Quantcast
Channel: MICHUZI BLOG
Viewing all 109593 articles
Browse latest View live

WANAWAKE WAFANYAKAZI WAKUTANA DODOMA KUJADILI CHANGAMOTO ZINAZOWAKABILI DUNIA IKIHADHIMISHA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI.

0
0
Mwakilishi wa Katibu Mkuu Maendeleo ya Jamii Bw. Patrick Golwike akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wanawake waliohudhuria Kongamano la wafanyakazi Wanawake jiijini Dodoma liliofantika kwa lengo la kuwakutanisha wafanyakazi hao kujadiliana na kupata namna bora za kuweza kumuwezesha kiuchumi mwanamke.Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano WAMJW


Mwakilishi wa Katibu Mkuu Maendeleo ya Jamii Bw. Patrick Golwike akifungua Kongamano la wafanyakazi Wanawake jiijini Dodoma liliofanyika kwa lengo la kuwakutanisha wafanyakazi hao kujadiliana na kupata namna bora za kuweza kumuwezesha kiuchumi mwanamke.
Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bi. Silvia Siriwa akieleza chimbuko la Siku ya Wanawake Duniani katika Kongamano la wafanyakazi Wanawake jiijini Dodoma liliofanyika kwa lengo la kuwakutanisha wafanyakazi hao kujadiliana na kupata namna bora za kuweza kumuwezesha kiuchumi mwanamke.
Mkurugenzi Msaidizi Wanawake kutoka Idara ya Jinsia Bi. Mboni Mgaza akielezea umuhimu wa Siku ya Wanawake Duniani katika kiuchumi mwanamke katika kongamano la wafanyakazi wanawake Dodoma. 
Baadhi ya Wafanyakazi Wanawake wa Mkoa wa Dodoma wakifuatlia mada mbalimbali zilizokuwa zikitolewa katika Kongamano la wafanyakazi Wanawake jiijini Dodoma liliofanyika kwa lengo la kuwakutanisha wafanyakazi hao kujadiliana na kupata namna bora za kuweza kumuwezesha kiuchumi mwanamke

Tanzania inaungana na Nchi nyingine duniani kuadhimisha Siku Wanawake Duniani kwa lengo la kutafakari mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto lakini pia kuwakomboa kifikra, kiutamaduni, kisiasa, kijamii na kiuchumi.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kongomano la wanawake wafanyakazi kuhadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Bw. Patrick Golwike alisema wanawake na wasichana wafanyakazi ni kundi kubwa na muhimu katika jamii linalohitaji kulindwa.

Bw. Golwike alitoa Rai kwa wanawake hao kuwa Haki inakwenda pamoja na Uwajibikaji lakini pia Usawa unakwenda pamoja na kukidhi vigezo, ambavyo ni sifa za kielimu, kitaaluma na uzoefu wa kazi.

Ameongeza kuwa Maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani hufanyika kila mwaka ifikapo Machi 8, kwa mwaka huu hapa Tanzania yanafanyika ngazi ya Mkoa, ambapo kila Mkoa umeadhimisha sikukuu hii kulingana na mazingira yake na rasilimali zilizopo kwa kuzingatia Kaulimbiu ya mwaka husika ambayo ni “Badili fikra kufikia usawa wa kijinsia kwa maendeleo endelevu”.

Aidha Bw. Golwike aliyataja Madhumuni ya Maadhimisho haya kuwa ni kutoa fursa kwa Serikali, Wananchi, Wadau, Wanawake na Jamii yote kubadili fikra na mtizamo ili kuleta Usawa wa Jinsia na kuonesha nia ya kuhamasisha jamii, juu ya umuhimu wa kutambua uwezo wa wanawake katika kuchangia na kuleta Maendeleo Endelevu lakini pia Kuwezesha ushiriki na kuchukua hatua za kukabiliana na changamoto zinazowakabili wanawake kufikia maendeleo jumuishi.

Wakati huo huo Msimamizi wa Maadhimisho hayo kutoka Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Bi. Silivia Siriwa alitaja mafanikio yaliyopatikana kutokana na juhudi za Wizara kuwa ni pamoja kutoa elimu kwa jamii kuhusu utatuzi wa changamoto zinazowakabili wanawake ikiwemo Madhara ya Mila na Desturi potofu ambazo zinaelekeza aina ya kazi na nafasi za uongozi za kushikwa na wanawake ambazo ni za kutoa huduma zaidi.

Aliyataja mengineyo ni kuhamasisha jamii kuhusu kuondoa madhara ya ndoa na mimba za utotoni, ambazo zinafifisha ndoto na matarajio ya mtoto wa kike, hamasa na ushiriki wa wafanyakazi katika majukwaa ya uwezeshaji wanawake ambayo yanatumika kwa ajili ya kuelimishana, kubadilishana uzoefu na kujiunga katika mtandao wa mashirikiano.

Bi. Siriwa pia alizitaja baadhi ya changamoto zinazojitokeza kwa wanawake mahali pa kazi ni pamoja na kukosa taarifa za mabadiliko ya Sheria na Kanuni za utumishi, Matumizi ya lugha ya kiingereza katika matumizi ya vifungu vya kisheria inawanyima baadhi ya wafanyakazi, haki ya kuzifahamu sheria.

Aidha Wingi wa shughuli na majukumu ya kifamilia, kikazi na kijamii ni hali inayopunguza ufanisi wao, kipato kidogo cha kumudu mahitaji ya familia na ongezeko la wahitaji kutoka katika makundi maalum ya jamii ambayo wanawake wafanyakazi wanayabeba.

Chimbuko la Siku ya Wanawake lilianza mwanzoni mwa miaka ya 1900 kufuatia maandamano ya wanawake wafanyakazi wa sekta ya viwanda nchini Marekani kupinga mazingira duni ya kazi.

Waandamaji hao, walilalamikia ukosefu wa huduma za kijamii na kuwepo kwa vitendo vya unyanyasaji katika ajira ikiwemo wanawake kulipwa mshahara mdogo kwa kazi sawa na wanaume

Umoja wa Ulaya EU watoa mafunzo ya udhibiti wa vyanzo vya mionzi kwa nchi Tano za Afrika.

0
0
mafunzo ya udhibiti wa uingizaji wa vyanzo vya mionzi yakitolewa na Umoja wa Ulaya ambayo yanafanyika kwa siku tano kwenye ofisi za Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania jijini Arusha.


Washiriki kutoka nchi za Kenya,Rwanda,Malawi,Zambia na wenyeji Tanzania wakimsikiliza kwa makini mkufunzi Bwana Olydcaegers Greet kwenye mafunzo ya udhibiti wa uingizaji wa vyanzo vya mionzi kwenye mipaka ya nchi isivyo fuata utaratibu.Mafunzo hayo yametolewa na Umoja wa Ulaya ambayo yanafanyika kwa siku tano kwenye ofisi za Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania jijini Arusha.


Umoja wa Ulaya EU umetoa mafunzo ya udhibiti wa uingizaji wa vyanzo vya mionzi kwa nchi tano za AFRIKA kwa lengo la kusaidia udhibiti wa uingizaji wa vyanzo vya mionzi bila kufuata utaratibu pamoja na utoroshwaji wa vyanzo vya mionzi vilivyoibiwa kwa matumizi yasiyo salaama na hatarishi. 

Washiriki wa mafunzo haya ni kutoka taasisi mbali mbali zikiwemo Mamlaka za Mapato, Forodha na vyombo vya ulinzi na usalama kutoka katika nchi za Malawi, Rwanda, Kenya, Zambia na wenyeji Tanzania kupitia Tume ya Nguvu za Atomiki. 

