Na Greyson Mwase, Dar es Salaam.
Zabuni kwa ajili ya mradi wa Ujenzi wa Bwawa la Kuzalisha Umeme wa Megawati 2100 la Steigler's Gorge katika Maporomoko ya Maji ya Mto Rufiji zimefunguliwa leo tarehe 02 Februari, 2018.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa zabuni hizo kwenye Ofisi za Wizara ya Nishati zilizopo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Idara ya Manunuzi kutoka Wizara ya Nishati, Amon MacAchayo amesema zabuni hizo ni za Awamu ya Pili kutokana na kukosekana kwa mshindi katika Awamu ya Kwanza iliyotangazwa mapema mwaka jana.
Alisema kuwa, katika awamu ya kwanza jumla ya kampuni 81 zilinunua nyaraka za zabuni ambapo nakala moja ilikuwa inauzwa kwa shilingi 200,000 lakini ni kampuni nne tu zilifanikiwa kurejesha maombi na kuongeza kuwa kampuni zote nne hazikuwa na vigezo vinavyohitajika hali iliyopelekea kutangazwa upya kwa zabuni tarehe 19 Desemba, 2017 katika vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi.
MacAchayo aliongeza kuwa, katika awamu ya pili kampuni 17 zilijitokeza katika ununuzi wa nyaraka kwa gharama ya shilingi 500,000 kwa kila moja ambapo mpaka siku zinafunguliwa ni kampuni tano tu zimerejesha nyaraka zenye maombi ya zabuni.
Alisema hatua inayofanyika kwa sasa ni ufanyaji wa tathmini ya zabuni hizo na kusisitiza kuwa mara baada ya kukamilika kwa tathmini ya zabuni hizo waombaji wote watajulishwa mshindi na baada ya hapo zitafuata taratibu za mazungumzo, barua na kuandaa mkataba kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi wa mradi mara moja.Aliwataka kampuni zilizowasilisha maombi kuwa watulivu wakati zoezi la tathmini likiendelea.
Mkurugenzi wa Idara ya Manunuzi kutoka Wizara ya Nishati, Amon MacAchayo (mbele) akizungumza na wawakilishi wa kampuni mbalimbali zilizoomba zabuni kwa ajili ya mradi wa Ujenzi wa Bwawa la Kuzalisha Umeme katika Maporomoko ya Maji ya Mto Rufiji kwenye ofisi za Wizara ya Nishati jijini Dar es Salaam tarehe 02 Februari, 2018
Mtaalam wa Manunuzi kutoka Wizara ya Nishati, Jackson William (kulia) akieleza jambo kwenye ufunguzi huo. Katikati ni Mkurugenzi wa Idara ya Manunuzi kutoka Wizara ya Nishati, Amon MacAchayo na aliyekaa kushoto ni mwakilishi wa kampuni zilizoomba zabuni, Khaled Makkawy kutoka kampuni ya The Arab Contractors
Sehemu ya wajumbe wakifuatilia zoezi la ufunguaji wa zabuni kwa ajili ya mradi wa Ujenzi wa Bwawa la Kuzalisha Umeme katika Maporomoko ya Maji ya Mto Rufiji katika kikao hicho.
Wataalam kutoka Idara ya Manunuzi, Wizara ya Nishati wakifungua nyaraka mbalimbali za zabuni katika kikao hicho.