Quantcast
Channel: MICHUZI BLOG
Viewing all 110167 articles
Browse latest View live

Amber Rutty amwaga chozi Mahakamani baada ya mumewe kuanguka

$
0
0
Na Karama Kenyunko,  globu ya jamii. 

Mnogeshaji wa video mbalimbali za wasanii (Video Queen) Rutyfiya Abubakary maarufu  'Amber Rutty’ amejikuta akiangua kulio katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya mume wake, Said Mtopali, kuanguka nje ya kizimba cha Mahakama Kufuatia kesi yao ya kufanya mapenzi kinyume na maumbile  kuahirishwa. 

Kabla ya kutokea kwa tukio hilo upande wa mashtaka ukiongozwa na wakili wa serikali Neema Bwana ulidai mbele ya Hakimu Mkazi Janet Mbando kuwa,  kesi hiyo leo January 10.2019 imekuja kwa kutajwa na upelelezi bado  haujakamilika.

 Mshitakiwa mwengine katika kesi hiyo ni James Charles maarufu kama James Delicious ambaye anakabiliwa na mashitaka ya kuchapisha video au picha za ngono  na kuzisambaza katika makundi ya mtandao wa kijamii wa WhatsApp.

Kufuatia taarifa hiyo, Hakimu Mmbando ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 11, 2019  na washitakiwa wote wako nje kwa dhamana.

Maro baada ya kesi hiyo kuahirishwa, mshtakiwa Mtopali wakati akitoka nje ya mahakama kuanguka ghafla na kumelelwa taharuki kwa ndugu zake ambao walimnyanyua kwa haraka na kumkimbiza Hospitali kwa uchunguzi zaidi. 

Katika kesi hiyo, Amber Rutty
anadaiwa kati ya Octobar 25, mwaka huu, jijini Dar es Salaam aliimruhusu Said Mtopali kumuingilia kinyume na maumbile jambo ambalo ni kinyume na sheria.

Pia inadaiwa kati ya Octobar 25, mwaka , maeneo ya jiji la Dar es Salaam, alifanya mapenzi kinyume na maumbile na mshitakiwa Mtopali.

WANAFUNZI VYUO VIKUU WAALIKWA KUJIFUNZA TEKNOLOJIA MPYA YA COMBINE CYCLE MITAMBO YA KUFUA UMEME WA GESI KINYEREZI II

$
0
0

NA K-VIS BLOG/Khalfan SaidMITAMBO ya kufua umeme wa gesi asilia kwenye kituo cha Kinyerezi II jijini Dar es Salaam imetumia teknolojia ya kisasa kabisa ijulikanayom kama combine cycle na kuwa nchi ya kwanza Afrika Mashariki kutumia teknolojia hiyo. 

Akifafanua kuhusu teknolojia hiyo, Meneja Miradi (uzalishaji) wa Shirika la Umeme Nchini TANESCO, Mhandisi Stephene S. A. Manda, amesema baada ya mitambo ya kufua umeme utokanao na gesi, mvuke unaozalishwa kwa awamu ya kwanza kutokana na joto hupelekwa tena kwenye mtambo mwingine na huko unazalisha umeme wa awamu ya pili. 

Alisema, tayari TANESCO imepokea maombi kutoka nchi mbalimbali zikiwemo zile za SADC kuja kujifunza teknolojia hiyo, ambapo katika mitambo nane ya kufua umeme iliyoko Kinyerezi II, miwili ni ile itokanayo na mvuke (steam turbines) “Tulivyokuwa na mkutano wa SAPP kule Arusha yaani Southern Africa Power Pool nchi mbalimbali zimeonyesha nia ya kuja kujifunza teknolojia hii.” Alisema. Mhandisi Manda ametoa wito kwa vyuo mbalimbali vinavyotoa taaluma ya uhandisi wa umeme kupeleka wanafunzi ili wajifunze teknolojia hiyo ya kisasa. “Wanafunzi wanao….Practice engineering wako kwenye field ambao hawajaona teknolojia inavyofanya kazi waje wajifunze.” Alisema.

Moja ya mitambo ya kufua umeme utokanao na mvuke (steam turbine) kwenye kituo cha kufua umeme wa gesi asilia Kinyerezi II jijini Dar es Salaam.

Meneja Miradi (uzalishaji) wa Shirika la Umeme Nchini TANESCO, Mhandisi Stephene S. A. (kulia) na Meneja wa kituo cha kufua umeme wa gesi cha Kinyerezi II, Mhandisi Ambakisye Mbangula, (katikati), wakimsikiliza mhandisi huyu kutoka nje anayehudumu kwenye mitambo hiyo wakati huu wa kumalizia ujenzi.

Mhandisi Manda akifafanua kuhusu mitambo ya kisasa iliyofungwa kwenye kituo hicho.

Mhandisi Manda akizungumza na wafanyakazi wa TANESCO kwenye chumba cha udhibiti mwenendo wa mitambo ya umeme (control room) Kinyerezi II.

NAIBU WAZIRI KANYASU AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA UINGEREZA NCHINI TANZANIA

$
0
0
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu (kulia) akizungumza na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Sarah Cooke  (katikati) mapema leo akiwa  na ujumbe wake,  wakati alipomtembelea ofisini kwake Mpingo House  jijini Dar es Salaam.
Balozi wa Uingereza nchini Tanzania,Sarah Cooke  (katikati) akizungumza na  Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu(kulia) kuhusiana  na mikakati mbalimbali ya kukabailiana na tatizo la ujangili wa tembo nchini mapema leo  ofisini kwake Mpingo House  jijini Dar es Salaam
 Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Sarah Cooke (kulia) akizungumza na  Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu(katikati)   mapema leo mara baada  ya kufanya  mazungumzo ofisini kwake Mpingo House  jijini Dar es Salaam
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu(katikati)  akizungumza na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Sarah Cooke (kulia) kabla ya kuagana naye wakati alipotembelewa ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
(PICHA ZOTE NA LUSUNGU HELELA-MNRT)

NAIBU WAZIRI TAMISEMI ATANGAZA KIAMA KWA SHULE BINAFSI NCHINI

$
0
0
*Shule ambazo hazifuati waraka wa elimu nazo kuchukuliwa hatua
*Azungumzia ada kubwa kwa shule binafsi, aapa kutafuta suluhu
*Wanafunzi wanaojiunga kidato cha kwanza wapewa siku 90...

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

SERIKALI imetangaza kuchukua hatua kali kwa mujibu wa sheria kwa shule zote binafsi ambazo hazifuati waraka wa elimu nchini huku ikitangaza kufanya msako kubaini wote wanaokiuka waraka huo. Pia Serikali imetoa onyo kwa shule zote binafsi ambazo zina tabia ya kupandisha ada kiholela, kukaririsha madarasa wanafunzi kinyume na waraka uliopo pamoja na michango mikubwa inayotoza bila kufuata utaratibu.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Mwita Waitara amesema, hiki ni kipindi cha elimu na kuna mambo lazima yawekwe sawa kwa wazazi, walezi, wadau wa elimu na shule kufahamu nini ambacho kinatakiwa kufuatwa. hayo ameyafafanua juzi alipokuwa kwenye kipindi katika kituo cha televisheni cha Taifa (TBC) ambapo alitoa namba yake ya simu ambayo ni 0767221344 na kusema kuwa kupitia namba hiyo amepokea meseji nyingi za wazazi ambazo nyingi ni za malalamiko na hasa kwa shule binafsi ambazo zimekuwa zikifanya unyanyasaji wa hali ya juu kwa wanafunzi, wazazi au walezi.

