Na Woinde Shizza Michuzi TV, Arusha
JESHI la Polisi Mkoa wa Arusha limefanikiwa kukamata madumu nane yakiwa yamesheheni dawa ya kulevya aina ya mirungi ambayo ni mbinu mpya inatumiwa na baadhi ya wananchi wanaojihusisha na biashara hiyo kama sehemu ya kulihadaa jeshi hilo.
Akizungumza leo ,Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Jonathan Shana amesema kuwa madumu hayo yamekamatwa leo saa nne asubuhi katika eneo la Sakina na kuongeza mirungi hiyo ina uzito wa kilo 140 na watuhumiwa walikuwa wanaitoa Namanga kuleta Arusha Mjini.
Kamanda Shana amewataja washtakiwa hao ni Philipo Mungasi Lairumbe na Mjomba Ngaruma Nairishoo wakiwa na pikipiki aina ya King lion yenye namba MC 404 CEE na nyingine aina ya MC 772 DVT aina ya King lion.
"Tulipata taarifa kuhusu hii staili mpya ya kusafirisha mirungi na ndipo Polisi wetu walipoweka mtego na kufanikiwa kuwakamata katika eneo la Sakina wakati wakija Arusha Mjini,"amesema Kamanda Shana.
Ameongeza kuwa kumekuwepo na mbinu mpya ya kusafirisha mirungi ambapo inawekwa kwenye madumu ya maji na kubeba kama maziwa na kwamba mbinu hiyo imekuwa ikitumika kwa muda mrefu sasa.
Amesema kutokana na tukio hilo Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi zaidi ili kuwabaini wale wote wanaoshirikiana nao na hata kama watakimbia watawakamata na uchunguzi utakapokamilika walioshiriki watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Wakizungumzia kuhusu tukio hilo la kunaswa kwa mirungi hiyo, watuhumiwa hao wamesema wamekuwa wakiitumia mbinu hiyo na hii ni mara ya pili kwao na wanapofikisha mzigo kwa mhusika wanalipwa Sh.80,000.
Wakati huo huo ,Jeshi la Polisi limeendesha msako wa nyumba kwa nyumba katika kuwasaka wahalifu na kufanikiwa kukamata wahalifu 35 wakiwa na vitu mbalimbali ikiwemo TV, radio, simu, sabufa na Laptop.
Amesema miongoni mwa mshtakiwa aliyekamatwa katika msako huo ni Jumanne Mjusi anayedaiwa kufanya uhalifu Mei 16 mwaka huu katika mtaa wa Olasiva uliopo Kata ya Olorieni katika nyumba ya Msafiri Msuya (47)ambaye aliibiwa kiasi cha Sh.milioni sita pamoja na bastola moja aina ya Browning yenye namba B 043601 ikiwa na risasi tisa.
Kamanda Shana amesema kuwa, Mjusi alikamatwa katika eneo la Ngarenaro baada ya siku mbili ya kufanyika kwa tukio hilo la wizi ambapo alikutwa akiwa na bastola hiyo pamoja na risasi zake isipokuwa fedha hizo.
Amewataka wananchi kutoa taarifa za uhalifu mbalimbali zinazofanyika katika maeneo yao ili kulisaidia jeshi hilo.Pia ametoa onyo kali kwa watu wote wanaoghushi vitambulisho vya uraia na kueleza iwapo mtu yeyote atakamatwa kwa kosa la kughushi hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.
Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha Jonathan Shana akionesha jinsi wasafirisha mirungi wanavyotumia mbinu mpya
Kamanda akionyesha moja ya muhalifu anaetuhumiwa kusafirisha mirungi
Mwananchi Abasi Mkindi akizungumza na waandishi wa habari ambapo aliliomba jeshi la polisi kuongeza ulinzi katika mipaka ili madawa ya kulevywa yapitishwe