Huu ni mwendelezo wa mafunzo kwa nchi za Afrika katika kusaidia kupambana na tabia ya uingizwaji wa vyanzo vya mionzi ambavyo kwa namna moja ama nyingine hupelekea kuleta madhara kwa binadamu. 

Mafunzo hayo yanahusisha mafunzo kwa vitendo ikiwemo utambuzi kwa kutumia vifaa maalumu vilivyopo katika mipaka yote katika nchi hizo ambapo husaidia kugundua uhalifu wa namna hiyo. 

Mshiriki wa mafunzo hayo kutoka Tanzania Mhandisi Exavier Zakaria amesema kuwa mafunzo hayo yatawasaidia sana hasa kwa wao waliopo katika mipaka amesema wamekuwa wakikutana na masuala mengi ikiwemo baadhi ya wafanyabiashara ambao huenda kinyume na sheria na taratibu zilizowekwa za usafrishaji wa vyanzo vya mionzi. 

‘’Ukweli mafunzo yamekuja kwa wakati sahihi na yatasaidia sana katika kuongeza ujuzi kwenye utambuzi wa vyanzo vya mionzi ambavyo ni hatarishi kwa binadamu’’ alisema Mhandisi Zakaria 

Naye mshiriki mwingine wa mafunzo hayo kutoka Tanzania , Bwana Patrick Simpokolwe amesema kuwa kutokana na mbinu za uhalifu za uingizaji wa mionzi isiyo salama katika mipaka mbali mbali katika nchi za Afrika anaamini mafunzo haya yatamsaidia katika kugundua mbinu mbali mbali za uhalifu na kuweza kudhibiti. 

‘’Tumekuwa tukikumbana na udanganyifu mkubwa kwenye mipaka kutokana na mbinu mpya zinazotumiwa na wasafirishaji wa bidhaa mbali mbali zikiwemo zenye vyanzo vya mionzi kutoka na kuingia ndani ya nchi hivyo mafunzo haya yatawezesha kuwabaini wahalifu wa namna hiyo’’ alisema Simpokolwe. 

Mshiriki mwingine kutokea nchini Kenya Bi Evalyne Rotich amesema kuwa kutokana na uwezekanao wa kutokea uhalifu kila wakati na kwamba mafunzo hayo yatawezesha sana kutambua watu ambao sio wema wenye lengo la kupitisha vitu vyenye vyanzo vya mionzi mipakani ambavyo vinaweza kudhuru wananchi katika nchi husika . 

‘’Umakin utaongezeka kwetu kwani mbinu tulizopatiwa zitatuwezesha kutambua vitu vyote ambavyo vitapitishwa bila kufuata utaratibu husika’’ alisema Rotich. 

Kwa upande wake mmoja wa wakufunzi wa mafunzo hayo kutoka umoja wa Ulaya (EU) , Bi Katrijin Vandersteen amesema kuwa katika nchi za Afrika kumekuwa na tatizo la uingizaji wa vyanzo vya mionzi visivyo salama hivyo kwakutolewa mafunzo hayo kutolewa yataweza kusaidia katika uimarishaji wa utambuzi na udhibiti katika maeneo ya mipaka kwenye nchi mbali mbali. 

‘’Tunaamini kuwa washiriki hawa watapata uelewa zaidi juu ya utambuzi wa vyanzo vya mionzi visivyo salama kwa lengo la kusaidia kutoleta madhara kwa binadamu kwenye nchi husika na dunia kwa ujumla mara baada ya kukamilika kwa mafunzo haya ’’ alisema Vandersteen. 

Mfunzo haya yanafanyika katika Makao Makuu ya Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania, jijini Arusha kuanzia tarehe 4 hadi 8 Machi 2019.

NMB WAKABIDHI MSAADA WA MABATI 1248, MADAWATI 62 KWA SHULE 8 MKOANI KATAVI

0
0


Meneja wa NMB Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Straton Chilongola akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Lilian Matinga (walioshikana mkono) sehemu ya msaada wa mabati 1,248 kwa ajili ya Shule 5 za Sekondari na shule 3 za Msingi zote kutoka halmashauri za Mkoa wa Katavi.
Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Lilian Matinga (katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa madawati 62 yaliyotolewa na Benki ya NMB kama msaada kwa ajili ya Shule kutoka halmashauri za Mkoa wa Katavi.

Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Lilian Matinga (katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa madawati 62 yaliyotolewa na Benki ya NMB kama msaada kwa ajili ya Shule kutoka halmashauri za Mkoa wa Katavi.
Wanafunzi wakiwa na sehemu ya madawati yaliyotolewa na Benki ya NMB kama msaada.


BENKI ya NMB imetoa msaada wa mabati 1,248 na madawati 62 kwa ajili ya Shule 5 za Sekondari na shule 3 za Msingi zote kutoka halmashauri za Mkoa wa Katavi ikiwa ni kusaidia kutatua changamoto anuai kwenye sekta ya elimu.

Msaada huo uliogharimu kiasi cha shilingi milioni 40 umekabidhiwa na Meneja wa NMB Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Straton Chilongola huku akisisitiza benki hiyo itaendelea kusaidia jamii katika sekta ya afya, elimu pamoja na majanga ikiwa ni kuchochea maendeleo kwa jamii.

Akipokea msaada huo, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Lilian Matinga aliishukuru Benki ya NMB kwa kuchangia maendeleo ikiwemo kuthamini sekta ya elimu kwa msaada huo wenye tija.

Awali akitoa taarifa, Afisa Elimu Taalum Sekondari Manispaa ya Mpanda, Raphael Mkupi amebinisha kuwa wanafunzi katika shule ya Sekondari Rungwa hulazimika kukaa wawiliwawili kwa kiti kimoja kutokana na kuwepo kwa upungufu wa viti zaidi ya 300.

WAFANYAKAZI FASTJET Plc NCHINI WACHARUKA,WAIOMBA SERIKALI KUZUIA NDEGE MBILI ILI WALIPWE FEDHA ZAO

0
0
 Mfanyakazi Mwandamizi ndani ya Ndege (Senior Cabin Crew) Mohamed Ngananya akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam kuhusu madai ya Wafanyakazi katika Kampuni ya FastJet PLC, 
Afisa Mwendeshaji Mkuu, Upande wa Airport, Alex Mjoge akizungumzia suala hilo la madai yao kama Wafanyakazi wa FastJet PLC. Kulia ni Mfanyakazi Mwandamizi ndani ya Ndege (Senior Cabin Crew) Mohamed Ngananya.
 Sehemu ya Wafabyakazi wa Kampuni ya Fastjet (Fastjet Plc)


*Waiomba Serikali chini ya Rais Dk. Magufuli kuingilia kati kuhakikisha haki inatendeka, 

* Wamshauri Masha akae kimya kwani naye ni mfanyakazi kama wao na anadai mshahara


Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

WAFANYAKAZI wa Kampuni ya Fastjet(Fastjet Plc) nchini Tanzania wameiomba Serikali kuzishikilia ndege mbili za kampuni hiyo ili walipwe madeni yao ambayo wanadai kwa sasa yanayofikia Sh.Bilioni 2.75.

Wamesema kuna madai mengi ya fedha ambayo wafanyakazi wa Fastjet Plc walioko nchini Tanzania wanadai huku wakitoa ombi kwa Serikali ya Awamu ya Tano kuwasaidia ili wapate haki zao ikiwemo malimbikizo ya mshahara wanayodai.