Waitara ameeleza kuwa TAMISEMI ndio inayosimamia elimu ya msingi na sekondari na ametumia nafasi hiyo kuzungumzia umuhimu wa ushirikiano kwa pande zote akiwa na maana upande wa wazazi na shule husika katika kupanga na kukubaliana mambo mbalimbali yakiwamo ya ada. Pia amesema wakati wanashughulikia changamoto zilizopo, Serikali imetoa siku 90 kwa kila mtoto anayetakiwa kuanza kidato cha kwanza kuripoti ndani ya muda huo na iwapo hatafanya hivyo hatua zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria, na amewatoa hofu wazazi kuwa watoto wote ambao wanatakiwa kuanza kidato cha kwanza ndani ya muda huo wa siku tisini watakuwa shuleni na kuchelewa kuanza masomo hakutakuwa sababu ya kumfanya mwanafunzi kufanya vibaya kwenye masomo yake.

VIPI KUHUSU ADA?

Waitara amesema moja ya malalamiko ambayo ameyapokea ni ada kupandishwa kiholela kwa baadhi ya shule binafsi jambo ambalo amesema ni marufuku shule kupandisha ada kiholela bila kumshirikisha mzazi. "Tunafahamu hakuna muongozo rasmi wa ada kwa shule binafsi , hivyo ipo haja ya kuuibua upya mjadala huu ili tuwe na ada ambayo itakuwa inaeleweka. Kuna shule binafsi ambazo zipo zinazotoza ada kuanzia Sh.milioni 1.5 hadi Sh.milioni sita na hapa ndipo yanapoanza maswali unapoona mwanafunzi anayelipiwa ada hizo anaomba mkopo akiwa Chuo Kikuu.Tunajua huenda kukawa na sababu nyingi lakini nachotaka kusema lazima hili la ada tulizungumze upya na kupata muafaka. Ada ni kubwa sana."amesema Waitara.

Hata hivyo amesema ada ambayo inalipwa ni makubaliano kati ya mzazi na shule lakini ni jambo la ajabu mzazi anapoambiwa ada imepanda bila kushirikishwa, hivyo ameagiza shule zote ambazo zimepandisha ada kiholela ni marufuku kumlipisha mzazi na hivyo ada ambayo anatakiwa kulipa ni ile ambayo walikubaliana na si hiyo iliyopandishwa bila utaratibu wa kushirikisha wazazi au walezi husika.

Amewataka wote wenye malalamiko kuhusu ada kupandishwa kiholela waende kwa maofisa elimu wa wilaya au kwa mkurugenzi ili hatua zichukuliwe kwa shule husika ili kukomesha tabia hiyo."Ni marufuku kumrudisha mwanafunzi nyumbani kwa sababu ya ada, aachwe asome, kama mzazi amelipa ada ya mtoto kwa miaka mitatu au minne kwanini ufukuze mwanafunzi kwa mzazi wake kushindwa kuleta ada. Mwanafunzi aachwe asome wakati mnajadiliana namna ya kulipana hiyo ada."amesisitiza Waitara.

AWEKA WAZI KUHUSU WASTANI
Pamoja na mambo mengine Waitara amezungumzia wastani wa alama za ufaulu kwa wanafunzi wa shule za msingi na shule za sekondari ambapo amefafanua tayari Serikali ilishatoa muongozo na huo ndio unatakiwa kufuatwa kwa shule zote nchini na si vinginevyo.

"Serikali ndio yenye kupima uwezo wa wanafunzi na hivyo kama kuna sababu za mtoto kubakia kwenye darasa kwasababu yoyote ile lazima kuwe na makubaliano ya kimaandishi ambayo ndiyo yatatumika kama kilelezo cha kwanini mwanafunzi amekakariri dasara.

"Kuna shule binafsi ambazo zimeweka wastani wake na wamekuwa wakiutumia huo kuwafanya wanafunzi wasiendelee na darasa linalofuata. Hilo ni kosa kwasababu mwenye kutoa muongozo wa kupima ufaulu ni Serikali tu, hakuna mtu au shule yoyote ambayo inaweza kwenda tofauti.Tutafuatilia shule zote na iwapo tubabaini wamekiuka utaratibu tutachukua hatua za kisheria na ikiwezekana tutafuta usajili wa shule husika." amesema Waitara.

Amesema kuna taarifa anazo kuna baadhi ya shule ambazo zimewarudisha wanafunzi kwasababu ya wastani ambao wameweka kwenye shule zao, hivyo ametoa maagizo wanafunzi hao waachwe waendelee na masomo na warudishwe shuleni kwa kuwa upimaji wa ufaulu kwa elimu ya msingi unafanyika darasa la nne na kwa sekondari inafanyika kidato cha pili, wanafunzi ambao wamefaulu waachwe wasome na hili agizo ni kwa shule zote zikiwemo hizo na binafsi.

Amesema anazo meseji kwenye simu yake ambazo zinazungumzia wanafunzi kurudishwa kwasababu ya kushindwa kufikia alama zilizowekwa."Shule ambazo zinashindwa kufuata muongozo baadhi tunazo na nimetoa maagizo zifuatiliwe ili tuchukue hatua,"amesema Waitara huku akitaja baadhi ya shule(majina tunayo) ambayo amedai yanakiuka utaratibu uliopo.

AONYA SHULE ZINAZOBADILISHA WANAFUNZI DINI
Wakati huohuo Waitara ametoa onyo kwa shule ambazo zimekuwa na tabia ya kubadilisha imani za watoto kwa kigezo cha kuwa sifa ya kujiunga na shule hizo ambapo amesema ni marufuku kama shule inamilikiwa na Wakistro basi Waislamu waachwe wasome na hivyo hivyo kama inamilikiwa na Waislamu, basi Wakristo wasome.

""Hatutaki kusikia mtoto amebadili imani yake ya dini au dhehebu lake kwasababu ya masharti ya shule. Serikali ndio inayotoa muongozo kuhusu elimu nchini, hivyo ni marufuku, wanafunzi waachwe wasome bila kusumbuliwa,"amefafanua Waitara.

MKUTANO WA SABA WA BARAZA LA WAFANYAKAZI LA TFS WAFANYIKA KWA SIKU MBILI AICC, JIJINI ARUSHA

$
0
0
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Prof. Dos Santos Silayo ambaye ndiye mwenyekiti wa Baraza la Saba la Wafanyakazi TFS akijadiliana jambo na katibu wa baraza hilo Ibrahim Mwanga muda mfupi baada ya kufungua kikao hicho cha siku mbili (Januari 10 - 11, 2019) katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha mapema hivi leo. Hata hivyo mwenyekiti huyo aliwaeleza wajumbe kuwa kikao hicho kitafunguliwa rasmi kesho na mgeni rasmi wa mkutano huo Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Prof. Adolf Mkenda baada ya kupatwa na dharula leo.
Baadhi ya wajumbe wa mkutano huo wakiwa wameshikana mikono huku wakiimba wimbo wa kuhamasisha mshikamano miongoni mwa wafanyakazi kama sehemu ya ufunguzi wa kikao hicho.
...baadhi ya wajumbe wakisikiliza mada ya uanzishwaji wa Chama cha Kuweka na Kukopa cha Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS SACCOS) iliyotolewa na Mwakilishi wa Chama cha Ushirika kutoka Wilaya ya Temeke, Dorina Mwanri (hayupo pichani) ambapo aliwataka viongozi wa muda walioteuliwa kuhakikisha wanazunguka kutoa elimu ya kutosha kwa wafanyakazai ili waweze kujiunga na chama hicho. TFS SACCOS imeanzishwa Disemba 2018.
Baadhi ya Wajumbe wa Mkutano wa Saba wa Baraza la Wafanyakazi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania wakijadiliana jambo kutoka kwenye bango kitita la mkutano huo.
Wajumbe wakifuatilia mkutano huo




Benki ya CRDB yakabidhi Milioni 20 katika Hospitali ya Sekou Toure Jijini Mwanza

$
0
0
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG

Benki ya CRDB imekabidhi hundi ya shilingi Milioni 20 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwanza, Sekou Toure ili kusaidia ukarabati na ununuzi wa vifaa tiba katika wodi ya upasuaji (Theatre) ya akina mama katika Hospitali hiyo.


