Quantcast
Channel: MICHUZI BLOG
Viewing all 110010 articles
Browse latest View live

BEI YA PAMBA NI SH. 1,200 KWA KILO – WAZIRI MKUU

$
0
0


*Amwagiza Katibu Mkuu Kilimo atume timu ichunguze Bodi ya Pamba

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema ana imani kuwa ununuzi wa zao la pamba utaanza mara moja kwa bei ya sh. 1,200 kwa kilo moja katika mikoa yote inayozalisha zao hilo.

Amefikia uamuzi huo baada ya kuwepo kwa sintofahamu ya bei kwa takriban ya wiki nne tangu bei elekezi ilipotangazwa Aprili 30, 2019 mkoani Shinyanga kwamba bei hiyo ianze kutumika kuanzia Mei 2, 2019.

Alikuwa akizungumza na wadau wa sekta ndogo ya pamba kwenye kikao kilichofanyika leo (Jumatano, Mei 29, 2019) kwenye ukumbi wa Chuo cha Benki Kuu, jijini Mwanza. Kikao hicho kilihudhuriwa na Naibu Mawaziri wa Kilimo na Viwanda, Makatibu Wakuu wa Kilimo na Ofisi ya Rais – TAMISEMI na Wakuu wa Mikoa ya Mwanza, Kagera, Mara, Shinyanga, Simiyu na Geita.

Wengine ni wawakilishi wa Wabunge wa mikoa hiyo, Makatibu Tawala wa mikoa, Wakuu wa Wilaya zote za mikoa hiyo, na Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya hizo. Pia kilihudhuriwa na wanunuzi wa pamba, wakulima na maafisa wa benki kadhaa.

Waziri Mkuu aliwaeleza wajumbe wa mkutano huo kwamba Serikali bado inaendelea kutafuta njia nzuri ya kuwakutanisha wadau wa mazao ya kibiashara ili yaweze kuwa na tija kwa wakulima. Alisema kazi hiyo inafanywa wa Wizara ya Kilimo. Mazao hayo ni pamba, chai, kahawa, korosho, tumbaku na chikichi.

Pia alisema Bodi ya Pamba iachiwe jukumu la kutoa leseni za ununuzi wa zao hilo na kwamba Wakurugenzi wa Halmashauri waliokuwa wakifanya kazi hiyo waache mara moja. “Kuna baadhi ya Wakurugenzi wanatoa leseni za ununuzi, lakini wenye Mamlaka ni Bodi ya Pamba. Mnunuzi nenda Bodi ukapate leseni yako,” alisema Waziri Mkuu.

Alitumia fursa hiyo kuwakemea baadhi ya wakurugenzi ambao wamekuwa wakizuia wanunuzi wapya kwenye maeneo na kuendelea kuwakumbatia wanaowataka wao. “Wakurugenzi baadhi yenu mnazuia wanunuzi wapya, mnamtaka fulani tu. Kwa kufanya hivyo, unapungua kiwango cha kilo ambacho wakulima wako wangeuza,” alionya.

‘Wanunuzi nendeni mkajitambulishe kwa Wakuu wa Wilaya au Wakurugenzi ili watambue kwamba mpo kwenye maeneo yao lakini kila mnunuzi anayo haki ya kwenda kununua pamba mahali popote hapa nchini.”
Kuhusu ubora wa pamba, Waziri Mkuu alitaka wananchi waelimishwe ili waache kuweka maji au mchanga kwenye pamba kwa minajili ya kuongeza uzito kwani kwa kufanya hivyo wanachafua jina la Tanzania pindi inapopelekwa kuuzwa nje ya nchi.

Pia alitaka vyama vikuu vya ushirika vijiridhishe kuhusu ubora wa maghala ya kuhifadhia pamba kwenye vyama vya msingi (AMCOS) kwani kwa kufanya hivyo, itawasaidia wakulima wauze mapema pamba yao mara baada ya kuivuna.

Kuhusu mizani, Waziri Mkuu aliiagiza wakala wa vipimo nchini (WMA) waende wakakague mizani ya kwenye AMCOS na kwenye vinu vya kuchambulia pamba (ginneries) kwa sbabu ya tofauti kubwa ya uzito inayojitokeza na kuwalazimisha wakulima kulipia upotevu wa kilo hizo.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mhandisi Mathew Mtigumwe atume wakaguzi kwenye Bodi ya Pamba ili wabainishe matumizi ya sh.100 kwa kila kilo ambazo zimekuwa zikilipwa kwenye bodi hiyo.

“Katibu Mkuu Kilimo lete wakaguzi ndani ya bodi ya pamba, waangalie kwa kipindi cha miaka mitatu toka tulipoanza kukusanya sh. 100 kwa kilo, zimekusanywa shilingi ngapi, na zimetumika kulipia nini.

“Na Mrajisi wa Ushirika nchini ufanye ukaguzi kwenye vyama vikuu vya Ushirika na AMCOS. Uangalie ziko ngapi na zinafanya nini. Kuna AMCOS zina hela, je fedha hiyo imetumika kufanya nini ili kuendeleza zao la pamba. Je zimenunua matrekta au zimelipia posho za vikao,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wanunuzi Binafsi wa Pamba (TCA), Bw. Christopher Gachuma ameshukuru Waziri Mkuu kwa maelekezo aliyoyatoa kuhusu utoaji wa leseni kwani yalikuwa ni kikwazo kikubwa kwa baadhi ya wanunuzi wa zao hilo.

“Suala la utoaji leseni linapaswa lianze mapema lakini kuna wengine hadi sasa bado hawajapata leseni zao.” Aliwataka wanunuzi wa pamba waanze kununua pamba ili msimu wa mauzo uanze kwa kasi.

CHAMA CHA WANASHERIA AFRIKA (PALU )NA TAASISI NYINGINE WAKUTANA ARUSHA KUJADILI MATUMIZI YA DIGITALI DUNIANI

$
0
0
Deonald Dea Afisa mtendaji mkuu wa chama cha Wanasheria wa Afrika (PALU)


Na.Vero Ignatus Arusha.


CHAMA CHA WANASHERIA AFRIKA (PALU )NA TAASISI NYINGINE WAKUTANA ARUSHA KUJADILI MATUMIZI YA DIGITALI DUNIANI

CHAMA cha Wanasheria wa Afrika (PALU) kwa kuahirikiana na Taasisi zingine ikiwemo inayosimamia matumizi ya kidijitali Duniani Article 19, wamekutana Jijini Arusha kwa ajili ya kujadili na kuweka mikakati ya kusimamia haki za watumiaji wa mitandao ya teknolojia ya kidijitali, ili kuwezesha wananchi wa nchi hizo kupata huduma.

Deonald Dea ni Afisa mtendaji mkuu wa chama PALU ambapo amesema kuwa, binadamu wana haki ya kupata huduma ya mawasiliano ya kidijitali ili waweze kuendesha shughuli za kibinadamu vizuri.

