ya Kongo hadi leo hii. Nyimbo walizoachia wakati huo zilikuwa za Indépendance Chacha na Table Ronde, zilizokuwa utunzi wake Joseph Kabasele ‘Grand Kalle’
Nyingine zilikuwa za Naweli Boboto na Sentiment Emonani, utunzi wake Vicky Longomba, Tosekana na Mawonso Pamba zilizotungwa na Dechaud Muamba , Sophia Motema na Merengue Soubidou mtunzi akiwa Niko Kasanda. Waliporudi Kinshasa mwaka 1961, pakatokea mzozo ulio sababisha baadhi ya Wanamuziki wa bendi hiyo ya Orchestra African Jazz kujiondoa.
Wanamuziki hao ni pamoja na Dokta Nico Kasanda, Dechaud, Vicky Longomba, Brazzos na wengine wengi. Licha ya kuondokewa na wanamziki hao bendi hiyo ilifaanikiwa kwa mara nyingine kupanda ndege na kwenda Jijini Brussels. Wakiwa huko wakarekodi baadhi ya nyimbo kupitia Studio yake Surboum.
Baadaye bendi ilirudi Kinshasa kwa mbwembwe, sifa zao zikawa nyingi mno. Uongozi wa bendi ya African Jazz chini ya uongozi wa Grand Kalle, ilimsajili mwanamuziki Manu Dibango. Manu Dibango alikuwa maarufu kwa upulizaji wa saxophoni. Mwaka 1962 Grand Kalle akatafuta suluhisho lipatikane ili wanamuziki wote walio jiondoa warudi kwenye bendi yake.
Hatimaye muafaka ukapatikana, ndipo akina Dokta Nico Kasanda, Dechaud Muamba na wengine, wakakubali kurudi katika bendi. Tabu Ley Rochereau alitoa ushauri wa kuchukuliwa kwa mwimbaji Mujos, akitokea bendi T.P. OK. Jazz.
Mwaka 1963, pakatokea kwa mara nyingine tena mgawanyiko mkubwa, sababu ikiwa ni wanamuziki kupiga kelele kutopewa pesa ingawa kazi wanaifanya ipasavyo. Takriban Wanamuziki wote walijiondoa akiwemo Tabu Ley Rochereau, wakaenda kuunda bendi yao mpya ya African Fiesta. Kitendo hicho kilimuumiza sana Grand Kalle, lakini alijipa moyo, akaanza kuisuka upya bendi yake ya African Jazz.
Rafiki na mfadhili wake Jean Foster Manzikala, alimnunulia vyombo vipya vya muziki. Kikosi cha wanamuziki wa bendi hiyo wakati huo kiliwajumuisha akina Nedule Papa Noël, Kambele Damoiseau, Jeannot Bombenga, Mathieu Kuka, Nsita Rolly, Alex Mayukuta, Casino Mutshipule, Munange Maproko na Yuma Michel Sax.
“Sikio la kufa halisikii dawa” usemi huo ulionekana dhahir baada ya katokea purukushani nyingine iliopelekea wanamuziki kujiondoa. Bendi hiyo ya African Jazz ikawa ndicho chanzo cha kuangamia kimuziki. Kwenye Miaka ya 1969-1970, Joseph Kabasele alihama jiji la Kinshasa, akaweka maskani yake jijini Paris nchini Ufaransa.
Akiwa jijini humo, alishirikiana vymema na wanamuziki akina Manu Dibango, Don Gonzalo, Lutula Edo Clary, Jeannot Bombenga, wakaunda bendi iliyopewa majina ya African Team. Bendi hiyo ikatoa vibao vingi vikiwemo vya Gauche-droite égal débordement, Africa mbiance, Bana Congo na Cuba, Laurent Fantôme na Cambridge. Nyingine zilikuwa wa Mayi ya Piyo,Safari Muzuri, Disciplini na KDL na Edona Souzy
Hata hivyo bendi hiyo ya African Team haikudumu kwa siku nyingi, nayo ikasambaratika. Kati ya miaka ya 1973 na 1980, Joseph Kabasele akawa adimu sana jukwaani, alifanya onesho lake la mwisho kwenye ukumbi wa hotel Intercontinental, jijini Kinshasa.
Baada ya Hapo, Hali yake kiafya ikawa inazorota, na kipesa akawa anadidimia vibaya sana. Joseph Kabasele ‘Ggrand Kalle’ aliyefahamika zaidi kama mzee wa msimamo, mzee wa kanuni, Baba wa rumba, alifariki dunia Desemba 11, 1983)akiwa na mri wa miaka 53 Jijini la Paris nchini Ufaransa.
Mwenyezi Mungu ailaze Roho yake mahala pema, Amina.
Mwisho.Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa namba:
0767331200, 0736331200, 0713331200 na 0784331200