1. Usuli:
1.1 Mama MTEI azaa na Binamu wa Mume wake:
Bi.NGIANAELI NGEKALIO, mama yake EDWIN MTEI, alikuwa ameolewa na Bw. VICTOR SHAMBARI MTEI ambaye alifariki mwaka 1928. Bw. VICTOR alikuwa akiishi jirani kabisa na binamu yake aliyeitwa Bw. ELIAPENDA NGAPANYI MTEI. Baada ya Bw. VICTOR kufariki, Bw. ELIAPENDA akawa akifika mara kwa mara nyumbani kwa mama yake MTEI kumfariji na kumsaidia kazi mbalimbali kwani aliachwa na watoto 2. Matokeo ya ziara hizo za kumfariji ni mama huyo kupata ujauzito!.
1.2 Kuzaliwa kwa EDWIN MTEI:
EDWIN MTEI alizaliwa asubuhi ya siku ya Jumanne, tarehe 12.7.1932 baba yake akiwa ni Bw. ELIAPENDA NGAPANYI MTEI. Siku hiyo, mama yake akiwa mja mzito na akiwa na rafiki na jirani yake, Bi. NDEAMBILIASIA, waliamka asubuhi sana na kwenda eneo la Rawuya kwenye shamba la mahindi na maharage lililokuwa kilometa 8 toka Marangu. Baadae asubuhi hiyo, Bi. NGIANAELI akajifungua mtoto EDWIN na mchana akarejea kibabe nyumbani huku baby MTEI akiwa amebebwa na Bi. NDEAMBILIASIA. Wanawake enzi hizo hawakuwa mayai, walikuwa ngang'ari kinoma!.
1.3 "Baba yake "Kuuchuna"
Bw. ELIAPENDA NGAPANYI MTEI, baba yake, hakutaka kabisa ijulikane kuwa dogo EDWIN ni mwanae kwani mwanzoni mwa mwaka huo, 1932, alikuwa amefunga ndoa na Bi. LUCY MAWOLLE. Vivyo hivyo, mama yake nae alifanya siri sana na hakupenda watu wajue kuwa EDWIN ni mtoto wa Bw. ELIAPENDA NGAPANYI MTEI, ingawa "mzee baba huyo" huyo alikuwa akipeleka matunzo.
2. Elimu:
2.1 Elimu ya Vidudu/Msingi:
MTEI alisoma "shule ya vidudu" Ngaruma Lutheran Church, 1941 akiwa na miaka nane. MTEI alikuwa akitoka shule anakwenda kuchunga mbuzi na maisha yao yalikuwa ya kubangaiza na ya kifukara sana huku wakiishi kwenye nyumba ya majani. Mwaka 1943, MTEI alihamia Marangu Native Authority Primary School ambako alisoma na WILBERT KLERUU aliyekuwa anatoka umbali wa 10 Kms kwenda na kurudi kila siku. Bw. KLERUU alikuwa ni mwenye kiu kubwa ya elimu. Baadae akawa mmoja wa watanganyika wa mwanzo kuwa na PHD na akawa RC Mtwara na Iringa, kabla ya Mnyalukolo SAID MWAMWINDI kufanya yake tarehe 25.12.1971.
2.2 MTEI "Apasua pepa" Darasa la 4;
MTEI alifanya mtihani STD IV Exams for Nothern Province mwaka 1944. Matokeo yalitangazwa na Headmaster mzungu, G.W. GINNER wa Old Moshi Sec. School Januari, 1945. MTEI akashika namba moja na hivyo kuitwa kujiunga na Old Moshi.
Tarehe 31.1.1945, MTEI akafika shuleni hapo na kupokelewa na Mwalimu ERASTO MANG'ENYA aliyekuja kuwa Waziri na Spika wa Bunge. Shuleni hapo alisoma na Bw. CLEOPA MSUYA, aliyekuja kuwa PM na Bw. HERMAN SERWATT, mbunge pekee aliyekuja kuishinda TANU, DANIEL MFINANGA aliyekuja kuwa Balozi, Bw. SOLOMON ELIUFOO na Bw. ISRAEL ELINAWINGA waliokuja kuwa Mawaziri na WILBERT KLERUU.