Deya alishauri badala ya serikali kukimbilia kufunga mitandao hiyo, wangeiachia Bunge lipitishe sheria nzuri za kusimamia suala hilo na huku Mahakama zikihakikisha zinapewa nafasi za kuhakikisha sheria hizo zinasimamiwa na anayekiuka anapata stahiki yake

Dea amesema kuwa Mawasiliano ni muhimu kwa wakati kama huu sababu mitandao inatumika katika kufanya biashara ,kutoa elimu na hata maswala ya Afya pamoja na mengine mengi.

"Sisi kama binadamu tuna uhuru wa kuzungumza na uhuru wa kupata taarifa sahihi na kwa mfumo wa sasa wa kutumia mawasiliano ya kidijitali kama Intenet ndio njia kubwa za kusambaza habari na hapo kuna sheria zinazotakiwa kuwepo ili kulinda uhuru huu kwa binadamu,”alisema"

Amesema wamekutana wanasheria, wanaharakati, toka nchi za EAC na Maofisa wa haki za binadamu wa jumuiya ya Afrika ya mashariki na Tume ya umoja wa Afrika ya kupambana na Rushwa ,na Mahakama ya Afrika ya Haki za binadamu na kijamii .

"Kwani kweli hata serikali inatumia mitandao hii kufanikisha kukamata wahalifu wa makosa mbalimbali , hivyo vema kila upande ukaheshimu haki ya wengine na sio kukimbilia kuzuia wngine wasipate haki ya mawasiliano,”alisema 

Amesema kuwa pamoja na haki hizo bado zipo baadhi ya serikali ya nchi hizo zinakiuka haki za binadamu za uhuru wa kuhakikisha wanapata mawasiliano kwa kufunga mitandaobya kijamii wakihofia kukashifiwa jambo balo siyo sahihi

Ephraim Kenyanito kutoka Afisa mipango wa kidigitali kutka Article 19 ya nchini Kenya kuwa ni vyema kukawepo na sheria zitakazowasaidia wananchi kutumia vizuri teknoloji kuweza kupata mawasiliano ya haraka na kufanya biashara.

“Hadi sasa hatuwezi kuzifikia nchi zilizoendelea katika matumizi ya kidijitali kwenye masuala mbalimbali , hivyo vema na nchi zetu za EAC tukafanya jitihada kuweka mipango madhubuti ya kusimamia hili na kueneza huduma hizo za mtandao kwa wananchi wote wa nchi za EAC, na hasa vijijini,”alisema Mwisho

Amesema hivi sasa katika nchi nyingi wanawake wananwake hawajaunganishwa kutumia teknolojiankama wanaume hivyo watafiti watumie sheria jinsi ya kufanya ili watu watumie mitandao.

MAGAZETI YA LEO ALHAMISI MEI 30,2019

SERIKALI KUENDELEA KUTATUA CHANGAMOTO ZA WAWEKEZAJI NCHINI.

$
0
0
Waziri wa Nchi – Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki (Mb) akitoa neon la ufunguzi wakati wa mkutano wake na wawekezaji wa Uingereza nchini alipokutana nao Mei 29, 2019 katika Ukumbi wa Mikutano wa Coral Beach Jijini Dar es Salaam ili kujadili masuala ya uwekezaji nchini.
Balozi wa Uingereza Nchini, Mhe. Sarah Cooke akizungumza jambo wakati wa mkutano wa wawekezaji wa nchi hiyo walipokutana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki alipokutana nao Jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira) Mhe.Anthony Mavunde akichangia jambo wakati wa mahojiano na waandishi wa habari walipokutana kujadili masuala ya wawekezaji nchini Jijini Dar es Salaam.Katikati ni Waziri wa Nchi wa ofisi hiyo anayeshughulikia Uwekezaji Mhe. Angellah Kairuki na wa kwanza kushoto ni Balozi wa Uingereza Nchini Mhe. Sarah Cooke.
Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Biashara la Taifa (TNBC) Bi. Oliver Vengula akichangia hoja wakati wa mkuatano huo.
Kamshina wa Kazi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw.Gabriel Malata akichangia hoja kuhusu vibali vya ajira wakati wa mkutano wa wawekezaji wa Uingereza uliofanyika Jijini Dar es Salaam.
Mmoja wa washiriki wa mkutano huo Bw. Russell Stuart akiuliza swali wakati wa Mkutano huo.
Kaimu Mkurugenzi wa Uwekezaji Ofisi ya Waziri Mkuu Aristides Mbwasi akijibu hoja za wajumbe kuhusu masuala ya uwekezaji wakati wa mkutano huo
Waziri wa Nchi – Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki (Mb)akiteta jambo na Balozi wa Uingereza Nchine Mhe. Sarah Cooke wakati wa mkutano huo.
Sehemu ya wajumbe wa mkutano huo wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Nchi – Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki (hayupo pichani) wakati wa mkutano huo.
Mkurugenzi wa Uhamasishaji Uwekezaji Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Bw. John Mnali akiwasilisha mada ya fursa za uwekezaji nchini wakati wa mkutano huo.
Waziri wa Nchi – Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki (Mb) akiteta jambo na Naibu Waziri wa Ofisi hiyo anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde wakati wa Mkutano huo.
Waziri wa Nchi – Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki (Mb) akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa mahojiano kuhusu masuala ya uwekezaji nchini.(PICHA ZOTE NA POFISI YA WAZIRI MKUU)



Serikali imedhamiria kuendelea kutatua changamoto zinazowakabili wawekezaji nchini ili kuhakikisha kunakuwa na mazingira rafiki yatakayowavutia kuwekeza nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji Mhe. Angellah Kairuki wakati akifungua mkutano wa wawekezaji wa Uingereza waliopo nchini walipokutana kujadili masuala ya Uwekezaji uliofanyika Mei 29, 2019 katika Ukumbi wa Mikutano wa Coral Beach Jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo ulihudhuriwa na Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe.Anthony Mavunde, Balozi wa Uingereza Nchini Mhe.Sarah Cooke pamoja na Mwenyekiti wa Makampuni ya Biashara ya Uingereza Bw.Kalpesh Mehta, viongozi wa makampuni ya uwekezaji nchini, pamoja na baadhi ya viongozi wa Taasisi za Sekta ya Umma na Binafsi.

Akizungumza wakati wa mkutano huo, Waziri Kairuki alieleza lengo la kukutana na wawekezaji kutoka Uingereza ni pamoja na kujadili masuala yote yanayowahusu wawekezaji kwa kuzingatia changamoto zinazowakabili na kuona namna bora ya kuzitatua ili kuendelea kufikia lengo la kuwa na mazingira bora ya biashara na uwekezaji nchini.

“Tumezingati umuhimu wa wawekezaji nchini, hivyo tumekutana hii leo ili kusikiliza kero na changamoto zinazowakabili ili kuona namna bora ya kuboresha mazingira na kutambua fursa zilizopo nchini ili kuendelea kuwekeza nchini”, alisema Waziri Kairuki.