Pamoja na kutoa kilio chao ,wafanyakazi hao wamesikitishwa na madai ambayo yametolewa na mfanyakazi mwenzao Laurance Masha ya kudai wafanyakazi wamelipwa mshahara wakati sio kweli kwani hata yeye naye anadai mshahara.

Wakizungumza leo Machi 6,2019 katika ofisi za Fastjet zilizopo Vingunguti jijini Dar es Salaam ,wamesema katika kuhakikisha wanapata haki zinazostahili wamechukua hatua mbalimbali ikiwemo ya kwenda kwenye mamlaka husika ambazo wanaamini zitawasaidia kupata haki zao.

Akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wengine wa Fastjet zaidi ya 125, Mfanyakazi Mwandamizi ndani ya Ndege (Senior Cabin Crew) Mohamed Ngananya amesema kuwa kikubwa ambacho wanaiomba Serikali ni kuzishikilia Ndege mbili za Fastjet ambayo moja ipo nchini Tanzania na nyingine ipo Nairobi nchini Tanzania.

 "Tunapenda kutoa dukuduku letu kwa Serikali yetu ya Tanzania kuingilia kati na kutusaidia kupata madai na maslahi yetu kama wafanyakazi wa Tanzania toka kampuni Mama(Fastjet Plc) ambayo ndio mmiliki wetu mpaka leo hii tunazungumza na vyombo vya habari," amesema.

Ametaja baadhi ya madai yao ni malipo ya kisheria ya kuvunjwa kwa mkataba wa mfanyakazi ,malipo ya kisheria ya kiinua mgongo ya iliyokuwa Fly540 Tanzania Ltd, michango yao ya mifuko ya hifadhi (NSSF na PSSSF ya tangu Agosti 2018.Pia madai ya mshahara ya January 2019 ambayo baadhi yao wamelipwa nusu mshahara na kuahidiwa kulipwa kiasi kilichobakia baada ya wiki mbili lakini hawajalipwa mpaka leo.

Madai mengine ya wafanyakazi hao ni mshahara yao ya Februari 2019 ambayo haijalipwa kabisa."Tunaomba Serikali yetu kuzuia ndege mbili aina ya Embrear 190 zenye usajili wa Tanzania 5H- FJH na 5H-FJI na zisifutiwe huo usajili au kuruhusiwa kuondoka nchini kabla ya kulipwa madai yetu haya,"amesema Ngananya.

Ameongeza kuwa.menejinenti ya Kampuni yao hapa nchini Tanzania ulishawishi kutoa muongozo kwa Fastjet Plc kuwa kampuni hiyo ifungwe kwa taratibu zilizo rasmi na kisheria ili kuwezesha kila mfanyakazi na watoa huduma wote walipwe stahiki zao lakini hilo halikuzingatiwa na matokeo yake kusikia ghafla kuwa kampuni ya Fastjet Tanzania imeuzwa,hivyo wamtoa mwito kwa taasisi za Serikali kufuatilia kwa makini ununuzi huo.

" Zaidi Menejimenti ilitoa ushauri kwa mamlaka husika  TCAA ambayo inaratibu safari za anga na mashirika ya ndege hapa Tanzania kuwa wasitambue au kukubali mbadilishano huo wa umiliki wa kampuni hii hapa nchini kwasababu menejimenti haikuwa na taarifa za kina na za kutosha kuhusu uwezo wa kifedha kuendesha shughuli za usafirishaji abiria na kwa muda gani,"amesema.

Ngananya ameongeza kwanautaarifu umma wa Wa Tanzania kuwa kinachoendelea Fastjet Tanzania si kwasababu za kisasi kama wengi wanavyosema au kufikiria bali ni matatizo ya kiutendaji ya mwajiri wao mkuu ambaye ni Fastjet Plc kwa kutaka kukimbia madeni ambayo wanakataa kuyalipa madai yetu

"Tunaomba ujumbe kwa wafanyakazi wenzetu waliopo Zimbabwe na Msumbiji ,wachukue tahadhari ili mambo kama haya yasiwakute," amesema.

Alipoulizwa kuhusu Laurance Masha ambaye amekaririwa na baadhi ya vyombo kuwa wafanyakazi wa Fastjet wamelipwa mshahara,amejibu madai hayo hayana ukweli na kwamba hata yeye Masha naye mshahara wa Januari mwaka huu na mshahara wa February bado hajalipwa.

Alipoulizwa Masha ndio mmoja wa wanahisa,Ngananya amejibu kuwa wanachojua wao Masha ni mfanyakazi mwenzao kama walivyo wengine na wala hausiki na chochote ikiwemo ya kulipwa mishahara.

"Ni mfanyakazi kama tulivyo wengine tu,naye anadai kama sisi na hapa kwetu tunaye kiongozi wetu ambaye tunashirikiana kwa kila hatua ambayo tunaifanya ili kupata haki zetu,"amesema.

Kwa upande wake mfanyakazi mwingine ambaye ni Mkufunzi Ignace Tarimo amesema chini ya utawala wa Rais Dk.John Magufuli wanaamini haki yao itapatikana ingawa amesisitiza umuhimu wa Serikali kuzuia ndege hizo kwani ndizo zitawafanya wao wapate haki yao.

Wakati huo huo wafanyakazi wa Fastjet wamemshauri Masha ni bora akawa kimya badala ya kutoa kauli ambazo hazina ukweli na matokeo yake umma unapotoshwa kwa kupewa taarifa ambazo hazina ukweli.

Hats hivyo Masha mwishoni kwa wiki akizungunza na kituo cha Azam TV ametumia nafasi hiyo kuzungumzia mambo ya kampuni hiyo ambapo aligusia suala la mishahara kuwa mishahara wa January umelipwa na mkakati wa kampuni hiyo ni kuingiza ndege sita.

UBALOZI WA JAPAN KUJENGA SEKONDARI KEIKEI KONDOA

0
0

Ubalozi wa Japan umeahidi kujenga Shule ya Sekondari ya kata ya Keikei ili kupunguza mrundikano wa wanafunzi katika Shule ya Sekondari ya kata ya Busi inayohudumia wanafunzi wa kata mbili.

Ahadi hiyo ilitolewa na mwakilishi wa ubalozi wa Japan Bwana Takao Kurukawa katika kata ya Keikei alipofika katika eneo lililotengwa kwaajili ya ujenzi wa sekondari hiyo hivi karibuni.

“Nimekuja kuangalia eneo ambalo litajengwa Shule ya Sekondari na ubalozi wa Japan baada ya kupokea maombi ya kuomba kujengewa shule kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa “Alisema Bwana Takao

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Mhe. Sezeria Makota aliwashukuru ubalozi wa Japan kwa msaada wao na kuwataka wananchi wa Keikei kujitoa kwa hali na mali ila kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kuwahudumia wananchi.

“Shukrani za dhati ziende kwa Mbunge Mhe.Ashatu Kijaji kutokana na agenda yake ya kuhamasisha elimu na sasa anatekeleza kwa vitendo baada ya kuona watoto wengi wanafaulu na kwenda shule ya Sekondari Busi hali iliyopelekea kuwa na upungufu wa madarasa hivyo mheshimiwa mbunge akaamua kwenda kuomba msaada ubalozi wa Japan na leo wamekuja.” Alisema Mhe.Makota

Hata hivyo Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Kondoa Mustapha Semwaiko alisema kuwa katika Kata 21 za Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa ni Kata ya Keikei pekee ambayo haikuwa na Sekondari ya Kata na kulikuwa na ufaulu mkubwa wa wanafunzi ambao ulisababisha msongamano katika Sekondari ya Busi na kupelekea kuwe na upungufu wa madarasa.

“Kutokana na kuwa na tatizo la madarasa Shule ya Sekondari ya Busi tulishirikiana na Mheshimiwa Mbunge tukapiga hodi katika ubalozi wa Japan ambao walikubali na watatujengea madarasa 8, matundu ya vyoo 10 na ofisi 2 za walimu na sisi tumetenga eneo la ekeri18 kwaajili ya ujenzi wa shule hiyo.”Alisisitiza Mustapha

Mmoja wa wananchi wa Kata hiyo Bwana Juma Ramadhani aliwashukuru viongozi wote walioshiriki katika kufanikisha jambo hilo kwa kuwa watoto wao walikua wakitembea umbali mrefu kufuata Sekondari katika kata jirani.

Eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari ya kata ya Keikei wilayani Kondoa.

Afisa kilimo wa halmashauri ya Wilaya ya Kondoa akisoma taarifa mbele ya mwakilishi wa ubalozi wa Japan na viongozi wa Wilaya ya Kondoa.
Wananchi wa kata ya Keikei wakimuonyesha mwakilishi wa ubalozi wa  Japan jinsi ya kuhifadhi vitu kiasili kwa kutumia kamba maalumu ambazo walimpa kama zawadi.
Mwakilishi wa ubalozi wa Japan Bwana Takao  Kurukawa akipokea zawadi ya mbuzi na asali kutoka kwa wananchi wa kata ya Keikei.

UWT PWANI WATOA MSAADA WA SH.LAKI TANO KWA WAZAZI,YATIMA NA WASICHANA WA SEKONDARI YA IKWIRIRI.

0
0
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT) wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani,Farida Mgomi akiwa amempakata mtoto Juma Abdul wakati jumuiya hiyo ilipotembelea Kituo cha Afya cha Ikwiriri jana katika maadhimisho ya wiki ya wanawake duniani. Aliyesimama Katikati ni Mbunge wa Viti Maaalumu wa CCM Mkoa wa Pwani na Naibu Waziri wa Nishati,Subira Mgalu. Msaada huo una thamani ya Sh.500,000.Picha Zote na Elisa Shunda
Picha ya Pamoja baada ya makabidhiano
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT) wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani,Farida Mgomi (katikati) akizungumza na watoto wanaoishi maisha magumu na yatima wa kituo cha kulelea watoto cha Home Childrens jana,baada ya kuwakabidhi vitu mbalimbali katika maadhimisho ya wiki ya wanawake duniani. Msaada huo una thamani ya Sh.500,000.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT) wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani,Farida Mgomi (Kulia) akikabidhi msaada wa unga,sabuni na mafuta kwa uongozi wa shule ya sekondari ya Ikwiriri baada ya kuzungumza na wasichana wa shule hiyo iliyopo wilayani Rufiji jana. Msaada huo una thamani ya Sh.500,000.
Mwenyekiti wa UWT CCM Mkoa wa Pwani,Farida Mgomi akizungumza na wasichana wa sekondari ya Ikwiriri juu ya kutambua thamani yao kusimamia malengo waliyojiwekea katika maisha yao.
Wakitembela Wodi ya Wazazi na Kujionea Changamoto Mbalimbali Zinazoikabili Kituo Hicho.

Viongozi wa UWT wakiwa pamoja na watoto wa Kituo cha Home Childrens kinacholea Watoto Wanaoishi katika Maisha Magumu na Watoto Wasio na Wazazi Yatima.




Kaimu Katibu wa Uwt Mkoa wa Pwani,Mwajuma Nyamka (katikati) akijadili jambo na Mwenyekiti wa Uwt Mkoa wa Pwani,Farida Mgomi na Naibu Waziri wa Nishati,Subira Mgalu wakati walipotembelea Kituo cha afya cha Ikwiriri jana.


NA:ELISA SHUNDA,RUFIJI


UMOJA wa Wanawake Tanzania (UWT) wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Mkoa wa Pwani Wamewatembelea na Kutoa Msaada wa Sabuni ya Miche na Unga,Vyakula na Mafuta ya Kula Zenye Thamani ya Shilingi Laki Tano kwa Wanawake Waliolazwa katika Wodi ya Wazazi ya Kituo cha Afya cha Ikwiriri,Wanafunzi Wasichana wa Sekondari ya Ikwiriri na Kituo cha Watoto Yatima cha Childrens Home.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo Mwenyekiti wa Uwt Mkoa wa Pwani, Farida Mgomi alisema kuwa wapo katika wiki ya maadhimisho ya wiki ya wanawake duniani ambacho kilele chake ni Machi 3 mwaka huu wao kama wakinamama wa mkoa wa pwani wameamua kuitumia wiki hiyo katika kutoa misaada ya vitu mbalimbali kwa watu wenye mahitaji maalumu na kutoa nasaha pamoja na kusikiliza changamoto zao ili kuwasaidia katika kuwakomboa wanawake na jamii kiuchumi,kisiasa na kifikra.

“Tumeamua kutumia wiki hii ya maadhimisho ya wanawake duniani kutoa misaada mbalimbali kwa watu maalumu wenye mahitaji ambapo katika maadhimisho haya sie uwt pwani tumewatembelea wodi ya wazazi na kuzungumza na wanawake kujua changamoto zao katika kituo cha afya cha ikwiriri,tumezungumza na wasichana wa sekondari ya ikwiriri juu ya kutambua thamani yao na kujitunza lakini pia tumetembelea kituo cha watoto waishio maisha magumu na yatima cha Ikwiriri tumekaa nao tumewasikiliza shida zao lakini pia kile tulichojaliwa kubeba tuliwapatia wenzetu kama njia ya kuwafariji na kuwaonyesha tupo pamoja nao;

“tumebahantika kuzungumza na wasichana wa sekondari ya Ikwiriri ambapo tumewaasa kuachana na masuala yote ya mtaani ikiwemo kurubuniwa na wanaume waishio karibu na shule hiyo,madereva bodaboda hata na walimu wao ili wapewe maksi nzuri lakini pia tumewaonya kutojipitisha pitisha na kuwatengenezea mazingira ya ushawishi walimu wao na mtaani kwa ujumla kwa kuvaa nguo zenye heshima na kuwa na staha katika shughuli zao ili waje kutimiza malengo yao tunatarajia kupitia wao tuje kupata viongozi wa ngazi za juu kama makamu wa Rais Mama Samia Hassan Suluhu na wengineo” Alisema Mwenyekiti Mgomi.

Aidha Mwenyekiti Mgomi ameipongeza Serikali ya Rais na Mwenyekiti wa CCM Taifa,Dk.John Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya katika utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa kuipatia uongozi wa kituo cha afya cha Ikwiriri Shilingi Milioni 4 iliyowezesha uboreshaji na ukarabati wa majengo ya kituo hicho.

Aidha katika msafara huo wa uwt pwani waliongozana na Naibu Waziri wa Nishati,Subira Mgalu Mbunge wa Viti Maalumu Anayetokea Mkoa wa Pwani alisema akiwa kama mbunge amepokea changamoto iliyosemwa na mganga mkuu wa kituo hicho na kusema bunge lijalo serikali itapeleka bungeni muswada wa kufanya bima ya matibabu badala kutibiwa sehemu uliyokatia utakuwa unahudumiwa mahali popote nchini.