Akizungumza kwenye hafla fupi ya kukabidhi hundi hiyo, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya CRDB, Dkt. Joseph Witts alisema benki hiyo ni mdau mkubwa katika kuboresha huduma za afya hapa nchini ambapo imekuwa ikitoa asilimia moja ya faida yake kwa ajili ya kuwasaidia wananchi.


Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwanza, Dkt. Bahati Msaki aliishukru Benki ya CRDB kwa mchango huo na kwamba utasaidia kuondoa changamoto ya utoaji huduma za afya kwa akina mama.


Mbali na hundi hiyo, pia Benki ya CRDB ilikabidhi luninga (TV) tatu za kisasa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa, Bugando  ili kutoa huduma kwa wananchi na wagonjwa wanaofika katika hospitali hiyo.

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya CRDB, Dkt. Joseph Witts akizungumza kwenye hafla hilo.
Baadhi ya watumishi wa Benki ya CRDB.
Mkuu wa Mkoa Mwanza, John Mongella akipokea hundi ya shilingi Milioni 20 kutoka Benki ya CRDB. Makabidhiano hayo yameshuhudiwa na Katibu Tawala mkoani Mwanza, Dkt. Christopher Kadio, Mwenyekiti wa Bodi Hospitali ya Sekour Toure, Christopher Gachuma, Mganga Mkuu Hospitali hiyo, Dkt. Thomas Rotachunzibwa pamoja na watumishi wa Hospitali hiyo.

BILIONEA WA DUNIA ABWAGANA NA MKEWE

$
0
0
Na Leandra Gabriel, Blogu ya jamii
JEFF Bezos (54) ambaye anashikilia nafasi ya kwanza akiwa mtu mwenye utajiri zaidi duniani akimiliki utajiri wa dola za kimarekani zaidi ya Bilioni 136.2 akimzidi Bill gates kwa dola za kimarekani Bilioni 45 ametangaza kuachana na mkewe MacKenzie Benzos (48) waliyedumu kwa miaka 25 ya ndoa.

Kupitia ukurasa kwake wa Twitter Jeff ameandika kuwa "Baada ya muda mrefu katika mapenzi na kujaribu kuachana  tumeamua kutengana na tutaendelea kuishi kama marafiki" Ameandika Bezos.

Licha ya kutangaza uamuzi huo sababu za kutengana kwao hawajaziweka wazi na inasemekana kuwa talaka hiyo itakuwa ghali zaidi kuwahi kutokea.

Wawili hao walioana mwaka 1993 na kujaliwa watoto wanne huku  MacKenzie akiwa mwandishi huku wakiwa wamiliki wa Amazon.com, kampuni za anga za juu ya Blue Orgin na jarida la biashara la Bloomberg na Washington post.

Jeff alimpiku Gate na kuwa mtu tajiri zaidi duniani mwaka 2017 akiwa na utajiri wa dola za kimarekani bilioni 90.6 na inasemekana Jeff anaweza kuporomoka katika nafasi hiyo kama atatoa nusu ya umiliki wa mali zake kwa MacKenzie.

NAIBU WAZIRI KANYASU ATEMBELEWA NA BALOZI WA UINGEREZA NCHINI TANZANIA

$
0
0

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu (kulia) akizungumza na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Sarah Cooke (katikati) mapema leo akiwa na ujumbe wake, wakati alipomtembelea ofisini kwake Mpingo House jijini Dar es Salaam
Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Sarah Cooke (kulia) akizungumza na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu(katikati) mapema leo mara baada ya kufanya mazungumzo ofisini kwake Mpingo House jijini Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu(katikati) akizungumza na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Sarah Cooke (kulia) kabla ya kuagana naye wakati alipotembelewa ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
Balozi wa Uingereza nchini Tanzania,Sarah Cooke (katikati) akizungumza na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu(kulia) kuhusiana na mikakati mbalimbali ya kukabailiana na tatizo la ujangili wa tembo nchini mapema leo ofisini kwake Mpingo House jijini Dar es Salaam.(PICHA ZOTE NA LUSUNGU HELELA-MNRT)

Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Sarah Cooke mapema leo Alhamisi Januari 10, 2019 amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu katika ofisi ndogo ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Mpingo House jijini Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine wamejadili namna ya kukabiliana na tatizo la ujangili wa tembo pamoja na mikakati ya kukuza utalii nchini. 

Maafisa Kilimo na ugani watakiwa kuwafuata wakulima mashambani kutoa elimu ya viwavi jeshi vamizi

$
0
0


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh.Joachim Wangabo (wa pili toka kulia) akiwa pamoja na mwenye shamba hili Alenx Ndenge (kulia) pamoja na wataalamu mbalimbali wakiangalia namna viwavijeshi vamizi wanavyoanza kushambulia mimea ya mahindi wilayani Nkasi.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh.Joachim Wangabo (wa pili toka kulia) akiwa pamoja na mwenye shamba hili Alenx Ndenge (kulia) pamoja na wataalamu mbalimbali wakiangalia namna viwavijeshi vamizi wanavyoanza kushambulia mimea ya mahindi wilayani Nkasi.



Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewaagiza maafisa ugani wote wa mkoani humo kuhakikisha wanawafikia wakulima kwenye mashamba yao na kuwapa elimu ya kukabiliana na wadudu aina ya viwavijeshi vamizi ambao wanaonekana kuanza kuleta athari katika wilaya ya Nkasi.

Amesema kuwa wakulima wengi hawana elimu ya kukabiliana na wadudu hao hasa kujua aina ya dawa ya kutumia ili kuwaua na wasiendelee kuharibu mazao na kuongeza kuwa ni wakati wao sasa maafisa ugani kufanya kazi ya kuwasaidia wananchi kupata matokeo bora ya mavuno kwa kutoa elimu ya kukabiliana na wadudu waharibifu na magonjwa.

“Kitu cha kufanya ni maafisa ugani wote na maafisa kilimo wote washuke kwenda kwenye mashamba, wakague na kutoa ushauri wa moja kwa moja, dawa zipo zinapatikana wanaanzia dawa gani inayofuata ni ipi, ili tuweze kuwasaidia wakulima waweze kuokoa haya mahindi, DC hawa watu wasimamiwe washuke asibaki mtu kwenye ofisi zao,” Alisisitiza.

Ameyasema hayo baada ya kuona athari ya viwavi jeshi alipotembelea shamba la mkulima wa mahindi Alex Ndenge katika ziara yake ya kuangalia maendeleo ya kilimo kwa wakulima na changamoto wanazokabiliana nazo ikiwemo upatikanaji wa pembejeo pamoja na mashambulizi ya wadudu na magonjwa ya mazao Wilayani Nkasi.

Kwa upande wake Afisa Kilimo wa Mkoa wa Rukwa Ocran Chengula alifafanua namna ya kupambana na wadudu hao na kutoa tahadhari kwa wakulima kuwa na tabia ya kupanda kwa kipindi kimoja na sio kupishana kwani hali hiyo hupelekea wadudu hao kuhama kutoka sehemu moja hadi nyingine ili kufuata mimea teke.