Waziri aliongezea kwamba, kwa kuzingatia kuwa mnamo mwezi Machi mwaka 2019 Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli aliutangaza mwaka huu kuwa ni mwaka wa uwekezaji alipokutana na waheshimiwa mabalozi wa nchi za nje ambao wapo nchini ikiwa ni kiashiria cha kufungua mwaka mpya.

Aliongezea kuwa, kwa kuzingatia mchango wa sekta binafsi katika ukuaji wa uchumi ikiwemo ongezeko la ajira hivyo tunapaswa kuzingatia na kuboresha mazingira yatakayochochea kuendelea kuchangia katika uzalishaji wa ajira nyingi nchini.

“Sekta binafsi ndiyo kiini cha ukuaji wa uchumi kwa upande wa kuongeza ajira hivyo tunatambua mchango huo ambapo hadi sasa wawekezaji wa uingereza wamechangia katika ukuaji wa ajira kwa kuzalisha ajira laki tatu,”alisisitiza Waziri Kairuki.

Kwa upande wake Balozi wa Uingereza Nchini Mhe.Sarah Cooke aliipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuona umuhimu wa kukutana pamoja kujadili masuala ya uwekezaji na kuendelea kujadili namna ya kuwezesha wawekezaji kutoka uingereza kuendelea kuwa wadau muhimu nchini na kuhakikisha nchi zote mbili zinanufaika.

“Ni kweli tumeenedelea kuwekeza Tanzania kwa kuzingatia mazingira yaliyopo hivyo ni vyema kukawa na maboresho zaidi katika mazingira hayo kwa kuendelea kutatua changamoto zilizopo kwa sasa ili tuendelea kushirikiana pamoja,” alieleza Balozi.Cooke

Aliongezea kuwa nchi ya Uingereza imelenga kuwa kinara cha uwekezaji katika nchi za Afrika hiyo ni wakati sahihi wa kuendelea kutumia fursa zilizopo barani humo ili kufikia malengo.

“Ifikapo mwaka 2022 Nchi yetu imeweka malengo ya kuwa wawekezaji bora barani Afrika hivyo tunaendelea kushirikianana nchi za Afrika ili kuwa na nia moja na kuwa na mahusiano yenye tija hasa katika masuala ya uwekezaji”,alisema Balozi Cooke.

Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde alieleza kuwa, Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya biashara ili kuchangia ongezeko la ajira kwa vijana wa Kitanzania ili kujikwamua kiuchumi.

Aidha alifafanua kuwa, ili kuendelea kukuza ujuzi kwa vijana na kuondokana na changamoto za ukosefu wa ajira Serikali itaendelea kulinda ajira za watanzania na kuboresha mazingira ya sekta binafsi ambao ni wadau muhimu katika kuzalisha ajira nchini.

MAHAKAMA WILAYA YA KISARAWE YAJINASUA KESI YA MGOGORO WA ARDHI WA WIZARA MALIASILI NA RWEHUMBIZA

$
0
0

NA MWAMVUA MWINYI,KISARAWE

MAHAKAMA ya wilaya ya Kisarawe,mkoani Pwani imejinasua kwenye kesi ya katibu wa kamati ya wakulima wa kijiji cha Chanika Jackson Rwehumbiza pamoja na wizara ya maliasili na utalii na kushauri ipelekwe kwenye mabaraza ya ardhi.

Kesi hiyo namba 24 ya mwaka 2018 ya mgogoro wa ardhi, ilisomwa mbele ya hakimu Devotha Kisoka na mwendesha mashtaka Joseph Mwaipaja ambapo alieleza, Rwehumbiza alishtakiwa kwa kosa la kuingia katika hifadhi ya Kazimzumbwi bila kibali.

Kesi imesikilizwa pande zote na mahakama imegundua kwamba eneo hilo lina mgogoro wa ardhi baina ya wananchi na maliasili.

Kwa mujibu wa sheria mahakama ya jinai inapogundua chanzo ni mgogoro wa ardhi inashauri kesi hiyo ipelekwe kwenye mabaraza ya ardhi,"::Kwa maana hiyo,imegundua ni mgogoro wa ardhi hivyo shauri hilo liende kwenye mamlaka ya ardhi ili kama likirudi lirudi kama jinai.

Alielezea kwamba,tafsiri yake mahakama haijatamka eneo ni la nani baina ya pande hizo mbili na haiwezi kutamka mmiliki halali wala mshindi ni nani wa kesi kwakuwa si mahakama husika wa usuluhishi wa migogoro ya ardhi.

Kwa upande wake, Rwehumbiza alishukuru maamuzi hayo na kudai hukumu imetenda haki .Alisema mgogoro huo ni wa miaka 18 na wao hawana nia ya kupingana na serikali hivyo wanaomba mipaka iwekwe ili kujua wananchi wanapaswa kuishia wapi.

Rwehumbiza alibainisha,hukumu hiyo ni ya tano tangu kuanza kushtakiwa na zote hazijakatwa rufaa ameiomba serikali ya awamu ya tano pamoja na chama cha mapinduzi (CCM) kuwasaidia kuingilia kati mgogoro huo ili waishi kwa amani.

"Sisi tunarudi mashambani kuanzia leo,tumepata hasara na kuishi bila kuendelea na shughuli zetu kipindi kirefu,"Tumelilia haki yetu miaka sasa na hatimae leo mungu katusaidia"alifafanua.

Mkulima mwingine Mohammed Sutty alisema wapo wananchi zaidi ya 1,000 katika sakata hilo ,haki imechelewa lakini hatimae wameipata.



WAZIRI LUKUVI ATOA MAAGIZO MAZITO KWA BODI YA WAKURUGENZI NHC

$
0
0
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi ameipa maagizo mazito Bodi mpya ya Wakurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ambapo ameipa miezi mitatu ya kufanyia maamuzi maagizo yake.

Waziri Lukuvi ametoa maagizo hayo katika Makao Makuu ya Wizara ya Ardhi jijini Dodoma wakati akizindua rasmi Bodi mpya ya Wakurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ambao wameteuliwa hivi karibuni hayo ameipa bodi hiyo mpya miezi mitatu ya kujifunza yale watakayoyasimamia kwani wengi wao wanatoka katika idara nyingine zisizo za NHC hivyo wapo huru kuchunguza idara yoyote na kama kuna mkurugenzi haoneshi ushirikiano wamlipoti na yeye atamchukulia hatua.

Mei 27 mwaka huu Uteuzi huu umefanyika baada ya kuvunjwa kwa Bodi hiyo Mwaka 2017 ambapo Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuri alimteuwa Mwenyekiti wa Bodi Dkt. Sophia Kongela kufuatiwa na baadae Mhe. Lukuvi kumteua Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba Maulid Banyani kukaimu nafasi hizo.

Wajumbe hao wapya ni pamoja na Bi. Sauda Msemo Kamishna Msaidizi Sera na Madeni Wizara ya Fedha na Mipango, Abdalla Mwinyimvua Mhasibu, Martin Madekwe Mstaafu kutoka Shirika la Nyumba la Taifa na Mr. Charles Singili Mkurugenzi Mtendaji Benki ya (TIB). 

Wengine ni Immaculata Senje Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Makazi Wizara ya Ardhi, Ndg Humphrey Polepole Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Mhandisi Mwita Rubirya ambapo kwa pamoja watashirikiana na Mwenyekiti wa bodi Dkt. Sophia Kongela pamoja na Mkurugenzi Mkuu Shirika la Nyumba Dkt. Maulid Banyani.

WAFANYABIASHARA WA MAZIWA WAIOMBA SERIKALI KUPUNGUZA KODI ZA TOZO ZA MAZIWA

$
0
0
Na Woinde Shizza, Arusha

Baadhi ya wafanyabiashara wa maziwa wameiomba serikali kupunguza kodi za tozo mbalimbali zinazotozwa  katika  bidhaa hizo ,ili kuwezesha wananchi wa  kufungua viwanda vya kusindika maziwa hapa nchini . 

Akizungumza na Waandishi wa habari katika maadhimisho ya Wiki ya unywaji maziwa duniani ambayo kitaifa yanafanyika mkoani hapa,Meneja wa mauzo wa kampuni ya Cowbell Vitus Mpanda Alisema kuwa kodi nyingi zilizopo katika nchi yetu zinawanyima wafanyabiashara wengi kufungu viwanda vya maziwa 

Alibainisha Kuwa gharama zimekuwa kubwa mno katika biashara hii ya maziwa, kwani tozo  ni nyingi mno hali inayosababisha baadhi ya viwanda vya maziwa kufungwa. 

Aidha aliomba serikali kuunganisha kodi ya TBS pamoja na TFDA kwani vitengo hivi vinafanana na tozo yake ni kubwa mno na pia mpaka upate vibali vyake ni kazi mno 

"gharama za kusindika maziwa pia hapa nchini ni kubwa mno kuliko nchi za wenzetu, kwani  Nchi za wenzetu wanasindika kwa bei ya chini hivyo mfanyabiashara anaona bora akasindike nje ndipo aje  auze hapa nchini "alisema Isaya Mbindi 

Alisema kuwa mbali na hapo wafugaji Wengi wanapenda kufuga lakini kutokana na garama  za ufugaji zilivyo juu wanashidwa kufuga. 

Alisema kuwa mbali na garama kubwa pia aliomba serikali kuwapatia elimu zaidi wafugaji ili waweze kufuga kisasa na kufanya ufugaji bora ili waweze kupata maziwa bora
 Baadhi ya mabanda yaliopo kwenye maonesho ya wiki unywaji  maziwa duniani ambapo kitaifa yanafanyika jijini Arusha katika viwanja vya kumbukumbu ya sheikh Amri Abeid 


KAMPUNI YA JATU KUFANYA MKUTANO MKUU WA WANAHISA WAKE JUMAMOSI,JUNI MOSI JIJINI DAR

$
0
0
MKUTANO mkuu wa Kampuni ya Umma ya Jenga Afya, Teketeza Umaskini (Jatu TLC) umepangwa kufanyika Jumamosi June Mosi, katika Ukumbi wa Mgulani jijini Dar es Salaam.

Pamoja na mambo mengine, wanachama wa Kampuni hiyo watachagua viongozi wapya wa bodi ambao watakua na jukumu la kuingiza kampuni hiyo kwenye soko la hisa ( DSE)

Mkurugenzi  Mtendaji wa JATU  PLC  Peter Isare alisema kuwa kampuni hiyo itaingia rasmi kwenye soko la hisa mapema mwezi August kwa mtaji wa Shilingi Bilion 7.5

Akizungumzia kampuni hiyo alisema ilianzishwa na vijana 2015 kuhusiana na masuala ya afya na lishe na haki za binadamu, watu wengi wanapata changamoto kwenye masuala mbali mbali, "Wengi ni maskini wanashindwa kumudu gharama za maisha na kusababisha migogoro kwenye jamii,"alisema na kuongeza

"Tuwe na afya lakini tuweze kujitegemea na kuwa na afya nzuri, tumejikita kwenye kilimo, masoko na bima ya afya, watu wengi wanahitaji kuwekeza katika biashara na kuhitaji mikopo.

Alisema kampuni hiyo ya umma imesajiliwa mwaka 2016 na imefanikiwa katika Kilimo cha Mpunga Kilombero, Manyara kilimo cha Alizeti na Mahindi, Tanga kulimo cha Maharage.

"Tunawawezesha wakulima kulima kilimo cha kisasa, na kuwapatia wataalamu ambao watawapa elimu, na kilimo ni cha muda wote kisichotegemea hali ya hewa.

"Igima kiwanda cha kukoboa mchele, Kibaigwa kiwanda cha mahindi na alizeti, tunaunganisha kilimo na viwanda, na soko tumelitengeneza wenyewe."

Alisema Jatu unaponunua chochote kama chakula, ni rahisi kukuza faida Kwani kuna mfumo rasmi wa kugawa faida, mteja akinunua bidhaa anapata bonasi ambapo gawio analipata mwisho wa mwezi.

Alisema kampuni hiyo imekuwa inawawezesha wakulima kulima kilimo cha kisasa, na kuwapatia wataalamu ambao wanawapa elimu, na kilimo ni cha muda wote kisichotegemea hali ya hewa.

“Kilimo kinalipa ukikitilia manani, Jatu tuna watu zaidi ya 13,000 ambao wanafanya kilimo na biashara, kama kampuni tunanufaika pia na kupata mazao moja kwa moja kutoka kwa mkulima bila kupitia kwa madalali wa kati.” alisema 

Alisemaunaweza kujiunga kwa kuuza bidhaa upata mgao kila mwezi au ujiunge kwenye kilimo, au kununua hisa kupata gawiwo ukapata faida kutokana na faida ya kampuni.
Mkurugenzi  Mtendaji wa JATU  PLC  Peter Isare

chama cha mapinduzi kujenga chuo kikubwa cha Mwalimu Nyerere Kibaha

MKURUGENZI MTENDAJI TASAF AWAFUNDA VIONGOZI WA PEMBA KUHUSU SHUGHULI ZA TASAF.

$
0
0
NA. Estom Sanga-Pemba 

Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF- Bwana Ladislaus Mwamanga, ametoa wito kwa viongozi wa serikali kisiwani Pemba kuendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi inayotekelezwa na Mfuko huo ili iendelee kutoa tija kwa wananchi. 