Mwaka 1946 kulikuwa na mtihani wa taifa wa STD VI kwa nchi nzima ili kwenda STD VII. Kwavile MTEI alifiwa na baba yake Mei 1945, ambaye alikuwa akimsaidia kulipa karo, ikawa kimbembe! Hata hivyo, kwavile MTEI alikuwa "amepasua pepa", ikabidi Headmaster amnusuru na kufanya kitu kisicho cha kawaida kwa kuwaandikia Machifu wa Kichaga!.
Mwezi Octoba 1950, MTEI alifanya "STD X Territorial Exams" na kufaulu vizuri sana na akachaguliwa kujiunga na Tabora Boyz Sec School. Januari 1951 'akakwea gogo" kwenda shule yake mpya ambako alipokelewa na Headmaster JOHN CRABBE, na akakutana na wanafunzi wengine akina GEOFREY MMARI, aliyekuja kuwa Vice Chancellor, Udsm, OSCAR KAMBONA na JOB LUSINDE waliokuja kuwa Mawaziri na MARK BOMANI aliyekuja kuwa AG.
2.3 MTEI "Apasua pepa" Darasani 1952 & 1953 Tabora Boyz
MTEI alikuwa si mtu wa spoti-spoti kwani kwa miaka miwili mfululizo akiwa shuleni hapo, 1952 na 1953, alishika nafasi ya 1 darasani licha ya kusoma na utitiri wa "Vipanga!.
2.4 MTEI "Kipanga" wa "debates"
MTEI, licha ya "kuwatimulia vumbi" wenzake darasani, alikuwa ni "kiboko wa kutema yai" na "mkali wa debates" shuleni hapo. Hii ilipelekea mwishoni mwa 1952, Headmaster J. CRABBE aandike "EDWIN MTEI is an Excellent debator" .
2.5 MTEI "Kipanga" nchi nzima (TANGANYIKA ONE)
Mwezi Octoba 1952, MTEI akafanya mtihani wa Cambridge Overseas School Certificate Exams. Huu ulikuwa ni mtihani kwa wanafunzi wa Tanganyika, Kenya na Uganda. MTEI 'aliipasua pepa' hii kwa si tu kupata ufaulu wa Daraja la Kwanza, bali pia yeye ndiye alikuwa Mwanafunzi Bora Tanganyika!. Hivyo akachaguliwa kwenda kusoma chuo kikuu cha Makerere, Uganda ambako alikutana na watanganyika wengine akiwapo PAUL SOZIGWA.
2.6 MTEI Ashinda Insha ya History Makerere
MTEI aliendelea na moto wake ambapo mwaka 1956, kulikuwa na History Essay competition iliyojumuisha nchi nyingi ambapo MTEI aliibuka mshindi na kupewa kabati lililojaa vitabu vyenye thamani ya £200.
Mwaka 1957, MTEI alifanya mtihani wa mwisho kumaliza chuo na kufaulu vizuri na kukabiziwa shahada na kisha akarejea nchini.
3. MTEI Akutana na Mwalimu NYERERE kwa mara ya kwanza
MTEI alikutana na Mwalimu NYERERE jijini Dsm kwa mara ya 1 mwaka 1959 baada ya kupelekwa na rafiki yake, MWANJISI. Mwalimu alimwambia MTEI kuwa ipo siku wakoloni wataondoka na Watanganyika watajitawala wenyewe.
4. MTEI Aenda kufanya kazi KENYA:
Baada ya kuona Bongo hamna dili kwani serikali ya kikoloni haikumpa kazi yoyote akaamua "kuishia" zake Kenya.
5. Mwalimu NYERERE Amteua MTEI Katibu Mkuu Fedha:
Mwezi Agost 1964, Mwalimu alimteua MTEI kuwa Katibu Mkuu Wizara ya fedha. Mh. MTEI akafanya jambo la kizalendo kwa kuhakikisha kampuni ya kizalendo ya MECCO inapewa kandarasi ya kujenga Benki Kuu ya TZ.
6. Mwalimu amteua MTEI kuwa Gavana-Mteule
Mwanzoni mwa 1965, nchi za TZ, KN & UG zilikubaliana kila nchi itoke kivyake kwani hakukuwa na dalili ya kuwa na Federation. Mwalimu akamteua MTEI kuwa Gavana-mteule mwezi Octoba 1965. Majukumu yake makubwa yalikuwa kutayarisha fedha ya TZ, kushughulikia sheria ya kuundwa Benki Kuu, kuajiri "experts" na kuandaa mafunzo mujarab ya wafanyakazi wazalendo. Baadaye, Mwalimu akamteua Mh. MTEI kuwa Gavana wa BOT.
7. Mh. MTEI Awaibua BALALI na YONA:
Mh. MTEI akiwa Gavana mdogo kuliko wote katika historia ya TZ(34) aliibukia US alikomkuta Bw. DAUDI BALALI akisoma chuo kikuu cha Howard. MTEI alivutiwa sana na uwezo mkubwa wa BALALI na akamshauri asomee masomo yanayoendana na BOT. Baada ya kumaliza chuo, Mh. MTEI akamwajiri BALALI BOT na akawa kijana hodari sana. Mh. MTEI pia alimuibua DANIEL YONA na kumuajiri pia. Baadaye, Mwalimu alimchukua YONA ili kwenda kuongoza benki ya THB baada ya Mh. MTEI kumsifia sana.
8. Mwalimu NYERERE Ajipunguzia mshahara, Gavana MTEI Afuata Nyayo:
Mwalimu aliamua kujipunguzia mshahara wake wa Buku-Tano hadi Buku-Nne Jero_ kwani kulikuwa na kutofauti kubwa. Mh. MTEI, ambaye yeye na Mwalimu tu ndio walikuwa wakilipwa pesa ndefu, alifanya uzalendo wa hali ya juu sana kwa kuamua nae kujipunguzia. Mh. MTEI angekuwa kama viongozi wengi wa sasa wanaojali matumbo yao tu, asingejipunguzia kwani Mkataba wake ulikuwa na kipengele mahsusi kuwa hakuna mamlaka yoyote iwezayo kumpunguzia.
Hii ikapelekea mishahara ya viongozi wengine nayo kupunguzwa.
9. Mwalimu amteua Mh. MTEI kuwa Katibu Mkuu wa EAC
Mwalimu alimteua Mh. MTEI kuwa Katibu Mkuu wa EAC mwaka 1975 ambapo alihudumu kwa miaka 2 hadi 1977.
10. Mwalimu NYERERE Amteua Mh. MTEI kuwa Waziri wa Fedha:
Mwalimu alimteua Mh. MTEI kuwa Waziri wa Fedha mwezi Februari 1977.
11. Mh. MTEI Aenda US, apewa masharti chechefu na IMF
Mh. MTEI alikwenda US kutafuta misaada. Hii ilikuwa baada ya hali kuwa ngumu kwani katika vita ya Kagera tulikuwa tukitumia $ 500,000 kwa siku kwa mwaka mzima. Mh.MTEI akapewa masharti na IMF ya kushusha thamani ya shilingi na kurekebisha mashirika hoehae ya umma, na aliporejea Mwalimu akayakataa masharti hayo ya IMF.
12. Mh. MTEI Aupeleka Ujumbe wa IMF Msasani:
Tarehe 29.11.1979, Mh. MTEI aliupeleka Msasani ujumbe wa IMF uliokuwa ukiongozwa na Bw. BO KARLSTROM ili "kumkata shule" Mwalimu.
Ujumbe huo, ukiwa Msasani, ulimwaga mwembwe zake ukiamini umekonga moyo wa Mwalimu.
13. Mwalimu "Ajikata", Auacha Solemba Ujumbe wa IMF
Mwalimu alipoona Watasha hao wanaongea "vepa" tupu, "alijifanya kama anajikuna" kisha, ghafla bin vuu, bila kuaga, akaenda nje nyuma ya nyumba karibu na baharini yaani bichi, akawa anapunga upepo na kuwaacha Watasha seblen!.
14. Mh. MTEI Amuibukia Mwalimu Bichi:
Mh. MTEI akaona Kama Mbwai, Mbwai tu hivyo akamfuata Mwalimu hukohuko bichi na kumuomba arudi. Mwalimu, akiwa amefura kwa hasira, akamwambia Mh. MTEI kuwa hawezi kuacha nchi yake ikiongozwe toka Washington. Mwalimu alisema- "Mimi nikikataa kitu msimamo wangu unabaki pale pale, sitaki nigeuke Mnara wa chumvi. Waambie hao jamaa zangu warudi makwao kwani nimewasikia ila sikubaliani nao".
Mh. MTEI alijaribu kumsihi Mwalimu arudi seblen japo awaage wageni ili kuwaonesha ukarimu wa Watanzania lakini Mwalimu hakutaka kuona pua wala sikio la mtu yeyote wa IMF!. Hivyo, Mh. MTEI kwa unyoonge akarudi seblen na kisha 'akajikata" na ujumbe wake.
15. MH. MTEI Akimbilia Ofisini na Kuandika Barua ya Kujiuzulu
Mh. MTEI alikuwa amekasirishwa mno, hivyo akatoka nduki na gari yake hadi Wizarani. Alipofika tu huku akitweta, akaandika kwa mkono barua ya kujiuzulu na kuiweka juu ya meza ili J3, Katibu Muhtasi akija aichape.
16. Mh. MTEI AMPA "UBUYU" Mh. MALECELA
Mh. MTEI, baada ya kuandika barua hiyo, aliamua kuwasiliana na Waziri wa Kilimo, Mh. JOHN MALECELA, juu ya dhamira yake hiyo ambapo Mh. MALECELA alistuka sana!. Mh. MALECELA akamweleza kuwa mmiliki wa Tanganyika Plantation Company anataka kuiuzia Govt kiwanda hicho kwa bei ya ubwete ila alipwe fasta.
Mh. MTEI alimjibu Mh. MALECELA kuwa jambo hilo haliwezekani kwani nchi imefulia vibaya sana na kwamba aliishaliongelea hilo na Gavana CHARLES NYIRABU kiisha wakaagana, kila mmoja "akasepa" kivyake.
Baadae kidogo, Mh. MTEI alipigiwa simu na Mh. MALECELA kwamba wote 2 wanaitwa na Mwalimu Msasani hivyo wakaenda.
Mh. MALECELA alitaka kiwanda hicho kinunuliwe akiungwa mkono na Mwalimu, huku MTEI akisisitiza kuwa nchi haina mbumba za kigeni.
Kikao kilipoisha, hasira ya Mh. MTEI ilikuwa ipo juu mno hivyo akakimbiza gari kwenda ofisini kwake kwa mwendo ambao hata Michael Schumacher angesubiri! Akaichukua ile barua aliyoandika kwa mkono akatoka nayo ofisini.
17. Mwalimu Amtumbua Mh. MTEI:
Mh. MTEI, alipomaliza tu kushuka ngazi za Wizara ya fedha, akakutana na Bw. BATHAO ambaye alikuwa msaidizi wa Mwalimu ambaye alimkabidhi barua toka kwa Mwalimu. Mh. MTEI, bila kuisoma, akaichukua na kuiweka ndani ya gari kisha akasaini Dispatch book na kuelekea Msasani.
18. Mh. MTEI Ajiuzulu, Mwalimu Amkubalia:
Mh. MTEI alimkabidhi Mwalimu barua ya kujiuzulu na Mwalimu akaisoma kwa makini na utulivu kisha akamuuliza kama alikuwa ameisoma barua yake. Mh. MTEI alikiri aliipokea lakini hakuisoma kutokana na uharaka wa kwenda kumuona. Mwalimu akamkubalia Mh. MTEI kujiuzulu.