“Kuna sumu nyingine ukipiga inakuwa kwenye mmea, kwasababu huyu (mdudu) anatoa kinyesi kwahiyo ile sumu inaingia kwenye mmea kwahiyo anapokula anapata madhara anakufa, kwahiyo katika hatua za kwanza tunashauri (dawa aina ya) Duduba na hatua ya pili tunashauri dawa inaitwa “systemic” japo zina majina tofauti tofauti ni amjina ya kibiashara ila itumike hiyo baada ya kuona kwamba wameshaanza kutoa huu uchafu” Alieleza.

Kwa mujibu wa Afisa kilimo wa halmashauri ya wilaya ya Nkasi Emanuel Sekwao amesema kuwa viwavijeshi vamizi hao wameshaathiri kwa asilimia 2 mpaka 5 kutegemea eneo lakini bado haijafikia hatua ya wadudu hao kuharibu mimea kiasi cha kushindwa kuzaa.

Katika kipindi cha mwaka 2018/19 mkoa unalenga kulima jumla ya hekta 599,345.45 za mazao mbalimbali, kati ya hizo hekta 517,482.15 ni za mazao ya chakula na hekta 81,863.3 za mazao ya biashara. Kutokana na eneo hilo mkoa unategemea kuzalisha jumla ya tani 1,817,171.84 za mazao ya chakula na biashara. Katika kiasi hicho tani 1,680,701.6 ni za mazao ya chakula na tani 136,470.25 ni za mazao ya biashara.

Milioni 50m/-za Tigo Jigiftishe zaenda kwa mkulima Songea

$
0
0

Mkulima na mfanyabiashara wa nyanya katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma Sadick Zabron, amejishindia kitita cha shilingi milioni 50 baada ya kuibuka mshindi katika droo kubwa ya promosheni iliyomalizika ya Tigo Jigiftishe.

Zabron ndiyo mshindi wa zawadi kubwa katika Promosheni ya Jigiftishe. Washindi wengine katika droo kubwa ni Emma Kauka mkazi wa Dar es Salaam na Abdulrazak Abdallah mkazi wa Zanzibar alijishindia Sh 15m/-

Akizungumza katika hafla fupi ya kukabidhiwa zawadi iliyofanyika katika Soko Manzese mjini Songea, Zabroni alisema maisha yake yatabadilika kwa kiasi kikubwa kupitia fedha hizo.

“Sikuwahi kuwaza kumiliki kiasi kikubwa cha fedha kama hiki…, maisha yangu yatabadilika. Nitajenga nyumba nzuri na kuachana na kibanda cha nyasi nilichokuwa nikiishi na familia yangu. Naishuru Tigo kwa kubadilisha maisha yangu,” alisema

Mshindi huyo alisema atatumia fedha hizo pia kupanua shughuli zake za kilimo cha nyanya kwa kulima mashamba makubwa zaidi na kwa klimo cha kisasa na pia atatumia fedha hizo kuwaendeleza watoto wake kielimu.

Zabron alisema kushinda kwake kunatokana na kuingiza vocha za Tigo kwa ajili ya kufanya mawasiliano na wateja wake wa nyanya pamoja na kutuma au kutumiwa fedha mara kwa mara kupitia Tigo –Pesa.

Akiongea wakati akimkabidi zawadi kwa mshindi, Meneja wa Tigo kwa Kanda ya Kusini Abbas Abrahaman aliwataka wakazi wa maeneo Songea na jirani kuendelea kutumia mtandao wa Tigo ili kuweza kunufaika.

“Zipo faida nyingi za kutumia Tigo. Ni mtandao wa uhakika na gharama nafuu. Leo mmeshuhudia mwenzenu akiweza kujishindia Sh milioni 50m/-kwa kutumia tu mtandao wa Tigo na hii inaonyesha kuwa Tigo inawajaili wateja wake,”alisema

Mshindi wa zawadi kubwa ya shilingi milioni 50 katika Promosheni iliyomalizika ya Tigo Jigiftishe Sadick Zabron Kilipamwambu kutoka Songea, akionyesha nyumba anayoishi muda mfupi kabla ya kukabidhiwa zawadi yake mjini Songea. 
Mshindi wa zawadi kubwa ya shilingi milioni 50 katika Promosheni iliyomalizika ya Tigo Jigiftishe Sadick Zabron Kilipamwambu kutoka Songea, akimuonyesha Meneja wa Tigo Kanda ya Kusini Abbas Abrahaman (wa kwanza kushoto) na Oliver Baltazar ambaye ni mratibu wa biashara na masoko wakwa kanda ya Kusini shamba lake la nyanya.

Mshindi wa zawadi kubwa ya shilingi milioni 50 katika Promosheni iliyomalizika ya Tigo Jigiftishe Sadiki Zabroni Kilipamwambu, akiwa amebebwa na wafanyabiashara wenzake wa nyanya wakati akienda kupokea zawadi yake katika hafla ya kumkabidhi zawadi iliyofanyika katika soko la Manzese mjini Songea.
Mshindi wa zawadi kubwa ya shilingi milioni 50 katika Promosheni iliyomalizika ya Tigo Jigiftishe Sadick Zabron Kilipamwambu (wa tatu kushoto) akipokea mfano wa hundi kutoka kwa Meneja wa Tigo Kanda ya Kusini Abbas Abrahaman (wa pili kushoto). Wanaoshuhudia ni wafanyakazi wa Tigo na mshereheshaji wa shughuli hiyo Okechi Okechi.

Tanzania Kutoa Taarifa Kuu ya Malengo Endelevu 2030, Julai Mwaka Huu

$
0
0

Mwandishi Wetu-MAELEZO.

Tanzania inatarajia kutoa taarifa ya takwimu ya malengo endelevu ya dunia 2030 Julai mwaka huu, huku suala la elimu likipewa kipaumbele katika taarifa hiyo.

Akizungumza Jijini Dar es Salaam kwenye mkutano na wadau wa takwimu kutoka Sweden, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dkt Albina Chuwa amesema kuwa lengo kuu lililowakutanisha na wadau hao ni kutoa taarifa kuhusu taarifa kuu ya malengo endelevu ya dunia ya mwaka 2030.

“Huu mkutano lengo lake kuu ni kuwapa wananchi taarifa ya maendeleo ya utengenzaji wa kanzi data ya takwimu za kuripoti katika malengo endelevu ya dunia ya mwaka 2030 ambayo inatarajia kuwekwa hadharani Julai mwaka huu”, Alisema Dkt.Chuwa.

Dkt Chuwa alisema kuwa utengenezaji wa kanzi data hii umeanza muda mrafu kwa Ofisi ya Takwimu ikishirikiana na mtaalamu kutoka Sweden (Alexandra Silfverstolpe) ambaye anafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na Ofisi ya Takwimu nchini humo.

Ofisi ya Taifa ya Takwimu ilipata uzoefu wa kutengeneza kanzi data hii kutoka nchi mbalimbali duniani ikiwemo Colombia kwa kuwa kanzi data hizo zinaonyesha namna ya kutatua matatizo ili kutimiza malengo endelevu kwa taifa.

“Kanzi data hii inaonyesha viashiria kwenye malengo endelevu kwa mfano viashiria vya namna gani Tanzania itaondokana na umasikini ifikapo mwaka 2030, kwa hiyo ni rahisi kwa watu wanaotekeleza sera, wanasiasa na watawala wanaotoa maamuzi katika uchumi wa nchi kwani kanzi data hizi zitawasidia katika kazi zao”, Alisema Dkt. Chuwa.