Mkurugenzi Mtendaji huyo wa TASAF ametoa rai hiyo alipofungua kikao kazi kilichojumuisha wakuu wa mikoa, wilaya, Maafisa Wadhamini ,makatibu tawala na waratibu walioko kisiwani Pemba ambao pamoja na mambo mengine walipewa fursa ya kujadili utekelezaji wa miradi ya ajira ya muda na namna ya kusimamia na kutunza vifaa vya utekeleza ji wa miradi hiyo. 

Bwana Mwamanga amesema serikali kupitia TASAF imekuwa ikitekeleza miradi ya ajira ya muda kwa lengo la kuwaongezea walengwa wake kipato na kupunguza kero zinazowakabili, kazi inayoambatana na ununuzi wa vifaa ambavyo amesema vinatakiwa kutunzwa ili viweze kudumu na kukidhi matakwa ya wananchi. 

Mkurugenzi Mtendaji huyo wa TASAF amebainisha kuwa dhamira ya serikali ya kuwapunguzia wananchi adha ya umaskini kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini imepewa msukumo mkubwa zaidi na serikali na hivyo kuwataka viongozi wa ngazi zote kwenye maeneo yao kuwa karibu zaidi na miradi inayotekelezwa kupitia Mpango huo unaohudumia zaidi ya Kaya Milioni Moja na Laki Moja kote Tanzania Bara, Unguja na Pemba. 

Aidha Bwana Mwamanga amewajulisha viongozi hao kuwa Serikali imekamilisha maandalizi ya utekelezaji wa sehemu ya pili ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ambao mkazo mkubwa utawekwa katika kuwashirikisha Walengwa wenye uwezo wa kufanyakazi kwenye miradi ya Maendeleo na kisha kulipwa ujira ili waweze kujiongezea kipato. 

Kwa upande wao viongozi hao wa Kisiwa cha Pemba walipongeza hatua ya serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ambao wamesema umeleta matumaini kwa wnaanchi ambao walikuwa wanaishi kwenye hali ya umaskini mkubwa. 

Wamesema serikali kupitia TASAF imeamusha ari ya wananchi hususani walengwa kujiletea maendeleo kwa kuanzisha miradi ya uzalishaji mali na hivyo wakashauri idadi kubwa zaidi ya wananchi wanaoishi kwenye umaskini uliokithiri ijumuishwe kwenye mpango huo ili pia waweze kunufaika na huduma zake.
Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF ,Bw. Ladislaus Mwamanga (wa tatu kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Pemba baada ya ufunguzi wa kikao kazi cha viongozi hao kilichofanyika kisiwani Pemba. 
Baadhi ya viongozi kisiwani Pemba wakiwa kwenye kikao kazi kilichojadili masuala mbalimbali yakiwemo wajibu wa viongozi katika kusimamia miradi na vifaa vya TASAF.Kikao kazi hicho kilifanyika kisiwani Pemba.
Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF,Bw. Ladislaus Mwamanga (aliyesimama) akifungua kikao kazi cha viongozi wa Pemba waliojadili utekelezaji wa shughuli za TASAF kisiwani humo.

Benki ya KCB Tanzania yaandaa Futari kwa wateja wake wa Dar es Salaam

$
0
0
  Benki ya KCB Tanzania leo jioni imeandaa Futari kwa ajili ya wateja wake katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam, ikihudhuriwa pia na wajumbe wa bodi pamoja na wafanyakazi wa Benki.

Akiongea kwenye tukio hilo, Mwenyekiti wa Bodi wa Benki ya KCB Tanzania, Zuhura Muro, amesema benki imeamua kuandaa futari hiyo ili kujumuika na wateja wake kama hatua ya kuonyesha mshikamano na umoja katika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani.

“Hapa Benki ya KCB, tunathamini na kutaambua wajibu wetu katika jamii hususani katika nyanja za elimu, mazingira na ujasiriamali.” Amesema Muro huku akiongeza kuwa benki imekuwa ikiwekeza katika masuala ya kijamii tangu ilipofungua milango yake nchini Tanzania mnamo mwaka 1997.

Amesema pia kuwa benki inaheshimu sana Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kutokana na ukweli kwamba, ni kipindi ambacho mwanadamu anajiweka karibu na Muumba kupitia sheria ya kufunga na kufanya maombi.

“Mwezi mtukufu wa Ramadhani ni ukumbusho kwetu wote kujiweka karibu na Muumba wetu. Ni mwezi ambao pia unatukumbusha kufanya kilicho chema mbele za Mungu wetu. Ndiyo maana hapa KCB tumeamua kuandaa futari hii ili kujumuika na wenzetu.” Amesema Muro.

Muro pia ameongeza kuwa benki ina idara maalum inayojikita katika kutoa huduma kwa wateja wake wa imani ya Kiislam, idara inayojulikana kama "Sahl Banking" inayopatikana kwenye matawi yote ya KCB.

Muro ameongeza kuwa KCB ina jumla ya matawi 14 nchi nzima na ni taasisi ya kwanza ya kifedha nchini Tanzania kuanzisha Shariah Banking kwa ajili ya kuwahudumia wateja wake wa Kiisalam.

“Benki ya KCB imekuwa ikijidhatiti katika kuboresha huduma kulingana na mapendekezo mbalimbali ya wateja”. Kimario amesema huku akitolea mfano Shariah Banking ambayo inafuata muongozo wa Imani ya Kiislam katika nyanja ya kifedha.

Muro amewaomba wale ambao hawajajiunga na Benki ya KCB kufungua akaunti zao ili waweze kufurahia huduma bora na za kipekee zinazotolewa katika matawi yote ya KCB nchini.

Benki ya KCB Tanzania imekuwa ikiandaa futari za aina hii kila unapofika mwezi mtukufu wa Ramadhani kama hatua ya kuungana na jumuiya ya waislam wote nchini katika kutimiza funga zao.









NEC Yatangaza Nafasi za Ajira za Muda za Uboreshaji wa Daftari la kudumu la Wapiga kura

$
0
0

Mwandishi wetu, NEC

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza nafasi za kazi za muda kwa ajili ya Uboreshaji wa Daftari la Wapiga Kura.

Kwa mujibu wa tangazo la maombi ya ajira hizo lililosainiwa na Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi Mabamba Rajabu Moses, Watanzania wenye umri kuanzia miaka 18 na wasiozidi miaka 45 wametakiwa kuomba.

Kwa mujibu wa tangazo hilo, sifa zingine za waombaji ni kuwa na elimu ya kidato cha nne na kuendelea na awe na ujuzi wa kutumia kompyuta.

“Awe na uwezo wa kutambua matatizo ya kompyuta ya hardware na software  na kuyatatua” ilisema sehemu ya tangazo hilo na kuongeza kuwa:.
“Awe na uwezo wa ku-istall programu za kompyuta na kutoa msaada wa kiuifundi wa TEHAMA kwa watumiaji.”

“Awe hajawahi kutiwa hatiani kwa makosa ya jinai an awe na uwezo wa kufanya kazi katika mazingira yenye usimamizi mdogo”
Sifa nyingine za ziada za kazi hiyo zimetajwa kwenye tangazo hilo linalopatikana kwenye Tovuti ya NEC ya www.nec.go.tz na mitandao ya kijamii ya NEC.