“faida ya mabadiliko hayo hata upatikanaji wa dawa utaongezeka,na kwa mujibu wa takwimu walau kwa sasa dawa zinapatikana tofauti na awali hasa kwa zahanati na vituo vya afya ambavyo havidaiwi,ila nitalifikisha kwa mkurugenzi wa msd kuhusu watumishi pia naishukuru serikali yangu kwa mkoa wetu mwaka wa jana tumepata watumishi 248 kati ya walioajiliwa mi hatua nzuri” Alisema Mgalu

Akizungumza baada ya kuwapokea uongozi wa uwt,Mganga Mkuu Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Ikwiriri,Dk.Iddy Malinda aliishukuru serikali kwa kuwapatia fedha Shilingi Milioni 4 ambazo walizitumia katika uboreshaji wa majengo ya kituo hicho lakini pia kuna changamoto ya uhaba wa watumishi na vifaa tiba pamoja na madawa na kuiomba serikali ishughulikie suala hilo kwa kuwa kituo hicho kinahudumia wagonjwa wa aina mbalimbali kulingana na sehemu ilipo. 

Lengo la Maadhimisho ya Wiki ya Wanawake Duniani ilitokea katika nchi za ulaya zilizoendela ambako wanawake waliamua kwa makusudi kupambana kutokana na uonevu waliokuwa wakiupata kwenye viwanda wengi wao waliuawa ndio maana siku hii ikawekwa kama kumbukumbu ya wapigania haki hao.

SERIKALI YAJITOSA KUTATUA MGOGORO WA WAWEKEZAJI WA KILIMO CHA KAHAWA WILAYANI HAI MKOANI KILIMANJARO

0
0

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akizungumza na Viongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Wawekezaji na Wanachama wa Ushirika wa kilimo cha zao la Kahawa wilayani Hai mkoani Kilimanjaro (Murososangi). 
Meza Kuu ikiongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (wa pili kulia) wakisikiliza kwa makini maelezo ya wanaushirika wa kilimo cha Kahawa wilayani Hai- Murososangi, kuhusu kiini cha mgogoro na Mwekezaji wa Kampuni ya Tudeley Estates Limited kutoka Uingereza kuwa ni kuletwa kwa Mwekezaji mwingine kutoka Ujerumani Bw. Marcus Shiber, bila ridhaa yao. 
Wanaushirika wa kilimo cha Kahawa wilayani Hai- Murososangi, wakiwa katika Mkutano na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Angela Kairuki (hawapo pichani) walipofika wilayani hapo kutatua mgogoro ya uwekezaji katika zao la kahawa. 
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Bi. Anna Mghwira, akizungumza na wadau wa kilimo cha Kahawa wilayani Hai wakati wa mkutano kati Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Angela Kairuki (hawapo pichani) na wadau wa kilimo cha kahawa wilayani Hai. 
Mwekezaji wa Kilimo cha Kahawa kutoka Ujerumani Bw. Robert Clowes (wa pili kulia) na Mkurugenzi wa Kampuni ya Kahawa ya Mbosho Bw. James Powell wakiwa katika mkutano wa kutatua mgogoro ya uwekezaji katika zao la kahawa chini ya uenyekiti wa Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), na kuwashirikisha Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Mhe. Angela Kairuki (Mb) (hawapo pichani) na wadau wa kilimo cha kahawa Wilayani Hai. 
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Bi. Anna Mghwira (kulia) akipeana mkono na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) alipofika wilayani Hai, kutatua mgogoro ya wawekezaji katika Sekta ya kilimo cha kahawa katika Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro. 
Wadau wakiwa katika mkutano wa kutatua migogoro kati ya wawekezaji na Chama cha Ushirika wa wakulima wa Kahawa Wilayani Hai, Mkoani Kilimanjaro (Picha na Josephine Majura, Wizara ya Fedha na Mipango) 


…………………………….. 


Na Josephine Majura na Peter Haule, WFM, Kilimanjaro 


Serikali imeitaka Kampuni ya Tudeley Estates Limited kutoka Uingereza iliyoingia mkataba na vyama vya Ushirika Wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro vinavyojishughulisha na uwekezaji wa Kilimo cha Kahawa (Murososangi), kurudi nchini ili kufanikisha utatuzi wa mgogoro uliosababishwa na kuibuka kwa mwekezaji mpya ambae mkataba wake haujulikani. 


Hayo yamebainishwa na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anaeshughulikia Uwekezaji Angela Kairuki walipofanya mkutano na Wawekezaji, Vyama vya Ushirika na Wadau wengine kuhusu mgogoro na Mwekezaji huyo Wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro. 

Dkt. Mpango alisema kuwa, Vyama vya Ushirika vya Murososangi, viliingia mkataba na Kampuni ya Tudeley Estates Limited ya nchini Uingereza ambapo washirika hao wenye mashamba eneo la Kibo na Kikafu wilayani Hai, yenye ukubwa wa hekari 2054 walimpa Mwekezaji huyo ili kuendeleza zao la kahawa kuanzia mwaka 1998. 

Alisema kuwa baada ya mwekezaji huyo, Bw. Conrad Legg, kuonesha nia ya kutoendelea na uwekezaji huo aliondoka nchini, wakaja wawekezaji wengine kutoka Ujerumani ambao waliingia mkataba na Kampuni ya Tudeley Estates Limited, kwa kununua hisa bila kuvishirikisha Vyama vya Ushirika vilivyoingia mkataba wa awali jambo lililosababisha sintofahamu kwa wana ushirika hao. 

“Aliyeingia mkataba na Murososange, arudi nchini ili kutatua mgogoro huo ili kuona Wananchi wanawezaje kuingia mkataba mwingine na mwekezaji mpya ambao utalinda maslahi ya wananchi wenye mashamba hayo na pia mwekezaji”, alisema Dkt. Mpango. 

Alisema Wanaushirika hao wanataka Mwekezaji wa kwanza arudi nchini ili wavunje mkataba wa awali kwa kuwa mkataba huo haujaisha muda wake hivyo hawawezi kuingia mkataba na mwekezaji mpya wakati ule wa awali bado unaendelea. 

Aidha, alisema kuwa mwekezaji mpya kutoka Ujerumanim Bw. Marcus Shiber, alianza kuleta fedha katika eneo la uwekezaji na kulipa baadhi ya kodi za mtangulizi wake, madeni, mishahara na kuboresha miundombinu ya mashamba hayo bila kupata muafaka na Vyama vya Ushirika jambo ambalo liliendelea kuleta mgogoro. 

Dkt. Mpango alisema kuwa, wamepata maelezo kutoka pande zote na baadhi ya maelezo hayo yanahitaji ushauri wa kisheria hivyo tumeiomba Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kuyafanyia kazi mambo hayo ili kuweza kumshauri Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, namna bora ya kumaliza mgogoro huo bila kuingizia Serikali hasara. 

Aliwatahadharisha watendaji wakuu wa serikali kutotumia ubabe na vitisho kwa wawekezaji ili kutoharibu taswira ya taifa katika masuala ya uwekezaji unaopigiwa chapuo hivi sasa na Serikali ya Awamu ya Tano, ili kuvutia mitaji, mapato ya serikali, ajira kwa vijana na kuvutia teknolojia za kisasa kwa maendeleo ya Taifa. 

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Angela Kairuki, alisema kuwa kutokana na mgogoro huo wa kiuwekezaji akaunti za Mwekezaji mpya kutoka Ujerumani ikiwemo ya Kampuni ya Kuza Afrika inayojishughulisha na kilimo cha parachichi Mkoani Mbeya ilifungwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, kuhusiana na masualaya kodi, jambo lililosababisha baadhi ya shughuli za Mwekezaji huyo kukwama. 