19. Mwalimu Amwagiza Bw. SOZIGWA Kuutangazia Umma
Mwalimu alimuagiza Bw. PAUL SOZIGWA, Katibu wake, kuwa amekubali kujiuzulu kwa Mh. MTEI hivyo umma utaarifiwe hivyo.
Mwalimu na Mh. MTEI wakaagana vizuri kwa kukumbatiana.
Bw. SOZIGWA akaandika barua fupi kisha akaipeleka Shihata, Upanga na umma ukatangaziwa.
Bendi ya Kimulimuli ya Mafinga ikatunga wimbo wa kumpongeza Mwalimu - Tumekataa kuyumbishwa na Mataifa Makubwa.
Baada ya wiki kadhaa Mwalimu akatangaza miezi 18 ya kujifunga mikanda.
20. Mh. MTEI Auza nyumba, Aenda Kuishi Tengeru;
Baada ya kujiuzulu, Mh. MTEI aliona "togwa limeingia nzi hapa mjini" hivyo akauza jumba lake na kununua shamba kubwa Tengeru, nje kidogo ya Arusha na kuhamia huko.
21. Mwalimu Ampa Ulaji Mh. MTEI "Mamtoni"
Miaka 3 baada ya kujiuzulu, Mwalimu alimteua Mh. MTEI kuwa "Executive Director" wa IMF Africa, US, akiziwakilisha nchi za Afrika zinazotwanga un'gen'ge. Mh. MTEI, naada ya kuifanya kazi hiyo kwa welefi akizunguka dunia nzima, hatimaye akarejea nchini mwishoni mwa 1986.
22. Rais MWINYI Amteua MSUYA Waziri wa Fedha
Rais ALI HASSAN MWINYI aliyechukua uongozi baada ya Mwalimu, mwaka 1986 alimteua Mh. CLEOPA DAVID MSUYA kuwa Waziri wa Fedha na akaruhusu soko huria na kulegeza masharti mengi ya biashara.
23. Mh. MSUYA Aenda Mamtoni Apewa Masharti ya IMF:
Mh. MSUYA "alitia timu" Washington kujadiliana na IMF na kukubaliana na masharti yao kisha akarejea nchini. Kisha tarehe 10.6.1986, Mh. MSUYA aliongoza ujumbe mzito wa mkutano wa siku 2 Paris akiwa pamoja na Mh. PAUL BOMANI, Waziri wa Kilimo, Gavana CHARLES NYIRABU na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Mh. GILMAN RUTIHINDA.
24. Mh. MWINYI Aitisha "Cabinet" Kujadili Masharti ya IMF:
Mh. MWINYI aliitisha kikao cha Baraza la Mawaziri kujadili masharti ya IMF. Katika kikao hicho, Mh. MSUYA alieleza makubaliano yake na IMF na Baraza likaafiki kwa kauli moja na kumuelekeza Mh. MSUYA akaandae bajeti itakayoendana na makubaliano hayo.
25. Mh. MWINYI Akosa Usingizi, "Amtwangia" simu Mh. MSUYA:
Siku 3 baadae "machale yakamcheza" Mh. MWINYI hivyo akampigia simu Mh. MSUYA na kumueleza; "Sijapata usingizi kabisa toka juzi kutokana na haya makubaliano uliyokuja nayo, je tunaweza kukutana tena tukayajadili upya katika Baraza la Mawaziri?"
26. Mh. MSUYA Amchimba Mkwara Mh. MWINYI kuwa Atajiuzulu kama Mh. MTEI:
Mh. MSUYA alikubaliana na Rais MWINYI na hivyo siku moja kabla Bajeti kusomwa, 18.6.1986, Rais MWINYI aliitisha "Cabinet meeting".