WADAU WA HABARI WATAKIWA KUZIDI KUELIMISHA JAMII KUHUSU WATU WENYE UALBINO NCHINI

$
0
0
Na Hussein Stambuli, Morogoro
Wadau wa tasnia ya habari nchini wameombwa kutumia maarifa yao kuielimisha zaidi jamii juu ya uwepo wa watu wanaoishi na ualbino kwani mpaka sasa bado kumekuwa na changamoto ya unyanyapaa dhidi ya watu hao ikiwemo ushirikishwaji wao katika ajira, kuendelea kuwepo kwa matukio machache yanayohusishwa na utekaji pamoja na kuitwa majina yasiyofaa katika jamii wanazoishi jambo linaloashiria unyanyapaa dhidi yao.
Maombi hayo yamefikishwa na Afisa mlaghibishi kutoka shirika la kimataifa lisilokuwa la kiserikali la kutetea usalama, ustawi na haki za watu wenye ualbino  la ‘Under the same Sun’ Kondo Sefu ambapo amesema bado jamii imebaki katika mkondo usio salama dhidi ya watu hao ikiwemo muendelezo wa matukio machache yanayohusishwa na Imani za kishirikina pamoja na ubaguzi.
“Bado hali haijakaa sawa kumekuwa na matukio ya kufukuliwa kwa mifupa ya watu wenye ualbino kwenye makaburi wanayozikwa, majaribio ya kutekwa katika baadhi ya mikoa hili jambo bado linaonesha changamoto ya kurejesha usawa dhidi ya watu wenye ualbino katika jamii bado inahitajika” alisema Kondo
Awali akifungua mafunzo hayo Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo la under the same sun Berthasia Ladislaus alisema kuwa shirika hilo kwa kushirikina na serikali limeweza kusaidia kupunguza matukio ya mauaji na vitendo vingine vya kikatili dhidi ya watu wenye ualbino.
“katika kipindi cha Januari hadi Mei kumekuwa na matukio mawili tu ya matishio ya utekaji wa watu wenye albino katika maeneo ya Ngorongoro na Kwimba ambapo watu wasiojulikana walitaka kuwadhuru watoto wawili wenye albino hata hivyo majaribio hayo hayakufanikiwa” alisema Berthasia.
Pia shirika la kimataifa lisilokuwa la kiserikali la kutetea usalama, ustawi na haki za watu wenye ualbino  la ‘under the same sun’ limewaomba waandishi wa habari kuwa na matumizi sahihi ya lugha wanaporipoti juu ya kundi hilo hasa kuwaita ‘watu wenye ualbino’ badala ya zeruzeru, albino, watu wenye ulemavu wa ngozi pamoja na kufanya Makala maalum juu ya maisha na changamoto wazozipitia jamii ya watu hao.
 Mkurugenzi Mtendaji wa shirika  la under the same sun Berthasia Ladislaus akifafanua jambo mbele ya wahariri mbalimbali waliojitokeza katika semina elekezi juu ya watu wenye ualbino
Wadau wa shirika la kimataifa lisilokuwa la kiserikali la kutetea usalama, ustawi na haki za watu wenye ualbino  la ‘under the same sun’
Wadau wa tasnia ya habari wakiwa katika picha ya pamoja katika semina elekezi inayohusu namna ya kuripoti habari za watu wenye ualbino kwa wahariri

SMZ YAPIGA MARUFUKU UINGIZWAJI NA UTUMIAJI WA MIFUKO YA PLASTIKI ZANZIBAR.

$
0
0
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mohamed Aboud Mohamed akizungumza na Waandishi wa Habari(hawapo pichani)kuhusiana na Kupiga marufuku Uingizwaji na Utumiaji wa Mifuko ya Plastiki amabayo inaonekana kuingizwa Nchini ikiwa na Rangi tofauti mkutano uliofanyika ukumbi wa Juu wa Baraza la Wawakilishi Mbweni Zanzibar. 
Mwandishi wa Habari wa ZBC Swaumu Khamis akiuliza maswali katika Mkutano wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mohamed Aboud Mohamed kuzungumzia kupiga marufuku Uingizwaji na Utumiaji wa mifuko ya Plastiki amabayo inaonekana kuingizwa Nchini ikiwa na Rangi tofauti mkutano uliofanyika ukumbi wa Juu wa Baraza la Wawakilishi Mbweni Zanzibar.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mohamed Aboud Mohamed akisisitiza jambo wakati akijibu maswali ya Waandishi wa Habari(hawapo pichani)kuhusiana na Kupiga marufuku Uingizwaji na Utumiaji wa Mifuko ya Plastiki amabayo inaonekana kuingizwa Nchini ikiwa na Rangi tofauti mkutano uliofanyika ukumbi wa Juu wa Baraza la Wawakilishi Mbweni Zanzibar. 
Baadhi ya Waandishi wa Habari waliohudhuria katika Mkutano wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mohamed Aboud Mohamed kuzungumzia kupiga marufuku Uingizwaji na Utumiaji wa mifuko ya Plastiki amabayo inaonekana kuingizwa Nchini ikiwa na Rangi tofauti mkutano uliofanyika ukumbi wa Juu wa Baraza la Wawakilishi Mbweni Zanzibar.
PICHA NA YUSSUF SIMAI/MAELEZO ZANZIBAR.

UBA Tanzania yasherekea wiki ya Bara la Afrika

$
0
0
BENKI ya UBA Tanzania imeungana na nchi zingine za Afrika kwa kushehereke siku ya Afrika kama sehemu ya kumbukumbuku ya kila mwaka ya kuanzishwa kwa OAU na sasa AU ambao ulianzishwa Mei 25, mwaka 1963 

Kwa hapa nchini benki hiyo iliadhimisha siku hiyo UBA Tanzania, iliadhimisha siku hiyo kwa wafanyakazi wake kuvaa ngu za mitindo mbalimbali yenye kuonyesha uhalisia wa waafrika.

Akizungumzia siku hiyo Mkuu wa Kampuni ya Benki ya UBA Tanzania, Mussa Kitambi, alisema kuasisiwa kwa benki hiyo kunajumuisha historia ya Afrika kupitia mavazi, umoja na vyakula vya jadi.

“Siku ya Afrika (zamani ya Uhuru wa Afrika na Siku ya Uhuru wa Afrika) ni kumbukumbu ya kila mwaka ya msingi wa Shirika la Umoja wa Afrika (OAU) inayojulikana kama Umoja wa Afrika mnamo 25 Mei 1963. Inaadhimishwa katika nchi mbalimbali katika bara la Afrika , pamoja na duniani kote,” alisema Kitambi 

Katika kukumbuka siku hiyo shughuli mbalimbali zilifanyika kuvunja nazi, kukata keki na wateja, ngoma ya jadi na wafanyakazi, ngoma ya jadi na kikundi cha flash.