Alisema kuwa kikosi chao kupitia Waziri wa Fedha na Mipango aliyetumwa na Mhe. Rais Dkt. John Magufuli kutatua mgogoro huo, wameangalia iwapo taratibu za kufungwa akaunti hizo zilifuatwa na kutafuta njia bora ya kutatua tatizo hilo na pia kuona ni Mwekezaji yupi anafaa kuingia mkataba na Vyama vya Ushirika vya Murososangi, nia ikiwa ni kuona Vyama hivyo vinanufaika na Uwekezaji unakua nchini. 

Kwa Upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Bi. Anna Mgwira, aliishukuru Serikali kwa hatua yake ya kutuma Mawaziri ili kutatua mgogoro huo wa muda mrefu ambao utatuzi wake utasaidia Wananchi kukuza uchumi wao na Taifa kwa ujumla. 

Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji nchini-TIC, Bw. Geofrey Mwambe, alisema kuwa katika mkutano kati ya Mawaziri, Wawekezaji na Vyama vya Ushirika wamebaini kuwa utaratibu walioukuta Wawekezaji kutoka Ujerumani haukuwa sawa na ule ambao waliwekeana na Mwekezaji wa kwanza kutoka Uingereza, hivyo kuleta ugumu kiutendaji kwa Mwekezaji wa pili. 

Alisema kuwa, Serikali inahitaji uwekezaji katika Sekta ya Kilimo ili kupata malighafi ya viwanda nchini, kuongeza mnyororo wa thamani na kukuza pato la Taifa, hivyo inafanya jitihadi za kuvutia wawekezaji watakaoleta mitaji na teknolojia ya kisasa ili Taifa liweze kukabiliana na ushindani wa bidhaa katika soko la Kimataifa. 

Mwakilishi wa mwekezaji mpya kutoka Ujerumani Bw. Robert Clowes, alimshukuru Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa kuwatuma Mawaziri wake kuja kutatatua mgogoro huo, alisema Tanzania kuna fursa nyingi za uwekezaji hivyo yupo tayari kuendelea kuwekeza zaidi nchini kwa lengo la kupata manufaa kwa pande zote ikiwa ni pamoja na Kampuni yake na vyama vya ushirika wa kilimo cha Kahawa Wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro.

Upandikizaji Figo Nchini Waokoa Mabilioni ya Fedha


DKT. KALEMANI ATOA AGIZO KWA TANESCO NDANI YA SIKU 5 LIWE LIMETEKELEZWA

0
0
Waziri wa Nishati Dkt. MEDARD KALEMANI akitoa maelekezo kwa Tanesco mara baada ya kutembelea Substation ya Njiro jana. Picha na Vero Ignatus
Mkuu wa substation ya Njiro Heriel Mbuya akitoa ufafanuzi kwa Waziri wa nishati Dkt. Medard Kalemani alipomtembelea jana, kushoto kwake ni mkuu wa wilaya ya Arusha mjini Gabriel Daqqaro. Picha na Vero Ignatus.

Meneja wa kituo cha gredi ya taifa kilichopo njiro Heriel Mbuya akiwa katika chumba maalumu cha kuongozea mitambo akitoa ufafanuzi kwa waziri wa nishati Dkt Medard Kalemani pamoja. Na viongozi wengine waliotembelea katika kituo hicho. Picha na Vero Ignatus



Na. Vero Ignatus, Arusha



WAZIRI wa Nishati Dk.Medard Kaleman ametoa siku tano kwa Shirika la umeme Tanesco Mkoa wa Arusha kufunga Transfoma tatu  eneo la Meru ili kuwawezesha wananchi wa eneo hilo kupata umeme mkubwa unaokidhi haja zao



Dkt. Kaleman ametoa agizo hilo jana wakati wa ziara yake ya kutembelea kituo kikuu cha kupokea umeme wa Gridi ya Taifa, kilichopo Njiro Jijini Arusha Dk.Kaleman alisema kumekuwa na malalamiko mengi ya wananchi wa eneo la Meru  Wilayani Arumeru Mkoani hapa,kuwa wanapata umeme mdogo.



"Sasa nimeamua kuja kuangalia kituo hiki kinachopokea umeme kama upo wa kutosha, sasa nimejiridhisha upo umeme mwingi tatizo ni wafanyakazi wa Tanesco kupeleka Transfoma za nyongeza tu, sasa nawapa siku tano mpeleke Transfoma mbili au tatu eneo la Meru mkawafungie wapate umeme wa uhakika,"alisisitiza



Dkt.Kaleman alisema umeme unapokuwa mdogo wananchi wanalalamika haswa wafanyabiashara ambao ndiyo waathirika wakubwa na ndiyo wengi Mkoani Arusha



Alisema baada ya kuongeza Taransfoma hizo hatategemea wafanyabiashara kulalamika tena na kupata visingizo vya kutolipa kodi, bali wautumie kuzalisha bidhaa nyingi katika viwanda vyao na bora, pamoja na kulipa kodi stahiki kwa serikali.



Pia aliiagiza Tanesco ndani ya mwezi huu kuagiza  kifaa maalum cha kukata umeme inapotokea hitilafu, mbili au tatu  (Saketi breka)na kuzihifadhi  katika stoo ya kituo hicho kama akiba, ili inapoharibika mashine moja inachukuliwa ya akiba na kufunga mara moja.



"Mkiwa nazo za akiba mtaondokana na kuwaletea kero wananchi, ambao wanalalamika na ukosefu umeme pale inapotokea mashine imeharibika mnachukua siku nne kusubiri kije kifaa hicho baada ya kuagiza, sasa hakikisheni ndani ya mwezi huu mnanunua viwili au vitatu vya akiba ili mashine ikiharibika mara moja mnakiweka na wananchi wanaendelea kupata umeme,"alisema 



Kwa upande mwingine aliagiza shirika hilo kuweka utaratibu wa kuwapa posho, walinzi wanaolinda miundombinu ya Shirika katika kituo hicho usiku na mchana bila kupumzika,ili kuwapa moyo zaidi wa kufanya kazi hiyo bila kukata tamaa.

Wizara ya Madini yatishia kuufunga mgodi wa Acacia North Mara

0
0
 Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Serikali kupita Wizara ya Madini, imetishia kuufunga mgodi wa dhahabu wa Acacia North Mara uliopo Nyamongo wilayani Tarime, kutokana na kutiririsha maji machafu hadi katika makazi ya wananchi wanaozunguka mgodi huo.


Waziri wa Madini, Doto Biteko alitoa onyo hilo jana Machi 05, 2019 alipofanya ziara katika mgodi huo akiambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa Mara, Wilaya Tarime pamoja na Maafisa mbalimbali kutoka Wizara hiyo.