Aidha aliongeza kuwa shabaha kubwa ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu ni kushirikisha wadau wa maendeleo katika kuweka Takwimu sawa kwa hiyo mkutano wa Ofisi ya takwimu na wadau wa Takwimu kutoka Sweden wamejadili pamoja hatua ya utengeneza kanzi data na kutoa kipaumbele malengo enedelevu ya mwaka 2030 katika sekta ya elimu.

“kwa sasa kazi hii imefikia kwenye hatua nzuri ya kuingiza data kutoka kwenye kanzi data kuziweka kwenye Taarifa kuu inayotarajia kutolewa Julai mwaka huu, kwa hiyo tutafanya kazi hii karibu sana na hawa wenzetu ili kutoa taarifa yenye kiwango cha kimataifa”, Alisistiza Dkt.Chuwa.

Akizungumzia marekebisho ya sheria ya takwimu, Mkurugenzi huyo wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu aliwatoa wasiwasi wananchi kuwa hakuna mtu yeyote atakayefungwa kwa kufuata taratibu za utoaji takwimu kwa kutumia data kamili kwani nchi zote duniani zinahitaji data zenye kufuata utaratibu.

WATOTO WACHANGA 475 WAFARIKI DUNIA MKOANI PWANI KUTOKANA NA UZAZI KATIKA KIPINDI CHA MWAKA 2018

$
0
0
NA MWAMVUA MWINYI, PWANI 
JUMLA ya watoto wachanga 475 wamefariki dunia baada ya akinamama 41,064 kujifungua mkoani Pwani, mwaka 2018 ,hali ambayo inaonyesha idadi ya vifo vitokanavyo na uzazi kimkoa bado ipo juu. 

Aidha kati ya akinamama hao 41,064 waliojifungua akinamama 67 walifariki dunia kutokana na uzazi. 

Hayo yalisemwa na mganga mkuu wa mkoa wa Pwani, Dkt. Gunini Kamba wakati mkuu wa mkoa wa Pwani, mhandisi Evarist Ndikilo aliposaini hati ya makubaliano na wakuu wa wilaya ya kampeni ya kuzuia vifo vya uzazi, kampeni ambayo itafanyika kwa miezi 12 nchini. 

Alisema, vifo vya watoto wachanga na akinamama wanaojifungua hali hairidhishi hivyo kampeni hiyo itasaidia kupunguza idadi hiyo. Kamba alisema, lengo hilo linaweza kufikiwa endapo akinamama watafuata maelekezo ya kiafya wanayopatiwa wakati wa uzazi ili waweze kuvuka salama katika kipindi cha uzazi. 

"Vifo 67 kwa waliojifungua na watoto wachanga 475 ukilinganisha na malengo ya Kitaifa bado hali sio nzuri sana "alisisitiza Kamba. Pamoja na hayo Kamba aliwataka ,akinamama wajawazito kuhakikisha wanaanza klinik ndani ya miezi 12 ya kwanza ili kujua afya zao. 

Pia waendelee na kufuatilia afya zao kulingana na utaratibu watakaopatiwa hadi wakati wa kujifungua bila kupuuzia. "Na wakijifungua inapaswa kuhakikishwa ndani ya lisaa limoja baada ya kujifungua mtoto anyonye "alifafanua Kamba. 

Awali mkuu wa mkoa wa Pwani, Ndikilo aliwaasa wakuu wa wilaya kwenda kusimamia malengo hayo ili kufanikisha kampeni hiyo kiwilaya, mkoa na Taifa kijumla.

MWENYEKITI WA UMOJA WA MABENKI NCHINI NA MKURUGENZI MTENDAJI WA BENKI YA CRDB AKUTANA NA WAKURUGENZI WA BENKI ZA TIB

$
0
0
Mwenyekiti wa Umoja wa Mabenki Tanzania na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela akimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya TIB, Charles Singili wakati wa mazungumzo yao yaliyofanyika leo jijini Dar es salaam. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya TIB Corporate, Frank Nyabundege.
 Mwenyekiti wa Umoja wa Mabenki Tanzania na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela akiwa katika mazungumzo na wajumbe wa Umoja huo, Charles Singili (Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya TIB) na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya TIB Corporate, Frank Nyabundege (kulia) walipomtembelea ofisini kwake leo Januari 10, 2019. 
 Kikao kikiendelea.

RC MAKONDA AWAALIKA WANANCHI KUUNGANA NA RAIS MAGUFULI KUPOKEA NDEGE YA SITA YA SERIKALI AIRBUS A220-300

$
0
0
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam  Paul Makonda 

Na Leandra Gabriel, Blogu ya jamii
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam  Paul Makonda amewaalika Wananchi  Wapenda maendeleo kuungana na Rais Dkt. John Magufuli kwenye mapokezi ya Ndege ya Sita ya Serikali  aina ya Airbus A220-300 itakayowasili Nchini Kesho January 11 Saa sita Mchana ikitokea Nchini Canada. 

Hafla ya mapokezi ya ndege hiyo itafanyika kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwl. Julius Nyerere jijini Dar es salaam.

Makonda amesema kuwa anatumaini wananchi wengi watajitokeza katika kuunga mkono jitihada za Mh. Rais ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kuleta maendeleo.

Rais Magufuli aliahidi na sasa anatekeleza.

WADAU WAKUTANA TABORA KUANDAA JUMBE ZA KUTOKOMEZA UKATILI WA WANAWAKE NA WATOTO

$
0
0
WANANCHI wametakiwa kuunganisha nguvu pamoja kuhakikisha wanatokemeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto na mimba za utotoni hapa nchini kama ilivyoekelezwa katika Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokemeza Ukatili wa wanawake na watoto(MTAKUWWA). Tatizo hilo linasababisha athari nyingi ikiwemo vifo, ulemavu , kuwa na kundi kubwa la watoto kukimbilia mitaani na umaskini kwa watoto wanaokatishwa masomo na ndoto zao la baadae na hivyo kudhofisha juhudi za ujenzi wa uchumi wa kati na viwanda hapa nchini.

Kauli hiyo imetolewa  na Katibu Tawala Mkoa wa Tabora Msalika Makungu katika hotuba yake iliyosomwa na Katibu Tawala Msaidizi Raphael Nyanda kwenye ufunguzi wa mafunzo ya kuandaa ujumbe wa kupinga ukatili dhidi ya wananwake na watoto na mimba za utotoni. Alisema suala hilo ni kubwa katika baadhi ya jamii na hivyo linahitaji kila mwanajamii kuwa mstari wa mbele kukemea na kutoa taarifa ambazo zitasaidia kukomesha ukatili kwa watoto , wanawake na kuondoa ndoa na mimba za utotoni hapa nchini na wahusika kufikishwa katika vyombo vya sheria.

 Nyanda alisema kuwa wakati mwingine vitendo vya ukatili vimekuwa vikifanyika katika jamii huku  wanajamii wanakaa kimya wakiwemo baadhi ya viongozi wa maeneo husika wakiwa wamefumba macho. Alisema ni lazima jamii itambue kuwa ukatili unafanyika kwa mtoto wa jirani kesho unaweza kufanyikwa kwa watoto wao na hivyo wanapaswa kuchukua hatua wanapoona vitendo vya namna hiyo vikifanyika.