Mkuu wa Kampuni ya Benki ya UBA Tanzania, Mussa Kitambi, akipokea hati ya kutambuliwa kutoka kwa Waziri Mkuu wa Kassim Majaliwa, baada ya benki hiyo kusaidia futari kwa ajili ya watoto yatima 320 wa vituo sita vya Mkoa wa Dar es Salaam. Ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Afrika.
Meneja Masoko na Mawasiliano wa Benki ya UBA Tanzania, Brendansia Kileo (wa pili wa kulia), akiwa na amembeba mtoto wa kituo kimojawapo cha yatima jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Afrika.
Wafanyakazi wa Benki ya UBA Tanzania, wakiwa katika mavazi ya kiasili ikiwa ni sehemu ya sherehe ya kumbukumbu ya nchi huru za Afrika
Wanyakazi wa Benki ya UBA Tanzania, wakiwa katika picha ya pamoja katika sherehe za wiki ya Afrika

WAKAZI WA KILUNGULE WASHAURIWA KUEKA DHANA YA KUFANYA UCHUNGUZI WA AWALI WA AFYA ZAO

$
0
0

      Na.Khadija seif,Globu ya jamii

MKAZI wa kata ya kilungule wilaya ya temeke jijini Dar es salaam Halima abdallah amewashauri wananchi kujijenga dhana ya kupima afya zao mara kwa mara ili kunusuru maisha yao .

Halima amesema kupitia huduma ya upimaji kwa hiari ilioandaliwa na madaktari wa kujitolea wa (TVMCS) ikishirikiana na diwani wa kata ya kilungule ameweza kubainika kuwa ana uvimbe tumboni.

"Huduma nilipatiwa bure na nikagundulika na uvimbe tumboni ambao ukiendelea kuwepo unaweza kuhatarisha maisha yangu, nawashukuru madaktari ambao baada ya kugundulika na tatizo hilo wapo bega kwa bega na mimi na wananipatia ushauri ,"

Hata hivyo kwa upande wa diwani wa kata ya kilungule Said fella amesema bado kuna changamoto kubwa kwa wananchi kujitokeza kwenye huduma za kijamii hasa kupima afya zao bure wengi wao hupuuza.

"Walijiandikisha wengi kupatiwa huduma hiyo takribani watu 500 lakini badala yake  watu 372 ndio waliweza kufanya vipimo na kugundulika na magonjwa mbalimbali,"

Aidha,fella ameeleza kuwa tayari ameshaweza kuchangia madawa kwa magonjwa tofauti tofauti huku akiwataka wananchi kujijenga dhana ya kuwahi vituo vya afya kabla ya ugonjwa hujaleta athari kubwa zaidi.

 Huku daktari kutoka (TVMCS)  Issa Mohammed Nassor akiendelea kusisitiza wanatanzania wote kujikinga,kujilinda na kuepuka visababishi vya magonjwa mbalimbali ili kuimarisha afya zao.

Mohammed amebainisha magonjwa ambayo wananchi wamekuwa wakiishi nayo bila kujijua kama presha,kisukari ,uvimbe na kifua kikuu.

"Wagonjwa wapatao 182 waligundulika kuwa na tatizo la presha huku ,52 walikua na kisukari.

Pia Mohammed ameeleza yapo magonjwa ambayo yanatibika na hivyo wagonjwa wengine wameshaanza matibabu huku mgonjwa wa uvimbe tumboni Halima abdallah akifanyiwa maandalizi ya awali kwa ajili ya operesheni.
Diwani wa kata ya kilungule Said fella akitoa ripoti ya wakazi wa kata ya kilungule wilaya ya temeke jijini Dar es salaam waliojitokeza kupima afya zao katika huduma hiyo ya bure akishirikiana na madaktari wa kujitolea wa TVMCS.

KAMATI YA MIUNDOMBINU YAFANYA TATHIMINI YA UKAGUZI WA MIRADI

$
0
0
 Katibu wa Kamati ya Miundombinu,Hosiana John akisoma taarifa ya tathimini ya utekelezaji wa ziara za kukagua miradi zilizofanywa na Kamati hiyo katika kipindi cha mwaka 2018/2019 kkwenye kikao cha kamati hiyo kilichofanyika katika Ofisi za Bunge Jijini Dodoma.
 Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu, Mhe. Moshi Kakoso akizungumza katika kikao cha kamati hiyo kilichofanyika katika Ofisi za Bunge Jijini Dodoma, Kamati ilikutana kwa ajili tathimini ya utekelezaji wa ziara zake za kukagua miradi kwa mwaka 2018/2019.

 Wajumbe wa Kamati ya Miundombinu wakiwa katika kikao cha kufanya ya tathimini ya utekelezaji wa ziara za kukagua miradi zilizofanywa na Kamati hiyo katika kipindi cha mwaka 2018/2019 kilichofanyika katika Ofisi za Bunge Jijini Dodoma.

DC AKATAA NYUMBA YA WALIMU YA MILION 52-SCRIPT PICHA NA SAUTI

$
0
0
 Na Ahmed Mahmoud Karatu
Mkuu wa wilaya ya Karatu Theresia Mahongo amegoma Kupokea Nyumba ya walimu ambayo inadaiwa kugharimu shilingi Milioni 52, zikiwa ni fedha kutoka kwa wafadhili milioni 34, nyingine zikitolewa na wananchi pamoja na serikali.

Mkuu wa Wilaya ya Karatu amefikia hatua hiyo wakati akipokea majengo mengine mawili ya bweni la Wanafunzi wa Kike pamoja na bwalo la Chakula yaliyojengwa na kwa ufadhili kutoka The African Foundations.
Huku akikaata nyumba ya walimu ya 3 in one ambayo imefadhiliwa na Serena hotel kwa madai fedha zilizotumika haziendani na uhalisia wa mradi. Katika mradi huo, Wananchi wameoa kiasi cha milioni Tisa, huku serikali ikitoa pia milioni Tisa kwaajili ya upauzi wa jengo.

Kwa upande wao wafadhili wa mradi huo wamekiri uwepo wa mapungufu hayo na kuahidi kuyafanyia Kazi.

Kuhusu msaada wa ujenzi wa Bweni la Wasichana pamoja na Bwalo la Chakula, Mkuu wa wilaya Mahongo amepongeza ujenzi huo, huku Meneja wa African Foundation, Mkomeni Ernest, amasema lengo ni kuhakikisha jamii inanufaika na uwepo wa makampuni yanayozunguka hifadhi zilizo karibu na wananchi.

NAIBU WAZIRI KANYASU-"SERIKALI HAINA MPANGO WA KUNYANG'ANYA ARDHII"

$
0
0
NA LUSUNGU HELELA-MARA
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu amewatoa hofu wananchi kufuatia zoezi linaloendelea la kupanga matumizi bora ya ardhi katika wilaya kumi nchini hasa katika maeneo yanayopakana na Hifadhi za Taifa kuwa zoezi hilo halina mpango wowote wa kunyang'anya ardhi ya wananchi kwa ajili ya kuanzisha Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori.

