Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Msama Promotions,Alex Msama(kulia) akikabidhi msaada wa Magodoro kwa Sheikh Abdushakur Omary, kwaajili ya kituo cha Luhila Pachane,kilichoko Songea mjini,kinacholea Watoto Yatima na wanaoishi katika mazingira magumu, Sheikh Abdushakur,ni mlezi wa kituo hicho,pia ni Katibu wa Bakwata Mkoa wa Ruvuma.
======= ===== ======
Na Mussa Mkama
MKURUGENZI Mtendaji wa Msama Promitions Alex Msama amekabidhi msaada wa magodoro yenye dhamani ya zaidi ya Shilingi milioni 4 kwa kituo cha watoto yatima Luhila Pachane kilichopo Songea Mkoani Ruvuma.
Akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya ofisi za Msama Promotions Kinondoni Jijini Dar es Salaam jana Msama alisema msaada huo umetoka kwenye mfuko wa Tamasha la Krismas ambalo linatarajiwa kuanza Desemba 25 jijini hapa na mikoa mingine.
Tamasha hilo la Krismas linatarajia kufanyika katika mikoa mitano, ambapo ni Dar es Salaam, Morogoro, Tanga, Arusha na Dodoma.
Msama alisema kuwa kutokana na maombi ya kituo hicho na kuguswa na hali waliyokuwa nayo ya yatima hao kulala katika mkeka, aliamua kunyofoa sehemu ya fedha zilizokuwa kwenye mfuko wa Tamasha la Krismas na kuamuo kuwasaidi watoto hao ili nao waweze kujisikia wapo katika jamii ya Watanzania.
“Nimeamua kufanya hivyo kutokana na kuguswa na hali halisi waliyonayo yatima hao wa kituo cha Luhila Pachane huko mkoani Ruvuma nikaamua kunyofoa fedha katika mfuko wa Tamasha la Krismas kwa ajili ya kuwasaidi ili nao wajisikie wako pamoja na Watanzania wenzao” alisema Msama na kuongeza kuwa;
“Msaada huo wa magodoro hayo ni zaidi ya shilingi milioni 4, hivyo ninaimani kubwa sasa kwa msaada huu yatima wataniombea kwa Mungu ili Tamasha la Krismas liwe la mafanikio kwani lengo la tamasha hilo ni kuweza kujenga kituo cha kisasa cha watoto yatima na wasiojiweza kwani kiwanja tumeshakiona kipo pale maeneo ya barabara ya Pugu Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa msaada huo Mlezi wa kituo hicho ambaye pia ni Katibu wa Bakwata mkoa wa Ruvuma Shekh Abdushakur Omary alisema anamshukuru Msama kwa wema wake aliouonyesha wa kusaidia jamii ya Watanzania wote bila kubagua dini, kabila wala rangi.
“Msama ni mtu wa aina yake hana ubaguzi anashughulikia maombi ya Watanzania wote bila kuangalia dini, kabila, rangi wala utaifa wake kwani amaamini kuwa wote ni wamoja, hivyo naomba nizidi kumuombea aendelee kuwa na moyo huo wa kujitolea kwa ajili ya watu wa taifa lake wasiyojiweza” alisema Omary.
Hata hivyo aliomba Wizara husika kuharakisha upatikanaji wa hati ya kiwanja kile kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha kisasa cha kutolea misaada (Center) pamoja na kiwanda cha kisasa cha kuzalishia kazi za wasanii kwa manufaa ya Taifa na watu wake, kwani kwa kufanya hivyo itakuwa imesaidia Watanzania wengi wenye ndoto ya kuwa wasanii wakubwa nchini.
“Uwepo wa Msama katika ulimwengu huu kunamuwakilisha Mwenye Mungu, kwani Mungu si mbaguzi kwa watu wake anawapenda wote na anatoa sawa kwa kila mtu, hivyo ndivyo alivyo Msama, kwa moyo mmoja namuombea yeye na taasisi yake isiyokuwa na ubaguzi wa dini kuendelea
kuwa hivyo wakati wote” alisema Omari na kuongeza kuwa;
“Naomba Wizara au Waziri husika kuona umuhimu wa ujenzi wa kituo hicho cha kisasa cha kutolea misaada pamoja na kiwanda cha kuzalishia kazi za wasanii, kwani wapo Watanzania wengi wenye vipaji lakini hushindwa kufanya kazi za kisanii kutokana na viwanda kuwa na gharama kubwa wasizoweza kuzimudu”