 Awali Mkurugenzi Msaidizi kutoka Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii ya Wizara ya Afya , Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Grace Mwangwa alisema mikoa ambayo ina vitendo vya juu vya ukatili wa wanawake na watoto ndio hiyo hiyo ipo juu katika tatizo la mimba na ndoa za utotoni. Aliitaja mikoa inayoongoza kwa mimba za utotoni kuwa ni Katavi kwa  asilimia 45, Tabora asilimia 43, Morogoro 39 na  Mara asilimia 39 na kwa upande wanajifungua kwa umri mdogo  ni Shinyanga kwa asilimia 59, Tabora 58, Mara 55, Dodoma 51 na Lindi 48.

 Mwangwa aliwaomba viongozi wa Dini hapa nchini kutumia ushwawishi wao wa kiroho kukemea ukatili wa wanawake na watoto kama vile upigaji wa wanawake na watoto, ukeketaji unaoendelea kwa siri katika baadhi ya maeneo, ndoa za utotoni na mimba za utotoni ambazo nyingine zinatokana na kubakwa.

 Aidha aliwataka wazazi au walezi wa watoto kuwa makini na kuwalaza watoto wao chumba kimoja na wageni kwa kuwa wakati unyanyasaji ikiwemo ubakaji na ulawiti unafanywa na watu hao ambao wamekaribishwa kama ndugu au marafiki. Alisema hatua hiyo inatokana na utafiti ambao umeonyesha asilimia 60 ya ukatili kwa watoto ufanyika nyumbani na 40 ndio unaofanywa katika maeneo ya Shule.

 Mkurugenzi Msaidizi huyo alisema ukatili kwa watoto ni pamoja na matusi, vipigo, kuchomwa moto wakifanya kosa, kunyimwa chakula, kubakwa, kulawitiwa na kuolewa katika umri mdogo. Aliitaka jamii kurudi katika mitazamo ya awali ambapo kila mtu mzima alimchukulia kila mtoto anayemuona mbele yake ni mwanae.
 Kaimu Katibu  Tawala Mkoa wa Tabora Raphael Nyanda (katikati) akifungua mafunzo ya kuandaa ujumbe wa kupinga ukatili dhidi ya wananwake na watoto na mimba za utotoni. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi kutoka Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii ya Wizara ya Afya , Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Grace Mwangwa na kushoto niAfisa aneyeshughulikia Maendeleo ya Jamii kutoka Ofisi ya Rais , Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mwajina Ally.
 Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya  kuandaa ujumbe wa kupinga ukatili dhidi ya wananwake na watoto na mimba za utotoni  wakiwa katika mafunzo hayo mjini Tabora.
Kaimu Katibu  Tawala Mkoa wa Tabora Raphael Nyanda(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na washiri wa  mafunzo ya kuandaa ujumbe wa kupinga ukatili dhidi ya wananwake na watoto na mimba za utotoni. Picha na Tiganya Vincent

Wanamuziki nyota wa Afrika kuwa kivutio kikubwa Tamasha la Sauti za Busara

$
0
0

Zanzibar na Afrika Mashariki wanajiandaa kufanya Tamasha la Sauti za Busara la mwaka 2019 likiwa na azma ya kuupeleka muziki wa kipekee wa Kiafrika unaopigwa mubashara (live) kwenda kwenye hatua nyingine kitaifa na kimataifa. 

Tamasha hilo linalofuatiliwa ulimwenguni kote linatarajiwa kuanza rasmi Februari 7, Old Fort likiwa na maonyesho ya kusisimua 46 kutoka kwa zaidi ya wasanii 400 katika majukwaa matatu tofauti kwa siku nne yaani mchana na usiku. 

Makundi mengi yatakuwa yanatumbuiza katika jukwaa hili la Sauti za Busara la aina yake kwa mara ya kwanza. 

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Tamasha la Busara, Yusuf Mahmoud, kuna mambo mengi ya kutazamiwa katika tamasha la mwaka huu. 

“Kwa miaka kadhaa sasa, watazamaji wamekuwa wakitarajia vitu vya kipekee na vipya kila wakati. Tunaamini orodha ya mwaka huu, pia ni bora kuwahi kutokea, kwani tunaendelea kuonyesha muziki halisia wa Kiafrika wenye utambulisho,” anasema Mahmoud. 

Wakati huo huo, Meneja wa Tamasha la Sauti za Busara, Journey Ramadhan anasema kutakuwa na mambo mapya na sauti mbalimbali za kuvutia kutoka Tanzania ikiwemo Wamwiduka Band na SKide, wasanii wa muziki aina ya “Singeli” ambao wataudhihirishia ulimwengu utajiri wa muziki huo wa kizazi kipya ambao asili yake ni Tanzania. 

“Ni imani yangu kuwa baada ya kuisha kwa burudani hizo katika Tamasha mambo hayatabaki kama yalivyokuwa, kama ambavyo historia imekuwa ikijirudia kwa makundi mengine yaliyowahi kutumbuiza katika tamasha la Sauti za Busara katika miaka iliyopita, makundi kama vile Sarabi, Jagwa Music, Tausi Women’s Taarab na mengine,” aliongeza Journey Ramadhan. 

Orodha ya wasanii watakaokuwepo katika tamasha la Sauti za Busara la mwaka 2019 ni pamoja na Mokoomba (Zimbabwe), Fid Q ( Tanzania), BCUC (Afrika Kusini), Afrigo Band (Uganda),Fadhilee Itulya (Kenya), Mkubwa na Wanawe Crew (Tanzania), SKide(Tanzania), Damian Soul (Tanzania),Jackie Akello (Uganda), Faith Mussa (Malawi), Asia Madani (Sudan/Misri), M’ToroChamou (Mayotte), HobaHoba Spirit (Morocco), Shamsi Music (Kenya), Sofaz (Reunion), Dago Roots (Reunion), Lydol (Cameroun), Stone Town Rockerz (Zanzibar), Ithrene (Algeria), Ifrikya Spirit (Algeria), Trio Kazanchis + 2 (Ethiopia/Switzerland), Rajab Suleiman & Kithara (Zanzibar) na wengine wengi. 

Tamasha la mwaka 2019 litakuwa ni jukwaa kwa wasanii na hadhira kutoka sehemu mbalimbali duniani kuungana kwa pamoja na kusema “hapana” dhidi ya vitendo vya rushwa, wakishinikiza viongozi kutoka katika kila sekta kutimiza majukumu yao ya kila siku pasi na mianya ya vitendo vya rushwa. 

Tamasha la Sauti za Busara linadhaminiwa na Ubalozi wa Norway, Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania na Zambia, Umoja wa Ulaya, Africalia, Ubalozi wa Ufaransa, Ubalozi wa Ujerumani, Pro Helvetia, Zanlink, Mozeti, Shirika la Ndege la Ethiopia, African Movie Channel, Zanzibar Media Corporation na wengine wengi. 

Taarifa Zaidi tembelea :www.busaramusic.org

Ujio wa ndege mpya AIRBUS A220-300 (NGORONGORO)kufika nchini kesho Ijumaa

KAMATI ZA USIMAMIZI WA MAAFA ZASHAURIWA KUWA NA MPANGO WA KUJIANDAA KUKABILIANA NA MAAFA.

$
0
0
Na OWM, SUMBAWANGA.

Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Uratibu wa Maafa, imezishauri Kamati za Usimamizi wa maafa nchini kuanzia ngazi ya kijiji hadi mkoa kuwa na mpango wa Kujiandaa na kukabili maafa ili kuwa na uwezo wa  utayari wa kujiandaa na kukabili maafa kwa ufanisi.

Akiongea wakati wa mafunzo kwa Kamati ya Usimamizi ya Maafa ya Mkoa wa Rukwa, juu ya Usimamizi wa Maafa kwa Mujibu wa Sheria ya Maafa Na. 7 ya mwaka 2015, Mkurugenzi Msaidizi (Utafiti na Mipango), Ofisi ya Waziri Mkuu, Bashir Taratibu, alifafanua kuwa Mpango huo ni muhimu kwa kuwa huainisha majukumu na hatua zitakazochukuliwa na Kamati za  maafa kuanzia  ngazi ya kijiji, wilaya na mkoa pamoja na wadau wengine wa maafa.

“Ili kuweza kukabiliana na maafa pindi yanapotokea na kuhakikisha kuwa wanazuia au kupunguza athari za maafa yanapotokea kwa ufanisi tumeishauri kamati ya Usimamizi wa maafa ya mkoa wa Rukwa katika bajeti ijayo watenge bajeti  kwa ajili ya maafa,  pia wabuni mbinu za upatikanaji wa rasilimali zinazohitajika katika usimamizi wa maafa,  hili linawezekana iwapo kamati zote nchini za Usimamizi wa maafa  katika ngazi zote zikiwa na Mpango wa kujiandaa na kukabili maafa” alisisitiza Taratibu

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi wa maafa ya  Mkoa wa Rukwa , Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa huo, Winnie Kijazi, aliihakikishia ofisi ya Waziri Mkuu kuwa mkoa huo umeamua kuandaa mpango huo kutokana na changamoto walizo zipata wakati wa maafa ya mvua yenye  upepo mkali uliotokea mwishoni mwa mwaka jana katika halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga na Nkasi.

“Tunaishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Uratibu wa Maafa kwa uratibu na misaada ya haraka pindi tulipopata maafa , na sisi tumeamua kuwa na ufanisi katika usimamizi wa maafa kwa kuandaa Mpango wa Kujiandaa na Kukabili maafa na tutaelekeza wilaya zote kuandaa mipango yao na  kutenga  bajeti kwa ajili ya utekelezaji huo” alifafanua Kijazi

Naye Mratibu wa maafa mkoani Rukwa Aziza Kalyatiilya alieleza kuwa, tayari wameandaa Mpango wa kutoa elimu ya  Maafa  kwa Umma  ili kuijengea jamii uwezo wa kujiandaa, kuzuia, au kukabili na kurejesha hali kwa haraka na ufanisi pindi maafa yatakapotokea mkoani humo.

Mnamo mwezi Desemba mwaka jana Halimashauri ya Wilaya ya Sumbawanga na Nkasi mkoani Rukwa zilipatwa na maafa ya mvua yenye upepo mkali iliyosabaisha vifo, uharibifu wa mali na Miundo mbinu. Aidha Kamati ya maafa kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri mkuu, Idara ya Uratibu Maafa, tayari shughuli za kurejesha hali zinaendelea.

Kwa mujibu wa sheria ya Usimamizi wa maafa Na. 7 ya mwaka 2015, inaainisha  majukumu ya  kamati za usimamizi wa Maafa kuanzia ngazi ya Kijiji hadi mkoa, ambapo kwa mujibu wa sheria hiyo, jukumu la msingi ni kutafuta rasilimali kwa ajili ya usimamizi wa maafa katika ngazi husika, pamoja na  Kuratibu na kusimamia shughuli za usimamizi wa maafa na operesheni za dharura ndani ya Kijiji  wilaya au mkoa. Pia kutoa taarifa za tahadhari ndani ya eneo husika.
 Mkurugenzi Msaidizi (Utafiti na Mipango), Ofisi ya Waziri Mkuu, Bashir Taratibu, akieleza umuhimu wa Kamati ya Usimamizi wa maafa ya mkoa wa Rukwa kuwa na Mpango wa Kujiandaa na kukabili maafa wakati wa Mafunzo ya Usimamizi kwa kamati hiyo mkoani Rukwa.
 Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Usimamizi wa maafa ya mkoa wa Rukwa wakiwa katika Mafunzo ya Usimamizi  wa maafa kwa mujibu wa Sheria Na. 7 ya mwaka 2015, wakati wa mafunzo kwa kamati hiyo mkoani Rukwa.
 Mratibu maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Charles Msangi, akieleza umuhimu wa Kamati ya Usimamizi wa maafa ya mkoa wa Rukwa kuzingatia  Mzingo wa Maafa, ambao ni Kuzuia maafa Kujiandaa na maafa, Kukabili maafa  na kurejesha hali, wakati wa mafunzo kwa kamati hiyo mkoani Rukwa.
 Kaimu Katibu Tawala mkoa wa Rukwa, Bi Winnie Kijazi, Mkurugenzi Msaidizi (Utafiti na Mipango), Ofisi ya Waziri Mkuu, Bashir Taratibu (katikati) na Mratibu wa Maafa  Manispaa ya Sumbawanga wakifuatilia majadiliano wakati wa Mafunzo ya Usimamizi  wa maafa kwa kamati  ya maafa mkoani Rukwa.
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Usimamizi wa maafa ya mkoa wa Rukwa wakiwa katika Mafunzo ya Usimamizi  wa maafa kwa mujibu wa Sheria Na. 7 ya mwaka 2015, wakati wa mafunzo kwa kamati hiyo mkoani Rukwa.

DKT.MARY MWANJELWA AVUTIWA NA MPANGO WA KUNUSURU KAYA MASKINI UNAOTEKELEZWA NA TASAF.

$
0
0

Na Estom Sanga-DSM

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ,Dr. Mary Mwanjelwa ameuagiza Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF kuendelea na Utaratibu bora zaidi wa kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ili Wananchi waweze kunufaika na Mpango huo ulioanzishwa na kutekelezwa na Serikali.

Dr. Mwanjelwa ametoa agizo hilo alipokutana na Menejimenti na Watumishi wa Mfuko huo akiwa katika ziara yake ya kikazi na kujitambulisha kufuatia uteuzi uliofanywa na Rais Dr. John Magufuli hivi karibuni ambapo Naibu Waziri huyo alihamishiwa katika Wizara hiyo.

Naibu Waziri huyo amesema pamoja na mafanikio makubwa ambayo Mfuko huo umeyapata katika kuhudumia takribani Kaya Milioni Moja na Laki Moja za Wananchi wanaoishi katika umaskini, haupaswi kubweteka kwani suala la kupambana na Umaskini ni agenda muhimu katika Mipango ya Serikali ambayo pia imeainishwa kupitia ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi.

Aidha Dr.Mwanjelwa ameagiza Watumishi wa TASAF kuwa Wabunifu na kufanya kazi kwa karibu zaidi na Wananchi hususani walioko katika Mpango ili Matokeo ya utekelezaji wa Shughuli za miradi yawe endelevu na yanayopimika ili hatimaye kero ya umaskini miongoni mwa Wananchi iweze kupunguzwa kama siyo kumalizika kabisa.

Akizungumzia utekelezaji wa shughuli za Miradi ya Ajira ya Muda, Naibu Waziri huyo wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ameagiza TASAF kuhakikisha kuwa miradi inayotekelezwa kupitia utaratibu huo ni ile inayowanufaisha wananchi na malipo yafanywe kwa kuzingatia kanuni na taratibu za Serikali.

Wakati huo huo Dr. Mwanjelwa ametoa rai kwa halmashauri za wilaya kusimamia kwa karibu miradi inayotekelezwa na TASAF kwenye maeneo yao na kuonya kuwa pale ambapo itadhihirika kuwa halmashauri inakiuka taratibu wa miradi hiyo hatua zitachukuliwa haraka iwezekanavyo dhidi ya wahusika .