Mh. MSUYA, bila kupepesa macho, kutikisa pua wala maskio, akatiririka "Mh. Rais, kama kuna hata mmoja katika Baraza hili la Mawaziri ambaye hatakubaliana na bajeti hii niliyoiandaa kutokana na masharti tuliyokubaliana na IMF, basi NITAJIUZULU ili uteue Waziri mwingine wa Fedha unaemtaka".
Rais MWINYI alieleza kwamba Mawaziri wote waongee kwa ukweli toka mioyoni mwao na kila mmoja aseme kama anakubaliana na masharti hayo.
Kila Waziri alieleza msimamo wake ambapo Mawaziri wengi walikubaliana na masharti hayo isipokuwa wachache akiwemo Waziri wa viwanda kwani wakati huo kulikuwa na "songombingo la kufa mtu" la maandamano nchini Jamaika na Moroko kupinga masharti ya IMF hivyo kuhofia yangefika Bongo. Mh. MWINYI "alimpiga shule" Waziri huyo kuwa viwanda vichache vilivyosalia vilikuwa vikifanya kazi kwa 25% tu na hivyo vilikuwa hatarini kufungwa. Hivyo, Baraza la Mawaziri likapitisha kwa mara nyingine masharti hayo. Kesho yake, alhamis, tarehe 19.6.1986, bajeti ikasomwa.
Tarehe 25.6.1986 wakati wa kujibu maswali ya wabunge waliohoji kuhusu kubadili msimamo wa Mwalimu kuhusu IMF, Mh. MSUYA, kwa weledi wa hali ya juu, alidadavua : "Hatuna adui wa kudumu bali tuna maslahi ya kudumu ya Watanzania. Tumewahi kuvunja uhusiano na nchi moja na baadae tukarejesha".
Hatimaye, thamani ya shilingi ikapunguzwa toka $1= TZS 17/= hadi $ 1= TZS 40/= (25%).
27. Prof. MBILINYI Aeleza Mwalimu Hakuambilika kuhusu IMF:
Prof. SIMON MBILINYI, aliyekuwa mshauri wa Mwalimu ameeleza kuwa ilikuwa vigumu kumbadili Mwalimu kuhusu msimamo wa kushusha thamani ya shilingi kwakuwa alikuwa hakubaliani kabisa na IMF & WB. Prof. MBILINYI anaeleza - "Bosi alikuwa akitaka ushauri kutoka kwetu, lakini ukitoa ushauri unaoendana na WB au IMF atakujibu "toka hapa"!
28. Prof. MBILINYI Aelezea Tofauti ya Mwalimu na MWINYI Kuhusu IMF
Prof. MBILINYI aliyekuwa pia mshauri wa Mh. MWINYI ameeleza: "Ilikuwa vigumu kumshauri Mwalimu kwakuwa alikuwa na msimamo thabiti kuhusu IMF, lakini ilikuwa kazi nyepesi kidogo kwa Rais MWINYI. Rais MWINYI alikuwa na fikra huria, ilikuwa rahisi kwetu kubuni sera kwani alikuwa huru kuchanganya kanuni za Kijamaa na Kibepari ili mradi nchi isonge mbele".
29. Rais MWINYI Ampa Mh. MTEI Ulaji:
Rais MWINYI, kwa kutambua uwezo mkubwa alionao Mh. MTEI, alimteua kwenye "Boards & Commissions" nyingi ambako alitoa mchango mkubwa.
30. Mh. MTEI Aaanzisha CHADEMA, 1992
Mh. MTEI, mwezi Julai 1992, alianzisha CHADEMA, chama kikuu cha upinzani nchini ambapo alienda Butiama na kumuonesha Mwalimu Katiba ya chama hicho ambapo Mwalimu aliisifia.
Huyu ndiye "Kipanga" EDWIN MTEI, mzalendo aliyetoa mchango mkubwa kwa taifa lake.
Tafakuri Tunduizi:
Je, Mh. MTEI alikosea kuhusu masharti ya IMF mwaka 1979?