Alisema Septemba 07, 2018 Rais Dkt. John Pombe Magufuli alipofanya ziara katika eneo la Nyamongo wananchi walilalamikia mgodi huo kutiririsha maji machafu hadi kwenye makazi yao ambapo Kamati Maalum kutoka Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Wizara ya Ofisi ya Makamu wa Rais inayoshughulikia Mazingira na Muungano iliundwa kuchungumza malalamiko hayo na kubaini kwamba yalikuwa ya kweli.
Waziri wa Madini, Doto Biteko akifafanua jambo baada ya kutembelea maeneo yanayolalamikiwa na wananchi kuwa yanatiririsha maji machafu katika mgodi wa Acacia North Mara wilayani Tarime.
Wananchi wa Nyamongo wilayani Tarime mtaro ambao umeanza kuchimbwa ili maji machafu yasitiririke kuelekea kwenye makazi yao.
Waziri wa Madini, Doto Biteko akiwa ameambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa Mara, Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya Tarime pamoja na Maafisa mbalimbali kutoka Wizara hiyo wakielekea kwenye maeneo yanayotiririsha maji machafu kutoka mgodi wa Acacia North Mara.
Tazama BMG Online TV hapa chini

Tanzania haturuhusu takwimu zinazopotosha - Dkt Albina Chuwa

0
0
Mahojiano na Dkt. Albina Chuwa, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Tanzania, NBS, akihojiwa na Arnold Kayanda kando mwa mkutano wa 50 wa Kamisheni ya Takwimu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani

HABARI ZA UMOJA WA MATAIFA KUTOKA NEW YORK, MAREKANI, MACHI 6, 2019

RC MAKONDA ATAHADHARISHA WANA DAR ES SALAAM KUHUSU MVUA NA MAFURIKO

PROFESA KANGALAWE AFUNGA KONGAMNO LA KIMATAIFA LA SIKU TATU JUU YA SERA NA UONGOZI

KUMEKUCHA Azam Sports Federation Cup (ASFC)

0
0
Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii


DROO ya Kombe Shirikisho Nchini Azam Sports Federation Cup (ASFC) imefanyika leo ambapo timu nane zilizotinga hatua ya nane bora zimetambua zitacheza na nani hatua ya robo fainali.

Timu hizo ambazo zilitinga hatua hiyo ni pamoja na Yanga, Alliance FC, African Lyon, Azam FC, Lipuli, KMC na Kagera Sugar.

Michuano hii inatarajiwa kuanza mapema mwezi Machi itakuwa namna hii:-

Yanga wataifuata Alliance ya Mwanza Uwanja wa CCM Kirumba, Kagera Sugar wataikaribisha Azam Uwanja wa Kaitaba.KMC wataikaribisha African Lyon Uwanja wa Uhuru. Lipuli wataikaribisha Singida United Uwanja wa Samora.

Baada ya michezo hiyo ya robo fainali timu mshindi katika mchezo wa Lipuli dhidi ya Singida atacheza na mshindi baina ya Alliance na Yanga kwenye nusu fainali.

Mchezo mwingine wa nusu fainali utakuw ani kati ya KMC na African Lyon mshindi wake atacheza na mshindi kati ua Kagera Sugar na Azam.

Tarehe ya michezo hiyo itatangazwa baade na shirikisho la mpira wa miguu nchini.

SERENGETI BOYS YAFANIKIWA KUINYUKA AUSTRALIA 3-2 MICHUANO YA UEFA ASSIST.

0
0
 TIMU ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 17 Serengeti Boys kimefanikiwa kuibuka mshindi wa goli 3-2 dhidi ya Australia katika mchezo wa pili wa michuano ya Uefa Assist nchini Uturuki.

Michuano hiyo ilianza mwanzoni mwa wiki hii, huo unakuwa ni mchezo wa kwanza kwa Serengeti Boys baada ya mechi ya kwanza kupoteza dhidi ya Guinea kwa goli 2-1.

Serengeti Boys ilianza mechi hiyo kwa utaratibu na kuwapa nafasi Australia kuwashambulia na kupata goli la kuongoza kabla ya  Edmund John katika dakika ya 16.

Bao hilo lilidumu hadi mapumziko na kipindi cha pili Australia walianza kupata bao la pili na baadaye  Serengeti Boys walikuwa wakishambulia kama mbogo hadi walipofanikiwa kupata bao la pili katika dakika ya 81, mfungaji akiwa ni Alphonce John.

Baada ya bao hilo, Serengeti Boys waliongeza mashambulizi na kuonyesha kuwazidi nguvu Australia kabla ya kupata bao la tatu katika dakika ya 89 mfungaji akiwa ni Kelvin John.

SERIKALI YAWATAKA MAWAZIRI WATANO WAFANYE MAPITIO YA TAASISI ZAO KUONDOA MIGONGANO YA MAJUKUMU

0
0
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Mawaziri wa Kilimo, Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mifugo na Uvuvi na Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wakutane na wafanye mapitio ya taasisi zao na kuangalia maeneo yanayogongana kiutendaji ili kila mmoja abaki na jukumu lake.

Ametoa agizo hilo leo (Jumatano, Machi 6, 2019) alipotembelea Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na kukagua shughuli mbalimbali zinazofanywa na taasisi hizo na amewaagiza mawaziri wakutane na wampelekee taarifa ya mapendekezo yao ifikapo Machi 30, 2019.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya kuwepo kwa malalamiko na manung’uniko kutoka kwa baadhi ya wafanyabiashara ambao wamedai kuwepo kwa muingiliano wa majukumu ya kiutendaji ya taasisi hizo, hivyo kuwasababisha washindwe kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Waziri Mkuu amesema taasisi hizo zinashughuli ambazo zinaingiliana na kusababisha malalamiko kwa wateja wao, ambapo ametolea mfano suala la kudhibiti ubora wa bidhaa ambalo linafanywa na TFDA na TBS kwa mujibu wa sheria. Amewataka wapitie sheria zao na wajue ukomo majukumu yao.

“Kutaneni pitieni maelekezo ya Serikali yanayoelekeza namna ya kuzifanya taasisi hizi na zingine zinazofanya shughuli zinazofanana zilizo katika wizara zenu bila kusanau Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara (blue print). Ifikapo tarehe 30 mwezi huu niwe nimepata mapendekezo yenu,” amesisitiza.

Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka watendaji wa taasisi hizo wabadilike na waache urasimu kwasababu hauna tija katika utekelezaji wa majukumu yao na badala yake unaweza kuwayumbisha kwenye ufanyaji wao wa kazi. “Kila mmoja atekeleze majukumu yake kwa uzingatia maadili ya taaluma yake.”

Pia, Waziri Mkuu amewataka waangalie namna ya kuwahisha majibu ya vipimo vya bidhaa wanazoletewa na wateja, kama watakuwa wamekamilisha kabla ya siku za kisheria wawajulishe wateja wao na kuhusu sampuli ambazo zitakuwa hazijaharibika wakati wa vipimo wawarudishie.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuzitaka taasisi hizo ziangalie namna ya kusogeza huduma kwa wananchi kwa kuwa na watumishi katika ngazi za wilaya na kwa TFDA ameitaka ianzishe maabara nyingine mbili kwenye kanda ya Nyanda za Juu Kusini na ya Kaskazini ili kusogeza huduma kwa wananchi.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Cunbert Kapilima wa Shirika la Viwango Tanzania  -TBS (kushoto) kuhusu upimaji wa ubora maguani unaofanywa na TBS wakati alipotembelea ofisi za TBS, Ubungo jijini Dar es salam, Machi 6, 2019.
   Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kuhusu upimaji wa betri kutoka kwa Mhandisi  Anectus Nduguru wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) wakati alipotembelea Ofisi za TBS, Ubungo jijini Dar es salaam, Machi 6, 2019. 
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kuhusu upimaji wa vifaa vya umeme kutoka kwa Mhandisi  Anectus Nduguru wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) wakati alipotembelea Ofisi za TBS, Ubungo jijini Dar es salaam, Machi 6, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na watumishi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) wakati alipotembelea ofisi za  TBS,  Ubungo jijini Dar es salaam, Machi 6, 2019.  Kulia ni Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhandisi Stella Manyanya, wa tatu kulia ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu na wa nne kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji, Angela Kairuki.