Akitoa taarifa ya Utekelezaji wa Shughuli, Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF ,Bwana Ladislaus Mwamanga amesema Mfuko huo umeendelea kutekeleza Maagizo ya Serikali ya kusaidia jitihada za Serikali katika kupambana na Umaskini nchini kote .

Bwana Mwamanga amezitaja sekta za Elimu, Maji,Afya ,Barabara,hifadhi ya Mazingira, Mifugo, Kilimo na uzalishaji mali na ujenzi wa rasilimali watu kuwa miongoni mwa maeneo yaliyopewa kipaumbele tangu kuanzishwa kwa Mfuko huo takribani miaka 20 iliyopita miradi ambayo amesema imetekelezwa kwa mafanikio makubwa kwa kuwahusisha wananchi kwenye maeneo yao.

Mkurugenzi Mtendaji huyo wa TASAF amebainisha pia kuwa utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini licha ya changamoto kadhaa zilizotokana na ukubwa wa Mpango huo kumekuwa na mafanikio makubwa hususani katika kubadili fikra za Walengwa ambao kwa sasa wanaendelea kuboresha maisha yao kwa kutumia huduma za Mpango huo.Amesema maboresho muhimu yatafanywa kwa kuzingatia maelekezo ya Serikali ili katika sehemu ya pili ya Mpango inayotarajiwa kuanza hivi karibuni kuwa na ufanisi zaidi ikiwa ni pamoja na kuyafikia maeneo ambayo hayakupata fursa hiyo katika awamu ya kwanza.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Dr. Mary Mwanjelwa(aliyeshika kipaza sauti) akizungumza na Watumishi wa TASAF (hawapo pichani) kushoto kwake ni Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bwana Ladislaus Mwamanga.
Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF,Bw. Ladislaus Mwamanga (aliyesimama) akitoa taarifa kwa Naibu Waziri Dr. Mary Mwanjelwa wakati alipofanya ziara ya utambulisho kwa watumishi wa taasisi hiyo.
Picha ya Juu na Chini baadhi ya Watumishi wa TASAF wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Dr. Mary Mwanjelwa (hayupo pichani) ambaye alifanya ziara katika taasisi hiyo.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Dr. Mary Mwanjelwa (aliyeketi katikati ) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Watumishi wa TASAF alipofanya ziara ya kujitambulisha .

NDUGU WADAIWA KUSHIRIKI KUFICHA USHAHIDI VITENDO VYA UKATILI DHIDI YA WANAWAKE NA WATOTO-SHINYANGA

$
0
0
Na Anthony Ishengoma.

Matendo ya ukatili yaliyolipotiwakatika Jeshi la Polisi hapa Nchini yamefikia 13 elfu mpaka kufikia mwaka jana tofauti na matukio takribani elfu 10 yaliyolipotiwa katika jeshi hilo kwa takwimu za mwaka 2016-17.

Akiongea wakati wa ufunguzi wa kikao kazi kinachoendelea katika Manispaa ya Shinyanga kujadili jumbe mahususi zitakazotumika katika jitihada za serikali kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto mkoani Shinyanga Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Watoto kutoka Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Sebastian Kitiku amesema vitendo vya ukatili vinazidi kuongezeka mwaka hadi mwaka hapa Nchini.

 Kitiku amewaambia wajumbe wa kikao kazi hicho kuwa Wizara ya Afya inatengeneza jumbe mahususi za kutokomeza ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto na wadau wa Mkoa wa Shinyinga kwa kuwa mkoa wa Shinyanga ni moja ya mikoa inayoongoza katika kiwango kikubwa cha Mimba na Ndoa za utotoni hapa Nchini.

Wakati huohuo Mkurugenzi wa Utawala wa Mkoa wa Shinyanga Albert Msovela amewataka viongozi wa Mkoa na Almashauri, viongozi wa dini, vyombo vya ulinzi na usalama vya Mkoa huo  kuhakikisha wanafanya kazi kubwa kumaliza tatizo hilo kwa kuwa haamini kama tatizo hilo linatokana na mila za wakazi wa mkoa wa Shinyanga.

‘’Siamini kama vitendao hivi vinatoka na mila potofu bali ni mmomonyoko wa maadili kwa kuwa wazazi na walezi wameacha jukumu lao la kuwalea watoto kama inavyostahili bali wanafuata hali ya sasa ya utandawazi’’. Alisema Msovela.

Aidha Msovela alionya kuwa Serikali ya Mkoa wa Shinyanga haitaendelea kuvumilia vitendo hivyo kwa kuwa kwa matukio ya Mkoa huo unaweza ukajiuliza kama unahitaji huruma ya mweneyezi Mungu kwasababu kumekuweko mauaji ya vikongwe, Watu wenye Uaribino, vipigo kwa akina mama na sasa mimba na ndoa za utotoni.

Msovela ametaja takwimu za hali ya ukatili Mkoani humo kuwa ni kubwa kwa kuwa kwasasa mkoa unaonesha una kiasi cha 34% za mimba za utotoni na ndoa za utotoni  ni asilimia ni asilimia 59%na kuzitaka jamii mkoani humo kubadilika ili watoto wa kike wapate fursa ya kutimiza ndoto zao.

Aidha amewaambia wajumbe wa kikao hicho kuwa tatizo la mimba za mapema ni kubwa sana kwani kwa Wilaya ya Kishapu pekee kwa mwaka jana jumla ya watoto 57 wa shule walipata ujauzito.

Ameongeza kuwa kwasasa wazazi wamekuwa wakishirikiana na waalifu kuficha ushaidi baada yukupewa ng’ombe na hivyo kushindwa kutoa taarifa ili waanga wa ukatili waweze kupata haki baada ya kugwa wamefanyiwa vitendao vya ukatili.

‘’Hata ikitokea suala la ukatili limepelekwa mahakamani wanajamii husika wamekuwa hawajitokezi mahakamani kutoa ushahidi jambo ambalo linasababisha utokomezaji wa vitendo vya ukatili kuwa mugumu kwa kuwa mahakama inawaachia huru wahusika kwa kukosa ushaidi’’. Alilamika Kiongozi huyo wa Utawala Mkoani hapo Msovela.

Amemwagiza Afisa Elimu wa Mkoa wa Shinyanga kuhakikisha walimu wanatoa taarifa za wanafunzi wanaoacha shule kwa sasbabu za ndoa na ujauzito ili mkoa uweze kuchukua zinazostahili ikiwemo kuwafikisha wahusika katika vyombo vya sheria.

Kazi ya kutengeneza ujumbe kwa ajili ya kutokomeza mimba na ndoa za utotoni inaendelea itaendelea katika mikoa yenye takwimu za juu katika ukatili dhidi ya wanawake na watoto ambayo ni mikoa ya Shinyanga, Tabora, Singida na Rukwa.   
  Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Watoto kutoka Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Sebastian Kitiku akiongea na wadau kujadili hali jumbe zitakazotumika kutokomeza vitendo vya ukatili mkoani Shinyanga leo mjini Shinyanga.
 Afisa Tawala Mkoa wa  Shinyanga Albert Msovela akiongea na wadau kujadili hali jumbe zitakazotumika kutokomeza vitendo vya ukatili mkoani Shinyanga leo mjini Shinyanga.
 Baadhi ya  wadau kujadili hali jumbe zitakazotumika kutokomeza vitendo vya ukatili mkoani Shinyanga leo mjini Shinyanga.
Baadhi ya  Wajumbe  kutoka Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii wakiwa Mkoani Shinyanga  kujadili hali jumbe zitakazotumika kutokomeza vitendo vya ukatili.
Viewing all 110167 articles
Browse latest View live




Latest Images