Na Stella Kalinga, Simiyu
Mhashamu Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la SHINYANGA Liberatus Sangu amewataka Vijana kutokubali kutumiwa kuleta vurugu, chuki na mafarakano hapa nchini.
Askofu Sangu ametoa wito huo wakati wa Ibada ya Sakramenti ya Kipaimara iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu John Mjini Bariadi.“Maandiko Matakatifu yanasema Vijana wana nguvu; kwa hiyo nawasihi vijana popote pale mlipo muwe chimbuko la Upendo, furaha na amani; watu wengine wasitumie nguvu zenu vijana kuleta chuki, fitina na mafarakano, muwe macho” alisema Askofu Sangu.
Askofu Sangu amewaasa waumini wa Kanisa hilo kuishi maisha mema ambayo hayatakuwa chanzo cha mateso kwa watu wengine katika familia, jumuiya , jamii wanaoishi na Taifa kwa ujumla.Aidha, amewataka Watanzania wote kupinga na kukemea mauaji ya watu wenye ualbino kwa kuwa wanayo haki ya kuishi kama watu wengine na watu wote wameumbwa kwa mfano wa Mungu.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka ametoa wito kwa Kanisa kuwa na mtazamo wa kuisaidia nchi katika kupambana na tatizo la ajira hususani kwa vijana.Ameongeza kuwa ni vema Kanisa liyavae maneno ya Mhe.Rais kuhusu Ujenzi wa Tanzania ya Uchumi wa Kati na kuona namna linavyoweza kushiriki katika kufikia Tanzania Mpya, kwa kuimarisha Idara za Kanisa na Vyama vya Kitume na kuzijenga idara na vyama hivyo katika mtazamo wa Kiujasiriamali.
Mhashamu Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la SHINYANGA Liberatus Sangu akiongoza Ibada ya Sakramenti ya Kipaimara katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu John Mjini Bariadi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na Waumini wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu John Mjini Bariadi katika Ibada ya Sakramenti ya Kipaimara iliyoongozwa na Mhashamu Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la SHINYANGA Liberatus Sangu.
Mhashamu Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la SHINYANGA Liberatus Sangu akiwapaka mafuta vijana wa Kipaimara katika Ibada ya Sakramenti ya Kipaimara iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu John Mjini Bariadi.
Mhashamu Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la SHINYANGA Liberatus Sangu akiwabariki vijana wa Kipaimara katika Ibada ya Sakramenti ya Kipaimara iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu John Mjini Bariadi.