Rai hiyo imetolewa leo na Mhe. Constantine Kanyasu kufuatia hofu kubwa iliyokuwa imetanda miongoni mwa wananchi wa vijiji 8 vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, wilayani Bunda mkoani Mara ambapo moja ya madai yao ni kwamba zoezi hilo limelenga kuchukua maeneo yao ya malisho kwa ajili ya kuanzisha Hifadhi ya Jumuiya ya Wanyamapori jambo ambalo sio kweli.

Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Sarakwa kinachotenganishwa kati ya mto Rubana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti , Mhe.Kanyasu amewaeleza wakazi hao kuwa zoezi la kupanga matumizi bora ya ardhi katika maeneo hayo lina faida kubwa ikiwemo kuepusha migogoro wa ardhi inayotokea mara kwa mara miongoni mwao.

Amesema mpango wa matumizi bora ya ardhi ni zoezi la kitaifa ambalo limelenga kutenga maeneo maalum kwa ajili ya malisho, kilimo pamoja na shughuli za maendeleo kwa malengo yakuepusha migongano inayotokea sehemu mbalimbali nchini na si kunyang'anya ardhi mpya kama inavyodaiwa.

"Nataka niwahakikishie Wizara yangu haina mpango wa kuanzisha msitu wa Hifadhi wala Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori katika kijiji chenu, Huu ni uzushi upuuzeni" Alisisitiza Kanyasu.

Aidha, Mhe.Kanyasu amewaeleza wananchi hao kuwa mpango wa matumizi bora ya ardhi utasaidia kuepusha watu wachache kujimilikishia eneo kubwa,"kinachofanyika kwa sasa ni kuweka rekodi na nyaraka kwa ajili ya vizazi vyenu" Alisisitiza.

Amesema katika zoezi hilo la mpango wa matumizi bora ya ardhi wanachoweza kufanya ni kutenga eneo la msitu asili wa kijiji kwa ajili ya manufaa yao ikiwemo kuokota kumi na eneo litakuwa chini ya umiliki wa kijiji na sio serikali kuu.

Katika hatua nyingine, Mhe.Kanyasu amewatoa wasiwasi wananchi hao kuwa licha ya kijiji hicho kuingia katika zoezi la mpango wa matumizi bora ya ardhi mifugo yao haitazuiliwa kwenda kunyweshwa maji katika mto Rubana.

"Nimesikia baadhi ya watu wakieneza uzushi kuwa baada ya mpango wa matumizi bora ya ardhi kukamilika hakuna mtu yeyote kupeleka mifugo katika mto Rubana, huu ni uwongo" alisema Kanyasu

Hata hivyo amewaeleza kuwa mita 500 kutoka katika mto huo ni eneo la kijiji kwa ajili ya malisho ya mifugo isipokuwa vitu ambavyo havitaruhusiwa kufanywa na mtu yeyote ni kulima pamoja na kujenga nyumba kwa vile eneo hilo ni shirikishi kwa Wanyamapori pamoja na mifugo.

Kwa upande wake, Mbunge wa Bunda vijijini, Boniface Getere amewataka wananchi kuwa watulivu kwani serikali haina mpango wowote wa kunyang'anya ardhi badala yake mpango huo utakuwa mkombozi kwa ajili ya kizazi cha sasa na cha badae.

" Mimi ni Mbunge wenu nisingeweza kukubali hata kidogo kama mpango huu wa matumizi bora ya ardhi umelenga kunyang'anya ardhi yenu." Alisisitiza Getere.

Naye, Mwenyekiti wa kijiji cha Sara, Samson Kapeta amekiri mbele ya Naibu Waziri kuwa mpango wa matumizi bora ni mpango mzuri isipokuwa kumejitokeza vikundi vya watu vilivyolenga kupotosha malengo mazuri ya serikali kwa ajili ya ardhi yao.

Mpango wa matumizi bora ya Ardhi ni mpango unaotekelezwa katika wilaya kumi nchini kwa ushirikiano katika ya Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi kwa kugharamiwa na Hifadhi ya Taifa ( TANAPA)
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu akizungumza na wananchi wa kijiji cha Sarakwa kuhusu umuhimu wa zoezi la mpango wa matumizi bora wa ardhi unaofanywa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Wizara ya Ardhi katika wilaya kumi katika wilaya kumi nchini kuwa haujikiti kupokonya maeneo mapya ya wananchi kwa ajili ya kuanzisha Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori kama inavyodaiwa.
 Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Sarakwa wakimsikiliza Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,Mhe, Constantine Kanyasu akiwaeleza kuwa serikali inaendesha zoezi la mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa ajili ya manufaa ya wananchi.
 Mbunge wa Bunda vijijini, Mhe, Boniface Getere akizungumza na wananchi wa Sarakwa kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe, Constantine Kanyasu kuzungumza na wananchi hao kuhusu nia ya serikali ya kuendesha zoezi la mpango wa matumizi bora ya ardhi katika kijiji hicho.
Mratibu wa mipango wa matumizi bora ya ardhi, Rose Mdendemi akitoa ufafanuzi kwa wananchi wa kijiji cha Sarakwa wilayani Bunda mkoani Mara kuhusu zoezi linaloendelea la mpango wa matumizi bora ya ardhi (Picha na Lusungu Helela-Wizara ya Maliasili na Utalii)

NEC yatangaza nafasi za ajira za muda za uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura

$
0
0
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza nafasi za kazi za muda kwa ajili ya Uboreshaji wa Daftari la Wapiga Kura.

Kwa mujibu wa tangazo la maombi ya ajira hizo lililosainiwa na Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi Mabamba Rajabu Moses, Watanzania wenye umri kuanzia miaka 18 na wasiozidi miaka 45 wametakiwa kuomba.

Kwa mujibu wa tangazo hilo, sifa zingine za waombaji ni kuwa na elimu ya kidato cha nne na kuendelea na awe na ujuzi wa kutumia kompyuta.

“Awe  na uwezo wa kutambua matatizo ya kompyuta ya hardware na software an kuyatatua” ilisema sehemu ya tangazo hilo na kuongeza kuwa:.

“Awe na uwezo wa ku-istall programu za kompyuta an kutoa msaada wa kuifundi wa TEHAMA kwa watumiaji.”

“Awe hajawahi kutiwa hatiani kwa makosa ya jinai an awe na uwezo wa kufanya kazi katika mazingira yenye usimamizi mdogo”

Sifa nyingine za ziada za kazi hiyo zimetajwa  kwenye tangazo hilo linalopatikana kwenye Tovuti ya NEC ya www.nec.go.tz na mitandao ya kijamii ya NEC.
Viewing all 110010 articles
Browse latest View live




Latest Images