Baraza la Wazee Asilia watoa msaada kwa Wagonjwa Mloganzila

0
0
Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila Redemptha Matindi akitoa neno la shukrani mara baada ya kupokea msaada wa sabuni, mafuta ya kujipaka uliotolewa leo hospitalini hapo.
Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi Sista Redemptha Matindi akiwa katika picha ya pamoja na wazee wa Baraza hilo leo katika Hospitali ya Mloganzila.
Kiongozi wa wodi ya wagonjwa wa magonjwa ya ndani Muuguzi Lucas Mwaijega (kulia) akikabidhiwa msaada na Katibu wa baraza hilo Mzee. Ahmad Tamla.


Baraza la Wazee Asilia Mbezi Luis Jijini Dar es salaam (BAWAZI) leo wametembelea Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila na kutoa msaada wa mafuta, sabuni pamoja na pampers kwa baadhi ya wagonjwa ambao hawajiwezi.

Akizungumza mara baada ya kupokea msaada huo Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga katika Hospitali ya Mloganzila Redemptha Matindi amewashukuru wazee hao kwa kujitoa na kuamua kuwasaidia baadhi ya wagonjwa ambao wanaendelea na matibabu hospitalini hapo na hawana uwezo wa kununua mahitaji yao mbalimbali.

“Tumefurahi kupokea msaada huu ambao kimsingi umewalenga wale wasiojiweza ni faraja kwetu kuona wazee kama nyinyi mkijitoa kwa ajili ya jamii hakika huu ni mfano wa kuigwa na watu wote’’. Amesema Sista Redemptha. 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa baraza hilo Mzee Abdallah Shomari amesema lengo la kutoa msaada huo ni kuunga mkono juhudi za serikali za kuboresha utoaji wa huduma za afya nchini.

“Tumeguswa na hali ya wagonjwa wasiojiweza na ndio maana tumeamua kuja kuwapatia tulichonacho, lakini pia hospitali hii ipo katika Manispaa yetu ya Ubungo hivyo tumeona ni muhimu kuja kuwatembelea wagonjwa hawa na kuwapatia msaada wa mafuta ya kujipaka, sabuni na pampers, tutaendelea kujitoa kadiri uwezo utakavyoruhusu’’. Amesema Mzee Shomari.

Pamoja na mambo mengine wazee hao pia wameelezea kuridhishwa na utoaji wa huduma za afya katika Hospitali ya Mloganzila na kutoa wito kwa jamii kuthamani na kutambua huduma zinazotolea hospitali hapo kwani ni za uhakika na zenye ubora wa juu.

Waziri Mkuu atembelea Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) jijini Dar es salaam

0
0
Na WAMJW - Dar Es Salaam
Serikali imedhamiria kushughulikia malalamiko yaliyotolewa na  wafanyabiashara kuhusu mkanganyiko wa majukumu baina ya Taasisi za Serikali zinazoingiliana majukumu na kuzitaka kila taasisi kama hizo ziwe na mipaka yake ya kazi na kupunguza urasimu.
Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa alipokuwa akizungumza na watendaji wa Mamlaka ya Chakula na Dawa TFDA mapema leo alipotembelea ofisi hizo kujionea utendaji wao wa kazi.
Waziri Majaliwa amesema Taasisi za Serikali ambazo zimekuwa zikiingiliana majukumu na zimekuwa zikisababisha adha kwa wananchi na kuongeza urasimu na upotevu wa muda mwingi katika kuwahudumia wateja.
“Serikali imedhamiria kutafuta ufumbuzi wa malalamiko ya mwingiliano wa majukumu baina ya taasisi za Serikali ili kumwondolea usumbufu mwananchi” amesema Waziri Majaliwa na kuendelea kusema kuwa mkanganyiko huo unapelekea watu kutokujua majukumu yao aidha kwa kutokujua sheria au kwa makusudi.
Waziri Majaliwa amesema kumekuwa na malalamiko mengi ya utendaji usiyo sahihi wa mwingiliano wa majukumu hasa kwenye eneo la ukaguzi na uchukaji wa sampuli baina ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na kuzitaka taasisi hizo kujiridhisha na kuyafahamu vizuri majukumu yao.
Kufuatia hali hiyo Waziri Kassim Majaliwa amewataka Viongozi wa Wizara ya Afya, Wizara ya Kilimo, Mifugo,Wizara ya Viwanda na Uwekezaji kuwasilisha ofisini kwake ripoti ya utekelezaji wa “Blueprint” ifikapo Machi 30 mwaka huu.
Aidha, Waziri Majaliwa ameitaka TFDA kujiimarisha zaidi kwenye ukaguzi wa vyakula na dawa na kuhakikisha bidhaa zisizokuwa na usajili haziingii sokoni na kuitaka TFDA kuongeza wataalam katika Mikoa na Wilaya ili kudhibiti mapito ya magendo ya bidhaa za chakula na dawa.
Kwa upande wake Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema Serikali imewekeza fedha nyingi katika maabara za uchunguzi wa vyakula na dawa na hivi sasa taasisi hiyo imefikia ngazi ya tatu ya ubora wa udhibiti wa dawa kimataifa hivyo kuaminika na mataaifa mbalimbali na kuvutia wafanyabiashara wengi zaidi kuja kuingiza bidhaa zao nchini.
Waziri Ummy amesema kuwa TFDA imepewa dhamana ya kulinda afya za watanzania kwa kuhakikisha vyakula na dawa zinazozitumia kila siku ni salama kwa afya za wananchi na kukiri kuwa kweli changamoto zipo na kupitia wizara yake atahakikisha changamoto hizo zinatatuliwa ndani ya muda mfupi.
Naye ,Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji Angellah Kairuki amesema kuwa Serikali imeanzisha huduma ya mahali pamoja iliyopo katika kituo cha uwekezaji (TIC) ambapo mpaka sasa zipo taasisi 16 ikiwemo TFDA huku akiomba Wizara husika kuongeza watumishi katika kitengo hicho ili kuweza kushughulikia kwa uharaka masuala ya uwekezaji katika vyakula na dawa.
Aidha,Waziri Kairuki amekiri kuwepo mkakanganyiko wa majukumu baina ya taasisi za Serikali huku akiitaka TFDA kutowahudumia wawekezaji wanaofika nchini wakiwa na Vyeti vya Usajili wa Vivutio kwani wanatakiwa kuhudumiwa na TIC.
"Naomba kuweka msisitizo, mara anapokuja mwekezaji, swali lenu la kwanza liwe ni kuuliza kama anacho Cheti cha usajili wa vivutio kutoka TIC au la, na endapo anayo basi nyinyi mwelekezeni TIC".Alisisitiza Waziri Kairuki
 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (kushoto) akisema jambo na watendaji wa ofisi ya Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) hawapo pichani alipotembelea ofisi hizo kuona utendaji kazi wao.  
 Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa wa (wa tatu kutoka kushoto) akiongozana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (wa pili kushoto) na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaj Mhe. Angellah Kairuki (kushoto) kuelekea maabara za Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) 
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa ameshika  dawa ya malaria aina ya DUO -COTECXIN,  halisi kulia na bandia kushoto zilizopimwa na  Maabara ya Mamlaka ya Chakula  na Dawa (TFDA)  wakati alipotembelea ofisi za  TFDA,  wa pili kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji, Angela Kairuki na wa tatu kulia ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.
Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa akionyeshwa sampuli na Dkt. Yonah Hebron Meneja wa Uchunguzi wa Dawa na Bidhaa katika maabara ya Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) mapema leo alipotembelea ofisi hizo kujionea utendaji kazi wao.

KONGAMANO LA WAFANYAKAZI WANAWAKE DODOMA KUELEKEA MAADHIMISHO YA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI

Viewing all 109593 articles
Browse latest View live




Latest Images