Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Wataalamu wa afya wa Jeshi la Polisi wametakiwa kujiweka tayari katika kujadili changamoto na kuibua mikakati endelevu ili waweze kuboresha huduma za afya kwa watu wenye uhitaji, askari pamoja na familia zao.
Hayo yamesemwa leo asubuhi katika hoteli ya SG Resort iliyopo jijini hapa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles Mkumbo kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, wakati wa ufunguzi wa semina ya siku mbili ya wakuu wa vituo tiba vya Polisi Tanzania pamoja na wafanyakazi na watumishi wa JSI kuhusiana na uboreshaji utoaji wa huduma za afya katika kukabiliana na jukumu la kupambana na uzuiaji wa maambukizi ya VVU na UKIMWI.
Alitoa wito kwa Madaktari, Wauguzi na watumishi wengine wanaofanya kazi katika Zahanati na vituo vya afya kuendelea kuwatambua wenye maambukizi ya VVU na UKIMWI kwa kuwapima, kuwaanzishia dawa na kuhakikisha wote walioanza matibabu wanaendelea kutumia dawa kwa kipindi chote cha uhai wao.
Kamanda Mkumbo aliendelea kuwakumbusha washiriki wa mkutano huo kuendelea kuwahudumia wananchi kwa uadilifu na utunzaji mkubwa wa siri za wateja wanaopatiwa huduma za VCT/CTC ikiwa ni sehemu ya kiapo chao juu ya taaluma yao.
Naye Mganga mkuu wa Kikosi cha Afya cha Jeshi la Polisi nchini Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Charles Msenga, alisema kwamba lengo la semina hiyo ambayo inawezeshwa na JSI/AIDS FREE ni kujitathmini namna ya utoaji huduma bora kwa askari, familia zao pamoja na wananchi wengine wanaotumia vituo hivyo.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles Mkumbo akiwahutubia wataalamu wa afya wa Jeshi la Polisi kutoka maeneo mbalimbali nchini wakati wa ufunguzi wa semina iliyofanyika katika hoteli ya SG Resort iliyopo jijini Arusha.
Baadhi ya wataalamu wa afya wa Jeshi la Polisi kutoka katika vituo mbalimbali nchini wakifuatilia hotuba ya ufunguzi wa mkutano huo ambayo ulifunguliwa na Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles Mkumbo kwa niaba ya IGP.
Mgeni rasmi wa ufunguzi wa semina kuhusiana na VVU na UKIMWI kwa wataalamu wa vituo vya afya vya Polisi nchini Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles Mkumbo akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa semina hiyo. Kulia kwake ni Mganga Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Dr. Charles Msenga na kushoto kwake (aliyevaa suti) ni Mkurugenzi wa AIDS FREE Dr. William Nyagwa.
Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha.